Je, kutakuwa na uvamizi wa Marekani?: Hatima ya Cuba ni nini baada ya mashtaka dhidi ya Raúl Castro

Wahamiaji wengi wa Cuba nchini Marekani wanatumaini kwamba serikali ya Havana itaangushwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Marekani imeimtuhumu rais wa zamani wa Cuba, Raúl Castro, mwenye umri wa miaka 94, kwa mauaji, jambo lililochochea uvumi kwamba Havana inaweza kuwa shabaha inayofuata katika orodha ya Washington ya kubadilisha tawala.

Katikati ya kampeni ya "shinikizo la juu zaidi" ambayo imesababisha uhaba mkubwa zaidi wa mafuta na umeme nchini Cuba kwa miongo kadhaa, maafisa wa Marekani wanaendelea kutoa wito wa kukomeshwa kwa serikali ya kikomunisti ambayo imekuwa madarakani visiwani humo kwa miaka 66.

Ingawa Rais Donald Trump amesema anaamini kuwa hakutakuwa na haja ya "kuongeza mzozo," Ikulu ya White House pia imeonya kuwa haitavumilia "dola potovu" iliyo umbali wa kilomita 144 kutoka pwani ya Marekani.

Kinachoweza kutokea baadaye hakijulikani. BBC inaeleza njia tatu zinazowezekana ambazo mgogoro wa Cuba unaweza kuendelea nazo.

1. Marekani inaweza kumkamata Raúl Castro

Ingawa Raúl Castro bado ana ushawishi mkubwa na ana uzito mkubwa wa kisiasa na kihistoria, kukamatwa kwake hakuwezi kulazimu kuimaliza serikali ya Cuba.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mashtaka dhidi ya Raúl Castro, yaliyotokana na tukio la mwaka 1996 ambapo ndege za kijeshi za Cuba zilidungua ndege mbili za kiraia, mara moja yalichochea uvumi kwamba majeshi ya Marekani yanaweza kuanzisha operesheni ya kumkamata na kumfikisha mahakamani nchini Marekani.

Operesheni kama hiyo isingekuwa ya kwanza katika historia.

Mnamo Januari, vikosi maalum vya Marekani vilifanya operesheni ya haraka nchini Venezuela kumkamata Rais Nicolás Maduro, mshirika wa muda mrefu wa Cuba, na kumhamishia mjini New York kukabiliwa na mashtaka ya dawa za kulevya na silaha.

Mnamo mwaka 1989, operesheni kubwa zaidi iliyoitwa Operation Just Cause ilihusisha maelfu ya wanajeshi wa Marekani kuivamia Panama ili kumuondoa na kumkamata kiongozi wa wakati huo wa nchi hiyo, Manuel Noriega.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Rais Donald Trump hadi sasa ameepuka kujibu moja kwa moja maswali kuhusu iwapo anafikiria kufanya operesheni kama hiyo nchini Cuba.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Marekani wamehimiza waziwazi operesheni kama hiyo kufanyika.

Seneta wa Florida, Rick Scott, aliwaambia waandishi wa habari: "Kilichomtokea Nicolás Maduro kinapaswa kumtokea Raúl Castro."

Wataalamu wanasema kuwa, kwa mtazamo wa kijeshi, operesheni ya kumkamata Castro inawezekana, lakini ingekuwa na hatari na changamoto nyingi, ikiwemo umri wake mkubwa na uwezekano wa kuwepo kwa upinzani.

Lakini kumkamata Castro, ambaye aliachana na urais mwaka 2018, huenda hakutakuwa na athari kubwa kwa serikali ya Cuba kwa ujumla, ambayo kwa muda mrefu imemwona kama mtu mwenye ushawishi mkubwa lakini zaidi wa kiishara.

"Sidhani kama hilo litaathiri sana mfumo wa mamlaka nchini Cuba kwa wakati huu. Ana miaka 94," alisema Isacson. "Nasaba ya familia ya Castro ina ushawishi, lakini si kiini cha mfumo walioujenga."

"Lakini kwa sababu za kisiasa za ndani, huenda hilo likaonekana kama ushindi mkubwa," aliongeza. "Watapenda kuiaibisha familia ya Castro na kumweka mmoja wa wanamapinduzi wa awali wa mwaka 1959 gerezani. Lakini thamani ya kimkakati ya jambo hilo ina mashaka."

2. Marekani inaweza kutafuta mabadiliko ya uongozi mjini Havana

Baadhi ya watu wanaamini kwamba Marekani inatarajia kuiga mfano wa Venezuela, ambapo Delcy Rodríguez alichukua madaraka, mjini Havana.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Baadhi ya watu wanaamini kwamba Marekani inatarajia kuiga mfano wa Venezuela, ambapo Delcy Rodríguez alichukua madaraka, mjini Havana.

Uwezekano mmoja ambao umezungumziwa na maafisa wa Marekani akiwemo Donald Trump, ni kwamba uongozi mpya utaibuka mjini Havana.

Kwa mujibu wa wataalamu, mbinu hiyo inaweza kufanana na jinsi Nicolás Maduro alivyobadilishwa na Delcy Rodríguez nchini Venezuela, hali ambayo iliiacha serikali ikiwa bado ipo kwa kiasi kikubwa, lakini sasa ikishughulika moja kwa moja na utawala wa Trump.

