Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Shambulio baya dhidi ya harusi Iran huenda lilisababishwa na kombora la Marekani - Reuters

Shirika la habari la Reuters liliripoti katika taarifa ya kipekee kwamba, kulingana na uchambuzi wa wataalamu wa silaha waliochunguza picha na video zilizothibitishwa na shirika hilo, mlipuko huo ulisababishwa na kombora la Marekani

Muhtasari

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu

  1. DR Congo yaahhidi kuhamisha ubalozi wake wa Israel mjini Jerusalem

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza siku ya Alhamisi kuwa itahamishia ubalozi wake nchini Israel hadi Jerusalem, ikijiunga na kundi dogo la nchi, ikiwemo Marekani, katika kuchukua hatua hiyo yenye uzito wa kidiplomasia ya kuunga mkono mamlaka ya Israel juu ya mji huo mtakatifu wenye utata.

    Kufuatia ziara ya Rais Felix-Antoine Tshisekedi, nchi hizo mbili zilisema katika taarifa kuwa zitachukua hatua za "kuhamisha ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem", bila kutaja muda maalum wa kufanyika kwa hatua hiyo.

    Taarifa hiyo ilieleza kuwa, katika mkutano wao, Tshisekedi na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu walizungumzia "nia yao ya pamoja ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia".

    Soma pia:

  2. Netanyahu atishia kuipindua serikali ya Iran

    Waziri Mkuu nchini Israel Benjamin Netanyahu amesema siku ya Alhamisi kuwa kuuangusha utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ni jambo "linalowezekana kufikiwa," akisisitiza kuwa utawala huo ni dhaifu kuliko wakati wowote ule na unapambana ili kusalia madarakani.

    Katika hafla iliyohusisha viongozi wa kijeshi, aliongeza kuwa anaamini inawezekana "kuondoa" kabisa tishio la Iran, akilitaja hilo kuwa ndilo jukumu kuu linaloikabili Israel bado.

    Netanyahu amesema kuwa hatua ya Iran kutolenga Israel katika mzunguko wa hivi karibuni wa mashambulizi haikuwa bahati mbaya, akiongeza kuwa Tehran inafahamu vyema nguvu, silaha, na azimio la Israel.

    Netanyahu anajiandaa kushiriki katika uchaguzi wa bunge wenye ushindani mkali mwishoni mwa mwezi wa Oktoba.

    Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yisrael Katz, alisema nchi yake iko tayari kujibu "kwa nguvu kubwa" iwapo Iran itashambulia wakati wa sikukuu za Kiyahudi, zinazoanza katikati ya mwezi wa Septemba, akibainisha kuwa Iran ililenga maeneo mbalimbali katika eneo hilo, isipokuwa Israel, wakati wa mzozo huo wa hivi karibuni.

    Soma pia:

  3. Mamlaka na wakaazi wapambana kuzima moto Mlima Kilimanjaro

    Mamlaka na wakazi wa kaskazini mwa Tanzania wanapambana kuzima moto unaowaka kwenye miteremko ya Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika.

    Moto huo unateketeza eneo lililoko katika mwinuko wa takriban mita elfu tatu na mia nne juu ya usawa wa bahari.

    Afisa wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania ameiambia BBC kwamba bado haijafahamika kilichosababisha moto huo kuwaka.

    Mlima Kilimanjaro, ambao ni muhimu kwa bioanuwai na utalii, umekumbwa na visa vingine vikubwa vya moto wa nyika viliyosababisha uharibifu katika miaka ya hivi karibuni.

    Mwaka 2023, moto uliodumu kwa takriban wiki moja uliharibu eneo la kilomita 17 za mraba, sawa na takriban asilimia moja ya eneo la hifadhi ya mlima huo.

  4. Korea Kusini inajitayarisha kutuma askari kwenye Mlango Bahari wa Hormuz

    Vyombo vya habari vya Korea Kusini vimeripoti kwamba serikali ya nchi hiyo inajiandaa kupeleka vifaa na vikosi vya kijeshi ili kuunga mkono kile kinachoitwa "uhuru wa urambazaji katika Mlango-Bahari wa Hormuz" na inapanga kuanza misheni hii kabla ya mwisho wa mwaka huu.

    Reuters iliandika Alhamisi (Septemba 3) kwamba ripoti katika vyombo vya habari vya Korea Kusini, zikinukuu vyanzo vya serikali na kijeshi, zilisema Seoul inachukua hatua muhimu za kisheria ili kupata idhini ya bunge kwa ajili ya kupelekwa huko.

    Kulingana na ripoti hizi, baada ya kukagua mpango huo katika Baraza la Mawaziri, serikali inapanga kuwasilisha ombi rasmi la idhini ya bunge mwezi huu.

    Uwezekano wa kupelekwa kwa vikosi vya Korea Kusini unakuja huku mvutano wa usalama katika Mlango-Bahari wa Hormuz na mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara yakiongezeka katika wiki za hivi karibuni, na nchi kadhaa zinachunguza njia za kushiriki katika kulinda usalama wa meli katika njia hii ya kimkakati ya maji.

    Maafisa wa serikali ya Korea Kusini bado hawajajibu rasmi ripoti hizi.

  5. Shambulio baya dhidi ya sherehe ya harusi nchini Iran huenda lilisababishwa na kombora la Marekani - Reuters

    Shirika la habari la Reuters liliripoti katika taarifa ya kipekee kwamba, kulingana na uchambuzi wa wataalamu wa silaha waliochunguza picha na video zilizothibitishwa na shirika hilo, mlipuko uliolenga sherehe ya harusi katika mji wa Kohstak kusini mwa Iran siku ya Jumanne, ambao uliua watu watano na kujeruhi angalau 68, una uwezekano mkubwa wa kusababishwa na shambulio la moja kwa moja la silaha ya Marekani, badala ya athari isiyo ya moja kwa moja au kuruka kwa silaha hiyo baada ya kugonga lengo jingine.

    Katika ripoti hiyo iliyochapishwa Alhamisi, Septemba 3, Reuters iliandika: "Reuters iliwasilisha picha na video za shambulio hilo kwa wataalamu wanne wa silaha.

    Wataalamu hao walisema kuwa namna uharibifu ulivyotokea inaashiria shambulio la moja kwa moja la silaha moja, na si mlipuko uliosababishwa na silaha hiyo kuruka kwingine baada ya kugonga lengo jingine."

    Watatu kati ya wataalamu hao pia waliambia Reuters kwamba "ushahidi uliopo unaonyesha kuwa silaha hizo zina uwezekano mkubwa wa kuwa zimetengenezwa Marekani, na si kombora la ulinzi wa anga la Iran lililopotea njia."

    Gareth Collet, brigedia jenerali mstaafu wa Jeshi la Uingereza na mtaalamu wa kutegua mabomu mwenye shahada ya uzamivu katika uhandisi wa vilipuzi, aliambia Reuters kuwa inawezekana silaha hizo zilikosa tu lengo lake lililokusudiwa.

    Reuters inasema afisa wa Marekani, aliyeomba kutotajwa jina, alithibitisha kuwa Marekani ilifanya shambulio la anga katika eneo la Kohstak usiku wa Jumanne, kwa lengo la kuharibu vifaa vya kijeshi vya IRGC.

    Zaida Soma Hapa:

  6. Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja