Moja kwa moja, Watu 7 hawajulikani walipo baada ya jengo kuporomoka Eastleigh, Kenya

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, amezitaka familia ambazo ndugu au jamaa zao hawajulikani walipo kufuatia kuporomoka kwa jengo hilo kutoa taarifa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kupitia nambari ya dharura ya 1199.

Muhtasari

Watu 7 hawajulikani walipo baada ya jengo kuporomoka Eastleigh, Kenya

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. TEC yaagiza misa maalumu kuwaombea waathiriwa wa uchaguzi Tanzania

    N

    Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeagiza kuadhimishwa kwa misa maalumu tarehe 29 Oktoba 2026, kwa ajili ya kuwaombea na kuwakumbuka watu waliouawa, kujeruhiwa na kuathiriwa na matukio ya uchaguzi mkuu nchini humo.

    Katika barua ya tarehe 23 Oktoba 2026, iliyosainiwa na Askofu wa Lindi na Rais wa TEC, Wolfgang Pisa, baraza hilo limesema misa hiyo itaadhimishwa katika parokia, vituo vya sala na taasisi za Kanisa Katoliki.

    “Tunaaomba Misa Takatifu ziadhimishwe kwa nia hizo; waliouawa, kupotea na kulilombea Taifa letu,” sehemu ya barua hiyo inasema.

    TEC imesema waumini wanaweza kutumia misa ya asubuhi ya kawaida au misa nyingine yoyote inayofaa, huku masomo ya siku hiyo yakitumika katika misa hizo.

    Baraza hilo pia limewataka waumini kuungana katika sala za kuombea amani, ukweli, haki, upendo na maridhiano nchini Tanzania.

    Katika barua hiyo, TEC imesisitiza umuhimu wa kuwaombea waliojeruhiwa, waliopoteza wapendwa wao na wote walioathiriwa na vurugu, pamoja na viongozi wa nchi na wananchi kwa ujumla.

    “Tunashukuru Misa hiyo ifanyike katika Parokia, vituo vya sala na Taasisi za Kanisa kadiri iwezekanavyo siku ya Alhamisi 29 Oktoba 2026,” barua hiyo imeeleza.

    Takriban watu 518 waliuawa wakati wa machafuko ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 nchini Tanzania, tume ya uchunguzi ya serikali imebaini.

    Huku idadi ya waliofariki wakati wa vurugu ikiwa ni watu 518, idadi ya waliofariki wanaume 490 sawa na asilimia 94.6, na wanawake 28, sawa na asilimia 5.4.

    Haya yanajiri baada ya ripoti ya Jaji Chande kutaja sababu za kisiasa, ikiwemo madai ya Tume huru ya uchaguzi, changamoto za kiuchumi ajira ugumu wa maisha, kijamii kama vile kukosekana kwa uzalendo kuwa miongoni mwa vyanzo vya ghasia za uchaguzi wa Oktoba 29. Soma zaidi:

  2. Watu 7 hawajulikani walipo baada ya jengo kuporomoka Eastleigh, Kenya

    C

    Watu saba hawajulikani walipo baada ya jengo la ghorofa lililokuwa likijengwa kuporomoka katika eneo la Eastleigh, kaunti ya Nairobi, nchini Kenya huku juhudi za uokoaji zikiendelea.

    Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, amesema watu 67 waliokuwa wakifanya kazi ya ujenzi wakati jengo hilo lilipoporomoka wamehesabiwa wote.

    Kati yao, 66 walinusurika bila majeraha, huku mmoja akijeruhiwa na kulazwa hospitalini kwa matibabu ya ziada.

    Katika taarifa yake, Murkomen amesema maduka 11 yaliyokuwa kwenye ghorofa ya chini na kwenye orofa ya chini ya ardhi yalikuwa na watu wakati wa tukio hilo.

    “Juhudi za uokoaji zinaendelea, na timu imefanikiwa kuwasiliana na baadhi ya watu wanaoripotiwa kutoweka,” amesema Murkomen.

    Timu ya mashirika mbalimbali, ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Huduma ya Polisi ya Taifa, serikali ya kaunti ya Nairobi, Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, inaongoza shughuli za utafutaji na uokoaji.

    Murkomen amewataka watu ambao ndugu au jamaa zao hawajulikani walipo kufuatia kuporomoka kwa jengo hilo kutoa taarifa kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kupitia nambari ya dharura ya 1199.

    Aidha, amesema serikali inatoa msaada unaohitajika ili kuharakisha shughuli za uokoaji, huku mipango ya kutoa usaidizi wa kisaikolojia kwa waathiriwa na familia zilizoathirika ikiendelea.

    Chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo kitachunguzwa na taasisi husika za serikali ya kitaifa na kaunti kwa kushirikiana na mashirika ya kitaaluma. Murkomen amesema waliohusika watapasa kuwajibishwa baada ya uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo.

    Jengo hilo liliporomoka Ijumaa alasiri wakati shughuli za kawaida zilikuwa zikiendelea kando yake.

  3. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 24/10/2026.