Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, akili mnemba inatishia ajira za wanawake?
- Author, سوزانا قسوس
- Nafasi, بي بي سي نيوز عربي
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Samar, mfanyakazi wa Idara ya utawala, amekuwa akifanya kazi za kuingiza data, kuandaa ripoti na kujibu maswali ya wateja kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, kufuatia kuanza kutumika kwa zana za akili mnemba katika mazingira yake ya kazi, alianza kujiuliza iwapo kazi anazofanya kila siku bado zitahitaji ushiriki wake, au mashine zitaweza kuzifanya kwa muda mfupi na gharama nafuu zaidi, na hivyo kumwacha akikabiliwa na mustakabali usio na uhakika wa kitaaluma.
Matumizi ya akili mnemba yanaongezeka kwa kasi, yakitengeneza fursa mpya katika kazi na uzalishaji. Hata hivyo, hali hiyo pia inazua maswali kuhusu athari zake kwa wanawake katika soko la ajira.
Wakati wasiwasi ukiongezeka kwamba teknolojia mpya zinaweza kuchukua nafasi ya baadhi ya ajira za jadi, wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingine inayotokana na uwakilishi wao mdogo katika ajira mpya za teknolojia. Hali hiyo inazua swali la iwapo ukuaji wa sekta ya akili mnemba utatengeneza fursa sawa kwa wanawake na wanaume, au utazidisha pengo lililopo kati yao.
Takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) zinaonesha kuwa asilimia 29 ya ajira katika taaluma zinazotawaliwa na wanawake ziko katika hatari ya kuathiriwa na akili mnemba zalishi, ikilinganishwa na asilimia 16 katika taaluma zinazotawaliwa na wanaume. Tofauti hiyo inaongezeka zaidi tunapoangalia makundi ya ajira yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kufanyiwa kazi na mashine, ambapo viwango ni asilimia 16 kwa wanawake dhidi ya asilimia 3 kwa wanaume.
Katika ishara nyingine ya pengo la fursa, takwimu za LinkedIn ziliripoti kuwa wanawake walikuwa asilimia 26 tu ya watu walioajiriwa katika kazi zinazohusiana na akili mnemba nchini Marekani mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 50 ya walioajiriwa katika kazi nyingine. Wakati huohuo, wanawake walishikilia asilimia 13 tu ya nafasi za juu za uongozi katika kampuni za akili mnemba katika nchi 27.
Siku chache zilizopita, gazeti la The Guardian lilichapisha makala yenye kichwa: "Akili mnemba inakua kwa kasi, wanawake wakiwekwa pembeni." Makala hiyo inaangazia pengo kati ya upanuzi wa haraka wa sekta ya akili mnemba na ushiriki wa wanawake ndani yake, katika fursa za ajira na upatikanaji wa nafasi za uongozi.
Makala hiyo inaonya kuwa wanawake wanaweza kukabiliwa na changamoto mbili kwa wakati mmoja: wengi wao wamejikita katika baadhi ya kazi za utawala na huduma ambazo ziko katika hatari kubwa ya kufanyiwa kazi na mashine, huku uwakilishi wao ukiwa mdogo katika ajira mpya za kiufundi zinazotengenezwa na sekta hiyo.
Ripoti za Shirika la Kazi Duniani zinaunga mkono wasiwasi huo, zikionesha kuwa ajira katika taaluma zinazotawaliwa na wanawake zina uwezekano mkubwa zaidi wa kuathiriwa na akili mnemba zalishi kuliko zile zinazotawaliwa na wanaume.
Katika mahojiano na BBC, Aya Jafar, mtaalamu wa uchumi wa ajira katika Shirika la Kazi Duniani, anasema kuwa kiwango cha wanawake kuathiriwa na akili mnemba kinahusiana kwa kiasi kikubwa na mgawanyo wao katika taaluma mbalimbali. Anasema idadi kubwa ya wanawake wamejikita katika kazi za utawala, ukatibu na usaidizi wa biashara, ambazo zinahusisha kazi za kawaida zinazojirudia na ambazo akili mnemba zalishi inaweza kuzifanya kwa kiwango kikubwa zaidi.
Anaongeza kuwa wanawake bado hawawakilishwi vya kutosha katika nyanja za akili mnemba, teknolojia, sayansi, uhandisi na hisabati. Hali hiyo inaweza kupunguza uwezo wao wa kunufaika na fursa mpya za ajira zinazohusiana na mabadiliko ya kidijitali.
Jafar pia alionya kuwa matumizi ya mifumo ya akili mnemba inayotegemea data yenye upendeleo au isiyokamilika yanaweza kuimarisha ukosefu wa usawa wa kijinsia uliopo, ikiwemo katika ajira, mishahara na maendeleo ya kitaaluma.
