Kwa nini unapata hamu ya kula usiku hata baada ya kushiba chakula cha jioni?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Umekula chakula cha jioni, umeshiba vizuri, lakini nusu saa baadaye unajikuta ukivamia kabati la jikoni kutafuta kitu cha kula. Je, hali hii unaifahamu?

Utafiti unaonyesha kuwa takribani theluthi moja ya watu hula vitafunio kila usiku baada ya chakula cha jioni. Kwa watu wenye umri wa miaka 18 hadi 24, idadi hiyo ni kubwa zaidi, huku watu wanne kati ya watano wakishindwa kujizuia.

Mtaalamu wa lishe, Dkt Kristine Beaulieu, anasema tabia hii inaweza kusababisha matatizo ya kiafya.

Anarejelea ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kuwa kadiri mtu anavyokula chakula ndani ya saa mbili kabla ya kwenda kulala, ndivyo uwezekano wa kuongezeka uzito na kupata unene kupita kiasi unavyoongezeka.

Kwa nini basi hamu ya kula huongezeka sana nyakati za jioni? Na unaweza kufanya nini ili kuidhibiti?

.

Hamu ya kula huongezeka zaidi nyakati za jioni

Licha ya kwamba tunakaa muda mrefu bila kula tunapokuwa tumelala, tafiti zinaonyesha kuwa hamu yetu ya kula huongezeka nyakati za jioni, bila kujali kiasi cha chakula tulichokula mapema wakati wa mchana.

Profesa James Betts, ambaye hufanya utafiti kuhusu jinsi mwili unavyotumia chakula na nishati katika Chuo Kikuu cha Bath, anasema sababu kubwa ni kwamba kiwango cha homoni ya ghrelin, inayojulikana kama homoni ya njaa, kwa kawaida huwa juu zaidi majira ya jioni yakikaribia.

Hata hivyo, aina ya chakula unachokula pia kina umuhimu. Vyakula vyenye protini nyingi, nyuzinyuzi na vinavyoongeza ujazo tumboni huwa vinakufanya ujisikie umeshiba kwa muda mrefu zaidi.

Betts anasema kutokula chakula cha jioni chenye virutubishi vya kutosha au kinachokushibisha kunaweza kusababisha mwili kupungukiwa na nguvu baadaye, hali inayowafanya watu kutafuta vitafunio.

Kwa wengine, hofu ya kuamka usiku wakiwa na njaa pia huwafanya wale kabla ya kulala, huku mazoea nayo yakichangia tabia hiyo.

Profesa Suzanne Higgs, mtaalamu wa masuala ya hamu ya kula katika Chuo Kikuu cha Birmingham, anasema:

"Ikiwa mtu huwa anakula vitafunio mara kwa mara katika mazingira yale yale, vitu vinavyomzunguka vinaweza kuanza kuchochea hamu ya kula."

"Kwa mfano, ikiwa mtu amezoea kula vitafunio anapotazama televisheni, kuwasha tu televisheni kunaweza kumfanya ahisi kutaka kula."

.

Kwa nini vyakula vitamu hutushawishi zaidi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Si hisia za njaa pekee zinazoongezeka kadri siku inavyoelekea jioni.

Utafiti unaonyesha kuwa hamu yetu ya kula vyakula vyenye kalori nyingi pia huongezeka. Hali hii huchochewa na mfumo wa ubongo unaohusika na hisia za kupata furaha na zawadi, badala ya hitaji halisi la mwili la kupata nishati.

"Jioni, tunakuwa na hamu na mvuto mkubwa zaidi wa kula vyakula vyenye mafuta mengi ikilinganishwa na vile vyenye mafuta kidogo," anasema Beaulieu.

"Msukumo huo wa kutafuta raha kupitia chakula unaweza kushinda ishara za mwili zinazoonyesha kuwa umeshiba, na hivyo kukufanya utake kula vitafunio licha ya kuwa tayari umeshiba."

