Tetesi za Soka Ulaya Alhamisi: Chelsea na Arsenal zapigana vikumbo kwa Eli Junior Kroupi

Chanzo cha picha, Getty Images
Chelsea imewasiliana na kiungo wa kimataifa wa Uholanzi Georginio Wijnaldum, mwenye umri wa miaka 35, kuhusu uwezekano wa kujiunga na klabu hiyo kwa uhamisho wa bure. Nyota huyo wa zamani wa Liverpool aliachana na klabu ya Saudi Pro League, Al-Ettifaq, mapema msimu huu wa joto. (Foot Mercato - kwa Kifaransa)
Arsenal itazingatia kumsajili mshambuliaji wa Kifaransa mwenye umri wa miaka 20 wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi, katika dirisha la usajili la Januari. (Independent)
Kocha msaidizi wa Arsenal, Gabriel Heinze, alimtafuta mshambuliaji wa Inter Milan na timu ya taifa ya Argentina, Lautaro Martinez, mwenye umri wa miaka 29, kuhusu uwezekano wa kuhamia Emirates kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Hata hivyo, klabu hiyo ya Italia ilikataa kujadili uhamisho huo. (Mail - usajili unahitajika)

Chanzo cha picha, Getty Images
Newcastle United na Aston Villa zinatarajiwa kuendelea na harakati za kumsajili mshambuliaji wa Cameroon wa Bayer Leverkusen, Christian Kofane, mwenye umri wa miaka 20, mara tu dirisha la usajili litakapofunguliwa tena. (Football Insider)
Manchester United iliamua kutomsajili beki wa kushoto katika siku za mwisho za dirisha la usajili baada ya kushindwa kumpata mchezaji ambaye angeimarisha kikosi chao. (Express)
Everton ilikataa ofa ya pauni milioni 65 kutoka Chelsea kwa ajili ya kiungo wa England, James Garner, aliye na umri wa miaka 25, kwa sababu iliwasilishwa kuchelewa katika dirisha la usajili. (Talksport)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil na klabu ya Tottenham, Richarlison, mwenye umri wa miaka 29, amekubali kujiunga na klabu ya Uturuki Trabzonspor, huku mshahara wake uliopendekezwa ukiwa mara tatu ya ule anaoupata kwa sasa Spurs. (Fabrizio Romano)
Mshambuliaji wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Ufaransa, Anthony Martial, 30, kwa sasa hana klabu na anatafuta njia ya kurejea kwenye Ligi Kuu ya England. (Teamtalk)
Everton haina mpango wa kuingia katika soko la wachezaji wasio na klabu licha ya kumaliza dirisha la usajili katika hali ngumu. (Telegraph)
Chelsea itakabiliwa na ushindani kutoka Liverpool katika mbio za kumsajili kiungo wa Senegal wa Monaco, Lamine Camara, mwenye umri wa miaka 22, iwapo itafufua nia yake ya kumsajili baada ya uhamisho wake wa siku ya mwisho ya dirisha la usajili kwenda Stamford Bridge kuvunjika. (Talksport)
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












