Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya 'atekwa nyara ' Kenya - Amnesty yaonya

Shirika la Amnesty International limesema Mwaipaya alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake mwendo wa saa nane mchana Jumapili alipodaiwa kuzuiwa na watu waliokuwa katika magari matatu, likiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Lula ashinda muhula wa nne wa urais Brazil

    Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, amechaguliwa kuhudumu kwa muhula wa nne baada ya kumshinda seneta Flávio Bolsonaro katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini humo.

    Baada ya asilimia 98.87 ya masanduku ya kura kuhesabiwa, Mahakama ya Uchaguzi ya Brazil (TSE) ilimtangaza Lula kuwa mshindi kwa mujibu wa hesabu za kura zilizokuwa zimepatikana. Lula alipata asilimia 51.79 ya kura, dhidi ya asilimia 48.21 alizopata Bolsonaro.

    Tofauti hiyo ya kura ilikuwa kubwa kuliko ushindi wa Lula dhidi ya baba yake Flávio, rais wa zamani Jair Bolsonaro, katika uchaguzi wa mwaka 2022.

    Matokeo hayo yalikuwa ya kushangaza, yakiwa mara ya kwanza tangu Brazil irejee katika mfumo wa demokrasia kwa mgombea aliyeshindwa katika duru ya kwanza kugeuza matokeo na hatimaye kushinda urais.

    Katika hotuba yake ya kwanza baadaya kutangazwa mshindi Lula amesema “Demokrasia iishi milele,”.

    Aidha, ameongezea kuwa, “Muhula huu wangu wa nne utakuwa bora kuliko muhula wowote wa rais katika historia ya nchi hii.”

    “Utakuwa muhula ambao nitawasikiliza zaidi wananchi wa Brazil.”

    Ushindi huo ulifuatia kampeni kubwa iliyofanywa na wafuasi wa Lula kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na maandamano yaliyovutia mamia ya maelfu ya watu katika miji mikuu ya nchi hiyo, ikiwemo Rio de Janeiro na São Paulo.

    Siku ya uchaguzi pia ilishuhudia idadi kubwa ya wapiga kura wakijitokeza. Kiwango cha kutoshiriki uchaguzi kilipungua kwa kiasi kikubwa zaidi kati ya duru ya kwanza na ya pili kuliko katika uchaguzi wowote wa urais nchini humo tangu mwaka 1989.

    Hata hivyo, uchaguzi huo haukukosa utata. Kampeni ya Lula ilidai kuwa baadhi ya wapiga kura walizuiwa kushiriki baada ya uhaba wa mabasi kufanya iwe vigumu kwao kufika katika vituo vya kupigia kura katika miji kadhaa, ikiwemo São Paulo na Salvador, kaskazini-mashariki mwa Brazil.

    Kampeni ya Flávio Bolsonaro nayo iliomba muda wa kupiga kura uongezwe kutokana na hali mbaya ya hewa kusini mwa Brazil. Hatimaye, Mahakama ya Juu iliongeza muda wa upigaji kura kwa saa mbili.

    Jair Bolsonaro kwa sasa yuko kizuizini baada ya kutiwa hatiani mwezi Septemba 2025 kwa kujaribu kufanya mapinduzi ya serikali kufuatia kushindwa na Lula katika uchaguzi wa mwaka 2022.

    Kwa ushindi huo, Lula anakuwa rais wa kwanza katika historia ya Brazil kuchaguliwa kuhudumu kwa muhula wa nne. Ataendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2030.

    Flávio Bolsonaro alikuwa mgombea ambaye Rais wa Marekani Donald Trump alimpigia upatu kuwa rais wa Brazil.

    Soma pia:

  2. Kiongozi wa upinzani Venezuela Maria Corina Machado arejea nchini baada ya miezi kadhaa uhamishoni

    Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, Maria Corina Machado, amerejea nchini humo baada ya kukaa nje ya nchi kwa zaidi ya miezi 10, wakati hali ya kisiasa ikiendelea kuwa na mvutano.

    “Nimerudi hapa, niko pamoja nanyi,” aliandika Machado kwenye mtandao wa kijamii wa X siku ya Jumapili.

    Edmundo Gonzalez Urrutia, aliyewahi kugombea urais nchini Venezuela na ambaye ni mshirika wa Machado, pia alithibitisha taarifa hizo dakika chache baadaye.

    “Nina furaha kuwajulisha kwamba kiongozi wetu, mpendwa wangu Maria Corina, yuko nchini Venezuela,” aliandika.

    Aliongeza kuwa hivi karibuni atajiunga na Machado nchini humo ili kuongoza juhudi za kuifikisha nchi hiyo kwenye “uhuru”.

    Mmoja wa washauri wa Machado alisema mwezi Septemba kuwa alikuwa amejaribu kurejea Venezuela mara saba katika wiki chache zilizotangulia, lakini alizuiwa kuingia nchini kila mara.

    Bado haijafahamika Machado anapanga kufanya nini baada ya kurejea. Hata hivyo, amewahi kusema kuwa atawania tena urais iwapo uchaguzi utafanyika.