Alisema: "Sehemu kubwa ya wanawake wamejikita katika kazi za utawala, ukatibu na usaidizi wa biashara, ambazo zinahusisha kazi za kawaida zinazojirudia na ambazo akili mnemba zalishi inaweza kuzifanya kwa kiwango kikubwa zaidi."
Kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Kazi Duniani, asilimia 5.3 ya ajira zinazofanywa na wanawake katika eneo la Kiarabu ziko katika hatari kubwa ya kufanyiwa kazi na mashine kwa kutumia akili mnemba zalishi, ikilinganishwa na asilimia 1.6 ya ajira zinazofanywa na wanaume.
Hata hivyo, shirika hilo lilisisitiza kuwa takwimu hizi hazimaanishi kwamba asilimia hiyo ya wanawake watapoteza ajira zao moja kwa moja. Lilieleza kuwa uwezekano wa ajira kuathiriwa na teknolojia ya kiotomatiki haumaanishi lazima ajira hizo zitapotea. Athari halisi itategemea jinsi teknolojia hizo zitakavyoingizwa katika maeneo ya kazi, ujuzi wa wafanyakazi na mazingira ya kiuchumi na kisheria yanayozunguka matumizi yake.
Shirika hilo lilibainisha kuwa kazi za kawaida na zinazojirudia, zikiwemo kazi za ofisini, kuingiza data, mauzo na huduma kwa wateja, ni miongoni mwa ajira zinazoweza kukabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya akili mnemba.
Sekta kama huduma za umma, uzalishaji wa viwandani wa msingi na biashara ya rejareja zinaweza kushuhudia kupungua kwa baadhi ya ajira, kulingana na mifano ya namna teknolojia inavyoweza kuingizwa katika soko la ajira la eneo la Kiarabu iliyochambuliwa na mifumo ya shirika hilo.
Mwezi Mei 2026, Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kiuchumi na Kijamii kwa Asia Magharibi (ESCWA) na Shirika la Kazi Duniani zilitoa ripoti ya pamoja iliyochunguza mustakabali wa akili mnemba na soko la ajira katika eneo la Kiarabu hadi mwaka 2035.
Ripoti hiyo ilikadiria kuwa takribani robo ya ajira katika eneo hilo zinaweza kuathiriwa na akili mnemba zalishi, iwe kupitia uwezekano wa baadhi ya ajira kutoweka, kuboreshwa kwa utendaji wa wafanyakazi au kuibuka kwa ajira mpya. Pia ilionya kuwa teknolojia za kiotomatiki zinaweza kupunguza fursa za ajira za ofisini na zile zinazohusisha kazi za kawaida zinazojirudia.
Kwa upande mwingine, akili mnemba inaweza kuongeza uwezo wa wafanyakazi badala ya kuwaondoa kabisa kazini. Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani, teknolojia hiyo inaweza kuwasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, kubeba majukumu magumu zaidi na kujifunza ujuzi mpya.
Shirika hilo linakadiria kuwa asilimia 22.7 ya ajira zinazofanywa na wanawake katika eneo la Kiarabu zinaweza kunufaika na maendeleo ya aina hii.
Hata hivyo, Aya Jafar, mtaalamu wa uchumi wa ajira katika Shirika la Kazi Duniani, anaonya kuwa "kuongezeka kwa uzalishaji hakumaanishi moja kwa moja kuwa kutakuwa na ajira bora au mishahara mikubwa zaidi." Anaeleza kuwa matokeo hayo yanategemea jinsi teknolojia inavyoingizwa katika maeneo ya kazi na namna faida zinazopatikana zinavyogawanywa kwa wafanyakazi.
Shirika hilo linatoa wito wa kushughulikia vikwazo vinavyopunguza fursa za wanawake, ikiwemo ubaguzi na kutokuwepo kwa usawa katika mgawanyo wa majukumu ya malezi na kazi zisizolipwa. Pia linataka kufunguliwa kwa njia zitakazowawezesha wanawake kupata ajira zinazokua kwa kasi na zenye ubora wa juu, ikiwemo zile zinazohusiana na teknolojia na akili mnemba.
Kwa upande wake, Ibrahim Al-Jarrah, mtaalamu wa akili mnemba, anaamini kuwa wanawake wanaweza kuathiriwa zaidi na athari za teknolojia hiyo katika soko la ajira. Anasema hali hiyo haisababishwi na ukosefu wa uwezo au kutoweza kuendana na maendeleo ya kiteknolojia, bali na aina ya kazi zinazofanywa na baadhi yao.
Anazitaja kazi za utawala na ofisini, huduma kwa wateja na uchakataji wa data kuwa miongoni mwa kazi hizo, kwa kuwa zinategemea shughuli zinazojirudia ambazo teknolojia mpya zinaweza kuzifanya.
