Magenge ya Mexico yageuza Afrika kitovu cha uzalishaji wa dawa za kulevya

Chanzo cha picha, Reuters
Ilikuwa siku ya kawaida mahakamni ambapo jaji alifika kuskiza kesi, ila mazingira yalikuwa tofauti.
Kesi hii haikusikizwa ndani ya mahakama kama ilivyotaratibu, badala yake, ilisikilizwa ndani ya maabara inayodaiwa kutumika kutengeneza dawa haramu, iliyojificha ndani ya msitu.
Raia watatu wa Mexico na Wanigeria saba walifikishwa mahakamani wakiwa wamefungwa pingu, huku Jaji Musa Kakaki akikagua kemikali na vifaa walivyotuhumiwa kutumia kutengeneza dawa haramu na hatari ya kulevya aina ya methamphetamine, inayojulikana kama "meth" au "crystal meth" au hapa nchini Nigeria kama "ice".
Harufu kali na yenye kuchoma ilitanda katika maabara hiyo ya muda, ikitoka kwenye pipa kubwa lililokuwa na dawa hiyo katika huku ikibadilika na kuwa fuwele.
Harufu nyingine kali ilitoka kwenye mapipa yaliyo wazi yaliyokuwa na kimiminiko kizito chenye rangi nyeusi, ambacho kilielezwa kuwa ni methamphetamine "mbichi" yaani, ambayo bado haijachakatwa.
Bidhaa nyingine zilitapakaa katika jengo hilo ambalo bado halijakamilika, zikiwemo mitungi ya gesi ya propane na mifuko ya kemikali ya caustic soda.
Kuhamishwa kwa muda kwa Mahakama Kuu ya Shirikisho kutoka Lagos hadi eneo hilo, lililokuwa umbali wa takriban saa mbili kwa gari, ilikuwa hatua isiyo ya kawaida katika mfumo wa mahakama wa Nigeria. Hata hivyo, Shirika la Kitaifa la kupambana na Dawa za Kulevya (NDLEA) ilisema hatua hiyo ilikuwa muhimu ili kuelewa ukubwa wa operesheni hiyo.
Washukiwa hao walipokamatwa mwezi Mei, shirika hilo lilisema operesheni hiyo ilikuwa imeweza kukamata methamphetamine nyingi zaidi kuwahi kukamatwa nchini humo. Zaidi ya tani mbili za dawa hiyo ziligunduliwa, zikiwa na thamani ya takriban dola milioni 360.
Baadaye, NDLEA ilitangaza kuwa ilikuwa imefaulu kuangamiza na kuvunja mtandao wa uzalishaji wa methamphetamine wa Nigeria na Mexico uliokuwa umeundwa kwa ustadi mkubwa na wenye thamani ya mamilioni ya dola.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwezi uliofuata, maafisa waligundua maabara nyingine ya methamphetamine iliyokuwa imefichwa ndani ya msitu katika jimbo jirani la Oyo. Safari hii, waliwakamata washukiwa watano, akiwemo raia mmoja wa Mexico aliyeelezwa kuwa "mtaalamu wa kutengeneza methamphetamine".
Misako hiyo inaelezea kuongezeka kwa nafasi ya Afrika, na hasa Afrika Magharibi, katika biashara ya kimataifa ya dawa za kulevya za kutengenezwa kwa kemikali, pamoja na mabadiliko ya mbinu za magenge ya uhalifu ambayo sasa yanaitumia bara Afrika kama kitovu cha kusafirisha dawa hizo, na pia kama eneo la kuzalishia dawa hizo.
Kulingana na mamlaka, wataalamu wa Mexico wa kutengeneza methamphetamine, ambao mara nyingi huitwa "wapishi", wanazidi kufanya kazi pamoja na wenyeji katika maabara zilizoko Ulaya na Afrika.
Uzalishaji wa methamphetamine umekuwa wa kisasa zaidi katika miongo kadhaa iliyopita.
"Wameufanya mchakato huo kuwa wa hali ya juu kiasi kwamba sasa wanazalisha methamphetamine safi na nguvu kubwa zaidi," James Griego, anayeongoza operesheni za kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya katika Kamandi ya Marekani barani Afrika (Africom), aliiambia BBC.
Africom, ambayo inasimamia operesheni za kijeshi za Marekani barani Afrika, imekuwa ikitoa taarifa za kijasusi kwa mashirika kadhaa ya kitaifa yanayopambana na dawa za kulevya ili kusaidia katika operesheni zao.
"Yeyote anayetaka kutumia methamphetamine anajua kwamba methamphetamine ya Mexico ndiyo bora zaidi duniani kwa matumizi hayo," aliongeza Griego.

Chanzo cha picha, Reuters
Maabara hizi, ambazo ziliendeshwa na raia wa Mexico, tangu wakati huo zimegunduliwa nchini Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini.
"Tangu mwaka 2023, tumeona jumla ya maabara 14 zinazoendeshwa na raia wa Mexico zikigunduliwa.
Tuligundua moja mwaka 2023 nchini Msumbiji, nyingine sita mwaka 2024, mbili mwaka 2025 na tano mwaka huu," alisema Griego.
" Mwaka jana, kati ya maabara hizo tano, nne zilikuwa nchini Nigeria," aliongeza.
Kulingana na Africom na shirika la Marekani la Kudhibiti Dawa za Kulevya (DEA) zimebaini uhusiano kati ya baadhi ya maabara hizo na magenge mawili makubwa zaidi ya biashara ya dawa za kulevya nchini Mexico,genge la Sinaloa na genge jipya la Jalisco.
Katika ushahidi wake mbele ya Bunge la Marekani mwezi Mei, Jenerali Dagvin Anderson, kamanda wa Africom, alisema makundi yenye misimamo mikali na wafanyabiashara wa dawa za kulevya walikuwa wakishirikiana.
"Makundi ya kigaidi yaliyo barani Afrika yanazidi kupata ufadhili kutoka kwa magenge ya dawa za kulevya, jambo linaloongeza uwezo wao wa kufikia maeneo mengi zaidi na kufanya mashambulizi yenye madhara makubwa,"
Tofauti na dawa za kulevya zinazotokana na mimea, kama vile cocaine au heroini, ambazo zinaweza kulimwa na kuchakatwa katika maeneo maalum pekee, dawa za kulevya zinazotengenezwa kwa kemikali kama methamphetamine zinaweza kuzalishwa mahali popote, mradi kemikali zinazohitajika na ujuzi wa kuzitengeneza vinapatikana. Hali hiyo inaziwezesha makundi ya uhalifu uliopangwa kuongeza uzalishaji wao kwa kasi.
Methamphetamine inajulikana kwa kuleta athari za haraka na za kudumu kwa muda mrefu. Husababisha hali ya furaha isiyo ya kawaida, lakini pia huambatana na madhara makubwa.
Matumizi yake yanaweza kuongeza hatari ya matatizo ya moyo na mishipa ya damu, utapiamlo kutokana na ulaji usio na uwiano, na ikiwa itadungwa kwa sindano, inaweza kusababisha maambukizi ya magonjwa yanayoenezwa kupitia damu.
Kuacha kutumia dawa hii pia ni jambo gumu sana, kwani mara nyingi huambatana na wasiwasi, msongo mkali wa mawazo, uchovu na hamu kubwa ya kutaka kuitumia tena.

Chanzo cha picha, Reuters
Afrika Magharibi ina faida nyingi kwa magenge ya Mexico, kuanzia na maeneo yake makubwa yenye misitu minene, ambayo yanafaa kwa kuanzisha vituo vya uzalishaji na viwanda vyao.
"Idadi ya watu pia ni rasilimali kwao, hasa kwa kuwa kuna vijana wengi. Hali inayowawezesha kupata wafanyakazi kwa gharama nafuu na pia soko la matumizi."Femi Babafemi, msemaji wa NDLEA, aliiambia BBC.
Mamlaka zina hofu kuwa matumizi ya methamphetamine yanaongezeka nchini Nigeria, ambapo utafiti wa mwaka 2018 ulibaini kuwa asilimia 14.4 ya watu wazima walikuwa wamewahi kutumia dawa haramu za kulevya.
Kulingana na Global Initiative Against Transnational Organized Crime, matumizi ya dawa hii yameenea katika maeneo mbalimbali ya bara la Afrika.
Afrika Mashariki, dawa hiyo imekuwa ikipatikana kwa wingi katika nchi kama Kenya na Tanzania, huku pia ikitumika sana Afrika Kusini, ambako inajulikana kama "tik".
Magenge ya dawa za kulevya yanavutiwa na masoko ya kimataifa pamoja na soko la ndani la Afrika linalokua kwa kasi. Eneo la kijiografia la bara hilo pia linawezesha wafanyabiashara hao kufikia masoko ya Asia na Ulaya.

Barani Ulaya, UNODC iliripoti ongezeko la asilimia 47 la matumizi ya methamphetamine kati ya mwaka 2014 na 2024.
Tangu kurejea madarakani mwaka 2025, Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza juhudi za kukabiliana na magenge ya dawa za kulevya ya Amerika Kusini.
"Magenge haya yako chini ya shinikizo kutoka maeneo mengine ya dunia," alisema Babafemi, "na hivyo yanaiona Afrika Magharibi kama kitovu cha uzalishaji wa biashara zao."
Baadhi ya wataalamu wanaamini kuwa udhibiti mkali zaidi wa njia za jadi za kusafirisha dawa za kulevya kutoka Amerika Kusini huenda ukawa miongoni mwa sababu zinazoyasukuma magenge hayo kutafuta maeneo mapya ya kuendeshea shughuli zao.
Lakini kuongezeka kwa misako dhidi ya maabara za siri za methamphetamine barani Afrika hivi karibuni kunaweza kuashiria kuwa magenge hayo yanazidi kujikita katika bara hili.
Kilicho wazi ni kwamba biashara hiyo haihusiani tena tu na Afrika kuwa njia ya kupitisha dawa za kulevya, bali sasa inahusisha pia kuanzishwa kwa maeneo mapya ya uzalishaji na kutafuta masoko mapya.















