Traoré na ndoto ya kuifanya dhahabu kuwa injini ya uchumi wa Burkina Faso

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, africa business insider
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Burkina Faso imepata dhahabu yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 6 kupitia njia rasmi katika nusu ya kwanza ya 2026, huku serikali inayoongozwa na jeshi ikizidisha juhudi za kurasimisha uchimbaji madini na kuimarisha usimamizi wa serikali katika moja ya nchi mchimbaji mkubwa wa dhahabu barani Afrika.
Taarifa hiyo ilifichuliwa wakati wa tathmini ya katikati ya mwaka 2026 ya mkataba wa madini, na Waziri wa Nishati, Migodi na Machimbo Yacouba Zabré Gouba, ambapo wizara iliripoti kiwango cha jumla cha utekelezaji wa mkataba ni 61.7% kufikia Juni 30.
Kulingana na serikali, tani 26 za dhahabu safi zilizalishwa na wachimbaji wakubwa nchini humo wakati wa miezi sita ya kwanza ya mwaka. Wakati huo huo, Kampuni ya Kitaifa ya Bidhaa za Thamani (SONASP) ilinunua takriban tani 29 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wale walio na mashine ndogo, huku lengo la mwaka mzima ni tani 45.
Kwa pamoja, wachimbaji wakubwa na wadogo wamekusanya zaidi ya tani 55 za dhahabu iliyopitia katika njia rasmi za uzalishaji na ununuzi za Burkina Faso katika nusu ya kwanza ya 2026.
Kwa bei za soko kiasi hicho kina thamani ya takriban dola bilioni 6 za kimarekani, huku nchi hiyo ikizidi kuwa mzalishaji mkubwa wa dhahabu duniani na nguvu inayoendelea ya bei ya dhahabu, wakati mahitaji yakiongezeka kutokana na vurugu za kijiografia.
Takwimu hizo pia zinaangazia mkakati wa serikali wa kuiweka dhahabu katika uchumi rasmi.
Makampuni makubwa ya uchimbaji madini yanaripoti uzalishaji wao moja kwa moja kwa serikali, dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wale wanaotumia mashine ndogo hununuliwa na SONASP, na hivyo kuruhusu serikali kuboresha ufuatiliaji, kupunguza magendo, kuongeza akiba rasmi na kupata sehemu kubwa ya mapato ya uchimbaji madini.
Mbinu hii inaunda nguzo kuu ya mageuzi mapana ya madini ya Burkina Faso, ambayo inalenga kuimarisha ushiriki wa serikali katika sekta hiyo huku ikikuza uwazi zaidi katika uzalishaji wa dhahabu kwa wachimbaji wakubwa na wadogo.
Mageuzi ya madini

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kama sehemu ya mageuzi chini ya Kanuni mpya ya Madini, mamlaka zilianzisha vyama tisa vipya vya ushirika vya uchimbaji madini katika maeneo tofauti na kuainisha maeneo manne ya uchimbaji madini ili kuboresha shughuli za uchimbaji madini kwa makampuni makubwa na wachimbaji wadogo.
Serikali pia ilisema inaendelea na shughuli za udhibiti, kumimina, kupima na kufungasha dhahabu ili kuimarisha usimamizi wa uzalishaji wa kitaifa, huku ikiimarisha juhudi za kuvunja mitandao haramu ya biashara ya dhahabu.
Mamlaka inasema kazi hiyo inaendelea kuboresha maarifa ya kijiolojia kuhusu rasilimali za madini za Burkina Faso na miradi ya maendeleo inayosimamiwa na Kampuni ya Ushiriki wa Madini ya Burkina Faso (SOPAMIB), chombo cha uwekezaji wa madini kinachomilikiwa na serikali kilichoundwa ili kupanua ushiriki wa serikali katika sekta hiyo.
Mageuzi hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali ya kijeshi ili kuongeza udhibiti wa serikali juu ya rasilimali za kimkakati za madini, kupunguza magendo na kuhakikisha sehemu kubwa ya mapato ya madini yanabaki ndani ya nchi.
Zaidi ya uchimbaji madini, serikali ilisema imepanua miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mitambo minne ya umeme, mitatu ikiwa ya umeme wa joto, ilikamilishwa wakati wa nusu ya kwanza ya mwaka, na kuongeza jumla ya megawati 126.4 za uwezo wa kuzalisha umeme.
Mamlaka pia ilikamilisha ujenzi wa mtambo wa umeme wa jua wa Zagtouli wenye megawati 17, huku mitambo ya umeme ya Komsilga na Donsin ikikaribia kukamilika.
Maendeleo haya yanakuja huku Burkina Faso ikilenga kuimarisha usalama wake wa nishati na sekta ya madini, nguzo mbili ambazo serikali imezitambua kuwa ni muhimu katika kufikia uhuru wa kiuchumi huku kukiwa na changamoto za usalama zinazoendelea na mazingira ya kijiografia yanayobadilika katika Sahel.















