"Ukikimbia wanakupiga risasi, ukijificha wanachoma nyumba"

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

"Ukikimbia kuingia chumbani, wanakichoma moto," anasema Fatima, akielezea shambulio la hivi karibuni katika kijiji chake Zamfara, kaskazini magharibi mwa Nigeria. "Ukitoka nje na kuanza kukimbia, wanakupiga risasi."

Watu hao waliojihami kwa silaha, waliofanya shambulio hilo saa nane usiku (saa 02:00), waligawanyika katika makundi ili kuwazingira wakazi, kundi moja kwenye lango la kuingilia kijijini, jingine katikati na la tatu nyuma.

"Walianza kufyatua risasi bila kujali lolote, wakipiga risasi ovyo ovyo," mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 55 aliambia BBC World Service kwa sauti ya chini.

Ilikuwa ni mojawapo ya mashambulio mengi yaliyosababisha taharuki katika jamii hiyo ambayo wakazi wake wengi ni Waislamu na wanaishi kwa hofu ya kutekwa nyara ili kudaiwa fidia.

Fatima anaelezea jinsi mashambulio hayo yanavyofanyika, "Unaweza kuona pikipiki 100, na kila moja ikiwa imebeba watu watatu."

Takriban watu 70, wakiwemo watoto, waliuawa katika kijiji cha Bia Buki mwezi Juni, kulingana na Fatima.

Anaelezea jinsi washambuliaji walivyowalenga wanakijiji waliokuwa wakikimbia na jinsi watoto walivyojeruhiwa kwa kuanguka kwenye mitaro. Miongoni mwa waliouawa walikuwa mumewe na ndugu zake sita kati ya saba.

Fatima ni mmoja wa watu wanaokadiriwa kufikia 800,000 nchini Nigeria ambao Umoja wa Mataifa unasema wameyakimbia makazi yao kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Sababu kuu ya watu kuhama makazi yao ni vurugu na mashambulio.

Baadhi ya mashambulio yamefanywa na makundi ya wapiganaji wa Kiislamu, lakini mengi katika eneo hili hufanywa na magenge ya wahalifu, wanaojulikana huko kama majambazi, ambao mara nyingi huzunguka kwa pikipiki, hushambulia kwa haraka na kisha kuondoka mbio kabla ya vikosi vya usalama kufika.

Maelfu ya watu wamejiunga na makundi ya ulinzi wa raia yanayoungwa mkono na serikali ili kukabiliana na makundi hayo, na BBC ilizungumza na mmoja wao ambaye alisema kundi lake lililojihami limewaua majambazi wengi.

Hata hivyo, magenge hayo yanaendelea kushambulia katika hali inayoonekana kuwa ni kudorora kwa usalama, huku vurugu na utekaji nyara vikienea kuelekea kusini.

Fatima anasema kuwa wakati majambazi waliposhambulia nyumba yake, alikimbilia msituni karibu na hapo pamoja na wanakijiji wengine ili kujificha, "Msitu ukawa mahali petu pa usalama. Tulikimbia tukiwa na watoto wetu, kama hukumpata mtoto wako, ulimchukua mtoto wa jirani."

Anasema watu walilala msituni kabla ya kuelekea kwenye makao makuu ya jimbo, Gusau, "ambako tulipata utulivu kidogo".

Kwa sasa Fatima anaishi katika kambi isiyo rasmi mjini Gusau pamoja na watoto wake saba, wenye umri kati ya miaka tisa na thelathini.

Wanawake wengi wamekaa katika makundi katika maeneo yenye vumbi katika eneo hilo la muda, wengi wakiwa wamevalia hijabu za rangi angavu. Anaamini kuwa kuna zaidi ya watu 1,000 hapo.

Mazingira ni magumu, huku kukiwa "hakuna hata mahali pazuri pa kulaza kichwa". Chakula ni haba na misaada hufika kwa vipindi visivyotabirika.

Fatima anasimulia matukio mawili ambapo "wasamaria wema" walileta mchele au viazi. Watoto hutumwa kutafuta kuni za kuuza ili familia ziweze kununua chakula, lakini watoto 22 wametekwa nyara na majambazi, anasema.

Akionyesha kwa ishara jengo lililo karibu, Fatima anasema kuwa huko "utakuta wanawake 100 au zaidi... labda wawili au watatu tu ndio waliopata kifungua kinywa.

"Tulipokuwa na amani, tulikuwa na mali zetu wenyewe, lakini sasa hali imebadilika na tumekuwa ombaomba."

Macho yake yanajaa machozi na analia kwa dakika kadhaa, huku akijifuta uso kwa mikono yake.

Licha ya kuwa umbali wa maili 16 (kilomita 25) kutoka kijijini kwake, tishio ambalo Fatima alilikimbia halijaisha.

Alipowasili kambini kwa mara ya kwanza, milio ya risasi ilimfanya akose usingizi usiku. Anasema hali imetulia tangu wakati huo, kutokana na doria zinazofanywa na jeshi pamoja na makundi ya ulinzi yanayoungwa mkono na serikali, lakini bado kuna hali ya wasiwasi.

