Unyanyasaji wa kingono kwa wanawake katika jeshi la Ukraine na propaganda za Urusi

Keti Leshkasheli

Chanzo cha picha, Keti Leshkasheli

Maelezo ya picha,
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Keti Leshkasheli, mhudumu wa afya kutoka Georgia aliyewahi kuhudumu katika jeshi la Ukraine, aliporejea kutoka mstari wa mbele takribani miaka mitatu iliyopita, simu yake haikuacha kuita.

Marafiki na ndugu walitaka kujua kama alikuwa salama. Walikuwa wameona machapisho kwenye Telegram yakidai kwamba alikuwa ametekwa na kubakwa.

"Nilijua kwamba video ilikuwa imeonekana ikidai kwamba baadhi ya wasichana na mimi tulikuwa tumetekwa. Kulikuwa na kitufe kilichoelekeza kwenye chaneli ya Telegram iliyokuwa ikionesha 'tunaadhibiwa'," aliiambia BBC.

Alijitambua kwenye picha hiyo. Ilikuwa picha yake mwenyewe, iliyopigwa miaka kadhaa iliyopita akiwa amevaa sare ya kijeshi huko Avdiivka, jiji lililoko mashariki mwa Ukraine ambalo sasa linakaliwa na Urusi.

"Waliandika kila aina ya mambo ya kutisha kunihusu," alisema. "Inanikasirisha. Siwezi kufanya chochote kuhusu hilo."

Chapisho hilo lilikuwa sehemu ya mtandao mpana wa matangazo ya udanganyifu kwenye Telegram. Matangazo hayo yalitumia madai ya kutungwa kwamba wanawake wa Ukraine walikuwa wamebakwa, pamoja na ahadi za kuonesha ushahidi wa video, ili kuwavutia watumiaji kujiunga na chaneli zinazounga mkono Urusi.

BBC World Service iligundua picha za zaidi ya wanawake 20, ambao wengi wao wanahudumu au waliwahi kuhudumu katika jeshi la Ukraine, zikitumiwa kama vishawishi vya kubofya (clickbait) katika kampeni hiyo. Tulizungumza na saba kati ya wanawake hao.

Kanuni

Keti Leshkasheli

Chanzo cha picha, Keti Leshkasheli

Maelezo ya picha,

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022, maelfu ya machapisho katika makundi au chaneli za Telegram yamekuwa yakiahidi kuonesha picha za video za wafungwa wa kike wa kivita kutoka Ukraine wakibakwa na kuuawa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Telegram ni programu ya kutuma ujumbe ambapo watumiaji hujiunga na chaneli au makundi makubwa ili kushiriki na kujadili maudhui. Machapisho katika maeneo haya mara nyingi huwa na matangazo yanayounganisha watumiaji na chaneli nyingine, makundi binafsi au tovuti za nje.

Ni jukwaa linalofaa sana kujenga hadhira, kwa kuwa ni programu maarufu zaidi ya kutuma ujumbe nchini Urusi. Vivyo hivyo, kwa Waukraine, mwaka 2025 Telegram ilikuwa chanzo kikuu cha habari, kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanyika kitaifa.

Kwa kutafuta katika zana za uchanganuzi maneno na majina bandia yaliyokuwa yakijirudia katika machapisho hayo ya Telegram, BBC World Service iligundua zaidi ya matangazo 6,500 yaliyohusisha madai ya unyanyasaji wa kingono.

Matangazo hayo yalichapishwa na takribani chaneli ndogo 1,700 zilizokuwa na mada mbalimbali, kuanzia maudhui ya "18+" hadi chaneli zinazohusu vita, fedha na vichekesho.

Kwa pamoja, machapisho hayo yalitazamwa na zaidi ya watu milioni 65. Mengi yalifuata mfumo uleule: yalitumia picha halisi za wanawake halisi, kisha kudai kwamba wanawake hao walikuwa wametekwa na kubakwa, na kuweka kitufe kilichoahidi kuonesha ushahidi wa video.

Ilikuwa mbinu iliyokusudiwa kwa makusudi kushtua watu, ikiwa na lengo la kuvutia hadhira kwa kuahidi kuwaonesha video za matukio ya kutisha.

Machapisho hayo pia yalidai kwamba wanawake hao waliwatesa wanajeshi wa Urusi au kwamba "walitoa wito wa watoto wa Urusi kuchomwa wakiwa hai." Madai hayo yaliambatana na lugha ya matusi na chuki inayolenga makundi ya kikabila na kijinsia.

Hata hivyo, mtumiaji alipobofya, maudhui yaliyoahidiwa hayakuwepo. Badala yake, vilimpeleka kwenye chaneli binafsi za Telegram zilizokuwa zimejaa maudhui yanayounga mkono vita.

Machapisho hayo yalisambaa pia nje ya Telegram. Video kwenye TikTok na YouTube, pamoja na machapisho kwenye mtandao wa kijamii wa Urusi unaoitwa VKontakte, yalikuwa yakiahidi maudhui hayo hayo huku yakitangaza chaneli hizo hizo binafsi za Telegram.

Valentyna Shapovalova, mtafiti anayechunguza upotoshaji wa habari unaolenga jinsia, anasema kampeni hiyo "inauza ahadi ya vurugu za kingono kama burudani" ili "kunyakua na kutengeneza fedha kutokana na" umakini wa watumiaji.

Anaongeza kwamba hata kama machapisho hayo hayajatengenezwa moja kwa moja na serikali, bado yanatumikia malengo ya Kremlin katika vita hivyo, kwa sababu yanawadhalilisha Waukraine na "kufanya vurugu za kingono dhidi ya 'adui' zionekane kuwa jambo la kawaida."

