Michael Carrick, kusalia kocha wa Manchester United licha ya matokeo mabaya
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Picha ya Michael Carrick, Kocha wa Manchester United
Michael
Carrick ataendelea kuwa kocha wa
Manchester United katika safari yao ya kukabiliana na Chelsea wikendi hii.
Vyanzo
tofauti vimeiambia
BBC Sport kuwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 atapewa fursa ya kubadili
mwelekeo wa matokeo ya klabu hiyo baada ya kuanza vibaya msimu huu.
Carrick
ameongoza mazoezi ya timu hiyo leo asubuhi huku Manchester United
ikilenga kupata ushindi dhidi ya Chelsea baada ya
kucheza mechi nane bila ushindi wowote
Chelsea
watachuana na Manchester United katika
uwanja wa Stamford Bridge siku ya
Jumamosi.
Kipigo
cha mabao 3-0 dhidi ya Bournemouth katika uwanja wa Old Trafford siku ya Jumapili kiliibua mashaka kuhusu
mustakabali wa Carrick, huku Manchester United ikiwa nafasi moja tu juu kabla ya kushushwa daraja.
Wahouthi: Msaada wa Misri kwa Saudi Arabia ni tangazo la vita dhidi ya Yemen
Chanzo cha picha, Getty Images
Afisa
mmoja wa kundi la Kihouthi
nchini Yemen, amesema kuwa uamuzi wa Bunge la
Misri kuidhinisha kutoa msaada
wa kijeshi kwa Saudi Arabia ili kuilinda dhidi ya mashambulizi ya Wahouthi ni
sawa na ‘kutangaza’ vita na kundi hilo
Mohammad
Ali Houthi, afisa wa kisiasa wa kundi la Wahouthi, aliandika ujumbe kwenye
mtandao wa Telegram akizungumzia mkutano wa jana mjini Tehran, Iran,
uliohusisha maafisa wa Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia.
“Misri na bunge lake linaunga mkono kile kinachoitwa
‘kuutetea Ufalme wa Saudi Arabia’, na kwa kufanya hivyo, wametangaza vita dhidi ya Jamhuri ya Yemen,”
aliandika afisa huyo.
Waziri
wa Ulinzi wa Saudi Arabia, Khalid bin Salman, Mkuu wa Jeshi la Pakistan,
Jenerali Asim Munir, na Mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Uturuki, Ibrahim Kalin,
walikutana jana mjini Tehran na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, pamoja na
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Mohsen Rezaei.
Saudi
Arabia imesema kuwa lengo la mkutano huo ni kujaribu kupunguza mvutano na
kuimarisha amani katika eneo hilo.
Saudi
Arabia, Pakistan na Uturuki zilitia saini mkataba wa ulinzi unaofanana na ule
wa NATO mjini Makka. Kwa
mujibu wa mkataba huo, shambulizi dhidi ya nchi yoyote kati ya hizo tatu
linachukuliwa kuwa shambulizi dhidi ya nchi zote tatu.
Hata
hivyo, tangu Wahouthi walipozidisha mashambulizi dhidi ya Saudi Arabia,
Pakistan na Uturuki hazijatangaza kutekeleza mashambulizi yoyote dhidi ya kundi hilo.
Kundi la RSF laishtumu jeshi la Sudan kwa kutekeleza mauaji Kusini mwa Darfur
Chanzo cha picha, Getty Images
Maafisa
wanaohusishwa na wapiganaji wa kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces
(RSF) nchini Sudan wamesema
mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika mji wa Nyala, jimbo la Darfur
Kusini, yamewaua watu 102 na kujeruhi zaidi ya
watu 100.
Hata
hivyo, ripoti nyingine imesema idadi ya waliofariki ni watu 21.
Jeshi
la taifa la Sudan na kikosi cha wanamgambo wa RSF wanazidi kutumia ndege zisizo na rubani
katika vita vinavyoingia mwaka wa nne sasa. RSF imetuhumiwa kufanya
mashambulizi dhidi ya vituo vya umeme katika siku za hivi karibuni.
