Wajumbe wa amani wa Trump kuzuru Moscow na Kyiv
Wapatanishi wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, watazuru Urusi na Ukraine wikendi hii, huku juhudi za kuhitimisha vita zikionekana kushika kasi.
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alithibitisha kuwa atakutana na wajumbe hao siku ya Jumapili, baada ya wao kutembelea Moscow siku ya Jumamosi kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Witkoff na Kushner wameongoza juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump za kufanikisha makubaliano ya amani, lakini bado kuna pengo kubwa kati ya pande hizo mbili zinazopigana. "Wanakuja na pendekezo la kuhitimisha vita," Trump aliwaambia waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu ziara hizo.
Mapema siku ya Ijumaa, Zelensky alisema ndege isiyo na rubani ya Urusi ilishambulia ofisi ya mkuu wa usalama wa Ukraine, Oleksandr Poklad, mjini Kyiv. Poklad anaonekana kuwa salama na hajajeruhiwa.
Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Zelensky alisema amemwagiza Poklad, ambaye anaongoza idara ya usalama ya SBU, kuchukua hatua stahiki kujibu shambulio hilo.
Siku ya Jumamosi, mamlaka za eneo hilo zilisema watu wanne waliuawa katika shambulio la Urusi dhidi ya mji wa Kamianske, ulioko kusini-mashariki mwa nchi hiyo. Witkoff na Kushner, ambaye ni mkwe wa Trump, wamekuwa Urusi mara kadhaa, lakini mazungumzo hayo yanayotarajiwa yatakuwa ya kwanza kufanyika nchini Ukraine.
Zelensky alisema atahakikisha usalama wa anga la Urusi wakati wa ziara ya wajumbe hao na kuitaka Urusi kufanya vivyo hivyo kwa upande wa Ukraine. Wakati huo huo, Putin aliambia kongamano la kimataifa la uchumi siku ya Alhamisi kuwa "kuna uwezekano" wa kufikiwa kwa makubaliano ya amani.