Badili jina, Futa , uza matangazo

BBC ilichambua chaneli tatu kubwa zaidi. Zote ziliundwa ndani ya muda wa saa 72 kutoka moja hadi nyingine, mwanzoni mwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.

Pryamoy Efir Novosti, chaneli ambayo iliunganishwa na zaidi ya machapisho 1,000 kati ya yale yaliyochambuliwa na BBC, sasa ina karibu wafuasi milioni 4, idadi kubwa kuliko watoa maoni wengi mashuhuri wanaounga mkono Kremlin na vyombo vingi vya habari vinavyomilikiwa na serikali.

Chaneli hiyo hujifanya kuwa chaneli ya habari, lakini awali iliitwa "MVD 18+", jina lililorejelea maudhui ya watu wazima. Sehemu kubwa ya historia yake ya machapisho, hasa kipindi ambacho kampeni ya kuvutia hadhira ilikuwa imefikia kilele, haipo tena.

Kwa sasa, inaonekana kama chaneli nyingine yoyote ya Telegram inayokusanya habari zinazounga mkono Kremlin. Huchapisha machapisho mara kadhaa kwa siku, hutumia vyombo vya habari vya serikali ya Urusi kama vyanzo, na huuza nafasi za matangazo kwa Alfa-Bank, mojawapo ya benki kubwa binafsi nchini Urusi ambayo imewekewa vikwazo na Uingereza, Umoja wa Ulaya na Marekani. Benki hiyo haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni.

Chaneli zote tatu hutumia maudhui kutoka vyombo vya habari vya serikali ya Urusi. Huelezea mafanikio ya kijeshi kama "ukombozi," huonesha Umoja wa Ulaya na Uingereza kama wachokozi, na kusherehekea vifo vya wanajeshi na raia wa Ukraine. Chaneli mbili kati yao hutumia mara kwa mara matusi ya kikabila dhidi ya Waukraine.

Ili kubaini kiasi cha fedha ambacho chaneli hizi zinapata kutokana na maudhui yanayounga mkono vita, BBC iliwasiliana nazo ikijifanya kuwa mtangazaji anayevutiwa kununua nafasi ya matangazo. Pryamoy Efir Novosti iliwaambia kuwa wanatoza kiwango cha chini cha rubles 500,000 (£5,000) kwa tangazo moja. Chaneli nyingine mbili, ambazo zina maudhui ya matusi na vurugu, zilisema zinatoza takribani rubles 40,000 (£400) kwa kila tangazo.

Pryamoy Efir haikujibu maswali yoyote ya BBC. Katika ujumbe mmoja, chaneli hiyo iliita BBC "chochezi na mpotoshaji wa habari" na kusema kwamba taarifa hizo "haziendani na uhalisia."

Kati ya zaidi ya machapisho 6,500 ya clickbait ambayo BBC imeyabaini, karibu 5,400 yamefutwa tangu wakati huo. Hata hivyo, machapisho mapya yanaendelea kujitokeza. Baadhi ya machapisho yana dalili za kutengenezwa kiotomatiki: maandishi yanayofanana kabisa, yakiwemo makosa yaleyale ya tahajia, yakichapishwa kwenye akaunti nyingi kwa wakati mmoja.

"Niliripoti akaunti hizi na kuzizuia, lakini ni nyingi sana," alisema Yuliia Mala. "Idadi ya taarifa hizi za uongo inaendelea tu kuongezeka."

m

Chanzo cha picha, Lesia Palahniuk

Maelezo ya picha,

Malalamiko rasmi yaliyowasilishwa na wanawake ambao picha zao zilitumiwa katika machapisho yanayohusisha vurugu yamekuwa, kwa kiasi kikubwa, hayajasaidia.

Keti alisema aliwasilisha malalamiko kwa Telegram mara kadhaa.

"Karibu haiwezekani kufanya chochote," alisema. "Ninataka watu wajue kwamba aina hii ya ulaghai ipo na wasidanganywe na propaganda hizo."

Oleksandra, raia wa Urusi aliyejitolea kupigana upande wa Ukraine, alisema aliona machapisho yaliyotumia picha zake mwaka 2022, 2023 na 2024 katika chaneli nyingi sana kiasi kwamba hatimaye aliacha kuzifuatilia.

"Niliona kwamba walitumia picha zangu na kuhariri uso wangu kwa Photoshop na kuuweka kwenye mwili wa uchi... Kulikuwa na picha nyingi sana kiasi kwamba wakati fulani niliacha kuitikia," alisema.

Telegram haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni. Tangu Februari 2026, mdhibiti wa vyombo vya habari wa Urusi ameweka vikwazo kwa Telegram nchini humo, akiishutumu kwa kushindwa kuzingatia sheria za Urusi. Hata hivyo, hatua hiyo haijapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya programu hiyo, kwa kuwa Warusi wanatumia VPN kufikia jukwaa hilo.

Lesia Palahniuk, diwani wa eneo kutoka Chernivtsi ambaye picha yake ilitumiwa katika machapisho yaliyokuwa na lugha chafu, alisema kwamba kuoneshwa kwa namna hiyo huwaacha wanawake wakibeba aibu ambayo si yao.

"Kwa mwanamke, kuona picha kama hizo ni jambo gumu sana," alisema. "Wanawake wanahitaji kujua kwamba hawako peke yao, kwamba wana msaada. Hawakufanya chochote kibaya."