Nyala
inatumika kama mji mkuu wa RSF na
umekuwa ukilengwa mara kwa mara na jeshi la Sudan.
Mashuhuda
walionukuliwa na Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) walisema soko moja
kaskazini mwa mji huo ulishambuliwa,
na takriban watu 20 kuuawa.
Hata
hivyo, afisa anayehusishwa na RSF amesema idadi ya waliouawa na kujeruhiwa ni
kubwa zaidi, akilaani kile alichokiita “janga la kibinadamu.”
Niger yaishtumu Chad kwa shambulizi la droni lililowaua watu watatu
Chanzo cha picha, Getty Images
Niger
imeishutumu nchi jirani ya Chad kwa kutekeleza shambulizi la ndege isiyo na rubani katika ardhi yake na kusababisha vifo vya watu watatu, ikidai kuwa shambulizi hilo
lilifanyika kwa uungwaji mkono wa Ufaransa.
Katika
taarifa iliyotangazwa kupitia televisheni ya taifajana usiku, serikali ya kijeshi ya Niger imedai kuwa ndege isiyo na rubani
iliyorushwa kutoka eneo la Chad ilishambulia
kijiji kimoja katika eneo la Agadez, kaskazini mwa nchi hiyo, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Shambulizi
hilo lilisababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine kadhaa.
Niger
imedai kuwa ina ushahidi wa kutosha
kuhusu shambulio hilo, ila hawajatoa hadharani Ushahidi huo.
Serikali
ya kijeshi ya Niger imesema kuwa imeanzisha uchunguzi wa kina, na itachukua hatua za kisheria
katika mahakama za kimataifa. Pia inapanga kumwita balozi wa Chad nchini Niger
ili kuwasilisha malalamiko kuhusu kile walichokitaja kuwa ukiukaji wa uhuru
na mamlaka ya Niger katika ardhi yake.
Chad
na Ufaransa bado hazijatoa tamko
lolote kuhusu tuhuma hizo.
Tuhuma
hizo zimeibuka wakati uhusiano kati ya Niger na Ufaransa ukiendelea kuzorota
tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika
mwezi Julai 2023 yaliyoileta serikali ya sasa madarakani na baadaye kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa kutoka
nchini humo.
Mamlaka
za kijeshi zinazoitawala Niger zimekuwa zikiishutumu mara kwa mara Ufaransa kwa
kujaribu kuyumbisha nchi hiyo, madai ambayo Paris imekuwa ikiyakanusha.
Mohammad
Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran, amesema kuwa kiongozi mkuu wa Iran Mojtaba
Khamenei, yuko katika hali nzuri ya afya na “ana udhibiti kamili
wa masuala yote ya serikali ya Iran”
Bwana
Qalibaf alisema hayo katika kikao cha wazi cha Bunge la Iran hii leo, “Kwa kawaida, mojawapo ya
maswali wanayouliza watu ni
kuhusu afya ya Kiongozi wa Iran. Ningependa
kuwafahamisha wawakilishi kwamba Bwana Mojtaba Khamenei ana afya njema kabisa.”
Vyombo
vya habari vya Iran hivi karibuni viliripoti kuwa Bwana Qalibaf alikuwa
amekutana na Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tangu
kuchaguliwa kumrithi baba yake, Ali Khamenei, aliyeuawa katika mashambulizi ya
pamoja ya Israel na Marekani, hakuna video wala sauti ya Mojtaba Khamenei ambayo imetolewa hadharani. Kilichochapishwa
ni jumbe za maandishi pekee zinazohusishwa naye.
Maafisa
wa Iran wamesema kuwa hatua za kiusalama ndizo
zimefanya kiongozi huyo asionekane
hadharani.
Takriban watu 60 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti Ethiopia
Chanzo cha picha, Getty Images
Takriban watu 60 wameuawa katika mashambulizi mawili tofauti yaliyotokea ndani ya wiki moja katika eneo la Oromiya nchini Ethiopia, ambalo limekumbwa na mizozo, Kanisa la Orthodox la Ethiopia limesema.
