Vijana wanavyotumia dawa "kukwepa uhalisia"

Chanzo cha picha, Getty Images
Akiwa na umri wa miaka 14, Xiaomei, mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa kutoka mkoa wa pwani nchini China, alianza kutumia dawa ya kikohozi kupita kiasi baada ya kushawishiwa na mvulana aliyekuwa mkubwa kumliko kwa umri. Ingawa dawa hiyo ilihitaji agizo la daktari, aliinunua mtandaoni kwa urahisi.
Mwanzoni, dawa hiyo ilimfanya ahisi kizunguzungu kidogo, lakini baadaye alimvutia zaidi kwa sababu ilimpa hisia ya kufa ganzi na kumsaidia kusahau kwa muda shinikizo la masomo na mitihani. Katika dozi kubwa, dawa hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa kama kuona vitu visivyokuwepo, kuchanganyikiwa na kupoteza uratibu wa mwili.
Baada ya muda, Xiaomei alianza kujaribu dawa nyingine alizoelekezwa katika vikundi vya mtandaoni. Baadhi zilikuwa za maumivu na nyingine za kifafa. Wakati mwingine alimeza vidonge vitano, na nyakati nyingine zaidi ya kumi ili kupata athari tofauti. Kwa miaka miwili, alitumia dawa nyingi bila hata moja kuandikiwa na daktari.
"Nilipokuwa chini ya shinikizo kubwa la masomo, nikifanya vibaya kwenye mitihani au nikigombana na wazazi wangu, nilitumia dawa hizi. Nilikuwa nikijaribu kukwepa uhalisia," aliiambia BBC.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wimbi la siri la "ulevi wa dawa"
BBC ilizungumza na vijana kadhaa wa Kichina katika mitandao ya kijamii ambao walieleza sababu zinazofanana za kutumia dawa. Wengi walikuwa wakijaribu kutoroka shinikizo la maisha kupitia kile wanachokiita "ulevi wa dawa".
Msichana mmoja alituma ujumbe wa sauti baada ya kutumia dozi kubwa ya dawa ya maumivu ya neva. Aliongea kwa shida na kusema: "Nahisi kama mwili wangu si wangu tena. Nahisi kizunguzungu kikali." Wenzake walimshauri tu alale wakiamini angeamka akiwa sawa siku iliyofuata.
Kijana mmoja alikiri kutumia agizo la zamani la baba yake kughushi agizo jipya la dawa. Wengine walibadilishana ushauri kuhusu dawa zinazoweza kusababisha hali ya kuona au kuhisi vitu visivyokuwepo. Baadhi yao hata walifundishana maneno ya kutafuta dawa hizo mtandaoni ili kuepuka kugunduliwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Dawa zinazopatikana kwa mibofyo michache
Ni vigumu kufahamu ukubwa halisi wa tatizo hili kwa sababu takwimu rasmi ni chache. Hata hivyo, serikali ya China imeanza kuchukua hatua kwa kuweka udhibiti mkali kwa baadhi ya dawa ambazo vijana wamekuwa wakizitumia vibaya.
Licha ya hatua hizo, BBC ilipata ofa ya kununua baadhi ya dawa hizo mtandaoni kwa bei nafuu. Ripoti ya mwaka 2025 ya Taasisi ya Kuzuia Uhalifu ya Wizara ya Sheria ilibainisha kuwa vijana hupata mbinu mbadala kwa haraka mara tu dawa fulani zinapowekewa vikwazo.
China ikiwa ni mmoja wa wazalishaji wakubwa duniani wa viambato vya dawa, upatikanaji wa dawa hizo ni rahisi zaidi. Xiaomei anasema alinunua dawa kwa mibofyo michache tu na zikafikishwa moja kwa moja nyumbani kwake.
"Ulihitaji tu kuandika namba yako ya utambulisho. Mfumo ulionyesha umri wangu, lakini bado waliuza dawa hizo bila kuuliza swali lolote," anasema.
Aidha, dawa hizo zilikuwa za bei nafuu. Mara nyingi vidonge 50 viligharimu chini ya dola moja.