    Katika taarifa iliyotolewa kwa Margaret Brennan wa CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, msemaji wa Machado alielezea kurejea kwake kuwa “hatua muhimu kuelekea mpito wa kidemokrasia na kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na unaoweza kuthibitishwa katika siku za usoni”.

    Soma Pia:

  3. KWS yamuua tembo aliyehusishwa na kifo cha mtu nchini Kenya

    Maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori nchini Kenya (KWS) wamempiga risasi na kumuua tembo anayehusishwa na kifo cha mtu mmoja katika eneo la Kamaindi, wadi ya Tharaka, kaunti ya Kitui.

    Tembo huyo aliuawa saa chache baada ya tukio hilo la mauaji, kufuatia malalamiko ya wakazi waliokuwa na wasiwasi kuhusu kuendelea kwake kuzurura katika eneo hilo.

    Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa, tembo huyo alikuwa akizunguka eneo hilo kwa wiki kadhaa na kujificha katika shamba la mkazi mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Mkulima.

    Kifo hicho kilisababisha maafisa wa KWS kuingilia kati, na hatimaye kumuua tembo huyo huku hofu kuhusu usalama wa wakazi ikiendelea kuongezeka.

    Mzoga wa tembo huyo unatarajiwa kuchomwa moto kama sehemu ya utaratibu wa kuutupa.

    Tukio hilo limezua tena wasiwasi kuhusu migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika eneo hilo, ambako kukutana kwa wakazi na tembo kunahatarisha maisha na shughuli zao za kujipatia riziki.

  4. Tetesi za soka Jumatatu: Howe yuko tayari kuzungumza na Man Utd kuhusu nafasi ya ukocha

    Aliyekuwa kocha wa Newcastle United,Eddie Howe, ambaye kwa sasa hana timu ya kufundisha, anavutiwa na uwezekano wa kuzungumza na Manchester United iwapo klabu hiyo ya Old Trafford itaamua kumtimua Michael Carrick, ambaye anakabiliwa na shinikizo kutokana na Man Utd kuandikisha matokeo duni. (Sky Sports)

    Manchester United inalenga kumsajili Jarrad Branthwaite, beki wa Everton na timu ya taifa ya England mwenye umri wa miaka 24, katika juhudi za kufanya mabadiliko makubwa katika safu yake ya ulinzi.(Football Insider)

    Sean Dyche, aliyewahi kuzinoa Watford, Burnley, Everton na Nottingham Forest, anatajwa kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi ya kuinoa Crystal Palace iwapo klabu hiyo itamfuta kazi kocha wake Pierre Sage. (Telegraph - subscription required)

    Thomas Frank, aliyewahi kuinoa Brentford, Vitor Pereira, aliyewahi kuifundisha Wolverhampton Wanderers, na Robbie Keane, aliyewahi kuinoa Ferencváros, pia wanatajwa kuwa wagombea wa nafasi hiyo. (Talksport)

    Kiungo wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Sweden, Lucas Bergvall, mwenye umri wa miaka 20, anafuatiliwa na Napoli na Barcelona. . (Tuttomercato via Teamtalk)

    Manchester United haitafuta usajili wa mshambuliaji wake wa akademia, JJ Gabriel, mwenye umri wa miaka 16. Hatua hiyo ina maana kwamba mchezaji huyo hataweza kuondoka klabuni hapo hadi Januari, huku Barcelona na Paris Saint-Germain zikijaribu kufikia makubaliano ya kumsajili. (Football Insider)

    Arsenal, Liverpool na Manchester United zinafuatilia maendeleo ya Lennart Karl, kiungo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 18. (Teamtalk)

    Beki wa Brazil, Dodo, anatarajiwa kuondoka Fiorentina mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu. AC Milan, Juventus na Barcelona zinahusishwa na uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27. (Football Italia)

    Brighton na RB Leipzig ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia Adin Licina, kiungo wa Juventus mwenye umri wa miaka 19 anayeichezea Cremonese kwa mkopo. Licina ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Ujerumani chini ya umri wa miaka 19. (Gianluca di Marzo)

    Soma pia:

  5. Netanyahu: Iran na washirika wake wanapanga kuvuruga uchaguzi Israel

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema Iran na washirika wake huenda wakajaribu kufanya mashambulizi ili kuvuruga uchaguzi nchini Israel, unaotarajiwa kufanyika Jumanne.

    Katika video iliyotolewa na ofisi yake Jumapili, Netanyahu amesema Israel ina taarifa za kiintelijensia zinazoashiria uwezekano wa maadui wake kujaribu kuathiri uchaguzi huo kupitia mashambulizi.

    Amesema: “Tuna taarifa za kiintelijensia kwamba maadui wetu, yaani Iran na washirika wake, wanaweza kutujaribu kwa kufanya mashambulizi yanayolenga kuvuruga uchaguzi.”

    Netanyahu pia ameeleza kuwa jeshi la Israel limejiandaa kukabiliana na hali hiyo, kwa hatua za kujilinda na kushambulia.

