Harry Kane na Lamine Yamal wa Barcelona kuwania tuzo ya Ballon d'Or

Chanzo cha picha, Getty
Macho na masikio ya wapenzi wa soka ulimwenguni kote leo yatakuwa yameelekezwa katika Jumba la Maonyesho la London Palladium, ambapo washindi wa tuzo mashuhuri za Ballon d'Or 2026 watatangazwa rasmi usiku wa leo.
Hii ni mara ya kwanza katika historia kwa sherehe hizi kubwa za utoaji wa tuzo hizo kufanyika nje ya nchi ya Ufaransa, hatua inayoongeza msisimko wa kipekee katika tasnia ya soka.
Sherehe hizo za awamu ya 70 zitahudhuriwa na magwiji wa soka, makocha, na watu mashuhuri, huku zikiendeshwa na mshambuliaji wa zamani wa Ufaransa, Thierry Henry, akishirikiana na mtangazaji mahiri Kate Scott.

Chanzo cha picha, Getty
Vita Vikali vya Kinyang'anyiro
Tofauti na miaka ya nyuma, msimu huu unatajwa kuwa na ushindani mkali zaidi, huku vigezo vya tuzo hiyo vikizingatia kiwango cha wachezaji kwa msimu mzima wa 2025–26 (kuanzia Agosti 3, 2025 hadi Julai 19, 2026) badala ya mwaka wa kalenda wa msimu wa soka
Wachambuzi wengi wa soka wanamtaja nahodha wa timu ya taifa ya Uingereza na mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, kama mchezaji anayepigia upatu mkubwa, wa kushinda tuzo hiyo.
Kane amekuwa na msimu mzuri wa ufungaji mabao nchini Ujerumani na barani Ulaya.
Hata hivyo, Kane anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa chipukizi wa Barcelona na Uhispania, Lamine Yamal, ambaye amewastaajabisha wengi kwa uwezo wake mkubwa uwanjani licha ya umri wake mdogo.
Nyota wa Real Madrid na Ufaransa, Kylian Mbappé, pamoja na viungo wa Uingereza Jude Bellingham na Declan Rice, pia wamo kwenye orodha fupi ya wachezaji 30 na wanatajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuleta mshangao usiku wa leo.

Chanzo cha picha, Getty
Burudani na Sherehe
Mbali na kutoa tuzo kwa mchezaji bora wa kiume na wa kike, usiku wa leo utapambwa na burudani kutoka kwa wasanii wakubwa wa kimataifa kama Jorja Smith na French Montana, kuhakikisha kuwa sherehe hiyo inabaki kuwa ya kihistoria.
Je, Harry Kane atatunukiwa heshima hii kubwa baada ya miaka mingi ya ukame wa mataji, au kijana mdogo Lamine Yamal ataandika historia mpya? Majibu yote yatapatikana usiku wa leo huko London.