Trump amerudia mara kadhaa kusema kuwa tayari yuko katika mawasiliano na watu ndani ya Cuba wanaotarajia msaada kutoka Marekani wakati mgogoro wa uchumi ukiendelea kuwa mbaya zaidi.

"Cuba inaomba msaada, na tutazungumza," aliandika kwenye Truth Social tarehe 12 Mei.

Siku chache baadaye, Mkurugenzi wa CIA, John Ratcliffe, alikutana na maafisa wa Cuba, akiwemo mjukuu wa Castro, Raúl Guillermo Rodríguez Castro, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani Lázaro Álvarez Casas.

"Tutashirikiana na Wacuba... mwisho wa siku lazima wafanye uamuzi. Mfumo wao hauwezi kufanya kazi tena," Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio aliwaambia waandishi wa habari huko Florida, akiongeza kuwa utawala huo unapendelea "makubaliano ya mazungumzo."

Mabadiliko ambayo Marekani inataka yanaweza kujumuisha ahadi ya kufungua uchumi, kuruhusu uwekezaji zaidi wa kigeni na ushiriki wa makundi ya Wacuba walioko uhamishoni, pamoja na kuondoa uwepo wa mashirika ya kijasusi ya Urusi au China kisiwani humo.

Ni muhimu kutambua kwamba mabadiliko hayo yanaweza kuiacha serikali ya Cuba ikiwa bado ipo kwa kiasi kikubwa.

"Kama walivyotaka kuepuka kuyumba kwa Venezuela, wanataka pia kuepuka kuyumba kwa Cuba," alisema Michael Shifter, profesa wa masomo ya Amerika ya Kusini katika Chuo cha Georgetown na mkurugenzi wa zamani wa taasisi ya Inter-American Dialogue yenye makao yake Washington.

"Kulazimisha mabadiliko ya utawala kutakuwa na hatari kubwa mno," aliongeza.

Wataalamu kadhaa waliozungumza na BBC walisema changamoto kwa utawala wa Trump ni kwamba hakuna mtu anayejulikana wazi ndani ya Cuba anayesubiri kuchukua nafasi hiyo kwa siri.

"Sidhani kama kuna Delcy Rodríguez wa wazi nchini Cuba, na mamlaka yanafanya kazi tofauti Cuba kuliko Venezuela," alisema Shifter. "Ni vigumu kujua hasa wanachotafuta, lakini naamini wanatafuta aina fulani ya mfumo mpya wa utawala."

Wacuba wanapitia mgogoro mbaya zaidi katika miongo kadhaa kutokana na uhaba wa mafuta.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Wacuba wanapitia mgogoro mbaya zaidi katika miongo kadhaa kutokana na uhaba wa mafuta.

3. Cuba inaweza kuporomoka

Uwezekano wa tatu ni kwamba Cuba inaweza kuporomoka kutokana na shinikizo kubwa la kiuchumi inaloendelea kukabiliana nalo, ambalo tayari linasababisha kukatika kwa umeme kwa saa kadhaa kila siku na uhaba mkubwa wa chakula kisiwani humo.

"Hatutakuwa na mzozo wa kijeshi. Sidhani ni lazima," alisema Donald Trump. "Sehemu hiyo inasambaratika. Ni janga, na kwa kiwango fulani wamepoteza udhibiti."

Hata hivyo, wataalamu wanaeleza picha iliyo tata zaidi, ambapo mifumo ya udhibiti ya serikali ya Cuba juu ya wananchi wake bado iko imara kwa kiasi kikubwa, licha ya mgogoro wa kiuchumi.

"Ni lazima tutofautishe kati ya uchumi wa Cuba na serikali na dola ya Cuba," alisema Michael Shifter. "Uchumi wa Cuba unaweza kuporomoka, na tayari unaporomoka… lakini serikali inaendelea kufanya kazi, hasa katika eneo la usalama."

Kuporomoka kwa dola kunaweza pia kuwa changamoto kwa utawala wa Trump iwapo idadi kubwa ya Wacuba wangeanza kukimbia nchi, hasa kuelekea Marekani.

Wacuba waliowasili hivi karibuni pia hawajapewa upendeleo mkubwa wa hifadhi ya kisiasa kutokana na vizuizi vya uhamiaji chini ya utawala wa Trump.

"Ikiwa kutatokea kuporomoka, utaona sehemu kubwa ya Wacuba wakijaribu kila njia kutoroka, kama ambavyo Wahaiti wamekuwa wakifanya kwa miaka mingi," alisema Adam Isacson.

"Florida ndio sehemu iliyo karibu zaidi, lakini pia ningetarajia kuona baadhi ya watu wakielekea Mexico."

Isacson aliongeza kuwa alishangazwa kwamba uhamiaji wa aina hiyo haujaanza tayari.

"Watu huenda wanaishi kwa kalori 1,000 au 1,500 kwa siku na hawawezi kupata huduma za afya za msingi," alisema. "Ungefikiri tayari wangekuwa wanajenga boti zao."