Uganda yawakamata zaidi ya raia 200 wa kigeni katika oparesheni ya uhamiaji haramu
Mamlaka nchini Uganda zimewakamata raia 231 wa kigeni katika oparesheni inayoendelea dhidi ya uhamiaji haramu, maafisa wamesema.
Katika oparesheni nyingine iliyofanyika katika kitongoji cha hali ya juu cha mji mkuu, raia 169 wa kigeni walikamatwa na Idara ya kudhibiti Uhamiaji baada ya kupatikana wakiishi ndani ya jengo bila nyaraka halali za uhamiaji.
Waliokamatwa ni raia kutoka Pakistan, Bangladesh, Ethiopia, India, Ghana, Myanmar, Sri Lanka, Malaysia na Cambodia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Simon Peter Mundeyi, amesema oparesheni hizo ni sehemu ya juhudi za serikali za kusimamia sheria za uhamiaji na kuvunja mitandao inayoshukiwa kujihusisha na uhalifu wa mtandaoni.
Wizara hiyo imesema baadhi ya waliokamatwa waliingizwa nchini kwa ahadi za uongo za ajira, huku wengine wakidaiwa kuhusika na shughuli za ulaghai wa mtandaoni.
Katika tukio jingine, maafisa wa uhamiaji katika mji wa Adjumani kaskazini mwa Uganda waliwakamata raia 69 wa Nigeria wanaodaiwa kufanya kazi bila vibali halali na kushiriki shughuli zisizoidhinishwa, ikiwemo kuendesha taasisi ya kidini.
“Watu hawa mara nyingi huingia nchini wakijitambulisha kama wahubiri wa injili, lakini baadaye hugundulika kujihusisha na shughuli zisizo halali,” alisema Mundeyi.
Wachunguzi wanasema mfululizo huo wa ukamataji unaonyesha kuongezeka kwa mitandao ya uhalifu wa mtandaoni inayohusisha raia wa kigeni nchini Uganda.
Mwaka 2020, mamlaka ziliwakamata raia 36 wa China katika operesheni kubwa ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, ambapo zilipatikana simu 3,500, kadi za simu 1,700 pamoja na kompyuta mpakato, modemu na seva.
Maafisa wamesema waliokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria kabla ya kurejeshwa katika nchi zao za asili.
Soma zaidi: