Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, risiti unazobeba kila siku zinaweza kuathiri uwezo wa kupata watoto?
- Author, • Kate Bowie
- Nafasi, Global Health reporter
- Akiripoti kutoka, London
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa wengi wetu, risiti ni kitu tunachoweka tu kwenye mifuko yetu baada ya kulipia bidhaa za dukani na mahitaji mengine. Lakini kwa wengine, kuna wasiwasi kwamba risiti hizi zinaweza kuwa na madhara kwa afya.
Katika miezi ya hivi karibuni, mitandao ya kijamii imejaa video zinazoangazia kuhusu hatari za risiti, zikiwemo kauli kama "Kugusa risiti kunaweza kuathiri uwezo wako wa kupata watoto siku zijazo" na "Risiti hizi zinaweza kuharibu maisha yako."
Takriban machapisho 2,500 kwenye TikTok yanatumia kipande maarufu cha sauti chenye mtu akisema, "Niligusa risiti." Wageni kwenye podcast ya Diary of a CEO, ambayo ina hadhira kubwa duniani kila mwezi, pia wameeleza wasiwasi kuhusu suala hilo.
Machapisho hayo mara nyingi yanadai kuwa kuathiriwa na kemikali zilizo kwenye risiti kunaweza kusababisha ugumba, kuvuruga afya ya homoni na kupunguza kiwango cha testosterone.
Kwa nini basi risiti hizi ndogo zinachukuliwa kuwa vitu vinavyopaswa kushughulikiwa kwa tahadhari?
Hii ni kwa sababu kwa kawaida risiti huchapishwa kwenye karatasi ya joto (thermal paper) ambayo hupakwa kemikali, mara nyingi ikiwemo bisphenol A (BPA).
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaitambua BPA kama kemikali inayoweza kuvuruga mfumo wa homoni. Tafiti zimehusisha kuathiriwa na BPA na mabadiliko katika utendaji wa homoni pamoja na uwezekano wa matatizo ya afya ya uzazi, ingawa kiwango ambacho madhara haya hutokea kutokana na mfiduo wa kawaida wa kila siku bado kinaendelea kuchunguzwa.
Hata hivyo, wanasayansi waliiambia BBC World Service kwamba kuna ushahidi unaoonyesha kuwa wanunuzi hawapaswi kuingiwa na hofu.
BPA iliyo kwenye risiti ni nini, na inaweza kuathiri vipi uwezo wako wa kupata watoto?
Risiti zimekuwa zikichapishwa kwa kutumia BPA tangu miaka ya 1960. Kemikali hiyo pia imetumika katika kutengeneza baadhi ya chupa za plastiki za maji na makopo ya vyakula.
Printa za kisasa za risiti hutumia joto badala ya wino. Kemikali iliyopakwa kwenye karatasi huguswa na joto kali kutoka kwenye printa, na kubadilisha rangi ya karatasi kuwa nyeusi, hivyo kuruhusu herufi na namba kuchapishwa papo hapo. Kwa kawaida, kemikali hiyo ilikuwa na BPA au kemikali zinazofanana nayo.
Hata hivyo, majaribio ya maabara yaliyotumia tishu za korodani za binadamu yameonyesha kuwa BPA inaweza kupunguza uzalishaji wa testosterone.
Tafiti nyingine pia zimeonyesha uhusiano kati ya kuathiriwa na kemikali hizi wakati wa ujauzito na matatizo ya ukuaji wa mfumo wa uzazi kwa watoto wa kiume.
Profesa Shanna Jayasena, mshauri wa masuala ya homoni za uzazi katika hospitali za St Mary's na Hammersmith jijini London, anasema idadi inayoongezeka ya wagonjwa katika kliniki za uzazi ina wasiwasi kuhusu suala hili.
"Wanandoa wengi wana wasiwasi mkubwa kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu afya zao. Wanataka kusafisha na kuondoa sumu mwilini, jambo ambalo linaweza kuwafanya kujaribu kuepuka plastiki," alisema.
Anakubaliana na kuongezeka kwa ushahidi unaoonyesha kuwa kemikali zinazovuruga mfumo wa homoni, kama BPA, zinaweza kuathiri uwezo wa uzazi.
Lakini mtaalamu huyo anasema tafiti hizi bado zinaacha maswali muhimu bila majibu, ikiwemo ni kiwango gani cha BPA ambacho mtu anapaswa kuathiriwa nacho kabla ya madhara ya kiafya kuanza kujitokeza.
"Kwa mtazamo wangu, ushahidi unaonyesha kemikali hizi zina uwezo wa kuathiri afya, ingawa bado kuna maswali kuhusu kiwango cha mfiduo kinachoweza kusababisha madhara kwa binadamu."
