Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wahouthi 'wadhibiti' kisiwa cha kimkakati kwenye njia muhimu ya meli duniani
Waasi wa Houthi wamedhibiti Kisiwa cha Perim katika Mlango-bahari wa Bab al-Mandab, kulingana na chanzo cha habari.
Muhtasari
- Waouthi wadai kutwaa udhibiti mkubwa nchini Yemen – mambo muhimu unayopaswa kujua
- Wanigeria sita wanaotuhumiwa ulaghai wa kimapenzi kupelekwa Marekani
- Waasi wa Houthi 'wadhibiti' Kisiwa cha Perim - ripoti
- Ubalozi Mdogo wa Iran mjini Dubai: Mabaharia 10 wa Iran waachiwa huru
- Alvarez akanusha tuhuma za kuhusika katika utekaji nyara
- Araqchi: Majeshi yetu yaliharibu kweli makao makuu ya majeshi ya Marekani
- Reuters: Idadi ya meli zinazopita Hormuz yashuka hadi chini ya 10
- Trump akataa ombi la Saudi Arabia la kuwashambulia Wahouthi
- Aina za makombora walizonazo Wahouthi na umbali yanayoweza kufika
- Iran yataka kuondolewa kwa vikwazo vya kijeshi dhidi ya Yemen na kuanza kwa mazungumzo
- Algeria yakata uhusiano wa kidiplomasia na UAE
- AU yamfuta kazi mwanadiplomasia wa Burundi baada ya kuikosoa Kenya kuhusu wafanyabiashara
- Watu watano wameuawa katika shambulio la anga la Urusi, Ukraine yasema
- Waasi wa Houthi nchini Yemen wameuteka mji wa kimkakati wa Mokha
- Tetesi za soka Ulaya: Chelsea, Real Madrid zinamtaka Zubimendi wa Arsenal
- Zaidi ya watoto 20 wamefariki kwa moto wa shule nchini DR Congo
Moja kwa moja
Na Lizzy Masinga & Faidha Ngaga
Waouthi wadai kutwaa udhibiti mkubwa nchini Yemen – mambo muhimu unayopaswa kujua
Wapiganaji wa kundi la Houthi linaloungwa mkono na Iran nchini Yemen “wametwaa udhibiti” wa Kisiwa cha Perim katika Bahari ya Shamu, kwa mujibu wa chanzo kutoka serikalini.
Kisiwa hicho kinagawanya Mlango wa Bab al-Mandab, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa bidhaa duniani.
Mlango huo, uliopo katika ncha ya kusini ya Bahari ya Shamu, unaunganisha Ulaya – kupitia Mfereji wa Suez – pamoja na bandari za magharibi za Saudi Arabia na Bahari ya Hindi, na hatimaye bara la Asia kwa ujumla.
Mambo muhimu ya kufahamu:
Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, kundi linaloungwa mkono na Iran limesema “usafiri wa majini uko salama kwa kampuni zote isipokuwa meli za Saudi Arabia”, ambazo limesema “zimewekewa zuio.”
- Wahouthi wanadai wamepata mafanikio makubwa nchini Yemen, baada ya kundi hilo kuripotiwa kuteka mji wa bandari wa Mokha katika Bahari ya Shamu siku ya Alhamisi.
- Kundi hilo pia linadai kuwa limewafurusha “wanajeshi wanaoungwa mkono na Saudi Arabia” kutoka pwani ya magharibi ya Yemen, lakini halikutaja Kisiwa cha Perim.
- Mlango wa Bab al-Mandab umekuwa njia muhimu ya usafirishaji kwa Saudi Arabia kutokana na usumbufu uliotokea katika Mlango-bahari wa Hormuz wakati wa vita kati ya Marekani na Iran.
Unaweza Kusoma;
Wanigeria sita wanaotuhumiwa ulaghai wa kimapenzi kupelekwa Marekani
Polisi nchini Afrika Kusini wanatarajiwa kuwakabidhi baadaye leo Ijumaa mawakala wa FBI wanachama sita raia wa Nigeria wanaotafutwa nchini Marekani kwa tuhuma za kufanya ulaghai wa kimapenzi mtandaoni.
Mamlaka za Afrika Kusini zimesema kundi hilo linatuhumiwa kuwalenga zaidi ya wanawake 100 nchini Marekani na kuwalaghai zaidi ya rand milioni 100 za Afrika Kusini, sawa na dola milioni 6 za Marekani (£5m).
Watu hao walikamatwa mwaka 2021 na wanaaminika kuwa wanachama wa Black Axe, genge la uhalifu lenye asili ya Nigeria linalohusishwa na biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu, ulaghai wa mtandaoni na mauaji.
Baadhi ya waathiriwa wao walioripotiwa ni wastaafu na wafanyabiashara, ambao kwa mujibu wa kitengo maalumu cha polisi cha Hawks nchini Afrika Kusini, walilengwa kupitia “mahusiano ya kimapenzi ya mtandaoni yaliyokuwa yakitumiwa kwa ustadi kuwahadaa na kuwanyang’anya fedha.”
Msemaji wa Hawks, Kanali Katlego Mogale, amesema katika taarifa kwamba kundi hilo litatolewa katika kituo cha marekebisho ya tabia mjini Cape Town na kupelekwa uwanja wa ndege Ijumaa asubuhi, ambako litakabidhiwa kwa maafisa wa FBI na Secret Service ya Marekani.
Ameongeza kuwa watuhumiwa hao watakabiliwa na mashtaka ya ulaghai wa kielektroniki (wire fraud) na utakatishaji fedha watakapowasili nchini Marekani.
Black Axe ni mtandao wa uhalifu unaofanya kazi kwa siri na unaojulikana kwa kutumia kiwango kikubwa cha ukatili. Mtandao huo unaendesha shughuli zake barani Afrika, Ulaya na Amerika Kaskazini.
Uchunguzi wa BBC Eye mwaka 2021 ulionyesha kuwa mtandao huo ulikuwa umeendelea kuwa miongoni mwa makundi ya uhalifu uliopangwa yenye ushawishi mpana na hatari zaidi duniani.
Nigeria ndiyo eneo kuu la kuajiri wanachama wa Black Axe, huku wengi wao wakiwa na elimu ya chuo kikuu na baadhi yao kuingizwa katika mtandao huo wakiwa bado masomoni.
Kundi hilo limekuwa likifuatiliwa na vyombo vya sheria kwa miaka kadhaa.
Unaweza kusoma;
Waasi wa Houthi 'wadhibiti' Kisiwa cha Perim - ripoti
Waasi wa Houthi wamedhibiti Kisiwa cha Perim katika Mlango-bahari wa Bab al-Mandab, hiyo ni kwa mujibu wa chanzo cha habari.
Awali, tuliripoti kuwa kundi hilo lilikuwa limefika katika kisiwa hicho muhimu.
Shirika la habari la AFP pia linasema kuwa Wahouthi wameteka Kisiwa cha Perim, ambacho pia hujulikana kama Mayyun, kulingana na mashuhuda na afisa wa serikali ya eneo hilo.
"Boti zilizobeba wapiganaji wenye silaha wa Houthi zilifika Kisiwa cha Mayyun baada ya vikosi vya serikali kuondoka hapo jana," afisa huyo aliambia AFP.
Huku hayo yakijiri, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ameiambia BBC kwamba Marekani iko katika mawasiliano ya mara kwa mara na washirika wake wa kikanda kuhusu Yemen na bado inaendelea kuzingatia malengo yake ya kupambana na ugaidi dhidi ya Wahouthi.
Taarifa hiyo inasema kuwa maslahi muhimu ya Marekani katika Mashariki ya Kati ni pamoja na kulinda uhuru wa usafiri wa meli katika Bahari Nyekundu na ukanda huo, pamoja na kuzuia usafirishaji wa ugaidi.
Aidha, imeeleza kuwa utawala wa Trump umeonyesha wazi dhamira yake ya kutetea maslahi hayo dhidi ya vitendo vya uchokozi vya Iran na makundi yanayoiunga mkono.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje haikutoa maelezo zaidi kuhusu hatua za karibuni za Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran za kusonga mbele kuelekea maeneo muhimu ya bandari.
Unaweza kusoma;
Ubalozi Mdogo wa Iran mjini Dubai: Mabaharia 10 wa Iran waachiwa huru
Ubalozi Mdogo wa Iran mjini Dubai umesema kuwa mabaharia 10 wa Iran waliokuwa wakizuiliwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wameachiwa huru na wameondoka bandarini kuelekea Bandar Abbas.
