Moja kwa moja, Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya 'atekwa nyara ' Kenya - Amnesty yaonya

Shirika la Amnesty International limesema Mwaipaya alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake mwendo wa saa nane mchana Jumapili alipodaiwa kuzuiwa na watu waliokuwa katika magari matatu, likiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop.

Muhtasari

Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya 'atekwa nyara ' Kenya - Amnesty yaonya

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Tetesi za soka Jumatatu: Howe yuko tayari kuzungumza na Man Utd kuhusu nafasi ya ukocha

    d

    Aliyekuwa kocha wa Newcastle United,Eddie Howe, ambaye kwa sasa hana timu ya kufundisha, anavutiwa na uwezekano wa kuzungumza na Manchester United iwapo klabu hiyo ya Old Trafford itaamua kumtimua Michael Carrick, ambaye anakabiliwa na shinikizo kutokana na Man Utd kuandikisha matokeo duni. (Sky Sports)

    Manchester United inalenga kumsajili Jarrad Branthwaite, beki wa Everton na timu ya taifa ya England mwenye umri wa miaka 24, katika juhudi za kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya ulinzi.(Football Insider)

    Sean Dyche, aliyewahi kuzinoa Watford, Burnley, Everton na Nottingham Forest, anatajwa kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi ya kuinoa Crystal Palace iwapo klabu hiyo itamfuta kazi kocha wake Pierre Sage. (Telegraph - subscription required)

    Thomas Frank, aliyewahi kuinoa Brentford, Vitor Pereira, aliyewahi kuifundisha Wolverhampton Wanderers, na Robbie Keane, aliyewahi kuinoa Ferencváros, pia wanatajwa kuwa wagombea wa nafasi hiyo. (Talksport)

    Kiungo wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Sweden, Lucas Bergvall, mwenye umri wa miaka 20, anafuatiliwa na Napoli na Barcelona. . (Tuttomercato via Teamtalk)

    Manchester United haitafuta usajili wa mshambuliaji wake wa akademia, JJ Gabriel, mwenye umri wa miaka 16. Hatua hiyo ina maana kwamba mchezaji huyo hataweza kuondoka klabuni hapo hadi Januari, huku Barcelona na Paris Saint-Germain zikijaribu kufikia makubaliano ya kumsajili. (Football Insider)

    Arsenal, Liverpool na Manchester United zinafuatilia maendeleo ya Lennart Karl, kiungo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 18. (Teamtalk)

    Beki wa Brazil, Dodo, anatarajiwa kuondoka Fiorentina mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu. AC Milan, Juventus na Barcelona zinahusishwa na uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27. (Football Italia)

    Brighton na RB Leipzig ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia Adin Licina, kiungo wa Juventus mwenye umri wa miaka 19 anayeichezea Cremonese kwa mkopo. Licina ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Ujerumani chini ya umri wa miaka 19. (Gianluca di Marzo)

    Soma pia:

  2. Netanyahu: Iran na washirika wake wanapanga kuvuruga uchaguzi Israel

    d

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema Iran na washirika wake huenda wakajaribu kufanya mashambulizi ili kuvuruga uchaguzi nchini Israel, unaotarajiwa kufanyika Jumanne.

    Katika video iliyotolewa na ofisi yake Jumapili, Netanyahu amesema Israel ina taarifa za kiintelijensia zinazoashiria uwezekano wa maadui wake kujaribu kuathiri uchaguzi huo kupitia mashambulizi.

    Amesema: “Tuna taarifa za kiintelijensia kwamba maadui wetu, yaani Iran na washirika wake, wanaweza kutujaribu kwa kufanya mashambulizi yanayolenga kuvuruga uchaguzi.”

    Netanyahu pia ameeleza kuwa jeshi la Israel limejiandaa kukabiliana na hali hiyo, kwa hatua za kujilinda na kushambulia.

    Ameonya kuwa iwapo mashambulizi hayo yatatokea, Israel itajibu kwa nguvu zaidi kuliko washambuliaji wanavyoweza kutarajia.

    Kauli hizo zinatolewa huku mvutano kati ya Israel na Iran ukiendelea kuongezeka, wakati uchaguzi wa Israel ukiratibiwa kufanyika kesho Jumanne.

  3. Kenya yatangaza huenda ikaumaliza ugonjwa wa Ebola ndani ya siku 42

    D

    Waziri wa Afya nchini Kenya, Aden Duale, amesema huenda Kenya ikatokomeza Ebola ndani ya siku 42, iwapo hakutakuwa na visa vipya vya maambukizi katika kipindi hicho.

    “Tumefanikiwa kuudhibiti ugonjwa huo, na nina uhakika kuwa Kenya itatangazwa kuwa huru dhidi ya Ebola tutakapofikisha siku 42. Huu si muda uliowekwa na Kenya, bali ni mwongozo wa kimataifa uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).”

    Kuhusu vikwazo vya safari, biashara na utalii nchini Kenya, Waziri Duale amesema, “Hakuna vikwazo vya safari, biashara wala utalii nchini Kenya. Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Afya zimejulishwa kupitia WHO. Msimamo wa WHO ni kwamba hakuna nchi inayopaswa kufunga mipaka yake au kuweka vikwazo hivyo''.

    AIdha Kenya imeeleza kuwa Balozi wa Uingereza aliyekuwa amezuru kaunti ya Mombasa aliwaambia kuwa Kenya inafanya kazi nzuri sana, na kwamba hakutakuwa na vikwazo vya safari.

    Kisa cha kwanza cha Ebola nchini Kenya kiligunduliwa tarehe 3 Oktoba 2026, baada ya mgonjwa kuingia nchini akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

    Duale amesema serikali inaendelea kuwapima watu wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa na kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

    Katika kipindi cha saa 48 zilizopita, watu 551 walipimwa virusi vya Ebola na matokeo yao yote yakawa hasi.

    Waziri huyo amesema baadhi ya watu waliowekwa karantini wanaweza kuruhusiwa kuondoka iwapo vipimo vyao vitaonyesha kuwa hawajaambukizwa. Watu 21 wanatarajiwa kufanyiwa vipimo zaidi.

    Hata hivyo, Kenya imerekodi vifo viwili vilivyohusishwa na mlipuko huo. Waathiriwa hao ni pamoja na mgonjwa wa kwanza, mwenye umri wa miaka 45, aliyeingia nchini akiwa ameambukizwa, na mwanamke mwenye umri wa miaka 65 aliyefariki tarehe 23 Oktoba.

    Wizara ya Afya imesema visa vyote vilivyothibitishwa hadi sasa vinahusiana na kundi moja la watu ambao walikuwa na mawasiliano yanayojulikana. Hadi sasa, hakuna ushahidi wa maambukizi yaliyoenea katika jamii kwa ujumla.

    Serikali imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, kudumisha usafi wa mikono na kufuata maelekezo ya maafisa wa afya.

    f
  4. Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya 'atekwa nyara ' Kenya - Amnesty yaonya

    s

    Mwanaharakati wa upinzani na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Tanzania, Twaha Mwaipaya, anaripotiwa kutekwa katika eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos, viungani mwa jiji la Nairobi, kwa mujibu wa Amnesty International Kenya.

    Shirika hilo limesema Mwaipaya alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake mwendo wa saa nane mchana Jumapili alipodaiwa kuzuiwa na watu waliokuwa katika magari matatu, likiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop.

    Amnesty imezitaka mamlaka za Kenya kuchukua hatua za haraka kubaini alipo Mwaipaya na kuhakikisha usalama wake.

    Pia limewaomba wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kujua alipo kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

    Mwaipaya ni kiongozi wa vijana katika chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

    Amekuwa akitetea mageuzi ya katiba, uwajibikaji na ulinzi wa haki za binadamu.

    Pia amekuwa akiikosoa serikali ya Tanzania kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.

    Kutoweka kwake kunakodaiwa kumezua wasiwasi miongoni mwa mashirika ya haki za binadamu na wanaharakati wa kikanda kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali wanaofanya shughuli zao katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.

    Mashirika ya haki za binadamu, yakiwemo Amnesty International Kenya na Defenders Coalition, yametaka hatua za haraka zichukuliwe kumtafuta.

    Kisa hicho pia kimeibua upya wasiwasi kuhusu kile ambacho mashirika hayo yanakitaja kuwa ukandamizaji unaovuka mipaka ya nchi dhidi ya wapinzani wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu.

    Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi au tamko lolote lililotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo la kutekwa kwa Mwaipaya.

  5. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 26/10/2026.