Maafisa wa kanisa hiyo wamesema kuwa wote waliouawa walikuwa Wakristo, lakini hawakutoa maelezo zaidi kuhusu jinsi walivyouawa au waliohusika na mashambulizi hayo.
Serikali ya eneo la Oromiya na muungano wa waasi wanaopambana na vikosi vya serikali katika eneo la kaskazini la Tigray, wametupiana lawama kuhusu mashambulizi hayo.
Kanisa takatifu la Orthodox la Ethiopia lililoko eneo la Tewahedo, limesema waumini 14 waliuawa katika eneo la Merti Woreda tarehe 20 mwezi Oktoba, huku wengine 46 wakiuawa katika eneo la Sherka Woreda tarehe 24 Oktoba.
Taarifa ya kanisa iliyotolewa hapo jana imesema kuwa zaidi ya nyumba 20 zilichomwa moto na zaidi ya watu 20 wamelazwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya.
Serikali ya eneo la Oromiya imesema muungano wa waasi ndiyo ulianzisha mashambulizi hayo kwa lengo la kuchochea mzozo wa kidini, ila hakuna ushahidi wa kutosha wa kuunga mkono madai hayo.
Kamanda mkuu wa jeshi la Tigray ajisalimisha kwa jeshi la Ethiopia
Chanzo cha picha, BraKheshow
Meja Jenerali Yohannes W/Giorgis, kamanda wa Kikosi cha Kusini cha majeshi ya Tigray, amejisalimisha kwa jeshi la Ethiopia na washirika wake, wanaojulikana kama Tigray Peace Forces, kwa mujibu wa vyanzo viwili vilivyo karibu na jeshi la Ethiopia vilivyozungumza na BBC.
Meja Jenerali Yohannes, anayejulikana pia kwa jina la John Medid, alikuwa mwanachama wa Kamandi Kuu na Kamandi ya Kijeshi ya majeshi ya Tigray.
Vyanzo hivyo vimesema Yohannes, walinzi wake na makamanda wengine wanane wenye vyeo vya kanali walizingirwa na Jeshi la Ulinzi la Taifa la Ethiopia (NDF) pamoja na washirika wake, katika kijiji cha Simret, wilayani Rama, eneo la kati la Tigray, siku ya Jumamosi.
Mmoja wa vyanzo hivyo ameiambia BBC kuwa Yohannes kwa sasa yuko Adwa.
Hata hivyo, BBC haijaweza kuthibitisha kwa kujitegemea taarifa hizo. Taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na wanaharakati wanaounga mkono serikali hazijaweza kuthibitishwa. Serikali ya Ethiopia nayo haijatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo.
Kikosi cha Kusini alichokuwa akiongoza Yohannes kilijumuisha majeshi 24, yaliyoko Alamata; 26, Samre; 22, Mekelle; 44, Adi Gudem; na 43, Mekoni.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, kabla ya kuteuliwa kuwa kamanda wa Kikosi cha Kusini, Yohannes alikuwa kamanda wa Jeshi la Pili.
Tetesi za Soka Jumanne: Arsenal yamfuatilia mshambuliaji Varela
Chanzo cha picha, Getty Images
Arsenal na Napoli zinavutiwa na mshambuliaji
wa Ureno Gustavo Varela, mwenye umri wa miaka 21, anayeichezea Monza na ambaye
amekuwa katika kiwango kizuri hivi karibuni. Benfica, klabu yake ya zamani, pia
inamtaka. (Gazzetta dello Sport kupitia Calciomercato)
Crystal Palace haitaki kumuuza winga wa
Senegal Ismaila Sarr, mwenye umri wa miaka 28, katika dirisha la usajili la
Januari, baada ya kufanya mazungumzo kuhusu mkataba mpya. Sarr alitaka kujiunga
na Liverpool katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi. (Football
Insider)
Brighton,
Liverpool, Real Madrid na Barcelona zinaendelea kumfuatilia kwa karibu beki wa
kati wa Croatia Luka Vuskovic, mwenye umri wa miaka 19, ambaye anaichezea
Brighton. (Teamtalk)
Liverpool inamthamini
kiungo wa kati wa Ujerumani Felix Nmecha, mwenye umri wa miaka 26, anayeichezea
Borussia Dortmund. Hata hivyo, haonekani kuwa miongoni mwa wachezaji wanaopewa
kipaumbele katika mipango yao ya usajili. (Florian Plettenberg)
Aliyekuwa
kocha wa Newcastle United, Eddie Howe, huenda akataka kuondoka na benchi lake
lote la ufundi iwapo Manchester United itamfikia kuhusu nafasi ya ukocha mkuu. (Express)
Manchester
United italazimika kulipa fidia ya takriban pauni milioni sita kwa Newcastle
ili kumsajili Howe, kwa mujibu wa masharti ya kuondoka kwake katika klabu hiyo.
(The Telegraph)
Mwenye
klabu ya Bournemouth, Bill Foley, ameidhinisha ofa mpya ya mkataba ambayo
itavunja rekodi ya klabu hiyo kwa kiungo wa kati wa England Alex Scott, mwenye
umri wa miaka 23. Chelsea, Liverpool, Arsenal na Tottenham zinafuatilia kwa
karibu maendeleo ya mazungumzo hayo. (Teamtalk)
Manchester
United imeelezwa kuwa italazimika kulipa zaidi ya pauni milioni 70 kumsajili
beki wa kushoto wa Newcastle United, Lewis Hall, mwenye umri wa miaka 22. (Football
Insider)
Ajax
inataka kumsajili moja kwa moja mshambuliaji wa Nigeria Tolu Arokodare, mwenye
umri wa miaka 25, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo katika klabu hiyo ya Uholanzi
kutoka Wolves. (Sport Witness)
Crystal
Palace itatafuta kocha ambaye hana klabu kwa sasa
iwapo itaamua kumfuta kazi kocha wake Mfaransa, Pierre Sage. (Football
Insider)
Aliyekuwa
makocha wa Brentford na Tottenham, Thomas Frank, pamoja na
aliyewahi kuzinoa Burnley, Everton na Nottingham Forest, Sean
Dyche, wanatajwa kuwa miongoni mwa wanaoweza kuchukua nafasi ya Sage iwapo
Crystal Palace itaamua kuachana naye. (The i)
Wataalamu wa China wajiunga na juhudi za uokoaji baada ya jengo kuporomoka Kenya
Chanzo cha picha, Mtandao wa X
Timu ya utafutaji na uokoaji ya China, Blue Sky Rescue, imejiunga na operesheni ya kutafuta watu walionasa kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka katika eneo la Eastleigh, Nairobi, ikiwa na vifaa maalumu vya kugundua manusura.
Akizungumza na umma muda mfupi baada ya kutembelea eneo la tukio, Mbunge wa Kamukunji, Yusuf Hassan, alisema timu hiyo imegundua watu wawili wakiwa hai katika sehemu ya chini ya jengo hilo, hatua iliyoongeza matumaini ya kuwapata manusura zaidi.
“Leo alasiri, timu ya utafutaji na uokoaji ya China, Blue Sky Rescue (USAR), imejiunga na juhudi hizi ikiwa na vifaa maalumu. Tayari wamegundua watu wawili wakiwa hai kwenye sehemu ya chini ya jengo,” alisema Hassan.
Blue Sky Rescue ni shirika lisilo la kiserikali la China linalojishughulisha na shughuli za dharura, likiwemo kutafuta na kuwaokoa watu wanaonaswa kwenye majanga kama vile kuporomoka kwa majengo, matetemeko ya ardhi na mafuriko.
Shirika hilo hutumia timu zilizopata mafunzo maalumu pamoja na vifaa vya kisasa kutafuta manusura na kusaidia operesheni za uokoaji.
Jengo hilo, ambalo lilikuwa bado linajengwa, liliporomoka Ijumaa, Oktoba 23, na kusababisha operesheni ya dharura huku familia zikitafuta taarifa kuhusu ndugu zao waliokuwa huenda ndani ya jengo hilo.
Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) limesema manusura sita wameokolewa hadi sasa, huku timu za uokoaji zikiendelea kutafuta watu wengine waliofukiwa na vifusi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Oktoba 26, KDF ilisema watu wengine wawili waliokolewa katika operesheni zilizofuata na kupelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta wakiwa katika hali nzuri kwa ajili ya matibabu na uangalizi zaidi.
Wakati huohuo, Gavana Sakaja amezua maswali kuhusu vibali vya ujenzi huo. Alisema serikali ya kaunti iliidhinisha mabadiliko ya matumizi ya jengo hilo kutoka makazi ya watu pekee hadi matumizi ya biashara na makazi mwezi Oktoba 2024, lakini haikuidhinisha michoro ya usanifu wa jengo hilo.
Sakaja pia amehoji jinsi maduka yalivyoruhusiwa kufanya kazi katika ghorofa ya chini licha ya taarifa kuwa jengo hilo halikuwa na cheti cha kuruhusu watu kulikalia au kulitumia.
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imeagiza Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuchunguza mazingira yaliyopelekea jengo hilo kuporomoka, ikiwemo nafasi ya maafisa wa kaunti na mkandarasi katika tukio hilo.
Chanzo cha picha, MITANDAONI
Serikali ya Kenya yasema haijapokea taarifa rasmi kuhusu madai ya kutekwa kwa Twaha Mwaipaya
Chanzo cha picha, MITANDAONI
Ofisi ya Msemaji wa Serikali ya Kenya imesema haijapokea taarifa rasmi kutoka kwa taasisi yoyote kuhusu raia wa Tanzania, Twaha Mwaipaya, anayedaiwa kutekwa nchini humo.
“Bado hatujapata taarifa kuhusu tukio hilo, hivyo tunalifuatilia,” ofisi hiyo imeiambia BBC Swahili.
Kauli hiyo inakuja baada ya Ubalozi wa Tanzania nchini Kenya pia kusema kuwa haujapokea taarifa zozote kuhusu madai ya kutekwa kwa mwanaharakati huyo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International Kenya liliripoti tukio hilo, likisema Mwaipaya alizuiliwa na watu waliokuwa wakitumia magari matatu, likiwamo Toyota Land Cruiser Hardtop.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii Jumapili, shirika hilo lilisema Mwaipaya, raia wa Tanzania, alidaiwa kutekwa majira ya saa nane mchana katika eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos.
“Alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki,” ilisema taarifa hiyo.
Mashirika ya haki za binadamu, yakiwemo Amnesty International Kenya na Defenders Coalition, yametaka hatua za haraka zichukuliwe kumtafuta.
Kisa hicho pia kimeibua upya wasiwasi kuhusu kile ambacho mashirika hayo yanakitaja kuwa ukandamizaji unaovuka mipaka ya nchi dhidi ya wapinzani wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha madai ya kuhusika na vitendo visivyo halali dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi au tamko lolote lililotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo la kutekwa kwa Mwaipaya.
BBC Swahili inaendelea kufuatilia suala hilo na kutafuta ufafanuzi kutoka kwa mamlaka husika nchini Kenya, ikiwamo ofisi inayoshughulikia masuala ya nje.
Israel yapiga kura huku Iran ikitikisa siasa za uchaguzi
Raia wa Israel wanapiga kura leo, ikiwa ni uchaguzi mkuu wa
kwanza tangu wapiganaji wa Hamas walipofanya mashambulizi Oktoba 7, mwaka 2023.
Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, mgawanyiko mkubwa
ulijitokeza kati ya Waziri mkuu anayetetea kiti chake Benjamin Netanyahu na
mkuu wake wa majeshi juu ya mpango wa kuishambulia Iran kabla ya uchaguzi.
Waziri wa Ulinzi Israel Katz amelazimika kukanusha taarifa
kadhaa kwamba Waziri mkuu Netanyahu ana nia ya kumfukuza kazi Jeneral Eyal
Zamir iwapo atashinda awamu nyingine madarakani.
Mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi huo Gadi Eisenkot,
amemtupia lawama Netanyahu kutumia kitisho cha Iran, kujinufaisha kisiasa.
