Johnson & Johnson yajitolea kulipa hadi $5.5bn kumaliza kesi za poda ya watoto

Chanzo cha picha, Getty Images
Kampuni ya Johnson & Johnson (J&J) imejitolea kulipa hadi dola bilioni 5.5 (pauni bilioni 4.14) ili kumaliza maelfu ya kesi zinazodai poda yake ya watoto pamoja na bidhaa nyingine zenye madini ya talcum husababisha saratani ya ovari au kifuko cha mayai.
Makubaliano hayo makubwa yanakusudia kumaliza mzozo wa kisheria uliodumu kwa miaka kadhaa na kuendelea kuigharimu kampuni hiyo kubwa ya huduma za afya nchini Marekani.
J&J imeendelea kusisitiza kuwa bidhaa zake zenye talcum hazisababishi saratani, na tayari imebadilisha viambato vya poda yake ya watoto inayotumiwa na watu wengi.
Makamu wa Rais wa masuala ya kesi za kisheria wa kampuni hiyo, Erik Haas, alisema Jumatatu kuwa madai hayo "hayana msingi", na kwamba J&J imeamua kufikia makubaliano ili kutatua kabisa suala hilo.
Kampuni hiyo imesema makubaliano hayo yatahusisha takriban kesi 69,000, ambazo ni sehemu kubwa ya madai yaliyosalia yanayohusiana na bidhaa za talcum. J&J imeeleza kuwa italipa hadi dola bilioni 3 mwaka ujao, na kusitarajiwe malipo mengine kabla ya mwaka 2028.
J&J pia imesema pendekezo hilo litalazimika kukubaliwa na kampuni za mawakili zinazowawakilisha asilimia 95 ya walalamishi wa kesi za saratani ya ovari katika mahakama za majimbo na za shirikisho, kabla ya makubaliano hayo kukamilika.
Katika taarifa yake, Haas alisema kampuni ina imani kuwa ingeibuka mshindi endapo kesi hizo zingeendelea mahakamani, kama ilivyofanikiwa katika kesi nyingi ambazo tayari zimeamuliwa.
Aliongeza kuwa makubaliano hayo yataiwezesha kampuni kuhitimisha suala hilo na kuelekeza nguvu zake katika jukumu lake la kutengeneza dawa na vifaa vya tiba vinavyookoa maisha.
Soma Zaidi:




