Waporaji hao kwa kiasi kikubwa ni watu kutoka kabila la Fulani, ambao kijadi hujipatia riziki kwa kufuga wanyama. Baadhi yao wameacha biashara ya mifugo na kujihusisha na utekaji nyara na uporaji wa nguvu, mambo yanayoonekana kuwa njia ya haraka na rahisi ya kutengeneza pesa.

Wanashambulia miji na vijiji au kuvizia wasafiri, wakiteka watu ili kudai fidia na kuiba chochote wanachotaka, na wakati mwingine kuua wale wanaopinga. Pia hulazimisha jamii kulipa pesa za ulinzi, na kuwaruhusu wakulima kuingia mashambani mwao tu iwapo watatoa kiasi kikubwa cha pesa taslimu.

Mashambulizi sasa yanafanyika mara kwa mara kuliko wakati wowote ule. Katika maeneo makuu yanayokumbwa na vitendo vya uporaji kaskazini magharibi mwa Nigeria, idadi ya matukio yaliyoandikwa na shirika la kimataifa linalofuatilia migogoro la Acled iliongezeka kwa asilimia 78 katika nusu ya kwanza ya mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025.

Kampuni moja ya ushauri wa masuala ya usalama inakadiria kuwa watekaji nyara kote nchini Nigeria walikusanya karibu dola milioni 5.8 (pauni milioni 4.3) kama fidia katika mwaka uliopita huku idadi ya utekaji nyara ikiongezeka kwa kasi. Shirika la SBM Intelligence linakadiria kuwa watu 7,825 walitekwanyara kati ya Julai 2025 na Juni 2026, ongezeko la asilimia 66 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Ongezeko la shughuli za uporaji linaonekana kuwa kichocheo kikubwa cha hali hii.

Malik Samuel wa shirika lisilo la faida la utafiti na utetezi la Good Governance Africa, anasema kuwa "hakuna eneo kaskazini mwa Nigeria kwa sasa ambalo halikumbwi na aina fulani ya utekaji nyara wa watu wengi".

Mapambano ya Nigeria dhidi ya waporaji ni sehemu tu ya hali ngumu zaidi ya kiusalama inayolikabili taifa hilo.

Mbali na magenge ya waporaji kaskazini magharibi, kuna uasi wa makundi ya Kiislamu kaskazini mashariki, machafuko ya kutaka kujitenga kusini mashariki na mapigano katika maeneo ya katikati, ambapo malalamiko makuu yanahusu upatikanaji wa ardhi na maji kwa ajili ya malisho na kilimo, na ambapo masuala ya kikabila na kidini pia yamechochea baadhi ya machafuko hayo.

Wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa makundi yaliyojihami kwa silaha yameendesha kampeni za vurugu zinazoathiri jamii zote, bila kujali asili au imani.

Shule ni shabaha ya kawaida. Tukio la kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram kuteka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule kutoka kijiji cha Chibok, kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo mwaka 2014, liliibua gumzo kubwa duniani.

Wakati huo, kundi hilo liliwalazimisha mateka wake kuingia katika utumwa wa kingono, kazi za nyumbani, au kuwatumia kama washambuliaji wa kujitoa mhanga.

Hata hivyo, makundi mbalimbali kote nchini Nigeria sasa yanatumia utekaji nyara kama njia ya kujipatia fedha, yakilenga maeneo yaliyo hatarini na yasiyo na ulinzi mkali kama vile shule, makanisa, misikiti na vijiji vya pembezoni.

Awali, vitendo hivi vilijikita zaidi katika ngome za Boko Haram kaskazini-mashariki au maeneo yanayokumbwa na uhalifu wa ujambazi kaskazini-magharibi,maeneo ambayo wakazi wake wengi ni Waislamu.

Kisha, mwezi Mei mwaka huu, watu waliojihami kwa silaha waliokuwa kwenye pikipiki walishambulia shule tatu katika jimbo la Oyo, kusini-magharibi mwa Nigeria, eneo ambalo hapo awali lilichukuliwa kuwa salama kiasi.

Watoto 39, akiwemo mdogo zaidi mwenye umri wa miaka miwili pekee, walitekwanyara pamoja na walimu saba. Mwalimu mmoja aliuawa wakati wa shambulio hilo, huku mauaji ya mwingine yakirekodiwa na kusambazwa mtandaoni.

Baada ya siku 56, mateka 44 waliosalia waliachiwa huru. Serikali ilisema ilikataa kulipa fidia yoyote na kwamba watoto hao waliokolewa kufuatia operesheni iliyofanywa na vikosi vya usalama.

Wanaume watatu walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kuhusika na mashambulio hayo, na walikiri kuwa wanachama wa kundi linaloshirikiana na Boko Haram.

Tukio hilo la utekaji nyara lilisababisha hofu katika mji wa Oriire ulioko kusini magharibi mwa nchi, huku wazazi katika eneo hilo wakiondoa watoto wao shuleni.

"Kuna hofu kwa sababu wakazi wengi wamekimbia na bado hawajarudi," anasema kiongozi wa kimila wa eneo hilo, Oba Tajudeen Abioye, ambaye mpwa wake wa kike alikuwa miongoni mwa watoto waliotekwa nyara.