Trump atilia shaka uadilifu wa uchaguzi wa Lula nchini Brazil
Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, amedokeza kuwa uchaguzi wa urais uliofanyika Brazil Jumapili iliyopita haukuwa huru na wa haki, akidai kuwa ulionekana kama uchaguzi mwingine uliochezewa matokeo.
“Sikuegemea upande wowote, lakini ulionekana kama uchaguzi mwingine ambao matokeo yake yalipangwa,” alisema Trump Jumatatu, akizungumzia uchaguzi ambao Rais wa sasa wa mrengo wa kushoto, Luiz Inácio Lula da Silva, alimshinda mgombea wa mrengo wa kulia, Flávio Bolsonaro.
“Uchaguzi unapaswa kuwa huru na usioacha nafasi ya mashaka, lakini kwa mtazamo wangu, hali ilionekana kuwa mbaya sana,” aliongeza Trump, bila kutoa ushahidi wowote mahususi kuunga mkono madai yake.
Hata hivyo, alipoulizwa kama alikusudia kuchukua hatua yoyote kuhusu uchaguzi huo, Trump alisema: “Mimi siiongozi Brazil. Ninaiongoza Marekani.”
Trump pia alisema kuwa ana uhusiano mzuri sana na Lula, lakini akaeleza kuwa muda wa uchaguzi kuendelea zaidi ya ilivyotarajiwa ulikuwa wa kushangaza sana.
Lula alipata ushindi wa kihistoria kwa kuwa mgombea wa kwanza tangu Brazil irejeshe utawala wa kidemokrasia kushindwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi, kisha kurejea na kushinda katika duru ya pili.
Kwa mujibu wa Tume ya Juu ya Uchaguzi ya Brazil (TSE), baada ya kura zote kuhesabiwa, Lula alipata asilimia 51.7 ya kura, huku Bolsonaro akipata asilimia 48.2.
Tofauti ya kura kati ya wagombea hao wawili ilikuwa takribani kura milioni 4.3.
Wanawake na wasichana wabeba mzigo mkubwa wa vita duniani, ripoti ya UN yaonya
Chanzo cha picha, Reuters
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na
Usalama imebaini kuwa wanawake na wasichana wanaendelea kubeba mzigo mkubwa
wa vita na migogoro ya silaha duniani, huku idadi ya vifo vyao ikiongezeka kwa
kasi katika miaka ya hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo mjini New
York, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa, Nyaradzayi Gumbonzvanda, amesema dunia imekuwa ikiruhusu hali hiyo
kuendelea licha ya kuwa vita na migogoro vinaweza kuzuiwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya raia 37,000 waliuawa
katika migogoro ya silaha duniani mwaka 2025, ambapo mmoja kati ya kila watu
wanne waliouawa alikuwa mwanamke au msichana. Umoja wa Mataifa unasema kiwango hicho
kimeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka 2021.
Ripoti hiyo
inaeleza kuwa angalau wanawake na wasichana 25 huuawa kila siku kutokana na
migogoro ya silaha, huku zaidi ya wanawake na wasichana milioni 750 duniani
wakiishi ndani ya umbali wa kilomita 50 kutoka maeneo yenye mapigano.
Gumbonzvanda
amesema kwa wanawake wengi wanaoishi katika maeneo hayo, vita si jambo la
kutazama kwenye runinga au simu, bali ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.
"Vita
vinafuata wanawake hadi katika wodi za wazazi, mashuleni, majumbani na sehemu
ambazo familia zinapaswa kuwa salama," alisema.
Ripoti hiyo
pia imeonyesha athari kubwa kwa afya ya uzazi katika maeneo ya migogoro. Umoja
wa Mataifa unasema mwanamke anayejifungua katika nchi iliyoathiriwa na vita ana
uwezekano mara tano zaidi wa kufariki kutokana na matatizo ya uzazi kuliko
mwanamke anayejifungua katika nchi iliyo imara.
