Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini magenge ya wahalifu nchini Haiti na Kenya yanajiita 'Taliban'?
- Author, Ali Hosseini
- Nafasi, BBC Pashto
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Video moja inaonyesha kijana aliyevalia jezi ya mpira wa kikapu na ndala akifyatua risasi hewani. Video nyingine inaonyesha helikopta ikiruka juu. Maandishi yaliyoambatana na picha hiyo yalisema: "Taliban Yo atè a".
Kwa mtazamo wangu, kifungu hicho hakikuwa na uhusiano wowote na harakati za Taliban nchini Afghanistan na Pakistan. Lakini, kwa nini neno "Taliban" limetumika?
Nilitafsiri maneno hayo kwa kutumia Akili Mnemba (AI), na matokeo yakawa: "Taliban wako ardhini".
Kauli hiyo ilimuashiria kijana aliyekuwa akifyatua risasi kuelekea kwa helikopta. Wapi? Haiti. Na maneno hayo yaliandikwa kwa lugha ya Krioli ya Haiti.
Nikajiuliza: Taliban wanafanya nini katika nchi iliyo karibu sana na Amerika Kaskazini?
Katika wiki mbili au tatu zilizopita, shughuli za makundi yenye silaha nchini Haiti, zimezidi kuwa kitovu cha mjadala.
Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa ilibainisha kuwa zaidi ya watu 5,700 waliuawa au kujeruhiwa katika muda wa miezi tisa kutokana na vurugu zinazohusishwa na makundi yenye silaha au operesheni dhidi yao. Zaidi ya watu 230,000 walitekwa nyara katika kipindi hicho, na inakadiriwa kuwa wanawake na wasichana wasiopungua 1,000 walibakwa.
Kwa miongo kadhaa, makundi yenye silaha yamekuwa na ushawishi mkubwa nchini Haiti. Miongoni mwao ni kundi linalojiita "Taliban".
Mada hii ilinivutia kwa kuwa nimekuwa nikifuatilia harakati za Taliban nchini Afghanistan na Pakistan kwa miaka mingi kama mwandishi wa habari.
Nilipochunguza zaidi, nilikutana na video nyingine zikionyesha wanaume wenye silaha waliovalia mavazi ya kiraia wakitumia neno "Taliban" katika mazungumzo yao.
Pia nilisikiliza nyimbo kadhaa za pop zilizolitaja neno "Taliban".
Je, neno "Taliban" linalotumiwa Haiti limetokana na harakati za Taliban za Afghanistan?
Niliwasiliana na mhariri mkuu wa chombo kimoja cha habari mtandaoni nchini Haiti na kumuuliza kama jina "Taliban" lilikuwa sawa na lile linalotumiwa Afghanistan au kama ni kufanana kwa majina tu.
Alijibu:
"Jina hili limetokana moja kwa moja kutoka kwa harakati za Taliban za Afghanistan. Kwa mtazamo wao, Taliban wa Afghanistan ni kundi la waasi jasiri wasioogopa vitisho. Wanasema pia hawaogopi hatari, na ndiyo sababu wamejiita Taliban."
Kisha alinitumia kiungo cha akaunti ya TikTok ambayo alisema inamilikiwa na Jeff Gulawe, kiongozi wa Taliban.
Haiti, yenye wakazi zaidi ya milioni 11, inakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi. Hakujafanyika uchaguzi nchini humo kwa miaka 10, na rais wake aliuawa miaka mitano iliyopita. Katikati ya hali hiyo, makundi yenye silaha yameongeza shinikizo dhidi ya serikali.
Makundi hayo sasa yanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince.
Mgogoro Mkubwa wa Haiti: Makundi yenye silaha
Romain Le Cour, mkuu wa kitengo cha ufuatiliaji wa Haiti na Karibea katika Taasisi ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kimataifa na Usalama wa Kimataifa, anasema kuna kati ya makundi 150 na 200 ya aina hiyo, yakitofautiana kutoka madogo hadi makubwa.
Anaongeza kuwa makadirio yanaonyesha kuwa kila kundi lina wanachama kati ya 8,000 na 20,000, wakiwemo watoto.