Tafiti mbalimbali zinasema nini kuhusu BPA kwenye risiti?
Utafiti wa mwaka 2014 ulionyesha kuwa BPA inaweza kufyonzwa kupitia ngozi, na kwamba kugusa risiti baada ya kutumia vitakasa mikono kulionekana kuongeza kiwango cha BPA kinachoingia mwilini.
Hata hivyo, suala muhimu si kemikali yenyewe pekee, bali ni kiasi kinachoingia mwilini, anasema Profesa Oliver Jones, mtaalamu wa kemia kutoka RMIT University mjini Melbourne, Australia.
Alilinganisha hali hiyo na unywaji wa pombe akisema:
"Ukinywa glasi moja ya divai, huenda isiwe na athari kubwa. Lakini ukinywa chupa nzima kila usiku kwa mwaka mzima, bila shaka itakuwa na athari."
Kwa sababu hiyo, alisema kuna uwezekano mdogo kwamba kiasi kidogo cha BPA kutoka kwenye risiti moja kinaweza kuwa na athari yoyote kwa afya yako.
"Kwa kusema kweli, nafikiri unaweza hata kula risiti nzima, na bado isingekuwa na kiwango cha kutosha cha kemikali hiyo iliyokolea kukusababishia matatizo," aliongeza.
Profesa huyo alikuwa akieleza kwamba kiwango cha BPA ambacho mtu hupata kutokana na risiti moja kinaaminika kuwa kidogo sana.
Lakini vipi kuhusu wahudumu wa maduka na makarani wanaoshughulika na risiti mara nyingi zaidi kuliko mtu wa kawaida?
Profesa wa Endocrinology, Shanna Jayasena, alisema:
"Sioni ongezeko la makarani wakikimbilia kliniki za uzazi."
Hata hivyo, alibainisha kuwa tafiti zaidi zinahitajika ili kubaini iwapo kuathiriwa na kemikali zinazovuruga homoni kwa muda mrefu au kwa kiwango kikubwa, hasa kazini, kunaweza kuwa na athari inayoweza kupimika kwenye uwezo wa uzazi.
Licha ya wataalamu hao kutoa maelezo hayo, risiti zenye BPA zimepigwa marufuku katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Uingereza. Japan na Korea Kusini pia zimeanza kuachana na matumizi ya risiti hizo.
Katika nchi hizo, biashara nyingi zimebadilisha na kutumia risiti zilizotengenezwa kwa bisphenol S (BPS), ambayo Profesa Jones anasema "inafanana tu na ile ya awali."
"Kitaalamu, [BPS] inaweza kuwa na hatari zaidi kwa sababu hatuna ushahidi mwingi unaoiunga mkono kama tulio nao kuhusu BPA. Lakini kwa ujumla, bado ninaona hatari yake kuwa ndogo," aliongeza.
Je, unapaswa kuepuka kugusa risiti kama tahadhari?
Ikiwa bado una wasiwasi, basi punguza kushika risiti kwa kuvaa glovu au kuchagua kutumiwa risiti kwa barua pepe.
"Ikiwa hilo linakufanya ujisikie vizuri na kupunguza msongo wa mawazo, basi fanya hivyo " Profesa Jones alisema.
Profesa Jayasena alisema kwamba ikiwa una wasiwasi kuhusu kuathiriwa na BPA, kuna mabadiliko mengine ya mtindo wa maisha ambayo yanaungwa mkono zaidi na ushahidi wa kisayansi.
Kuepuka kutumia tena au kupasha moto vyombo vya plastiki vya chakula cha kuchukua, ambavyo mara nyingi havitakiwi kuwekwa kwenye microwave, ni hatua nzuri ya kuanzia.
"Ikiwa unataka kuboresha uwezo wako wa uzazi au kupata watoto wenye afya, au kuzuia mimba, mambo muhimu zaidi unayoweza kufanya ni kuacha kuvuta sigara, kunywa pombe kwa kiasi, kufanya mazoezi na kudumisha uzito unaofaa kulingana na urefu wako," aliongeza.
Ingawa BPA imehusishwa na matatizo ya kiafya yanayohusiana na homoni katika baadhi ya tafiti, wataalamu wanasema kwa sasa hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kwamba kushika risiti za kawaida kunaweka watu wengi katika hatari kubwa ya matatizo ya uzazi. Utafiti kuhusu madhara ya muda mrefu ya kemikali zinazovuruga mfumo wa homoni bado unaendelea.
"Kuna mambo mengi tunayoweza kuyadhibiti, na kuna mambo mengi ambayo tuna uhakika yana athari halisi kwenye afya yetu ya uzazi, lakini risiti si mojawapo ya mambo hayo."