Siku moja tu ya maisha yako inaweza kutabiri utaishi miaka mingapi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Sayansi iko hatua moja karibu kuweza kutabiri kwa usahihi maisha yako kulingana na tabia zako za kila siku, kutokana na utafiti mpya kutoka Chuo Kikuu cha Stanford.

Watafiti walifuatilia tabia ya samaki aina ya Killifish 81 kutoka Afrika wenye katika matangi na kamera katika kipindi chote cha maisha yao - yaani, miezi minne hadi minane.

Baada ya kuchanganua mabilioni ya video, wanasayansi waliweza kuhusisha mifumo ya tabia ya kila siku na uwezekano wa kuishi maisha marefu zaidi.

"Ugunduzi mmoja mkubwa kutoka kwa utafiti huu ni kwamba tabia inahusika na mchakato wa kuzeeka," mtafiti Dkt. Claire Bedbrook, mwanabiolojia na mwanasayansi wa neva, aliiambia BBC Science Focus.

"Hii inaonyesha kwamba mambo kama vile shughuli za kila siku na usingizi, katika mzunguko wa saa 24 yanaweza kutufahamisha kuhusu mahali tulipo katika ukuaji wetu wa uzee - na hata kutabiri maisha yetu ya baadaye."

Bedbrook anaeleza kwamba, wanasayansi hivi karibuni wataweza "kuelewa na kupima mahali mtu alipo katika safari yake kutoka utu uzima hadi kifo."

Wakati huo huo, matokeo kutoka utafiti huu yanaweza kutufundisha kuhusu mchakato wa kuzeeka kwa wanyama wenye ubongo.

Utafiti wa Samaki

Utafiti juu ya samaki uligundua kuwa kufikia katikati ya maisha yao - karibu siku 70-100 katika maisha yao - samaki ambao wangeendelea kuishi maisha marefu walikuwa tayari wana tabia tofauti na samaki ambao wangekufa mapema.

"Nadhani inavutia sana kwamba tuliweza kuchukua tabia ya mnyama akiwa na umri mdogo, na kukadiria kwa usahihi umri wake na kama angeishi maisha marefu au mafupi," mtafiti Dkt. Ravi Nath , mwanasayansi wa neva na mtaalamu wa jeni, aliiambia BBC Science Focus.

Hasa, wanasayansi waligundua tofauti katika mifumo ya kulala. Samaki wenye maisha marefu zaidi walilala usiku, ilhali samaki wenye maisha mafupi zaidi walilala mchana zaidi wakiwa vijana.

Wakati huo huo, samaki wenye shughuli nyingi zaidi - wale walioogelea kwa nguvu zaidi, haraka na kwa hiari kuzunguka matangi yao wakati wa mchana - walikuwa na uwezekano wa kuishi kwa muda mrefu zaidi.

Wanasayansi walifanikiwa kutambua jumla ya vitendo 100 tofauti vya kitabia', wakimaanisha vitendo vifupi vinavyounda tabia ya killifish, ambavyo vingi waliviunganisha na maisha yao.

Kwa kutumia mifumo ya mashine, watafiti waliweza kutabiri kwa usahihi muda wa kuishi wa samaki mmoja mmoja, kulingana na data ya kitabia kutoka katikati maisha ya samaki.

"Hapo awali nilidhani kwamba kuzeeka ni mchakato wa taratibu, huku kila siku ikiwa mbaya kuliko ya mwisho," alisema Bedbrook. "Badala yake, ufuatiliaji wa tabia unaonyesha vipindi virefu vya utulivu vinavyoambatana na mabadiliko ya ghafla, ambapo wanyama huzeeka haraka na kuingia katika hatua mpya ya maisha."

Wanasayansi walisema tafiti za siku zijazo zinaweza kuchambua tabia katika mazingira ya asili zaidi, na kuruhusu samaki hao kuwasiliana zaidi kijamii.