Kwa nini baadhi ya watu hupoteza hamu ya tendo la ndoa?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Kupungua au kupotea kwa hamu ya tendo la ndoa ni changamoto inayowasumbua watu wengi duniani, tena wa jinsia zote mbili, yaani wanaume kwa wanawake.

Ingawa mara nyingi suala hili huchukuliwa kama jambo la aibu na mara nyingi hubaki kuwa siri ya mtu. Lakini madaktari wanasema ni hali ya kibayolojia na kisaikolojia inayoweza kumtokea mtu yeyote katika hatua fulani ya maisha.

Kuelewa chanzo cha tatizo hili ni hatua ya kwanza kuelekea kupata suluhisho na kurudisha furaha na maelewano katika uhusiano. Zifuatazo ni sababu kuu zinazochangia watu kupoteza hamu ya tendo la ndoa:

Changamoto za kisaikolojia na kihisia

Ubongo ndio kiungo kikuu cha kwanza kinachochochea hamu ya mapenzi. Ikiwa akili haijatulia, mwili hauwezi kutoa ushirikiano katika kuamsha hisia.

Kwa hiyo mtu mwenye msongo wa mawazo, kutokana na labda ugumu wa maisha, matatizo ya kifedha, au majukumu mazito ya kazi huufanya mwili kuzalisha homoni ya cortisol. Homoni hii inapokuwa nyingi, inaathiri hamu ya tendo la ndoa.

Pia watu wenye sonona, yaani wanaosumbuliwa na sonona au wasiwasi wa mara kwa mara mara nyingi, nao pia hupoteza hisia za furaha na msisimko wa kimwili.

Katika upande wa hisia, mizozo ndani ya uhusiano huchochea mtu kupoteza hamu. Mfano, hasira iliyofichika, kutosameheana, ukosefu wa mawasiliano mazuri, na kutoaminiana kati ya wanandoa, haya mambo huua sana hamu ya mapenzi.

Bayolojia na mabadiliko ya homoni

Mwili unapoingia kwenye mabadiliko fulani ya kikemia au kimaumbile, hamu ya tendo la ndoa huathirika moja kwa moja.

Mfano, kupungua kwa Hormoni ya Testosterone kwa wanaume. Homoni hii inaposhuka hasa kutokana na umri kusonga, nguvu na hamu ya tendo hupungua kwa kiasi kikubwa.

Kukoma kwa hedhi (Menopause) na Ujauzito, ni mambo ambayo hupunguza hamu ya tendo kwa baadhi ya wanawake.

Nyakati za ujauzito, baada ya kujifungua (wakati wa kunyonyesha), au wanapofikia ukomo wa hedhi, viwango vya homoni za estrogen na progesterone hushuka sana. Hali hii husababisha ukavu ukeni na maumivu wakati wa tendo, jambo linalofanya wakimbie tendo hilo.

Matatizo ya kiafya na magonjwa sugu

Magonjwa yanayodhoofisha mwili au kuathiri mfumo wa neva na mzunguko wa damu huchangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma hisia za mapenzi.

Magonjwa hayo ni pamoja na: Ugonjwa wa kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na kansa na matatizo ya tezi ya shingo/dundumio.

Matumizi ya dawa na mitindo ya maisha

Wakati mwingine, tabia zetu za kila siku na vitu tunavyoingiza mwilini ndio vinavyopunguza uwezo wetu wa kufurahia tendo la ndoa au kutamani tendo la ndoa.

Kuna baadhi ya dawa, hasa zile za kupunguza msongo wa mawazo (antidepressants), dawa za shinikizo la damu, na baadhi ya vidonge vya uzazi wa mpango, hupunguza hamu ya tendo la ndoa.

Kufanya kazi ngumu kwa masaa mengi bila kupumzika huacha mwili ukiwa umechoka sana, na nishati pekee inayobaki hutumika kwa ajili ya kulala tu.

Jambo jingine ni unywaji wa kupindukia wa pombe na uvutaji wa sigara huharibu mfumo wa mzunguko wa damu na neva, jambo linalosababisha ugumu wa kusisimka.

Ushauri

Kupotea kwa hamu ya tendo la ndoa sio mwisho wa dunia na wala sio ishara kwamba upendo umeisha. Ni ujumbe kutoka mwilini au akilini kwamba kuna kitu kinahitaji kurekebishwa.

Kushughulikia tatizo hili kunahitaji uwazi na subira. Hatua ya kwanza ni kuzungumza kwa uwazi na mwenza wako bila kulaumiana, ili kujenga uelewa wa pamoja.

Hatua ya pili ni kufanya mabadiliko ya mfumo wa maisha kwa kula mlo kamili, kufanya mazoezi, na kupata muda wa kutosha wa kupumzika. Hatimaye, ikiwa tatizo linaendelea, ni muhimu kumuona daktari au mshauri wa saikolojia ili kufanya vipimo vya homoni au kupata tiba sahihi ya kisaikolojia na magonjwa.