"Na sisi tuliosalia hapa, tunawategemea maafisa wa usalama, yaani askari," ambao walitumwa kulinda jamii hiyo, anasema.

Nigeria tayari ina idadi kubwa zaidi ya watoto wasioenda shule duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linakadiria kuwa idadi hiyo ni takriban milioni 19.

Changamoto nyingi na zinazoingiliana za kiusalama zinamaanisha kuwa jeshi na polisi wa Nigeria wamelemewa na majukumu, na hivyo wanapata shida kukabiliana na vurugu hizo.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2025 ilibainisha kuwa vituo vya polisi mara nyingi vilikosa fedha za kutosha na havikuweza kufanya kazi kikamilifu; ripoti hiyo ilinukuu vyanzo huru vilivyowatuhumu maafisa hao kwa kukosa ujuzi wa kufanya mazungumzo ya kuokoa mateka na kufanya uchunguzi wa kitaalamu wa uhalifu (forensics).

Serikali ya Rais Bola Tinubu imetenga bajeti kubwa zaidi ya ulinzi na usalama katika historia ya nchi hiyo, ikiiongeza kwa asilimia 10 mnamo Desemba 2025 ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita. Hivi karibuni ameidhinisha kuajiriwa kwa askari wapya 28,000.

Wakati huo huo, jamii zinaendelea kuteseka na huko Zamfara, maelfu ya wakazi wamejiunga na makundi ya ulinzi wa raia yanayoungwa mkono na serikali ili kuziba pengo la kiusalama.

Hata hivyo, kuna wasiwasi kuhusu kuhusika kwao. Mnamo mwaka wa 2020, jimbo la Zamfara lilipiga marufuku kundi kubwa la ulinzi wa raia kutokana na hofu kwamba mauaji ya kiholela yalikuwa yakichochea vurugu zaidi, kulingana na shirika la habari la AFP.

Mamlaka zinasema kuwa walinzi hao wapya wa raia wamepata mafunzo bora zaidi, lakini Samuel, kutoka shirika la Good Governance Africa, anawaelezea kama "bomu la saa linalosubiri kulipuka".

"Ikiwa raia watajilinda kwa silaha, utawadhibiti vipi baada ya mgogoro kwisha? Utawezaje kuwapokonya silaha hizo?" anahoji.

Mmoja wa walinzi hao anakutana nasi nje ya makao makuu ya kundi lake,jengo la ghorofa moja la zege, na kukubali kuzungumza kwa sharti la kutotajwa jina wakati wa ziara yetu mwezi Julai.

Amekaa juu ya pikipiki yake, huku bunduki aina ya AK-47 ikiwa imetundikwa begani mwake, kitambaa kikiwa kimefunika uso wake kama barakoa ya kujitengenezea, na vidole vyake vikiwa na pete za dhahabu na fedha zenye michoro ya fuvu la kichwa.

"Sisi ni miongoni mwa watu walioajiriwa na gavana kulinda jamii," anasema, akieleza kuwa wakati mwingine hupewa taarifa kuhusu mahali walipo majambazi na kwamba "kwa msaada wa Mungu, tunapambana nao na kuwashinda".

"Majambazi na wafahamu kuwa wanaposhambulia eneo na kuua, nao pia wanaweza kuuawa," anaongeza.

Anakadiria kuwa amepambana na majambazi angalau mara 20 na anasema maombi ya msaada kwa kundi lake yanaendelea kuingia.

"Ni vigumu kupita wiki bila kupokea ripoti hizi," anasema. "Kuna maeneo ambayo yamekuwa salama zaidi... lakini kuna maeneo mengine ambayo hali hiyo haiwezi kusemwa."

Anatoa wito kwa gavana wa jimbo hilo, ambaye anamuunga mkono, kuwaajiri na kuwapa silaha watu zaidi ili kupambana na majambazi. "Watu hawa hawatakuogopa isipokuwa unapokuwa na silaha sahihi za kupambana nao," anasema.

Fatima pia anatoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi, "Watekaji hawa wapo kila mahali.

"Sisemi kwamba serikali imeshindwa, lakini hata kama inajitahidi, inahitaji kufanya zaidi. Kuna changamoto, na tunaamini kwamba kwa juhudi zaidi na kuongezwa kwa maafisa wa usalama, vijiji vitakuwa na amani."

Anataka kurejea nyumbani, lakini ana shaka kama hilo litawezekana kwani amesikia kuwa kijiji chake sasa kimegeuzwa kuwa kambi ya wanamgambo waliofanya shambulio hilo.

Anasema kuwa kiongozi wa waporaji wa eneo hilo ndiye anayeshikilia mamlaka halisi, na familia humwendea ili kutatua migogoro ya kifamilia.

Fatima anasema kijiji kingine cha karibu "kiko tupu kabisa, hakuna hata kuku anayeishi huko... vijiji vingi visivyo na watu kama hivyo vipo."

"Hata ukirudi eneo letu, utakumbana na matatizo tu. Hakuna kitu huko, hakuna chakula... unalima, lakini unapokwenda kuvuna, wanakuzuia au kukuteka nyara."