Chanzo cha picha, Getty Images
Shinikizo la kufaulu kwa gharama yoyote
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, China imepunguza matumizi ya dawa haramu, lakini matumizi mabaya ya dawa zinazohitaji agizo la daktari yanaongezeka, hasa miongoni mwa vijana.
Xiaomei anasema wanafunzi wengi katika darasa lao la wanafunzi wenye uwezo mkubwa walizungumzia matumizi ya dawa kama njia ya kukwepa hisia za kushindwa.
"Ni vigumu sana kubaki katika madarasa ya wanafunzi bora. Mfumo wetu huondoa wanafunzi wanaoshuka kimasomo. Ukifeli, unajihisi kama umefeli maishani kabisa," anasema.
Kwa mujibu wa Xiang Biao, mtaalamu wa sosholojia kutoka China, sehemu ya shinikizo hilo hutokana na matarajio makubwa ya wazazi, hasa katika familia zilizokuwa na mtoto mmoja pekee.
"Kinachowatofautisha vijana wa China ni mazingira yao ya kutengwa. Hutumia saa nyingi shuleni na wana nafasi chache za kujenga mahusiano ya kijamii," anasema.
Wakati dawa zinapoanza kuharibu akili
Kadiri mtihani muhimu wa kujiunga na shule ya upili ulivyokuwa ukikaribia, Xiaomei alijaribu dawa nyingine akitumaini kupunguza wasiwasi wake.
Badala yake, kumbukumbu zake zilianza kudhoofika.
"Sikuweza kukumbuka mambo kwa uwazi. Nilihisi kama ninaishi katika hali ya kuchanganyikiwa," anasema.
Alipoeleza madhara hayo katika kundi la mtandaoni, vijana wengine walimpendekezea dawa nyingine ya maumivu. Mwanzoni ilionekana kumsaidia, lakini baada ya muda alihitaji kuongeza dozi ili kupata athari zilezile.
Miezi michache kabla ya mtihani wake muhimu, alimeza vidonge 50 kwa wakati mmoja.
"Niliogopa sana. Nilihisi kitu kibaya kingeweza kutokea. Mwishowe nililazimika kuwaambia wazazi wangu."

Chanzo cha picha, Getty Images
Huruma ya wazazi iliyobadili kila kitu
Wazazi wake waliposikia kilichotokea, hawakumkemea wala kumhukumu.
"Waliniambia jinsi walivyohuzunika kuniona katika hali ile. Hawakunilaumu. Walinionyesha huruma," anasema.
Mwitikio huo ulimsaidia sana na kuwa mwanzo wa kupona kwake.
Kwa mujibu wa Biao, watoto wengi hawahitaji tu usimamizi bali pia kusikilizwa.
"Watoto wengi wanataka kuulizwa wanahisije. Wana upweke? Wana msongo wa mawazo? Mara nyingi wazazi hupuuzia hisia hizo na kuwaambia wawe wakakamavu."

Chanzo cha picha, Getty Images
Tatizo kubwa zaidi kuliko udhibiti wa dawa
Wataalamu wengi wanaamini kuwa tatizo hili haliwezi kutatuliwa kwa kudhibiti mauzo ya dawa pekee. Wanasisitiza kuwa ni sehemu ya changamoto kubwa ya afya ya akili miongoni mwa vijana nchini China.
Utafiti wa mwaka 2023 ulionyesha kuwa karibu watu milioni 95 nchini humo walikuwa na matatizo ya msongo wa mawazo, huku zaidi ya asilimia 30 wakiwa chini ya miaka 18.
Kutokana na hali hiyo, serikali imeanzisha vituo vya ushauri nasaha shuleni, kuimarisha huduma za afya ya akili hospitalini na kuongeza idadi ya wataalamu wa afya ya akili. Hata hivyo, bado kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wanaobobea katika afya ya akili ya watoto na vijana.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mustakabali usio na uhakikakwa vijana
China ya wazazi wa Xiaomei ilikuwa na ahadi kwamba kufanya kazi kwa bidii kungeleta mafanikio. Leo, hata vijana wenye alama nzuri na shahada za vyuo vikuu hawana uhakika wa ajira au maisha bora ya baadaye.
Baada ya janga la Covid-19, changamoto za kiuchumi zimeongeza hali ya kutokuwa na uhakika, jambo ambalo limeongeza msongo kwa vijana na wazazi wao.
"Kwa ujumla, watu wamekuwa na mtazamo hasi zaidi," anasema Biao.
Kutoka uraibuni hadi kuwasaidia wengine
Kwa bahati nzuri, Xiaomei alipata msaada kutoka kwa familia yake.
"Hapo awali nilihisi kama sikuwa na msaada wowote. Lakini baada ya tukio lile, wazazi wangu walianza kunisikiliza na kuzungumza nami."
Anasema kujua kwamba hakuwa peke yake kulimsaidia kurejea katika hali nzuri na hata kufanya vizuri katika mtihani aliokuwa akiuhofia.
Si kila mtu hupata msaada huo. Ndiyo sababu Lu Jingchan, mwenye umri wa miaka 22, ameamua kuwasaidia wengine.
Aliwahi kulazwa hospitalini mara nne baada ya kutumia dawa kupita kiasi na sasa hutumia mitandao ya kijamii kuwaonya vijana kuhusu hatari hizo.
"Natumaini vijana wataweza kukabiliana na maisha bila kutegemea dawa kuficha hisia zao. Ninaamini maisha yao yanaweza kuboreka na kila mtu anaweza kupata furaha," anasema.
Majina yamebadilishwa ili kulinda utambulisho wa vijana hao.















