Lavrov aionya Marekani kuhusu kupeleka silaha Ukraine
Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imesema kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, aliiambia Washington iachane na hatua ya kuendelea kupeleka silaha nchini Ukraine wakati wa mkutano na mwenzake wa Marekani, Marco Rubio, mjini Manila Alhamisi, akitaja hatua hiyo kuwa "isiyokubalika."
Wizara hiyo ilisema katika taarifa kwamba Bw. Lavrov alimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani: "Kuendelea kutoa silaha kwa Kyiv hakukubaliki."
Katika mkutano huo, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN), Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi pia alikosoa kile alichokiita "sera za kuyumbisha utulivu za nchi za Ulaya," akisema kuwa nchi hizo zinaendelea kutafuta njia za kuisababishia Urusi "kushindwa kimkakati."
Huu ni mkutano wa kwanza rasmi kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Marekani tangu mnamo mwezi Septemba mwaka jana. Mkutano huo ulifanyika wakati ambapo Marekani imehamisha shinikizo lake kutoka upatanishi wa vita vya Ukraine na kuelekeza zaidi juhudi zake katika kushughulikia mgogoro wa vita vya Mashariki ya Kati.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza katika taarifa fupi kwamba Bw. Rubio na Sergey Lavrov walijadili "uhusiano kati ya Marekani na Urusi pamoja na umuhimu wa kumaliza vita vya Urusi na Ukraine."
Kwa mujibu wa taarifa ya Moscow, Bw. Lavrov alisisitiza tena kwamba Urusi iko tayari kufikia "suluhisho la kisiasa na kidiplomasia la mzozo huu."
Mawaziri hao wawili wakuu wa mambo ya nje wako nchini Ufilipino kuhudhuria mkutano wa ASEAN. Pia wanatarajiwa kujadili vita vya Mashariki ya Kati, mgogoro ambao Urusi imezituhumu na kulaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya mshirika wake, Iran.
Soma Zaidi: