Vita vya siri vya GPS vinavyotikisa usafiri wa anga duniani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Ndege ya Jeshi la Anga la Uingereza (RAF) iliyokuwa imembeba Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey, ilikuwa ikipaa katika anga za Estonia karibu na mpaka wa Urusi wiki iliyopita wakati ambapo kitu ambacho si cha kawaida kilitokea.

Kulingana na taarifa za safari ya ndege zilizochambuliwa na BBC World Service, kifaa cha kutuma taarifa za mahali ilipo ndege ghafla kilianza kuonyesha kwamba ndege hiyo ilikuwa ndani ya eneo la Urusi, kilomita 300 kutoka mahali ilipokuwa ndege hiyo.

Taarifa hizo pia zilionyesha kana kwamba ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kwa kasi ya kilomita 11 kwa saa juu ya ziwa karibu na mji wa St. Petersburg.

Ila taarifa hiyo haikuwa ya kweli. Mfumo wa urambazaji wa ndege hiyo ulivurugwa kutokana na udanganyifu wa mawimbi ya GPS.

Hali hii hutokea wakati eneo fulani linajazwa mawimbi ya redio yanayoiga mawimbi halisi yanayotumwa na satelaiti za GPS.

Udanganyifu huu wa GPS (GPS spoofing) kwa kawaida hufanywa na majeshi yanayotaka kupunguza usahihi malengo ya silaha za adui zinazotegemea urambazaji wa GPS, kama vile makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani.

Majeshi mengi yana vitengo maalumu vinavyounda na kuendesha huduma kama hizi.

Safari za ndege za kibiashara pia zimeathirika na aina hii ya vita vya kielektroniki.

Marubani wa Jeshi la Anga la Uingereza (RAF) walilazimika kuongoza ndege hiyo kwa kutumia mfumo wa zamani wa urambazaji ambao si sahihi sana na ambao hufanya kazi pamoja na mfumo wa GPS.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema kuwa usalama wa ndege hiyo haukuwa hatarini kwani haikuwa ndege pekee. Zaidi ya ndege 100 zilikuwa zikituma taarifa ambazo si sahihi kutokana na udanganyifu wa GPS.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na ukanda wa Baltic, Ghuba ya Uajemi, Bahariya Shamu, India, Pakistan, pamoja na maeneo yanayozunguka Myanmar.

Katika Ghuba ya Uajemi, kulikuwa na ongezeko kubwa la ndege zilizoripoti kuathiriwa na udanganyifu wa GPS baada ya kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran Mwezi Februari tarehe 28.

Njia nyingine nyingi za anga zenye shughuli nyingi barani Ulaya, Mashariki ya Kati na Asia pia zimeathiriwa na udanganyifu wa GPS au kuingiliwa kwa mawimbi, huku wastani wa zaidi ya ndege 800 duniani kote zikiathiriwa kila siku mwaka huu.

Teknolojia inayohitajika kufanya udanganyifu huu inapatikana kwa urahisi katika nchi nyingi, wataalamu wana wasiwasi kuwa tatizo hili litaendelea kuenea na kuwa la kawaida zaidi duniani.

Rubani mwenye uzoefu

Hili ni tatizo ambalo rubani wa Uingereza, Sam Rutherford, alikumbana nalo alipokuwa akiendesha ndege ndogo ya watu wanne kutoka Saudi Arabia kwenda Oman mwezi uliopita.

Ndege hiyo ilipokuwa karibu na mpaka kati ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), mifumo yake ya urambazaji na mfumo wa kujiendesha wenyewe ghafla iliacha kufanya kazi.

Mwanzoni, Rutherford alidhani huenda kulikuwa na hitilafu kwenye ndege, lakini baadaye aligundua kuwa mashirika kadhaa ya ndege yaliyokuwa katika eneo hilo yalikuwa yakiripoti tatizo kama hilo.

Ilibainika kuwa ndege yake ilikuwa imeathiriwa na udanganyifu wa GPS pamoja na kuingiliwa kwa mawimbi ya GPS.

Rutherford, ambaye ameendesha ndege aina ya helikopta katika Jeshi la Uingereza kwa miaka minane, alilazimika kutumia dira ya sumaku ya ndege yake na kuwasiliana na waongoza ndege wa trafiki ya anga ili kupata msaada wa kuelekea alikokuwa anakwenda.

Hatari za udanganyifu wa GPS

Moja ya hatari za udanganyifu wa GPS ni kwamba ikiwa ndege itadanganywa na kufikiria iko mahali tofauti, marubani wanaweza kulazimika kuzima au kupuuza tahadhari zinazotolewa na mifumo ya onyo la migongano ardhini, anasema Tanja Harter, rais wa Jumuiya ya Marubani ya Ulaya.

Mfumo huu huwatahadharisha marubani pale unapoona kuwa wanaweza kugonga ardhi au vikwazo vingine kama vile milima.

Harter anasema kuwa kuna ripoti nyingi za marubani kupata tahadhari za uongo .

Pia anaongeza kuwa rada zinazosaidia ndege kuepuka hali mbaya ya hewa zinaweza pia kuacha kufanya kazi.

Uingiliaji unaoruhusiwa

Si haramu kwa nchi kuingilia mifumo ya GPS.

Shirika la Kimataifa la Mawasiliano ITU, linaruhusu hatua kama hizi kwa madhumuni ya usalama au ulinzi, wa ndege

Ila hatua hizi huja na tahadhari kubwa kwamba matumizi yake kwa kiwango kikubwa yanahatarisha usalama wa usafiri wa anga.

Kwa sasa watengenezaji wa ndege wanafanya kazi kwa karibu na wasambazaji wa teknolojia ya anga kutafuta suluhisho za kiufundi dhidi ya udanganyifu huo.

Wataalamu wa sekta hiyo wanapendekeza kuwe na uharaka zaidi wa kutafuta suluhisho.

"Mashirika ya ndege yanahitaji maboresho kwa haraka," anasema Todd Humphreys, profesa wa uhandisi wa anga katika Chuo Kikuu cha Texas.

"Sekta ya anga inatumia teknolojia ya GPS ambayo ni ya zaidi ya miaka 20." Humphreys anaeleza kuwa sekta hiyo inahitaji "vifaa vya kupokea GPS vinavyoweza kustahimili udanganyifu na kuingiliwa kwa mawimbi."

"Nafikiri tutalazimika kutengeneza teknolojia mpya ambazo ni imara zaidi na zinazoweza kuhimili changamoto hizi."

Suluhu

Suluhisho zinazowezekana ni pamoja na kuboresha programu za ndege ili kupunguza athari za kuingiliwa kwa mawimbi, kutumia antena zenye mwelekeo maalum zinazosaidia ndege kupuuza ishara za uongo kutoka ardhini, pamoja na kuanzisha mifumo mipya ya urambazaji inayofanya kazi sambamba na GPS.

Hata hivyo, kuleta mabadiliko katika vifaa vinavyohusiana na usalama wa ndege ni mchakato unaoweza kuchukua muda mrefu.