Netanyahu aongoza, lakini serikali bado kitendawili: Nini kinafuata Israel?

Eisenkot (kushoto) na Netanyahu (kulia) wanatarajiwa kukosa idadi ya viti vinavyohitajika kuunda serikali.
Maelezo ya picha, Eisenkot (kushoto) na Netanyahu (kulia) wanatarajiwa kukosa idadi ya viti vinavyohitajika kuunda serikali.
    • Author, Tom Bennett
    • Nafasi, Tel Aviv
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Israel inaonekana kuelekea katika mkwamo mwingine wa kisiasa. Huku asilimia 85 ya kura zikiwa zimehesabiwa, dalili zinaonyesha kuwa Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Benjamin Netanyahu, na mpinzani wake mkuu, Gadi Eisenkot, hawajapata idadi ya viti vinavyohitajika kuunda serikali yenye wingi bungeni.

Katika hali hiyo, moja ya vyama vikuu huenda ikalazimika kuvunja baadhi ya ahadi zake za kampeni ili kufanikisha muungano wa serikali. Iwapo hilo halitatokea, nchi inaweza kujikuta ikirejea tena kwenye uchaguzi mpya.

Haya ndiyo mamba manne yanayoweza kujitokeza.

Serikali ya umoja wa kitaifa inayoongozwa na Netanyahu

.

Je, Netanyahu anaweza kumshawishi Eisenkot kuunda serikali ya umoja wa kitaifa?

Ili hilo litokee, Gadi Eisenkot atalazimika kuachana na ahadi yake kuu ya kisiasa. Tangu mwanzo wa kampeni, amejitambulisha kama mbadala pekee wa Benjamin Netanyahu, akiahidi kumng'oa madarakani.

Akihutubia wafuasi wake katika makao makuu ya kampeni yake usiku wa uchaguzi, Eisenkot alimtaka Netanyahu "atangaze kustaafu siasa leo hii." Pia alisema Waisraeli wamechoshwa na kile alichokiita "utamaduni wa uongo", pamoja na siasa za "mgawanyiko na uchochezi" zinazohusishwa na Netanyahu.

Hata hivyo, kauli hizo zilitolewa kabla ya moja ya tafiti kuu za kura ya maoni baada ya upigaji kura kufanyiwa marekebisho. Tofauti na makadirio ya awali yaliyokuwa yakionyesha kambi ya Eisenkot ikiongoza, matokeo yaliyorekebishwa yalimpa Netanyahu nafasi ya mbele.

Katika mazingira hayo, Netanyahu anaweza kujaribu kushawishi chama cha Yashar cha Eisenkot kuingia katika muungano na chama chake cha Likud na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo, hilo linaweza kutegemea utayari wake wa kuachana na washirika wake wa sasa wa mrengo mkali wa kulia pamoja na vyama vya Kiyahudi vya Kiorthodoksi vinavyomuunga mkono.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini dalili za mwanzo hazioneshi mwelekeo huo. Akizungumza katika makao makuu ya Likud baada ya uchaguzi, Netanyahu aliwashukuru "washirika wake waaminifu" na kusisitiza haja ya kuunda "serikali imara ya mrengo wa kulia". Kauli hiyo imefasiriwa na baadhi ya wachambuzi kama ishara kwamba hana nia ya kuvunja ushirikiano wake wa sasa.

Jambo linaloweza kuongeza uwezekano wa serikali ya umoja ni kuzuka kwa mgogoro mpya wa kiusalama, hasa ikiwa mvutano na Iran utaongezeka. Katika mazingira kama hayo, shinikizo linaweza kuongezeka kwa viongozi wa kisiasa kuweka kando tofauti zao na kushirikiana kwa maslahi ya taifa.