Ofisi ya mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika mkoa wa Hormozgan ilitangaza tarehe 6 Septemba kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) uliwazuia wavuvi hao kuondoka licha ya uamuzi wa kuachiwa kwao kufikiwa.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, tiketi za kurejea Bandar Abbas zilikuwa tayari zimetolewa kwa wavuvi hao waliokamatwa nchini UAE, na maandalizi yote yalikuwa yamekamilishwa kati ya maafisa wa Iran na UAE. Hata hivyo UAE uliwazuia ghafla kuondoka bila kutoa sababu za msingi.
Taarifa za kutoweka kwa mabaharia hao zilichapishwa mwishoni mwa mwezi Agosti.
Shirika la Utangazaji la Iran (IBC) liliripoti wakati huo kwamba kuingia kimakosa katika maji ya nchi jirani si jambo lisilo la kawaida, lakini mazingira ya vita yalikuwa yameongeza wasiwasi kuhusu matukio kama hayo.
Unaweza kusoma;
Alvarez akanusha tuhuma za kuhusika katika utekaji nyara
Kiungo wa klabu ya West Ham, Edson Alvarez, amekanusha tuhuma za kuhusika katika madai ya kutekwa nyara kwa mtayarishaji wa filamu nchini Mexico.
Juan Jose Lopez Ordonez aliliambia gazeti la Mexico TV Notas kwamba alilazimishwa kuingia kwenye gari kwa kutishiwa kwa bunduki katika eneo la Polanco, Mexico City, mwaka 2024. Anadai tukio hilo lilihusisha familia ya Jonathan Toache Bedolla, ambaye ni baba mkwe wa zamani wa Alvarez.
Ordonez, ambaye anadai Alvarez hakuhusika moja kwa moja katika utekaji huo lakini alikuwa akifahamu mpango huo, alisema alipewa kazi ya kutengeneza filamu ya hali halisi kuhusu maisha ya mwanasoka huyo na bado anadai kulipwa pauni 150,000 kwa ajili ya mradi huo.
Alvarez, ambaye alicheza mechi yake ya kwanza kwa timu ya taifa ya Mexico mwaka 2017, alitoa taarifa kupitia mitandao yake ya kijamii kukanusha tuhuma hizo na kusema anazingatia kuchukua hatua za kisheria.
“Ninakanusha tuhuma yoyote au jaribio lolote la kuhusisha jina langu na matukio, migogoro au mienendo ambayo haihusiani kabisa na mimi,” Alvarez, ambaye pia ni nahodha wa Mexico, aliandika kwenye mitandao ya kijamii.
“Kwa miezi kadhaa iliyopita, jina na picha yangu vimekuwa vikitumiwa mara kwa mara kuongeza mvuto wa vyombo vya habari kuhusu suala ambalo halihusiani nami kwa namna yoyote.
“Hadi sasa, nilikuwa nimeamua kutotoa majibu. Hata hivyo, kuna mipaka, na kunihusisha na ujuzi, uwajibikaji au kushiriki katika masuala ya aina hii bila kuwasilisha ushahidi wowote kunavuka wazi mipaka hiyo.”
Aliongeza kuwa baadhi ya vyombo vya habari vinaweka kipaumbele kwenye “uchochezi wa hisia” badala ya “usahihi na ukweli”, na akasema ataendelea kuelekeza nguvu zake kwenye familia yake na taaluma yake.
Alvarez ameichezea West Ham mechi 74 tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Ajax mwaka 2023, lakini msimu huu amecheza mara moja pekee hadi sasa, katika mchezo dhidi ya Portsmouth wa Carabao Cup.
Unaweza Kusoma;
Araqchi: Majeshi yetu yaliharibu kweli makao makuu ya majeshi ya Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameshukuru kile alichokiita “uwazi” wa Kaimu Waziri wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, akisisitiza kuwa majeshi ya Iran kwa kweli yaliharibu kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Bahrain.
Gazeti la The Epoch Times lilimnukuu Hong Cao, Kaimu Waziri wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, akisema kuwa majeshi ya Iran “yaliharibu” makao makuu ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji cha Marekani nchini Bahrain.
Kwa mujibu wa makala hiyo ya The Epoch Times, Jeshi la Wanamaji la Marekani linaendelea “kutathmini” hatua za kuchukua kuhusu makao yake makuu ya uongozi nchini Bahrain.
Cao alitoa kauli hiyo kwa The Epoch Times baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza meli huko Philadelphia.
Gazeti hilo liliandika: “Ingawa picha kutoka vyanzo vya wazi zinaonyesha uharibifu katika kituo cha wanamaji cha Bahrain, kauli za Cao ni uthibitisho wa moja kwa moja na rasmi wa athari za mapigano katika kituo hicho.”
Unaweza kusoma;
Reuters: Idadi ya meli zinazopita Hormuz yashuka hadi chini ya 10
Idadi ya meli zilizopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz ilishuka hadi saba siku ya Alhamisi. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za awali za ufuatiliaji wa meli zilizotolewa leo.
Siku iliyotangulia, meli 11 zilipita katika mlango huo, huku wastani wa siku 10 ukiwa ni meli 15.
Kwa mujibu wa Reuters, takwimu kutoka mfumo wa ufuatiliaji wa meli wa Kepler zinaonesha kuwa hadi saa 3:00 asubuhi kwa saa za GMT, meli mbili kati ya hizo saba zilikuwa za aina ya Panamax. Moja ilikuwa imebeba mbolea za kemikali, huku nyingine ikiwa tupu.
Meli nyingine tano pia ziliingia katika mlango huo: meli ya mizigo kavu, meli ya kubeba chuma, meli ya kubeba nafaka, meli ya mafuta iliyobeba bidhaa nzito za petroli, na meli nyingine ya mizigo kavu.
Takwimu hizo hazijumuishi meli ambazo huenda zilipita katika mlango huo huku vifaa vyao vya Automatic Identification System (AIS) vikiwa vimezimwa ili kuzuia kugunduliwa.
Unaweza kusoma;
Trump akataa ombi la Saudi Arabia la kuwashambulia Wahouthi
Kwa mujibu wa Axios, Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, alimpigia simu mara mbili Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Alhamisi, akimshinikiza kuamuru mashambulizi dhidi ya Wahouthi.
Wakati huo huo, Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran wanaendelea kuingia na kutwaa udhibiti wa bandari ya Mokha, hatua inayoongeza ushawishi wao katika Mlango wa Bab el-Mandab.
Ripoti hiyo imesema Trump hakukubaliana na ombi hilo, huku maafisa wa Marekani wakisisitiza kuwa kwa sasa serikali ya Marekani haina mpango wa kushiriki moja kwa moja katika mapigano dhidi ya Wahouthi.
Asubuhi ya leo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitoa taarifa ikitaka kukomeshwa kwa vikwazo vya kijeshi dhidi ya Yemen na kuanza kwa mazungumzo.
Aina za makombora walizonazo Wahouthi na umbali yanayoweza kufika
Wahouthi, ambao mwanzoni walikuwa kundi dogo sana, hivi karibuni wameonyesha uwezo wao wa kusababisha changamoto kubwa.
Aina za makombora walizonazo Wahouthi na umbali wanaoweza kufikia:
- Scud B1C ya Umoja wa Kisovieti – umbali wa kilomita 300.
- Hwasong-5 ya Korea Kaskazini – umbali wa kilomita 300.
- Hwasong-6 ya Korea Kaskazini – umbali wa kilomita 600.
- Scarab 21 ya Umoja wa Kisovieti – umbali wa kilomita 70.
- Earthquake-3 – kombora lililotengenezwa nchini Iran, lenye umbali wa kilomita 250.
- Qaher-1 – kombora lililotengenezwa kwa teknolojia ya Umoja wa Kisovieti, lenye umbali wa kilomita 250.
- C-802 ya China – umbali wa kati ya kilomita 120 na 180.
Nguvu za kijeshi baharini
- Mandab-1 – kombora la China lenye umbali wa kilomita 40.
- Mandab-2 – kombora la Iran lenye umbali wa kilomita 250.
- Shale ya Iran – umbali wa kilomita 180.
- Rubies ya Umoja wa Kisovieti – umbali wa kilomita 80.
- Jerusalem ya Iran – pia linatengenezwa, na linaweza kufikia kilomita 800.
- Storm ya Iran – umbali wa kilomita 450.
- Fuse ya Iran – umbali wa kilomita 140.
- Red Sea missile – pia limetoka Iran, lakini umbali wake haujulikani.
Iran yataka kuondolewa kwa vikwazo vya kijeshi dhidi ya Yemen na kuanza kwa mazungumzo
Asubuhi ya Ijumaa, Septemba 10, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitoa taarifa kuhusu hali ya vita nchini Yemen, ikitaka kukomeshwa kwa vizuizi vya kijeshi dhidi ya nchi hiyo na kuanza kwa mazungumzo.
Taarifa hiyo, iliyochapishwa na shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, ilisema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka maslahi ya ulimwengu wa Kiislamu yazingatiwe, hasa wakati eneo la Asia Magharibi linakabiliwa na kile ilichokiita “uovu, ukatili na upanuzi usio na kifani wa utawala wa Kizayuni kwa ushirikiano na Marekani.”
Iran ilisema kuwa “suluhisho la masuala ya Yemen haliwezi kupatikana kupitia kuendelea kwa vikwazo na mashambulizi ya kijeshi.”
Mwisho wa taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisisitiza “haja ya haraka ya kurejesha mazungumzo, kwa kuzingatia ramani ya njia iliyokubaliwa, na kutekeleza masharti yake.” Ilisema Tehran iko “tayari kwa juhudi zozote katika suala hili.”
Taarifa ya Iran ilitolewa saa chache baada ya kuripotiwa kuwa Wahouthi walikuwa wakisonga mbele katika maeneo kadhaa, yakiwemo karibu na bandari ya Mokha nchini Yemen, na kuwasukuma nyuma wanajeshi wa serikali ya Yemen wanaopokea msaada wa kijeshi kutoka Saudi Arabia.
Alhamisi, Septemba 10, pia kuliripotiwa kuwa vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia na washirika wake vilijiondoa katika bandari nyingine ya pwani katika eneo hilo, Dhubab.
Kutekwa kwa Mokha kunaweza kuimarisha uwezo wa Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran kudhibiti njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na bidhaa.
Mokha iko karibu na Mlango wa Bab-el-Mandab, unaounganisha Bahari ya Shamu na Bahari ya Hindi.
Algeria yakata uhusiano wa kidiplomasia na UAE
Algeria imesitisha ghafla uhusiano wa kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) siku ya Alhamisi, ikisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mfululizo wa vitendo ilivyovitaja kuwa “vya uchochezi au vya uhasama” kutoka Abu Dhabi, bila kutoa sababu mahususi ya uamuzi huo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE ilisema baadaye siku hiyo kwamba ilitarajia uamuzi wa Algeria wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia ungekuwa wa muda, na kuongeza kuwa Abu Dhabi bado imejitolea kudumisha uhusiano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili pamoja na maslahi yao ya pamoja.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umekuwa ukizorota katika miaka ya hivi karibuni, huku vyombo vya habari vya Algeria vikiikosoa vikali UAE na kuituhumu kwa kujaribu kuchochea mgawanyiko katika eneo hilo.
“Wizara ya Mambo ya Nje inathibitisha kuthamini kwake wananchi wa Algeria ambao ni ndugu, pamoja na kujivunia uhusiano unaowaunganisha wananchi wa nchi hizo mbili, hususan kupitia jumuiya ya Waalgeria wanaoishi UAE na wageni kutoka Algeria,” wizara hiyo ilisema.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria ilisema vitendo vya UAE vimefikia hatua ambayo haviwezi tena kuchukuliwa kuwa vinakubalika au kuvumilika, na kwamba Algeria “imetumia njia zote za kuhifadhi uhusiano wa nchi hizo mbili.”
AU yamfuta kazi mwanadiplomasia wa Burundi - Kunani?
Tume ya Umoja wa Afrika (AU) imemfuta kazi mwanadiplomasia mwandamizi wa Burundi siku moja baada ya kukosoa jinsi Kenya inavyowashughulikia wafanyabiashara wa Burundi, wakati serikali ikiendelea na operesheni dhidi ya raia wa kigeni wasio na nyaraka zinazohitajika.
