Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanaume wanaotumia majina ya ukoo wa mama zao nchini Kenya wanavyokabiliana na kejeli
Watoto wengi nchini Kenya wamekuwa wakirithi jina la kwanza la baba yao na kulitumia kama jina la ukoo, lakini kuna ongezeko la watu wanaopewa au kutumia jina la mama kama jina lao la ukoo.
Hali hii imeenea sana miongoni mwa jamii kubwa zaidi nchini Kenya, ya Wakikuyu, na limekuwa suala la mjadala. Baadhi ya wanaume wenye majina ya ukoo ya mama zao wamekuwa wakidhihakiwa.
Wasichana na wanawake waliopewa majina ya mama zao hawakabiliwi na ukosoaji huo. Mara nyingi wanapoolewa wanaweza kuchagua kutumia jina la kwanza la waume zao kama jina la ukoo.
Baadhi ya watu wanasema kuongezeka kwa wanaume wenye majina ya ukoo ya kina mama kunaonyesha mabadiliko katika mtazamo kuhusu nafasi ya wanawake na ushawishi wao katika jamii ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ya mfumo dume.
Wengine, huwakosoa wale waliopewa majina hayo au wale wanaochagua kuyatumia kwa hiari.
Zamani ilikuwa nadra kuwaona wanaume wenye majina ya ukoo ya wa upande wa mama zao wakishikilia nyadhfa maarufu, lakini sasa kuna hata baadhi ya wanasiasa wenye majina hayo kama vile Mbunge John Njũgũna Wanjikũ.
Akiwa amelelewa na mama yake pekee, alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2021 kuwa mbunge na anajulikana kwa jina la utani "Ka-Wanjikũ", linalomaanisha mtoto wa Wanjikũ.
Baadhi ya watu kama Wanjikũ walipewa jina la mama yao tangu kuzaliwa, huku wengine wakichagua kutumia majina hayo kwa heshima ya mama zao.
Mmoja wa watangulizi kuvunja desturi hiyo kuhusu majina ya ukoo ya wanaume alikuwa Peter Kĩgia, mwanamuziki wa Kenya ambaye alichagua jina la mama yake kama jina lake la kisanii.
Kĩgia wa Esther (mwana wa Esther), ambaye sasa ana umri wa zaidi ya miaka 60, anajulikana kwa kucheza muziki wa benga, aina ya muziki wa gitaa wenye mdundo wa kasi, kwa lugha ya Kikuyu.
"Unapochukua jina la mama yako, ina maana unampenda na kumheshimu," aliiambia BBC, akisema hata alisajili kampuni yake ya kurekodi muziki kwa jina la Wa Esther Productions.
Suala hili limeanza kupewa thamani fulani katika tasnia ya muziki, huku wanamuziki wengine wachanga wakifuata nyayo zake. Mabango ya matangazo ya wasanii wenye majina ya ukoo ya mama zao, kama vile Waithaka wa Jane na 90K Ka Msoh, mara nyingi huonekana kwenye mabango na maeneo ya matangazo jijini Nairobi.
Hata hivyo, katika visa hivi majina rasmi ya wasanii hao bado hubaki kuwa ya kiume
Mwanahabari Simon Macharia Wangũi aliiambia BBC kwamba aliamua kwa makusudi kutumia jina la mama yake kama jina lake rasmi la ukoo.
"Kwa nini kumpa mtu sifa ambayo hastahili?" alisema akimzungumzia baba yake, ambaye hakuwepo katika sehemu kubwa ya maisha yake.
Akiwa alilelewa zaidi na bibi yake, mama yake alifariki mwaka wa 2003 alipokuwa na umri wa miaka 12. Hakuwa na jina la ukoo hadi mwaka wake wa mwisho wa shule ya upili, alipokuwa akiomba cheti cha kuzaliwa.
Baadhi ya Wakenya bado wanaamini kwamba mtoto anayelelewa na mzazi mmoja "hukosa maadili fulani", anaeleza Evans Kibe Waceke, mtangazaji mwenye jina la ukoo la mama yake.
"Watu wanakuona kama mtu asiye na nidhamu, hasa unapolelewa na mama au mzazi mmoja," aliiambia BBC.
Mjadala mkali kuhusu faida na hasara za kuwa na jina la ukoo la mama ulianza miaka miwili iliyopita baada ya mzungumzaji maarufu wa kutoa motisha Robert Burale kusema kwamba majina hayo yanadhoofisha uanaume wa mwanaume.
Hilo lilimfanya mtangazaji wa televisheni Fred Mũitĩrĩri kwenda hadharani kueleza changamoto alizopitia kwa kuwa na jina la ukoo wa mama na jinsi alivyoishia kuliacha jina la mama yake, akiamua kutumia majina yake ya kwanza ya Kiingereza na Kikuyu pekee.
"Unajua unaweza kuaibika kama mvulana kuitwa, mbele ya chumba kilichojaa watu, jina la msichana?" aliandika kwenye mtandao wa Facebook, akielezea jinsi jambo hilo lilivyoathiri hali yake katika jamii.
"Kutokana na baadhi ya matukio hayo, nilianza kupata msongo wa mawazo nilipokuwa na umri wa miaka 23," alisema.
Hata hivyo, anaongeza kuwa kupewa jina la ukoo wa mama yako ni jambo lisilo la kawaida kitamaduni.
"Ikiwa mama yako hatakuambia baba yako ni nani au baba huyo anakukataa, kaka mkubwa wa mama yako huchukua nafasi hiyo," aliiambia BBC.
Hata hivyo, Mũkũrũ anaeleza kuwa wakati mwingine kunaweza kuwa na kusitasita kufanya hivyo kwa sababu kumpa mtoto jina la mjomba wake kunampa pia haki ya kurithi mali.
Mũgwe wa Njũhĩ, afisa wa kikundi cha kitamaduni cha Wakikuyu cha Kiama Kĩa Ma, anakubaliana kuwa ndugu wa kiume wa akina mama wasio na waume wanaweza kukataa kumpa mtoto jina lao ili kuepuka migogoro ya urithi.
Lakini pia anasema hakupaswi kuwa na dharau dhidi ya majina ya ukoo wa mama, kwa kuwa kulingana na simulizi za jadi, Wakikuyu hufuata nasaba yao kutoka kwa mabinti 10 wa wanandoa wa kwanza wa jamii hiyo Gikũyũ na Mũmbi.
Wakikuyu mara nyingi huitwa "Nyumba ya Mũmbi", kutokana na mama huyo wa kihistoria wa kizushi anayeaminika kuwa mwanzilishi wa jamii hiyo.
Wa Esther, mwanamuziki mkongwe, anakubaliana kwamba watu kutoka jamii nyingine wanaokosoa matumizi ya majina ya kike na wanaume Wakikuyu, hawaelewi "jinsi wanavyoishi"
Mtaalamu wa masuala ya kitaaluma George Gathigi anaeleza kwamba ingawa wanaume Wakikuyu huenda walikuwa wakijitambulisha kupitia majina ya mama zao kuanzia zamani, jambo hilo lilikuwa likifanyika kwa njia isiyo rasmi. Kutumia rasmi majina ya kike kama majina ya ukoo ni jambo jipya.
Kwa mfano, wakati ndoa za wake wengi zilipokuwa zimeenea zaidi, watoto walikuwa wakitambulishwa kwa majina ya mama zao wanapokuwa katika makundi makubwa ili kuepusha mkanganyiko, kwa sababu pia kitamaduni kulikuwa na idadi ndogo ya majina ya kwanza katika kila familia.
Mwandishi maarufu wa Kenya aliyefariki, Ngũgĩ wa Thiong'o, ambaye baba yake Thiong'o wa Ndūcũ alikuwa na wake wanne, aliandika katika kumbukumbu zake Dreams in a Time of War kwamba, alipokuwa akikua kwa kawaida alijulikana kama Ngũgĩ wa Wanjikũ, Wanjiku ikiwa jina la kwanza la mama yake.
Gathigi, ambaye hufundisha katika Chuo Kikuu cha Nairobi na kutoa maoni kuhusu masuala ya kijamii ya Wakikuyu, anaamini kuwa matumizi ya majina ya ukoo wa mama yanaonyesha "nguvu za wanawake" katika jamii ya kisasa, hasa katika hali ambapo wanaume wamekuwa wakikwepa majukumu yao.
"Utamaduni hubadilika, na sasa lazima tukabiliane na hali halisi ya kisasa," aliiambia BBC, akielezea kuwa wanawake wamezidi kuchukua nafasi ambazo hapo awali zilionekana kuwa za wanaume.
Anafafanua kuwa katika hali kama hizo, ambapo watoto "hawapati faida ya kulelewa na baba yao... mama anakuwa mama na baba kwa wakati mmoja" akiongezea kuwa ni "jambo baya ambalo sasa linafanywa kuwa la kawaida".
Ingawa mwanahabari Wangũi anakubali kwamba si rahisi kila wakati kuwa na jina la ukoo wa mama na kwamba jambo hilo linaweza kuleta aina fulani ya "mgogoro wa utambulisho", anajivunia uamuzi wake.