Katika siku chache kabla ya uchaguzi, vyombo vya habari vya Israel na Marekani viliripoti kuwa Netanyahu alikuwa akishinikiza kufanyika kwa mashambulizi mapya dhidi ya Iran na kwamba alikuwa amemwomba Donald Trump kuidhinisha ushiriki wa Marekani.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanaweza kutafsiri hatua yoyote ya aina hiyo kama jaribio la kuimarisha nafasi yake ya kisiasa kwa kuingiza Israel katika mzozo mwingine wa kikanda. Kwa sasa, uwezekano wa serikali ya umoja bado upo, lakini utahitaji mmoja wa viongozi hao kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa ambayo hadi sasa amekuwa akiyapinga hadharani.

Muungano unaoongozwa na Eisenkot pamoja na vyama vya Waarabu

.

Hili lingekuwa mabadiliko makubwa katika siasa za Israel. Tangu kuanzishwa kwa taifa hilo, ni chama kimoja tu huru cha Kiarabu ambacho kimewahi kuwa sehemu ya muungano rasmi wa serikali, mwaka 2021, na ushirikiano huo haukudumu kwa muda mrefu.

Eisenkot pamoja na vyama vingine vya Kiyahudi vilivyo katika kambi yake tayari wamekataa wazo la kuunda serikali kwa ushirikiano na vyama vya Kiarabu. Hata hivyo, kwa kuzingatia hesabu za sasa za viti, huo unaweza kuwa ndiyo njia pekee kwa upinzani kupata mamlaka.

Vyama vya Kiarabu ndivyo vilivyovutia zaidi katika uchaguzi huu. Kinyume na matarajio ya wengi, vinaonekana kuelekea kupata jumla ya viti 19, idadi ambayo inaweza kuwa rekodi mpya. Mafanikio hayo yamechangiwa na ongezeko kubwa la ushiriki wa wapiga kura Waarabu wa Israel, ambao ni karibu asilimia 20 ya wakazi wa nchi hiyo na wengi wao hujitambulisha kama Wapalestina raia wa Israel.

Kwa miaka mingi, sehemu ya jamii hiyo ilikuwa ikisusia uchaguzi wa Israel, ikidai kuwa kushiriki kupiga kura kunahalalisha mfumo ambao wanaona unawabagua na kuwachukulia kama raia wa daraja la pili. Hata hivyo, safari hii wapiga kura wengi walijitokeza kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya mrengo wa kulia zaidi katika historia ya Israel, hatua ambayo imebadili kabisa hesabu za kisiasa.

Orodha ya Waarabu, inayokadiriwa kushinda takriban viti saba, imesema iko tayari kushiriki katika serikali ya upinzani. Wakati huohuo, The Joint List, inayotarajiwa kupata karibu viti 12, imeeleza kuwa inaweza kuiunga mkono serikali hiyo kutoka nje ya muungano rasmi.

Hata hivyo, hadi sasa ni viongozi wachache sana wa Kiyahudi wanaounga mkono mpango wa aina hiyo. Miongoni mwao ni Yair Golan wa chama cha Democrats. Hata kama muungano kama huo ungeundwa, ungekuwa dhaifu na wenye migogoro ya mara kwa mara, hasa kuhusu masuala nyeti kama vita vya Gaza na mustakabali wa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

Kwa ujumla, msimamo wa vyama vingi vya Kiyahudi wa kupinga ushiriki wa vyama vya Kiarabu serikalini unaonyesha ukubwa wa mgawanyiko wa kisiasa na kijamii unaoendelea kuikumba Israel.

Netanyahu na wengi wa wanasiasa wa mrengo wa kulia wa upinzani

Je, Netanyahu anaweza kuwashawishi wanasiasa wa mrengo wa kulia katika kambi ya Eisenkot wahamie upande wake?

Njia nyingine inayoweza kumwezesha Netanyahu kuunda serikali ni kuwashawishi baadhi ya vyama vya mrengo wa kulia vilivyo katika kambi ya Eisenkot kujiondoa na kujiunga na muungano wake.

Wanasiasa wanaotajwa mara nyingi katika muktadha huo ni Naftali Bennett, kiongozi mwenza wa muungano wa Beyachad, na Avigdor Lieberman, kiongozi wa chama cha Yisrael Beiteinu. Wote wawili ni wanasiasa wa mrengo wa kulia wenye msimamo mkali kuhusu masuala ya usalama na kwa kiasi fulani wanashiriki misingi ya kisiasa inayofanana na ya Netanyahu.

Hata hivyo, uwezekano wa hatua hiyo unaonekana kuwa mdogo. Bennett na Lieberman walifanya kampeni wakiahidi kumuondoa Netanyahu madarakani. Pia wamekuwa wakisisitiza upanuzi wa huduma ya lazima ya kijeshi kwa Wayahudi wa Kiorthodoksi, msimamo unaowaweka katika mgongano wa moja kwa moja na vyama viwili vya Kiorthodoksi ambavyo ni washirika muhimu wa Netanyahu serikalini.

Kutokana na tofauti hizo, ni vigumu kuona jinsi pande hizo zingekubaliana kuunda muungano mmoja.

Baadhi ya wachambuzi wamependekeza kuwa vyama vya Bennett na Lieberman vinaweza kuchukua nafasi ya vyama vya Kiorthodoksi katika muungano wa Netanyahu. Hata hivyo, kulingana na hesabu za sasa za kura, mpangilio huo huenda bado usitoshe kufikisha idadi ya viti vinavyohitajika kuunda serikali yenye wingi bungeni.

Uchaguzi mpya

Kama hakuna mojawapo ya njia zilizotajwa hapo juu itakayowezesha kuundwa kwa serikali, Israel huenda ikalazimika kufanya uchaguzi mwingine.

Kwa wengi, hali hiyo inaweza kuwa habari njema kwa Netanyahu. Hata kama hatapata idadi ya kutosha ya viti kuunda serikali sasa, ataendelea kuhudumu kama Waziri Mkuu wa mpito hadi uchaguzi mpya utakapofanyika. Hilo linaweza kumpa muda zaidi wa kujiandaa na kujaribu kuboresha nafasi yake ya kushinda.

Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa ushiriki mkubwa wa wapiga kura Waarabu ulioshuhudiwa katika uchaguzi huu huenda usijirudie tena. Wengi wa wapiga kura hao walijitokeza kwa matumaini ya kuleta mabadiliko ya kisiasa. Ikiwa ongezeko lao la uwakilishi bungeni halitaleta matokeo ya haraka, baadhi yao wanaweza kukata tamaa na kutoshiriki kwa wingi katika uchaguzi mwingine.

Wakati huohuo, uchaguzi mpya unaweza kuwahamasisha zaidi wapiga kura wa mrengo wa kulia kujitokeza kupiga kura. Netanyahu pia anaweza kutegemea ukweli kwamba maelfu ya Waisraeli waliorejea kutoka nje ya nchi kushiriki uchaguzi huu, ambao wengi wanaaminika kumuunga mkono upinzani, huenda wasifanye safari kama hiyo tena.

Aidha, baadhi ya vyama vidogo vya mrengo wa kulia vilishindwa kufikia kizingiti cha asilimia 3.25 kinachohitajika kuingia bungeni. Katika uchaguzi mwingine, baadhi ya vyama hivyo vinaweza kuungana na vyama vikubwa au kuamua kutoshiriki kabisa, jambo ambalo linaweza kuelekeza kura nyingi zaidi kwa Likud na washirika wake.

Israel tayari ina historia ya kurejea mara kwa mara kwenye uchaguzi kutokana na mkwamo wa kisiasa. Kati ya mwaka 2019 na 2022, taifa hilo lilifanya uchaguzi mara tano kwa sababu hakuna upande ulioweza kupata nguvu za kutosha kuunda serikali thabiti.

Kwa hiyo, ikiwa viongozi wa kisiasa watashindwa kufikia mwafaka baada ya uchaguzi huu, Waisraeli wanaweza kujikuta wakirejea tena kwenye sanduku la kura. Hilo linaweza kuonekana kama ishara ya mkwamo unaoendelea, lakini kwa Netanyahu linaweza kuwa fursa nyingine ya kujaribu kurejea madarakani akiwa na nguvu zaidi.