Ngoga aliandika kwenye mtandao wa X akieleza wasiwasi wake kuhusu namna wafanyabiashara wa Burundi wanavyoshughulikiwa, akiuliza kwa nini raia wa Burundi wanaonekana kulengwa, wakati raia wa mataifa mengine ya kigeni pia wanaendesha biashara nchini Kenya.
Kauli zake zilijiri wakati serikali ya Kenya ilipoongeza ukaguzi na utekelezaji wa sheria dhidi ya raia wa kigeni wanaoendesha biashara ndogo ndogo bila kuwa na nyaraka zinazohitajika za uhamiaji na biashara.
Balozi Fred Gateretse Ngoga, ambaye alikuwa ametumikia Tume ya Umoja wa Afrika kwa miaka 17, alitangaza kujiuzulu muda mfupi baada ya kuhoji kwa nini raia wa Burundi walikuwa wakilengwa nchini Kenya.
Hata hivyo, Tume ya Umoja wa Afrika imekanusha taarifa kwamba mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Burundi, Fred Gateretse Ngoga, alijiuzulu baada ya miaka 17 ya utumishi. AU imesema alifutwa kazi mara moja kutokana na utovu mkubwa wa nidhamu.
Watu watano wameuawa katika shambulio la anga la Urusi, Ukraine yasema
Ukraine imetangaza kwamba watu watano wameuawa na wengine 67 kujeruhiwa baada ya droni ya Urusi kushambulia kituo cha ununuzi katika mji wa Pavlograd, katika mkoa wa Dnipropetrovsk.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Ivan Vihefsky, alisema maduka na magari yalishambuliwa mchana kweupe, “wakati barabara zilikuwa zimejaa watu.”
Vyombo vya habari vya Ukraine viliripoti kwamba vituo vingine viwili vya ununuzi katika miji ya Zaporizhzhia na Sumy vililengwa na mashambulizi ya anga ya Urusi mapema wiki hii.
Urusi ilikuwa imetangaza kwamba droni ya majini ya Ukraine ilishambulia mji wa mapumziko wa Sochi Jumatano usiku, na kusababisha watu 28 kujeruhiwa.
Aidha, watu wengine watatu waliripotiwa kuuawa katika mashambulizi mengine yaliyofanywa na Ukraine.
Vita vimekuwa vikiendelea kwa nguvu kati ya Urusi na Ukraine tangu Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alipoanzisha uvamizi zaidi ya miaka minne na nusu iliyopita.
Juhudi mpya za kuleta amani zilizoongozwa na wajumbe wa Rais wa Marekani, Donald Trump, mwishoni mwa wiki zinaonekana kuwa zimeleta matokeo machache tu, kufuatia mazungumzo yao na Putin mjini Moscow na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, mjini Kyiv.
Unaweza kusoma;
Waasi wa Houthi nchini Yemen wameuteka mji wa kimkakati wa Mokha
Waasi wa Houthi nchini Yemen wameuteka mji wa kimkakati wa bandari wa Mokha, uliokuwa ukidhibitiwa na vikosi vinavyounga mkono serikali vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia, vyanzo vya kijeshi na mashahidi wamesema.
Kutekwa kwa Mokha kumeacha kundi hilo linaloungwa mkono na Iran likiwa umbali wa kilomita 75 tu kutoka Mlango wa Bab al-Mandab, lango la kusini la njia ya biashara inayounganisha Asia na Ulaya.
Houthi wamesema hawana tishio lolote kwa usafirishaji wa kimataifa wa majini, lakini wamerudia tishio lao la kulenga meli kutoka Saudi Arabia, ambayo imekuwa ikitegemea Bahari ya Shamu kwa usafirishaji wa mafuta nje ya nchi tangu vita vya Marekani na Israel vilipofunga kwa kiasi kikubwa Mlango bahari wa Hormuz katika Ghuba.
Kuongezeka kwa mzozo kati ya Houthi, serikali ya Yemen na Saudi Arabia kumechangia kupanda kwa bei ya mafuta.
Inaripotiwa kwamba mamia ya watu wameuawa na maelfu wameyahama makazi yao tangu Houthi walipoanzisha mashambulizi katika eneo la kusini-magharibi wiki moja iliyopita.
Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia pia umefanya mashambulizi ya anga katika maeneo ya magharibi mwa Yemen yanayodhibitiwa na Houthi, ukiunga mkono vikosi vinavyounga mkono serikali. Kwa upande wao, Houthi wamefyatua makombora na kutumia ndege zisizo na rubani kushambulia miji na vituo vya mafuta kusini mwa Saudi Arabia.
Unaweza kusoma;
Tetesi za soka Ulaya: Chelsea, Real Madrid zinamtaka Zubimendi wa Arsenal
Martin Zubimendi anaweza kutaka kuondoka Arsenal mwezi Januari baada ya kupoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza, huku Chelsea na Real Madrid zikimvizia kiungo huyo wa Hispania mwenye umri wa miaka 27. (Teamtalk)
Mshambuliaji wa Argentina ambaye hana timu kwa sasa Mauro Icardi, 33, yuko tayari kujiunga na Everton baada ya kuondoka Galatasaray mwezi Julai. (Teamtalk)
Hata hivyo, vyanzo kutoka Everton vimekanusha taarifa zinazomhusisha Icardi na klabu hiyo pamoja na mshambuliaji mwingine aliye huru, Anthony Martial.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 30 alicheza kwa mara ya mwisho akiwa na klabu ya Monterrey ya Mexico. (i Paper)
Liverpool ilikuwa ikimfuatilia beki wa Italia Marco Palestra, 21, ambaye baadaye alihama Atalanta na kujiunga na Chelsea.
Liverpool ilishindwa kumsajili kwa sababu ilihitaji kuimarisha zaidi safu yake ya ushambuliaji. (The Athletic )
Real Madrid imempa kiungo wa Uturuki Arda Guler, 21, mkataba wa miaka sita. Kocha wa Chelsea Xabi Alonso ni miongoni mwa wanaomkubali mchezaji huyo. (Fabrizio Romano via Teamtalk)
Beki wa Italia Giorgio Scalvini, 22, anayesakwa na Newcastle, amesaini mkataba mpya wa muda mrefu kusalia Atalanta. (Fabrizio Romano)
Aston Villa iko katika mazungumzo na beki wa kushoto wa Uholanzi Ian Maatsen, 24, kuhusu mkataba mpya ili kubakia Villa Park. (Football Insider)
Mshambuliaji wa Crystal Palace Eddie Nketiah, 27, anafikiria kubadili uraia wake kutoka England na kuichezea Ghana. (The Standard)
Mshambuliaji wa Colombia Kevin Viveros, 26, yuko mbioni kusaini mkataba mpya na Athletico Paranaense baada ya vilabu vya Sunderland na Aston Villa kuonesha kumtaka wakati wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi. (ESPN Brazil via Sunderland Echo)
Unaweza kusoma;
Zaidi ya watoto 20 wamefariki kwa moto wa shule nchini DR Congo
Takribani watoto 24 wa shule wamefariki katika mkanyagano walipokuwa wakijaribu kuukimbia moto ulioteketeza shule mbili katika eneo la Bukavu linalodhibitiwa na waasi, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, maafisa wa eneo hilo wamesema.
Watu wazima pia wanaripotiwa kufariki katika moto huo, na kuna hofu kwamba idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi katika eneo la Kadutu lenye msongamano mkubwa wa watu.
Walionusurika wamepelekwa katika hospitali za karibu, huku picha za tukio zikionesha watoto wakiwa wamelala kwenye sakafu za hospitali huku wakiwa kwenye maumivu.
Takribani nyumba 300 pia zimeteketea katika moto huo, ambao chanzo chake bado hakijajulikana.
Mamlaka zilizoteuliwa na waasi zilitangaza idadi ya awali ya vifo kuwa 24 Alhamisi jioni, na kuthibitisha taarifa zilizokuwa zimeripotiwa hapo awali. Hata hivyo, kuna hofu kwamba huenda watu zaidi wamefariki.
Picha zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha watoto wadogo wakiwa wamelala chini.
Shahidi aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters alisema moto huo ulikuwa umezimwa kufikia mchana, lakini moshi ulikuwa bado ukipanda kutoka kwenye vifusi na mabati.
Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini na mojawapo ya miji yenye msongamano mkubwa zaidi kwenye maeneo ya milima nchini DR Congo, ilitekwa na waasi wa M23 mwezi Februari mwaka jana.
Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu hii leo