Katika
Ukanda wa Gaza, ripoti hiyo inasema uharibifu wa hospitali na vituo vya afya ya
uzazi umechangia kupungua kwa asilimia 41 kwa watoto wanaozaliwa hai na
kuongezeka kwa asilimia 300 kwa visa vya mimba kuharibika.
Kwa upande
wa elimu, wasichana katika nchi zinazokumbwa na migogoro wana uwezekano mara
mbili na nusu zaidi wa kukosa masomo kuliko wenzao katika mazingira ya kawaida.
Umoja wa Mataifa umeitaja Afghanistan kuwa miongoni mwa maeneo yenye mgogoro
mkubwa zaidi wa haki za wanawake duniani, ambapo mamilioni ya wasichana bado
hawaruhusiwi kupata elimu.
Ripoti hiyo imeeleza pia ongezeko kubwa la ukatili wa
kingono unaohusishwa na migogoro ya silaha. Mwaka 2025, Umoja wa Mataifa
ulithibitisha visa 9,788 vya ukatili wa kingono unaohusiana na vita, idadi
ambayo ni zaidi ya mara mbili ya ile ya mwaka uliotangulia.
Nchini Haiti pekee, visa vilivyoripotiwa vya ukatili wa
kingono viliongezeka kwa asilimia 163, huku wanawake na wasichana wakitajwa
kuwa miongoni mwa walengwa wakuu wa aina hiyo ya ukatili.
Licha ya changamoto hizo, Umoja wa Mataifa umesema wanawake
wanaendelea kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kujenga amani kwa kusuluhisha
migogoro ya kijamii, kusaidia manusura wa ukatili na kuunganisha jamii wakati
taasisi za serikali zinaposhindwa kufanya kazi.
Hata hivyo, ripoti hiyo imebaini kuwa wanawake bado hawapewi
nafasi ya kutosha katika maamuzi ya amani. Mwaka 2025, wanawake walikuwa
asilimia tano tu ya wajadiliano katika michakato 57 ya amani duniani.
UN Women imezitaka serikali na jumuiya ya kimataifa kuongeza
ushiriki wa wanawake katika mazungumzo ya amani, kuheshimu sheria za kimataifa
na kuchukua hatua za haraka kulinda raia dhidi ya madhara ya vita.
"Vita
ni uchaguzi wa binadamu, na amani pia ni uchaguzi wa binadamu," alisema
Gumbonzvanda. "Dunia haihitaji taarifa zaidi kuhusu mateso ya raia.
Inahitaji hatua za kuyamaliza."
Soma Pia:
Saudi yadai kudungua makombora matatu na droni nne za Houthi
Chanzo cha picha, EPA
Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen umesema
Jumanne ulidungua na kuharibu makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na
rubani zilizorushwa na waasi wa Houthi kuelekea maeneo mawili ya Saudi Arabia.
Kwa mujibu wa muungano huo, Wahouthi walirusha makombora
matatu ya balestiki kuelekea Mkoa wa Mashariki wa Saudi Arabia na ndege nne
zisizo na rubani kuelekea kusini mwa nchi hiyo.
Mamlaka ya Ulinzi wa Raia ya Saudi Arabia ilitoa tahadhari
za mapema kuhusu tishio la shambulizi katika Mkoa wa Mashariki na wilaya ya
Al-Kharj, kabla ya kutangaza baadaye kuwa hatari ilikuwa imeondoka.
Saudi Arabia imeongeza mashambulizi yake dhidi ya Wahouthi
tangu mwezi uliopita, baada ya kundi hilo kudhibiti maeneo ya kimkakati kando
ya pwani ya Bahari ya Shamu nchini Yemen na kusonga kuelekea Mlango wa Bab
el-Mandeb, njia muhimu ya usafirishaji wa kimataifa kwa wazalishaji mafuta wa
Ghuba.
Mapigano mapya kati ya pande hizo mbili yamevuruga
makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa mwaka
2022, ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yamesitisha mashambulizi kati ya
muungano unaoongozwa na Saudi Arabia unaounga mkono serikali inayotambuliwa
kimataifa ya Yemen, na Wahouthi, ambao wanadhibiti mji mkuu wa Sanaa.