Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump aongeza muda wa kusitisha mapigano Iran

Hatua ya Rais wa Marekani, Donald Trump kukubali kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran bila kikomo maalum inatajwa kuwa ni mabadiliko makubwa ikilinganishwa na msimamo wake wa saa chache zilizopita.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Iran haijaamua kushiriki duru ijayo ya mazungumzo na Marekani - Msemaji

    Kabla ya Donald Trump kutangaza kwamba ataongeza muda wa kusitisha mapigano, wizara ya mambo ya nje ya Iran iliiambia BBC kwamba Tehran bado haijaamua kama itahudhuria duru mpya ya mazungumzo ya amani na Marekani baadaye wiki hii.

    Katika mahojiano na mwandishi wa kimataifa wa BBC Lyse Doucet, msemaji Esmail Baghaei alisema Iran imeingia katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya Islamabad "kwa nia njema na hisia ya uzito, lakini kuna upande wa mazungumzo umeonyesha kukosa umakini na nia njema".

    Aidha alitaja "mapumziko yasiyo na maana, vitisho vya uhalifu wa kivita" kutoka kwa Marekani akirejelea mfululizo wa machapisho na mahojiano ya Trump kwenye mitandao ya kijamii katika siku mbili zilizopita, ambapo alitishia tena “kuharibu kila kituo cha umeme na kila daraja” ikiwa Iran haitakubali kile alichokiita pendekezo la Marekani “la haki na lenye busara sana.”

    White House ilithibitisha Jumanne usiku kuwa safari ya makamu wa rais JD Vance kwenda Pakistan kwa ajili ya duru ya pili ya mazungumzo ya amani imefutwa.

  2. Kufungwa kwa Mlango wa Hormuz kwaongeza uhitaji wa mafuta Marekani - Wataalamu

    Kupitia chapisho kwenye jukwaa la mtandao wa Truth Social Jumatatu usiku, Rais Donald Trump alisema uongozi wa Iran "umelazimisha mamia ya meli" kuelekea majimbo yenye utajiri wa mafuta ya Marekani, kama vile Texas, Louisiana, na Alaska.

    Ingawa haijulikani ni aina gani ya meli alizokuwa akizirejelea, wachambuzi wa meli na biashara wanaiambia BBC Verify kwamba hatua ya Iran kufunga Mlango Bahari wa Hormuz imesababisha ongezeko la uhitaji wa mafuta ghafi nchini Marekani.

    Hatua hiyo ni kikwazo kikubwa cha usafirishaji wa mafuta ya Ghuba, lakini usafirishaji umevurugika zaidi tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran mnamo Februari 28.

    Kwa kuwa hawawezi kupata mafuta ghafi kutoka Mashariki ya Kati kupitia mlango huo, waagizaji wamelazimika kutafuta wauzaji mbadala.

    Data kutoka kwa kampuni ya ufuatiliaji wa safari za bahari Kpler inaonyesha kuwa meli 71 za mafuta zinazojulikana kama Very Large Crude Carriers (VLCCs) zinaelekea Marekani kuchukua mizigo ikilinganishwa na wastani wa meli 27 kwa siku katika kipindi cha mwaka jana.

  3. Majadiliano na Marekani hayana mantiki kwa sasa – Iran

    Mahmoud Nabavian, mbunge wa Iran ambaye alikuwa sehemu ya ujumbe katika duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani huko Islamabad, ameeleza kupitia mtandao wa X kwamba "kuanzia sasa", kujadiliana na Marekani ni "jambo la hatari na lisilo na mantiki".

    Kando na hayo, msemaji wa makao makuu ya Khatam al-Anbiya ya Iran, kamandi kuu ya kijeshi ya Iran, ameonya kwamba vikosi vya Iran, iwapo kutakuwa na shambulio dhidi ya Iran, "vitashambulia maeneo yaliyopangwa awali na kutoa somo, hata kali zaidi" kwa Marekani na Israeli.

    Katika chapisho la Nabavian na taarifa ya Khatam al-Anbiya, hakukutajwa muda wa kusitisha mapigano, ingawa vyote viliripotiwa na vyombo vya habari vya Iran baada ya tangazo la Donald Trump.

    Bado Iran haijatoa kauli yoyote kupitia wizara ya mambo ya nje ya Iran au maafisa wake, au kutoka kwa msemaji mkuu wa bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf.

  4. Waziri mkuu wa Pakistan amshukuru Trump kwa kuongeza muda wa kusitisha mapigano

    Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif amemshukuru rais wa Marekani Donald Trump baada ya kutangaza kuongeza muda wa kusitisha mapigano kwa muda usiojulikana muda mfupi kabla ya muda wa awali kuisha.

    "Ninamshukuru Rais Trump kwa dhati kwa kukubali ombi letu la kuongeza muda wa kusitisha mapigano ili kuruhusu juhudi zinazoendelea za kidiplomasia kuchukua mkondo wake," anasema katika taarifa ya mtandaoni.

    "Kwa imani na imani iliyopo, Pakistan itaendelea na juhudi zake za dhati za utatuzi wa migogoro kwa mazungumzo," taarifa hiyo inaongeza.

    "Ninatumai kwa dhati kwamba pande zote mbili zitaendelea kuzingatia usitishaji mapigano na kuweza kuhitimisha 'Makubaliano ya amani' kamili wakati wa duru ya pili ya mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Islamabad kwa ajili ya kukomesha kabisa mgogoro huo."

  5. Trump aongeza muda wa kusitisha mapigano Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump anasema Marekani itaongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran, kwa ombi la Pakistan, na kuendelea na vizuizi vya kijeshi katika bandari za Iran.

    Tangazo la Donald Trump kwamba amekubali kuongeza muda wa kusitisha mapigano na Iran bila kikomo maalum ni mabadiliko makubwa ikilinganishwa na msimamo wake wa saa chache zilizopita.

    Trump alisema kupitia mitandao ya kijamii "kwa kuzingatia kwamba serikali ya Iran imegawanyika sana, jambo ambalo halikutarajiwa kuwa tofauti, na kufuatia ombi la Field Marshal Asim Munir pamoja na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif wa Pakistan, tumeombwa kusitisha shambulio letu dhidi ya nchi ya Iran hadi wakati ambapo viongozi wao na wawakilishi wao wataweza kuwasilisha pendekezo la pamoja"

    Aliongeza; "kwa hiyo, nimeelekeza jeshi letu kuendelea na zuio, na katika mambo mengine yote, liendelee kuwa tayari kikamilifu. Hivyo basi, nitaongeza muda wa kusitisha mapigano hadi pendekezo lao litakapowasilishwa na mazungumzo kukamilika, kwa namna yoyote ile.”

    Awali akizungumza na CNBC, Trump alisema “natarajia tutakuwa tunashambulia” na kwamba jeshi lilikuwa “tayari kabisa kuanza.” Aidha alirejea tishio lake la kuharibu madaraja yote na mitambo ya umeme nchini Iran.

    Hata hivyo, saa chache kabla ya muda wa awali wa kusitisha mapigano kuisha, amekubali kusitisha mapigano kwa muda usio na kikomo. Katika kipindi chote cha mgogoro huu, Trump amejaribu kutumia vitisho dhidi ya serikali ya Iran kwa matamshi makali. Sasa inaonekana dhahiri hataki kuanza tena kuhusu mashambulizi dhidi ya Iran.

  6. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Aprili 22, 2026