Moja kwa moja, Umoja wa Mataifa wapitisha ramani mpya ya Afrika

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuidhinisha kubadilishwa kwa ramani ya kawaida ya dunia na kuweka nyingine inayoonyesha ukubwa halisi wa bara Afrika.

Moja kwa moja

Sarafina Robi & Mariam Mjahid

  1. Wajumbe wa amani wa Trump kuzuru Moscow na Kyiv

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wapatanishi wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, watazuru Urusi na Ukraine wikendi hii, huku juhudi za kuhitimisha vita zikionekana kushika kasi.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alithibitisha kuwa atakutana na wajumbe hao siku ya Jumapili, baada ya wao kutembelea Moscow siku ya Jumamosi kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

    Witkoff na Kushner wameongoza juhudi za Rais wa Marekani Donald Trump za kufanikisha makubaliano ya amani, lakini bado kuna pengo kubwa kati ya pande hizo mbili zinazopigana. "Wanakuja na pendekezo la kuhitimisha vita," Trump aliwaambia waandishi wa habari alipoulizwa kuhusu ziara hizo.

    Mapema siku ya Ijumaa, Zelensky alisema ndege isiyo na rubani ya Urusi ilishambulia ofisi ya mkuu wa usalama wa Ukraine, Oleksandr Poklad, mjini Kyiv. Poklad anaonekana kuwa salama na hajajeruhiwa.

    Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Zelensky alisema amemwagiza Poklad, ambaye anaongoza idara ya usalama ya SBU, kuchukua hatua stahiki kujibu shambulio hilo.

    Siku ya Jumamosi, mamlaka za eneo hilo zilisema watu wanne waliuawa katika shambulio la Urusi dhidi ya mji wa Kamianske, ulioko kusini-mashariki mwa nchi hiyo. Witkoff na Kushner, ambaye ni mkwe wa Trump, wamekuwa Urusi mara kadhaa, lakini mazungumzo hayo yanayotarajiwa yatakuwa ya kwanza kufanyika nchini Ukraine.

    Zelensky alisema atahakikisha usalama wa anga la Urusi wakati wa ziara ya wajumbe hao na kuitaka Urusi kufanya vivyo hivyo kwa upande wa Ukraine. Wakati huo huo, Putin aliambia kongamano la kimataifa la uchumi siku ya Alhamisi kuwa "kuna uwezekano" wa kufikiwa kwa makubaliano ya amani.

  2. Trump: Huenda tukashambulia Mlima Kalang hivi karibuni

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Siku ya Ijumaa, Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa Marekani inaweza kuushambulia Mlima Kalang nchini Iran hivi karibuni.

    Mlima Kalang, uliopo karibu na kituo cha kurutubisha urani cha Natanz, ni eneo lililolindwa sana la kijeshi lenye mifumo miwili ya mahandaki ya kina kirefu.

    Katika sehemu nyingine ya maelezo yake, Rais huyo wa Marekani alisema kuwa vita dhidi ya Iran ni "jambo dogo" kwa Marekani.

    Awali, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alisema siku ya Alhamisi kuwa asingeliita mgogoro na Iran kuwa ni "vita."

    Siku ya Ijumaa, Donald Trump alitoa ufafanuzi alipoulizwa na mwandishi wa habari awaeleze wananchi wa Marekani maana ya vita na Iran ikiwa hali hiyo haitaitwa "vita", alisema, "Naam, nawaambia, watu wengi hawaiiti hali hi kuwa vita.

    Mimi naiita mgogoro wa kijeshi, kwa sababu kwetu sisi ni jambo dogo kiasi. Sio jambo kubwa. Tulichukua hatua nchini Venezuela na tukafanikiwa. Hatukupoteza maisha ya watu nchini Venezuela.

    Tulipoteza watu 18 katika mgogoro na Iran. Tulipoteza watu 100,000 nchini Vietnam."

  3. Umoja wa Mataifa wapitisha ramani mpya ya Afrika

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuidhinisha kubadilishwa kwa ramani ya kawaida ya dunia na kuweka nyingine inayoonyesha ukubwa halisi wa bara Afrika.

    Azimio hilo lenye lengo la "Kurekebisha Ramani," lililowasilishwa na Togo na kuungwa mkono na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), lilipitishwa kwa uungwaji mkono wa mataifa 164, yakiwemo Ufaransa na Uingereza.

    Marekani ndiyo nchi pekee iliyopiga kura ya kupinga, huku nchi sita zikijizuia kupiga kura. Ingawa kura hiyo ya Umoja wa Mataifa haina nguvu ya kisheria ya kulazimisha utekelezaji, itasababisha mabadiliko katika ramani zinazotumiwa na taasisi mbalimbali duniani kote.

    Ramani ya Mercator, ambayo imekuwa ikitumika sana tangu karne ya 16, imekabiliwa na ukosoaji kwa sababu inaonyesha Afrika kuwa na ukubwa sawa na Greenland, licha ya ukweli kwamba Afrika ni kubwa mara 14 zaidi ya Greenland.

    Wakosoaji wanasema hali hii inasababisha kupuuzwa kwa mahitaji ya maendeleo na uwezo wa nchi zilizo karibu na ikweta.

    Ramani ya Mercator iliundwa mwaka wa 1569 na mtengenezaji wa ramani kutoka Flanders, Gerardus Mercator, ili kuwasaidia wavumbuzi wa Ulaya kusafiri kote duniani.

    Upotoshaji katika ramani yake unatokana na ukweli kwamba haiwezekani kuwakilisha kwa usahihi uso wa dunia kwenye ramani ya pande mbili.

  4. Hujambo, natumai umzima, karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 05/09/2026.