Akizungumza na BBC, Bw Le Cour alisema:
"Yanadhibiti barabara zote zinazoelekea mji mkuu. Hii ina maana kwamba ukitaka kufika mjini, lazima upitie vituo vya ukaguzi vinavyosimamiwa na makundi yenye silaha. Bidhaa zinazosafirishwa kutoka bandarini kwenda mjini pia hupitia vituo hivyo, na malipo hulazimika kufanywa. Viwanja vya ndege vya kimataifa vimefungwa. Wamedhibiti maeneo makubwa ya mikoa ambayo polisi hawawezi kuyafikia na wanaweka sheria zao wenyewe."
Mashirika ya kimataifa, yakiwemo Umoja wa Mataifa, huyataja kama "makundi yenye silaha", lakini wanachama wake wanasema wanapigania "haki na usawa".
Mmoja wa viongozi wao hata aliwania na kushinda kiti katika Seneti ya Haiti.
Katika ripoti iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Taliban walitajwa pamoja na magenge mengine kadhaa. Ripoti hiyo ilisema:
"Makundi haya yanafanya kazi kama mashirika ya kihalifu na hujihusisha na shughuli mbalimbali haramu, zikiwemo magendo ya silaha, dawa za kulevya na mafuta, unyanyasaji wa wahamiaji, ulaghai kwa njia ya vitisho na shughuli nyingine zisizo halali."
Redio ya Taliban FM
Pia nilimuuliza Romain Le Cour kwa nini makundi haya yanaitwa "Taliban".
Alijibu:
"Kuhusu kundi la Taliban, watu walituambia kuwa jina la kundi hilo, ambalo liko katika eneo la Canaan mjini Port-au-Prince, linatokana na matumizi ya neno 'Taliban' katika lugha ya mitaani kumaanisha mtu mwenye nguvu, heshima na ushawishi mkubwa. Hatujui neno hilo liliingiaje katika matumizi hayo, lakini watu wa kawaida hulitumia."
Pia kuna dhana kwamba kundi hilo linaonekana, kwa namna fulani, kama kundi la upinzani; yaani, kundi lenye nguvu linaloipinga dola na, kwa kiasi fulani, ukandamizaji na dhuluma.
Miaka mitatu iliyopita, Taliban walichukua udhibiti wa kituo cha redio mjini Mirabalais na kukibadili jina kuwa "Taliban FM".
Kituo hicho kilikuwa kikirusha propaganda na hotuba za kiongozi wa kundi hilo, Jeff Gualua.
Genge la Taliban nchini Kenya na Peru
Nilipokuwa nikiandaa ripoti kuhusu kundi la "Taliban" nchini Haiti, niligundua kuwa hali hiyo haipo Haiti pekee.
Kuna kundi jingine linalofanya shughuli zake nchini Kenya, Afrika Mashariki, ambalo pia linajiita "Taliban".
Kundi hilo lilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 baada ya kujitenga na kundi la "Baghdad Boys". Kwa mujibu wa ripoti, shughuli zake zinahusisha kuwatoza madereva wa usafiri wa umma fedha kwa vitisho, biashara ya dawa za kulevya, wizi na kuhamasisha watu kushiriki mikutano ya kisiasa.
Mfano mwingine ni Peru huko Amerika Kusini.
"Los Taliban" ni genge lenye silaha linalofanya shughuli zake katika mji wa Trujillo. Kwa mujibu wa ripoti, kundi hilo limehusika katika kuzitoza kampuni za usafiri fedha kwa vitisho, kuwatishia madereva na kushiriki mapigano ya kutumia silaha dhidi ya makundi hasimu.
Mwaka jana, polisi wa Peru walitangaza kukamatwa kwa wanachama wa kundi hilo na kuvunjwa kwa moja ya seli zake.
Nchini Kenya na Peru, shughuli za makundi hayo zinafanana na zile za kundi linalojiita "Taliban" nchini Haiti.
Baadhi ya wataalamu wanaofuatilia masuala ya Haiti wanaamini kwamba, ingawa makundi hayo yanatoa madai yasiyoeleweka wazi chini ya kaulimbiu ya kuanzisha mfumo wa haki na usawa, kwa uhalisia yameyageuza maisha ya wananchi wa kawaida katika mji mkuu na maeneo yanayouzunguka kuwa mateso makubwa.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi