Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Cicada: Aina mpya ya COVID-19 inayoibua maswali duniani ni hatari kiasi gani?
Shirika la Afya Duniani WHO, linafuatilia kwa karibu aina ya virusi vya COVID-19 inayosemekana kuwa hatari na imegunduliwa katika zaidi ya mataifa 23.
Aina hii ya virusi, inayojulikana kama BA.3.2, imeonekana katika mataifa yakiwemo Marekani, Hong Kong, Msumbiji, na Uingereza.
Bado hakuna maelezo ya wazi yanayoeleza kwa nini aina hii inaweza kuwa hatari zaidi kuliko aina nyingine zilizotokea.
Wataalamu wanasema virusi hivyo vinaonekana kuathiri zaidi watoto kuliko watu wazima.
Hii ni aina gani ya virusi?
Aina hii ya BA.3.2 imepewa jina la "cicada" kwa sababu inaishi kwa muda mrefu ikiwa imejificha. Imefananishwa na mdudu aina ya cicada ambaye hukaa chini ya ardhi kwa miaka mingi bila kuonekana.
Mwezi uliopita, Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kiliripoti kuwa visa vya virusi hivyo vimegunduliwa katika majimbo 25 ya Marekani.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa virusi vya BA.3.2 vilipatikana katika sampuli za pua zilizochukuliwa kutoka kwa wasafiri wanne, na sampuli 132 za maji machafu.
Shirika la Afya Duniani limeorodhesha aina hii ya virusi katika kundi la "aina zinazofuatiliwa," likisema inahitaji "umakini wa hali ya juu" na kwamba wataalamu wanapaswa kuchunguza kwa karibu ikiwa inaweza kusababisha hatari ya kimataifa.
Ryan Heissner, mtafiti anayechunguza aina za COVID katika jiji la New York, amesema kuwa watoto wanaweza kuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuambukizwa na aina hii ya BA.3.2 kuliko watu wazima.
Profesa Ravindra Gupta, profesa katika Taasisi ya Cambridge, amesema kuwa athari za virusi"bado hayajachunguzwa vizuri wala kuthibitishwa kikamilifu, lakini yanaonekana kuwa na msingi fulani."
Moja ya maelezo aliyotoa ni kwamba mfumo wa kinga ya mwili wa binadamu hautambui vizuri aina hii ya "cicada" kwa sababu haujawahi kukumbana nayo.
Gupta alieleza kwamba,"Kwa ujumla, watoto wana kinga ya mwili iliyo chini zaidi ukilinganisha na watu wazima kwa sababu hawajawahi kukutana na vimelea vingi vya magonjwa kama COVID-19, hivyo ulinzi wao dhidi ya virusi hivi pia huwa mdogo."
Dalili za ugonjwa huu ni zipi?
Hadi sasa, hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa aina ya "cicada" husababisha ugonjwa mkali zaidi kuliko aina nyingine za virusi vya COVID-19.
Paul Hunter, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza kutoka Chuo Kikuu cha East Anglia nchini Uingereza, amesema, "Hakuna dalili maalum zinazoitofautisha wazi aina hii mpya."
COVID-19 huhusishwa na dalili kama vile homa, kikohozi, maumivu ya koo, kuziba kwa pua, uchovu mkali, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili mzima, kupumua kwa shida, na kuharisha.
Kwa nini aina hii mpya imebadilika sana?
Virusi vyote hubadilika kadri muda unavyokwenda, na virusi vya RNA kama COVID-19 hubadilika kwa kasi zaidi.
Kituo cha Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kinaeleza kwamba aina ya BA.3.2 "inatofautiana sana kijenetiki," ikimaanisha ina tofauti zinazoonekana ukilinganisha na aina za awali za Omicron.
Je, chanjo ya Covid bado inafanya kazi?
Mabadiliko ya virusi yanaweza kufanya chanjo za COVID-19 zisitoe ulinzi kikamilifu dhidi ya maambukizi ya aina ya "cicada". Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa bado zinatoa kiwango fulani cha kingo
Kwa mujibu wa WHO, 67% ya watu duniani tayari wamepokea angalau dozi moja ya chanjo ya COVID-19.
Hata hivyo, chanjo zilizoboreshwa zinazolenga aina mpya za virusi hazipatikani kwa wingi katika maeneo yote ya dunia.
Je, kuna sababu ya kuwa na hofu?
Paul Hunter mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza anasema si jambo la kushangaza kuona aina mpya za COVID-19 zikiendelea kuibuka.
Anaeleza kuwa "Ilimradi watu bado wapo duniani, tutaendelea kuona virusi vikibadilika na kujitokeza katika aina mpya. Sidhani kama virusi vya Covid vitaweza kutokomezwa kabisa."
Anasisitiza kuwa ongezeko la visa vya "cicada" halimaanishi moja kwa moja kwamba maambukizi au vifo vitaongezeka pia.
Mwezi Disemba, WHO ilitangaza kuwa hakuna ushahidi wa ongezeko la wagonjwa mahututi, waliolazwa hospitalini au vifo vinavyosababishwa na aina ya "cicada," jambo linaloonyesha kuwa ina athari ndogo kwa afya ya umma.