Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Baleba mwenye thamani ya £70m yuko tayari kwa mtihani wake Man Utd?
- Author, Simon Stone
- Nafasi, Manchester United reporter
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Carlos Baleba ametoka mbali tangu siku aliyolazimika kujiondoa kwenye mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Cameroon kwa sababu ya mtihani wa shule.
Sasa, mitihani ya Baleba imejikita zaidi uwanjani na mtihani mkubwa unamsubiri Old Trafford wikendi hii.
Si haki kumtazama mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 22 kama mtu anayeweza kuokoa msimu wa Manchester United.
Hata hivyo, kwa ada ya pauni milioni 70, Baleba ndiye mchezaji ghali zaidi kati ya wachezaji watatu muhimu waliosajiliwa na United katika dirisha la usajili uliopita.
Pia yeye ndiye mchezaji anayelengwa kuziba pengo katika nafasi ya kiungo mkabaji, nafasi ambayo imekuwa changamoto kuijaza ipasavyo tangu kuondoka kwa Casemiro mwezi Mei.
United walijua kuwa Baleba alikuwa na jeraha la kifundo cha mguu walipomsajili kutoka Brighton mnamo tarehe 25 Agosti, na huenda wakalazimika kusubiri hadi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa kabla ya kiungo huyo wa Cameroon kucheza mechi yake ya kwanza.
Hawakutarajia kuwa wangekuwa katika nafasi ya 12 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, wakiwa na ushindi mmoja tu na pointi tano kutoka kwa mechi zao tano za kwanza.
Zaidi ya hayo, Brighton walifanikiwa kugeuza matokeo baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 Old Trafford na kuwatoa kihalali kwenye Kombe la EFL.
Hivyo, ni dhahiri kuwa kuna shinikizo kubwa kwa Baleba na klabu yake mpya kabla ya kuikaribisha Tottenham, timu iliyo mkiani mwa msimamo wa ligi na kufuatiwa na mfululizo wa mechi tatu za ugenini.
Mechi za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atletico Madrid na Como zitachezwa kabla na baada ya safari ya kwenda kukabiliana na Leeds.
Ndivyo anavyoelezea mtu wa ndani ya klabu ya United kuhusu mtazamo wa awali juu ya Baleba. "Anajua kutumia vyema eneo la uwanja anapocheza."
Kufanya mazoezi mara chache kabla ya kuingizwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba katika sare ya 1-1 dhidi ya Fulham mnamo tarehe 20 Septemba, pamoja na mechi dhidi ya timu ya Lausanne-Sports ya Uswisi mnamo tarehe 2 Oktoba wakati wachezaji wa United walioitwa kwenye timu zao za taifa walipokuwa hawapo ni kipimo kidogo mno cha kutoa tathmini ya uhakika.
Hata hivyo, kasi ya Baleba ni sifa inayoweza kuleta faida kubwa kwa safu ya kiungo ya United.
Andrey Santos anayo sifa hiyo; lakini si kwa kiwango kikubwa kwa Kobbie Mainoo na Youri Tielemans, ambao wamepangwa pamoja na Carrick katika mechi nne zilizopita za ligi kutokana na uwezo wao mkubwa wa kiufundi.
Imekuwa rahisi sana kwa wapinzani kupenya kwenye safu ya United, na hatari haijawa ikibainishwa kwa wakati mwafaka.
Timu ya Carrick ni miongoni mwa timu nne pekee katika ligi hiyo ya daraja la juu ambazo bado hazijafanikiwa kuzuia wapinzani kufunga bao hata moja katika mechi (clean sheet).
Wameruhusu mabao mawili katika mechi nne kati ya saba walizocheza kwenye mashindano yote. Hadi pale suluhisho litakapopatikana, ni vigumu kutarajia kuona mabadiliko chanya katika kiwango cha timu.
Ni wazi kuwa Baleba anahitaji kufanya zaidi ya kukimbia kwa kasi, na mchango wake unapaswa kuonekana vyema ndani ya chumba cha kubadilishia nguo na pia uwanjani.
Taarifa zinaonyesha kuwa hali ya awali ya aibu na wasiwasi ambayo inaeleweka inaonekana kuanza kutoweka. Baleba hana ujasiri mkubwa wa kuzungumza Kiingereza, lakini amepiga hatua kubwa tangu alipohamia Brighton akitokea Lille kwa ada ya pauni milioni 23.2 mwaka 2023.
Ameanzisha urafiki na Amad Diallo. Ni bahati nzuri kwamba wachezaji wawili vijana kutoka Afrika wanapitia mchakato wa kupona majeraha kwa wakati mmoja, lakini pia inasaidia kuwa na asili moja inayojenga uhusiano wa asili ambao umeimarika zaidi katika wiki za hivi karibuni.
Amad alionekana akicheka kwenye video aliyoiweka mitandaoni, ambapo Baleba alikuwa akimtania baada ya Cameroon kuifunga Ivory Coast katika mechi ya kirafiki mnamo Oktoba 3.
Akiwa aliwahi kucheza timu moja na Leny Yoro (ambaye sasa anaiwakilisha timu ya taifa ya Ufaransa) walipokuwa Lille, pamoja na Bryan Mbeumo katika ngazi ya kimataifa, Baleba tayari ana uhusiano mwingine usiotarajiwa katika uwanja wa mazoezi wa United huko Carrington; hii inadhihirishwa na jinsi alivyokuwa akitania na Patrick Dorgu baada ya mechi ya mwisho ya msimu uliopita kwenye Uwanja wa Amex.
Jambo la msingi kwa United ni Baleba kuonyesha kiwango bora kama kile kilichomfanya kung'aa katika msimu wa 2024-25 na kuzua tetesi za uwezekano wa kuhamia Real Madrid, badala ya kiwango cha chini alichoonyesha mara kwa mara msimu uliopita.
Madai kwamba Baleba alivurugika kisaikolojia kutokana na nia ya ghafla ya United kumsajili katika majira ya joto ya mwaka 2025 yametupiliwa mbali na vyanzo vya Brighton, ingawa hakuna sababu mbadala iliyotolewa kuelezea kushuka kwa kiwango chake.
Hatimaye, ilibainika kuwa kazi ya awali iliyofanywa na timu za uchambuzi wa takwimu na usajili huko Carrington miezi 12 iliyopita haikupotea bure. Baada ya kushindwa kuwapata Elliot Anderson na Mateus Fernandes, na huku chaguzi nyingine zikionekana kutofaa, United ilimfuatilia Baleba muda mfupi kabla ya kupokea kichapo cha kushtukiza katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Hull, na kukamilisha usajili huo muda mfupi baadaye.
Ikizingatiwa kuwa waliambiwa walipe zaidi ya pauni milioni 100 kwa ajili ya kiungo huyo mnamo Agosti 2025, wanaona kuwa kulipa pauni milioni 70 ni dili nzuri. Hata hivyo, Baleba bado hajaingia uwanjani, na kama ambavyo Fernandes ameonyesha kupitia viwango vyake vya awali vya kukatisha tamaa akiwa na Tottenham, tathmini yoyote ya awali kuhusu ubora wa usajili inapaswa kusubiri hadi hatua hiyo ifikiwe.
'Never give up'
Itakuwa jambo la kuvutia kuona jinsi Baleba na Fernandes watakavyokabiliana iwapo wataanza mchezo katika uwanja wa Old Trafford, ambapo kushindwa kwa upande wowote kunaweza kugeuza hali ya kukatishwa tamaa mapema msimu huu .
Haiba ya asili ya Baleba ya kupenda utani inapaswa kumsaidia katika maandalizi yake. Atatumai kupata fursa ya kuonyesha mtindo wake wa kushangilia bao kwa kuruka nyuma (back flip) – ingawa uwezo wa kufunga mabao si sababu iliyofanya United imsajili.
Muhimu zaidi, anayo nia thabiti ya kufanikiwa, jambo alilopandikizwa na baba yake.
Baba yake alimhimiza kupitia vipindi vigumu sana vya mazoezi akiwa kijana mdogo, jambo ambalo Baleba amesema lilikuwa muhimu sana katika yeye kuwa mchezaji wa kulipwa.
Kwa namna fulani, tayari amefanikiwa kwani ametimiza ahadi aliyompa mama yake ya kumjengea nyumba jijini Douala. Jambo la kuhuzunisha kwa Baleba ni kwamba mama yake alifariki miezi michache kabla hajaondoka Lille na hakuwahi kuiona nyumba hiyo.
Bado anaendelea kujituma na kuhamasika kufanya vizuri kwa ajili ya mama yake, kama alivyosimulia katika mahojiano na gazeti la Guardian mwezi Aprili 2025.
Ukirejea nyuma zaidi, kwenye mazungumzo na jarida la soka la Ufaransa la Onze Mondial mnamo Septemba 2023, utaelewa kiini cha kile kinachomchochea Baleba na kumpa motisha.
Akielezea mambo anayoyapenda nje ya soka, Baleba anazungumzia manga ambayo Makumbusho ya Uingereza (British Museum) inaielezea kama 'vitabu vya katuni au riwaya za michoro vya Kijapani' ambavyo sasa vina 'mashabiki kote duniani'.
Msururu anaoupenda zaidi ni Fist of the North Star , ambao shujaa wake ni Kenshiro.
"Alipoanza, kila mtu alimpiga na alijaa makovu, kisha akawa imara," Baleba alieleza. "Baada ya hapo, yeye ndiye alianza kuwapiga wengine. Hakukata tamaa kamwe. Naipenda hiyo tabia."