Al-Jarrah anaiambia BBC kuwa athari za akili mnemba hazitaishia katika kutoweka kwa baadhi ya ajira, bali pia zitabadilisha namna kazi nyingine zinavyofanywa, huku fursa mpya za kitaaluma zikiibuka.
Anaeleza kuwa kazi zinazotegemea kwa kiasi kikubwa shughuli zinazojirudia zinaweza kupungua uhitaji wake. Wakati huohuo, majukumu ya wafanyakazi katika ajira nyingine yanaweza kubadilika kutoka kuingiza data na kuandaa ripoti kwenda kuchambua matokeo, kuthibitisha usahihi wake na kushiriki katika kufanya maamuzi.
Anaongeza: "Hatuoni tu kazi zikifanyiwa na mashine, bali pia tunaona majukumu yakigawanywa upya kati ya binadamu na mashine."
Utafiti wa kiuchumi ulioandikwa kwa ushirikiano na mchumi Stefania Albanese ulichunguza athari za akili mnemba kwa ajira za wanawake katika nchi 16 za Ulaya kati ya mwaka 2011 na 2019.
Utafiti huo ulihitimisha kuwa wastani wa uwiano wa wanawake katika nguvu kazi uliongezeka katika taaluma zilizoathiriwa zaidi na teknolojia hizi. Hali hiyo ilionekana hasa katika nchi ambazo wanawake wana viwango vya juu vya elimu na ushiriki mkubwa katika uchumi. Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la Journal of the American Economic Association mwaka 2025.
Kwa mtazamo wa Al-Jarrah, fursa zinazotokana na akili mnemba kwa wanawake haziko katika kazi maalumu za kiteknolojia pekee, bali pia katika sekta kama elimu, afya, masoko na huduma za kifedha.
Teknolojia hiyo inaweza pia kufungua milango ya kufanya kazi kwa njia ya mtandao na kuanzisha biashara, pamoja na fursa katika uchanganuzi wa data, uundaji wa programu tumizi, usalama wa mifumo ya kidijitali na usimamizi wa mifumo mahiri.
Anasisitiza kuwa kunufaika na fursa hizo hakumaanishi kwamba wanawake wote wanapaswa kujifunza programu za kompyuta pekee. Badala yake, wanapaswa kupata uwezo wa kutumia zana zinazohitajika.
Anasema: "Ujuzi muhimu zaidi katika siku zijazo hautakuwa tu uwezo wa kutumia zana za akili mnemba, bali pia uwezo wa kuuliza swali sahihi, kutathmini jibu na kufanya uamuzi sahihi mahali pa kazi."
Hata hivyo, Al-Jarrah anaonya kuwa akili mnemba inaweza kuchangia kupanua pengo kati ya wanawake na wanaume katika fursa za ajira na mapato ikiwa wanawake wataendelea kujikita katika kazi zilizo katika hatari kubwa ya kufanyiwa na mashine, wakati upatikanaji wao wa mafunzo ya kiufundi, ajira maalumu na nafasi za uongozi ukiwa mdogo.
Anabainisha kuwa hatari haihusiani tu na mabadiliko ya aina za ajira, bali pia na uwezekano wa mifumo ya kidijitali kurithi upendeleo uliopo katika soko la ajira. Hali hii inaweza kutokea hasa pale zana za kuajiri na kutathmini utendaji wa wafanyakazi zinapotegemea data za kihistoria zinazoakisi tofauti na ukosefu wa usawa kati ya wanawake na wanaume.
Al-Jarrah anasema: "Hatari halisi si kwamba akili mnemba ina upendeleo kwa asili, bali ni kuruhusu ijifunze kutokana na ukosefu wa usawa na upendeleo uliopo katika jamii zetu, kisha kuurudia kwa kiwango kikubwa zaidi katika ajira mpya."
Katika kipindi hiki cha mabadiliko, mustakabali wa wanawake katika soko la ajira hautategemea tu kiwango ambacho akili mnemba inaweza kufanya kazi zao, bali pia uwezo wa taasisi na serikali kuweka mazingira yatakayowawezesha kuendana na mabadiliko hayo.
Ingawa teknolojia mpya zinaweza kufungua milango ya fursa tofauti za kitaaluma, zinaweza pia kupanua pengo kati ya wale wenye ujuzi wa kunufaika nazo na wale wasiopata fursa za mafunzo na maandalizi.
Katika eneo la Kiarabu, changamoto bado ni kuhakikisha kuwa "mapinduzi ya akili mnemba" hayawi sababu mpya ya kupunguza fursa za kiuchumi kwa wanawake, bali yanakuwa chombo cha kupanua ushiriki wao katika soko la ajira.