Iran haijaamua kushiriki duru ijayo ya mazungumzo na Marekani - Msemaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Kabla ya Donald Trump kutangaza kwamba ataongeza muda wa kusitisha mapigano, wizara ya mambo ya nje ya Iran iliiambia BBC kwamba Tehran bado haijaamua kama itahudhuria duru mpya ya mazungumzo ya amani na Marekani baadaye wiki hii.
Katika mahojiano na mwandishi wa kimataifa wa BBC Lyse Doucet, msemaji Esmail Baghaei alisema Iran imeingia katika duru ya kwanza ya mazungumzo ya Islamabad "kwa nia njema na hisia ya uzito, lakini kuna upande wa mazungumzo umeonyesha kukosa umakini na nia njema".
Aidha alitaja "mapumziko yasiyo na maana, vitisho vya uhalifu wa kivita" kutoka kwa Marekani akirejelea mfululizo wa machapisho na mahojiano ya Trump kwenye mitandao ya kijamii katika siku mbili zilizopita, ambapo alitishia tena “kuharibu kila kituo cha umeme na kila daraja” ikiwa Iran haitakubali kile alichokiita pendekezo la Marekani “la haki na lenye busara sana.”
White House ilithibitisha Jumanne usiku kuwa safari ya makamu wa rais JD Vance kwenda Pakistan kwa ajili ya duru ya pili ya mazungumzo ya amani imefutwa.