    Ameonya kuwa iwapo mashambulizi hayo yatatokea, Israel itajibu kwa nguvu zaidi kuliko washambuliaji wanavyoweza kutarajia.

    Kauli hizo zinatolewa huku mvutano kati ya Israel na Iran ukiendelea kuongezeka, wakati uchaguzi wa Israel ukiratibiwa kufanyika kesho Jumanne.

  6. Kenya yatangaza huenda ikaumaliza ugonjwa wa Ebola ndani ya siku 42

    Waziri wa Afya nchini Kenya, Aden Duale, amesema huenda Kenya ikatokomeza Ebola ndani ya siku 42, iwapo hakutakuwa na visa vipya vya maambukizi katika kipindi hicho.

    “Tumefanikiwa kuudhibiti ugonjwa huo, na nina uhakika kuwa Kenya itatangazwa kuwa huru dhidi ya Ebola tutakapofikisha siku 42. Huu si muda uliowekwa na Kenya, bali ni mwongozo wa kimataifa uliowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).”

    Kuhusu vikwazo vya safari, biashara na utalii nchini Kenya, Waziri Duale amesema, “Hakuna vikwazo vya safari, biashara wala utalii nchini Kenya. Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Afya zimejulishwa kupitia WHO. Msimamo wa WHO ni kwamba hakuna nchi inayopaswa kufunga mipaka yake au kuweka vikwazo hivyo''.

    AIdha Kenya imeeleza kuwa Balozi wa Uingereza aliyekuwa amezuru kaunti ya Mombasa aliwaambia kuwa Kenya inafanya kazi nzuri sana, na kwamba hakutakuwa na vikwazo vya safari.

    Kisa cha kwanza cha Ebola nchini Kenya kiligunduliwa tarehe 3 Oktoba 2026, baada ya mgonjwa kuingia nchini akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

    Duale amesema serikali inaendelea kuwapima watu wanaoshukiwa kuwa wameambukizwa na kufuatilia watu waliokutana na wagonjwa ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

    Katika kipindi cha saa 48 zilizopita, watu 551 walipimwa virusi vya Ebola na matokeo yao yote yakawa hasi.

    Waziri huyo amesema baadhi ya watu waliowekwa karantini wanaweza kuruhusiwa kuondoka iwapo vipimo vyao vitaonyesha kuwa hawajaambukizwa. Watu 21 wanatarajiwa kufanyiwa vipimo zaidi.

    Hata hivyo, Kenya imerekodi vifo viwili vilivyohusishwa na mlipuko huo. Waathiriwa hao ni pamoja na mgonjwa wa kwanza, mwenye umri wa miaka 45, aliyeingia nchini akiwa ameambukizwa, na mwanamke mwenye umri wa miaka 65 aliyefariki tarehe 23 Oktoba.

    Wizara ya Afya imesema visa vyote vilivyothibitishwa hadi sasa vinahusiana na kundi moja la watu ambao walikuwa na mawasiliano yanayojulikana. Hadi sasa, hakuna ushahidi wa maambukizi yaliyoenea katika jamii kwa ujumla.

    Serikali imewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, kudumisha usafi wa mikono na kufuata maelekezo ya maafisa wa afya.

  7. Mwanaharakati wa Tanzania Twaha Mwaipaya 'atekwa nyara ' Kenya - Amnesty yaonya

    Mwanaharakati wa upinzani na mtetezi wa haki za binadamu kutoka Tanzania, Twaha Mwaipaya, anaripotiwa kutekwa katika eneo la Kamulu, Kaunti ya Machakos, viungani mwa jiji la Nairobi, kwa mujibu wa Amnesty International Kenya.

    Shirika hilo limesema Mwaipaya alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake mwendo wa saa nane mchana Jumapili alipodaiwa kuzuiwa na watu waliokuwa katika magari matatu, likiwemo Toyota Land Cruiser Hardtop.

    Amnesty imezitaka mamlaka za Kenya kuchukua hatua za haraka kubaini alipo Mwaipaya na kuhakikisha usalama wake.

    Pia limewaomba wananchi wenye taarifa zozote zinazoweza kusaidia kujua alipo kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

    Mwaipaya ni kiongozi wa vijana katika chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

    Amekuwa akitetea mageuzi ya katiba, uwajibikaji na ulinzi wa haki za binadamu.

    Pia amekuwa akiikosoa serikali ya Tanzania kuhusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu.

    Kutoweka kwake kunakodaiwa kumezua wasiwasi miongoni mwa mashirika ya haki za binadamu na wanaharakati wa kikanda kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali wanaofanya shughuli zao katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.

    Mashirika ya haki za binadamu, yakiwemo Amnesty International Kenya na Defenders Coalition, yametaka hatua za haraka zichukuliwe kumtafuta.

    Kisa hicho pia kimeibua upya wasiwasi kuhusu kile ambacho mashirika hayo yanakitaja kuwa ukandamizaji unaovuka mipaka ya nchi dhidi ya wapinzani wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu.

    Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi au tamko lolote lililotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo la kutekwa kwa Mwaipaya.

  8. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 26/10/2026.