Hata baada ya kula chakula cha jioni cha kutosha, vyakula vyenye sukari, mafuta au chumvi nyingi vinaweza kuendelea kuchochea mifumo ya ubongo inayohusishwa na hisia za furaha na kupata zawadi. Hali hii inasaidia kueleza kwa nini watu wengi hujikuta wakitafuta kitu kingine cha kula hata baada ya kushiba.

Kwa hiyo, unapojikuta umesimama mbele ya kabati la biskuti saa tatu usiku ukitafuta kitu cha kula, huenda tatizo lisiwe ukosefu wa uwezo wa kujizuia. Bali, huenda biolojia ya mwili wako inachangia kukufanya ushindwe kujidhibiti.

Je, kula vitafunio usiku kunaweza kufanya iwe vigumu kupata usingizi?

Ushahidi wa kisayansi kuhusu suala hili bado haujawa na hitimisho moja.

Hata hivyo, kula chakula kingi nyakati za usiku kunaweza kuathiri mfumo wa mmeng'enyo wa chakula na namna mwili unavyojiandaa kwa kawaida kupata usingizi.

Vipi kuhusu kula vitafunio? Hapa tafiti bado hazijatoa majibu yaliyo wazi.

Kuna baadhi ya ushahidi unaoonyesha kuwa vyakula vyenye wanga uliosindikwa sana na sukari iliyoongezwa, kuanzia mkate mweupe na wali mweupe hadi biskuti na keki, vinaweza kuhusishwa na usingizi usioridhisha.

Watafiti wanadhani huenda hali hii inatokana na vyakula hivyo kusababisha mabadiliko makubwa ya viwango vya sukari kwenye damu na huenda pia kubadilisha baadhi ya ishara za homoni zinazohusika katika kudhibiti usingizi na hamu ya kula.

Hata hivyo, ni vigumu kubaini kwa uhakika uhusiano wa chanzo na matokeo. Watu wenye matatizo ya usingizi wanaweza kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kula vitafunio vyenye sukari nyingi.

Profesa Jonathan Johnston, mtaalamu wa masuala ya usingizi katika Chuo Kikuu cha Surrey, anasema:

"Inafahamika kuwa kukosa usingizi wa kutosha hakuongezi tu hamu ya kula, bali pia huongeza hamu ya kula vyakula vyenye nishati na kalori nyingi."

Hali hii inafanya iwe vigumu kutoa hitimisho la uhakika kuhusu iwapo kula vitafunio nyakati za jioni kunaathiri usingizi, anasema Betts.

Jinsi ya kula vitafunio vyenye afya

Kwanza, tambua ni nini kinachokuchochea kula vitafunio.

Ikiwa una njaa ya kweli, kula milo inayokushibisha zaidi.

Ikiwa kula vitafunio ni mazoea tu, kubadilisha ratiba yako na kupanga mapema aina ya vitafunio utakavyokula kunaweza kusaidia.

Higgs anasema kula huku akili yako ikiwa imeelekezwa kwenye shughuli nyingine, kwa mfano kutazama televisheni, kunaweza kukufanya ule zaidi kwa sababu huzingatii kiasi cha chakula unachotumia.

Hata hivyo, Beaulieu anasema hakuna haja ya kupiga marufuku kabisa kula vitafunio nyakati za jioni.

Kula kiasi cha wastani cha chakula unachokipenda mara nyingi ni njia endelevu zaidi.

Hakikisha unakuwa na vyakula vyenye afya kama matunda, mtindi na karanga.

Hata kula kiasi kidogo cha chokoleti mara kwa mara si tatizo kubwa.

"Ni sawa kula vyakula unavyovitamani mara moja moja, mradi ufanye hivyo kwa kiasi."

Anasema siri ni kufanya uchaguzi wa vyakula vyenye afya kuwa chaguo lako la kawaida.

"Ikiwa vyakula unavyovitamani havipo mara kwa mara kwenye kabati lako, lakini vyakula vyenye afya vinapatikana, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kula vyakula bora kwa afya yako"

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi