Wiki mbili za ukimya wa Nchimbi

Chanzo cha picha, Screengrab
Wiki mbili zilizopita, Emmanuel Nchimbi alionekana hadharani akiwa bado Makamu wa Rais wa Tanzania, katika uzinduzi wa bwawa la Umeme wa Julius Nyerere, Rufiji, Pwani.
Picha za siku hiyo zilimwonyesha akimsindikiza Rais Samia Suluhu Hassan katika tukio kubwa la kitaifa. Hakukuwa na ishara ya wazi kwa umma kwamba hiyo ingekuwa mara yake ya mwisho kuonekana katika shughuli rasmi akiwa Makamu wa Rais.
Siku tatu baadaye, Agosti 25, 2026 Nchimbi alitoa taarifa iliyobadili kabisa mwelekeo wa siasa za Tanzania. Alisema amemwandikia Rais Samia kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais na kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma. Alisema uamuzi huo ungeanza kutumika Septemba 4.
Katika taarifa hiyo, Nchimbi alisema alifanya hivyo baada ya kujiridhisha kuwa Rais alitaka mabadiliko, akisema: "Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu."
Lakini Septemba 4 ilipofika, Nchimbi hakuwa tena mtu aliyekuwa akisubiri siku yake ya mwisho ofisini. Nafasi yake ilikuwa tayari imechukuliwa na Deogratius Ndejembi, huku yeye akiwa hajatoa kauli nyingine ya hadhara kuhusu yaliyotokea.
Na sasa, karibu wiki mbili baada ya tangazo lake, swali la Nchimbi limerudi tena kwenye mjadala kupitia mahojiano ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Kenani Kihongosi, na mwandishi wa habari Edwin Odemba kupitia Star TV. Alipoulizwa alipo Nchimbi, Kihongosi alisema hajui.
"Kuonekana kwa mtu ama kutoonekana kwa mtu, ni uamuzi wa mtu mwenyewe, mimi binafsi sijui yuko wapi lakini naamini yupo," alisema.
Wiki mbili zilizobadilisha kila kitu

Chanzo cha picha, DailyNews
Uamuzi wa Nchimbi wa kujiuzulu haukuacha nafasi hiyo wazi kwa muda mrefu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Siku moja tu baada ya tangazo lake, CCM ilitangaza kumvua uanachama. Katibu Mkuu wa chama hicho, Asha-Rose Migiro, alisema Halmashauri Kuu ya CCM ilifikia uamuzi huo kwa madai ya ukiukaji wa kanuni za nidhamu na maadili ya chama.
Kisha jina la Deogratius Ndejembi likaletwa. Waziri huyo wa Nishati akapitishwa na CCM kuwa mtu wa kuchukua nafasi ambayo Nchimbi ambaye alikuwa ameandika kwamba angeiacha rasmi Septemba 4.
Agosti 28, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alieleza Bunge kwamba Nchimbi alikuwa amekoma kuwa Makamu wa Rais tangu Agosti 26, baada ya kupoteza uanachama wa CCM, hivyo tarehe ya Septemba 4 aliyoiandika katika barua yake haikufika akiwa bado katika nafasi hiyo.
Katika muda mfupi, mtu aliyekuwa Makamu wa Rais alikuwa amepoteza pia nafasi yake ndani ya chama tawala, wakati mrithi wake alikuwa tayari anapigiwa kura Bungeni.
Na Bunge likafanya hivyo kwa kasi na kishindo. Wabunge wote 324 waliopiga kura Agosti 28 waliunga mkono uteuzi wa Ndejembi, bila kura ya kupinga wala kura iliyoharibika.
Siku iliyofuata, Agosti 29, Ndejembi akaapishwa kuwa Makamu wa Rais katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, mbele ya Rais Samia.
Kwa hiyo ndani ya siku nne tu, simulizi la Nchimbi lilikuwa imebadilika kutoka "Makamu wa Rais anajiuzulu" na kuwa "aliyekuwa Makamu wa Rais."
Lakini kuna jambo lingine linalofanya wiki hizi mbili kuwa tofauti. Wakati Nchimbi akiwa hajaonekana kuzungumza hadharani, shughuli za ofisi aliyokuwa akiiongoza ziliendelea.
Ndejembi tayari ni Makamu wa Rais, lakini hakuna maelezo ya hadhara yanayoeleza kwa kina kama kulikuwa na makabidhiano rasmi na Nchimbi, na yalifanyika lini.
Hiyo pengine ingekuwa fursa ya kuonekana kwakwe na pengine kuzungumza kwakwe hadharani. Lakini haikuwa hivyo, na si kwamba hakukuwa na watu waliotaka kuwasiliana naye.
Agosti 25, siku alipotangaza kujiuzulu, Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba alimtafuta kwa simu baada ya kuona taarifa hiyo ikisambaa. Nchimbi alipokea simu na kuthibitisha kuwa kweli alikuwa ameandika barua ya kujiuzulu. Warioba akamuuliza kuhusu majibu ya Rais; Nchimbi akasema bado hajapata majibu.
Lakini siku iliyofuata, Kwa mujibu wa Warioba alipompigia tena simu, haikupokelewa. Alituma pia ujumbe ambao haukujibiwa.
"Kwa kawaida nikiandika alikuwa ana respond mapema tu," alisema Warioba.
Ukimya wake ukaendelea.
Kihongosi: "Sijafanya jitihada hizo"

Chanzo cha picha, DailyNews
Alipoulizwa na Odemba kama amefanya jitihada zozote za kumtafuta Nchimbi, Kihongosi hakusema amemtafuta na kushindwa kumpata. Alisema hajafanya hivyo.
"Sijafanya jitihada hizo kwa kweli, muda ukifika ninaweza kufanya tu lakini sijaona sababu ya kufanya hivyo," alisema.
Kwa upande mmoja, Kihongosi anasema hajui alipo Nchimbi, lakini anaamini yupo. Kwa upande mwingine, anasema hajafanya jitihada za kumtafuta kwa sababu hajaona sababu ya kufanya hivyo.
Kauli hiyo inarudisha swali ambalo lilianza kuonekana baada ya Nchimbi kujiuzulu, je amechagua tu kukaa kimya, au kuna sehemu ya hadithi ambayo bado haijaelezwa?
Kihongosi, katika mahojiano hayo hayo, pia alifafanua jambo jingine kuhusu hatua ya CCM dhidi ya Nchimbi. Alisema Nchimbi aliitwa "kama kada, si Makamu wa Rais" na kwamba hakuitwa mbele ya Kamati Kuu, bali kwenye Kamati ya Maadili kama mwanachama wa CCM.
CCM imesema kulikuwa na ukiukaji wa nidhamu na maadili, lakini maelezo ya kina hayajawekwa hadharani. Kihongosi amesema masuala mengine ni ya ndani ya vikao na ni siri kati ya mwanachama na kamati.
Ukimya ambao haujamaliza maswali

Chanzo cha picha, URT
Katika siasa, kuondoka madarakani si lazima kumaanishe kuondoka kwenye mjadala, au kutoonekana hadharani. Lakini kwa wiki mbili hizi, imekuwa kinyume kwa Nchimbi.
Aliondoka akiwa ameandika mwenyewe kwamba ameamua kutimiza ahadi aliyowahi kutoa kwa Rais. Lakini ndani ya saa chache, uamuzi huo ukafuatiwa na hatua ya chama, kisha uteuzi wa mrithi, kura za Bunge na uapisho wa Makamu mpya wa Rais.
Na wakati hayo yote yakitokea, sauti ya Nchimbi haikusikika tena.
Hata mtu aliyekuwa akijaribu kumpigia simu, Warioba, hakupata majibu baada ya siku ya kwanza. Sasa Kihongosi naye anasema hajui alipo na hajafanya jitihada za kumtafuta.
Kwa hiyo, baada ya wiki mbili, kinachojulikana si mahali alipo Nchimbi, bali ni mahali alipotoka: kutoka katika nafasi ya pili kwa ukubwa nchini, kutoka CCM, na kutoka kwenye maisha ya kisiasa ambayo mwenyewe alisema angeyaacha.
Kinachobaki ni kile ambacho hakijasemwa na mhusika mwenyewe ambaye ni Nchimbi kwamba anasemaje kuhusu yaliyotokea baada ya barua yake ya kujiuzulu? Kwa nini CCM ilifikia uamuzi wa kumfukuza? Anakubaliana na uamuzi huo na bado msimamo wake ni kustaafu siasa?
Wengi wanasubiri kumuona na kumsikia akijibu baadhi ya maswali hayo. Pengine ni suala la muda anaweza kujitokeza kuzungumza kwa sababu wiki mbili unaweza kusema anazitumia kutafakari yaliyotokea.















