Axios: Marekani yatumia ndege ya kivita ya B-1 dhidi ya Iran

Chanzo cha picha, Reuters
Tovuti ya Axios iliripoti, ikinukuu maafisa wa Marekani, kwamba jeshi la Marekani lilitumia ndege ya kivita ya masafa marefu aina ya B-1 siku ya Jumanne (Julai 21) katika shambulio dhidi ya "maeneo ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) nchini Iran."
Kulingana na ripoti hiyo, hii ni mara ya kwanza tangu kuanza tena kwa uhasama na Iran siku kumi na mbili zilizopita ambapo jeshi la Marekani limetumia aina hii ya ndege ya kivita katika operesheni zake.
Axios ilisema ndege hiyo ya B-1 ilianza safari yake ya kijeshi kutoka "kituo cha jeshi la anga nchini Uingereza" na mienendo yake ilionekana kwenye tovuti zinazofuatilia safari za ndege mtandaoni.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa "matumizi ya ndege za B-1, ambazo zina uwezo wa kubeba mabomu 24 yenye uzito wa zaidi ya kilo 900 au makombora mengi ya aina ya 'cruise', yanaashiria kuongezeka kwa kiasi kikubwa na kupanuka kwa wigo wa kampeni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran."
Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) haikutaja matumizi ya ndege hiyo ya B-1 katika taarifa yake ya Jumanne kuhusu mashambulizi yaliyofanyika siku hiyo.
Taarifa ya CENTCOM ilisema kuwa vikosi na vifaa vya kamandi hiyo "vililenga vituo vya operesheni za kijeshi vya Iran, uwezo wa majini, hanga za ndege, vituo vya matengenezo ya ndege zisizo na rubani (droni), na miundombinu ya usafirishaji wa vifaa vya kijeshi ili kudhoofisha zaidi uwezo wa Iran kutishia usafirishaji wa meli za kibiashara katika Mlango-bahari wa Hormuz."
























