Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump: Tuliwashambulia Iran vikali na tutawashambulia tena leo

"Kila kitu tayari kimejadiliwa kikamilifu na kukamilishwa. Tuna makubaliano yaliyokamilika baada ya mazungumzo ya kina, lakini Iran wanaendelea kuchelewesha," asema Trump.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Mariam Mjahid

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Usiku mwema.

  2. Ujumbe wa Qatar watua Tehran kwa mazungumzo na Iran

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Qatar umewasili Tehran mchana wa leo kwa mazungumzo na maafisa wa Iran.

    Gazeti la serikali ya Iran limeripoti kuwa ujumbe huo umefika kwa lengo la kujadili uhusiano wa pande mbili pamoja na hali ya usalama na maendeleo ya kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wajumbe hao pia wanatarajiwa kujadiliana kuhusu hatua za kidiplomasia zinazolenga kumaliza mzozo unaoendelea kati ya Marekani na Iran, sambamba na masuala ya ushirikiano wa nchi hizo mbili na maendeleo ya kikanda.

    Ziara hiyo inafanyika wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka kufuatia kuangushwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani, tukio ambalo limechochea mashambulizi na hatua za kulipizana kati ya pande hizo mbili.

    Mapema leo, Donald Trump alisema Iran imechelewesha kwa muda mrefu mazungumzo na sasa italazimika "kulipa gharama" ya hatua hiyo.

    Kwa upande wake, Iran imesema itafanya tathmini upya kuhusu kuendelea na mazungumzo hayo kufuatia mashambulizi mapya ya Marekani.

    Unaweza kusoma;

  3. Trump: Iran imechelewa kufikia makubaliano, sasa italipa gharama

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran imechelewa mno kufikia makubaliano na Marekani na sasa italazimika “kulipa gharama” ya kuchelewa huko.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social Jumatano, Trump amesema Iran imepata pigo kubwa na kwamba imebaki kutoa matamshi pekee bila kuchukua hatua za maana.

    "Mnyanyasaji wa Mashariki ya Kati sasa ameshindwa," alisema Trump.

    Aliongeza kuwa Iran ilichelewesha kwa muda mrefu kufikia makubaliano ambayo, kwa mujibu wake, yangekuwa na manufaa makubwa kwa taifa hilo.

    "Walichelewa mno kufikia makubaliano ambayo yangekuwa bora kwao. Sasa watalazimika kulipa gharama yake," alisema.

    Kauli hiyo imekuja huku mvutano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuongezeka tangu Jumatano asubuhi, ambapo pande zote mbili zimedai kufanya mashambulizi dhidi ya malengo ya upande mwingine.

    Mapema leo, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani Mashariki ya Kati (CENTCOM) ilisema vikosi vyake vilichukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran kujibu kuangushwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani.

    "Operesheni hii ni jibu kwa uchokozi wa Iran ambao haukuchochewa," ilisema CENTCOM katika taarifa yake.

    Kwa upande wake, Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran walidai kuwa Marekani ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo kadhaa ya Jask, Sark na Qeshm, yaliyosababisha kuharibiwa kwa mnara wa mawasiliano na matangi mawili ya maji ya matumizi ya raia.

    Katika taarifa yao, Walinzi hao walidai kuwa walijibu kwa kushambulia malengo manne muhimu ya kijeshi ya Marekani kwa kutumia makombora ya masafa marefu.

    Shirika la habari la Iran, IRNA, lilinukuu Walinzi wa Mapinduzi wakisema kuwa malengo hayo yalijumuisha maghala ya ndege za kivita aina ya F 35 na kituo cha amri na udhibiti wa jeshi la Marekani katika eneo la Al Azraq nchini Jordan.

    Picha za video zilizosambazwa na IRNA zilionyesha makombora ya masafa marefu ya Qadr, Emad na Khyber Shakan yakifyatuliwa kuelekea malengo ya Marekani katika eneo hilo. Hata hivyo, BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru uhalisi wa picha hizo.

    Awali, Trump alikuwa ameishutumu Iran kwa kuangusha helikopta ya kijeshi ya Marekani aina ya Apache.

    Kwa mujibu wa CENTCOM, wanajeshi wawili waliokuwa ndani ya helikopta hiyo waliokolewa na ndege isiyo na rubani ya jeshi la majini la Marekani.

    Unaweza kusoma;

  4. Netanyahu atangaza kuwania tena uchaguzi mkuu wa Israel

    Chama tawala cha Likud kimetangaza kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, atagombea katika uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo.

    Katika taarifa fupi iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, chama hicho kilisema kuwa Netanyahu si tu atashiriki uchaguzi huo, bali pia "atashinda kwa amri ya Mungu."

    Kauli hiyo imekuja wakati Israel ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.

    Netanyahu, ambaye amekuwa mmoja wa viongozi waliodumu kwa muda mrefu zaidi katika siasa za Israel, anatafuta muhula mwingine huku akikabiliwa na changamoto za kisiasa na kiusalama zinazoendelea nchini humo.

  5. Iran yasema itatathmini upya hatima ya mazungumzo baada ya mashambulizi mapya ya Marekani

    Iran imesema itafanya tathmini upya kuhusu kuendelea kwa mazungumzo yake na Marekani kufuatia mashambulizi mapya ya kijeshi yaliyofanywa na Washington.

    Akizungumza baada ya duru mpya ya mashambulizi kati ya mataifa hayo mawili, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema mazingira ya sasa hayawezi kuhimili mchakato wa kidiplomasia bila kuwepo kiwango cha chini cha utulivu na kuaminiana.

    "Mchakato wa kidiplomasia hauwezi kufanyika katika ombwe. Ili mazungumzo yoyote yaweze kusonga mbele, lazima kuwepo mazingira yanayoruhusu juhudi hizo kuendelea," alisema.

    Baghaei aliishutumu Marekani kwa kudhoofisha juhudi za mazungumzo kupitia kile alichokiita ujumbe unaokinzana, mabadiliko ya mara kwa mara ya misimamo na matakwa, pamoja na ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya usitishaji mapigano.

    Mapema Jumatano, Marekani ilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo kadhaa kusini mwa Iran, ikisema hatua hiyo ilikuwa jibu la kuangushwa kwa helikopta yake katika Bahari ya Oman.

    Kwa upande mwingine, Kambi ya Khatam al Anbiya ilitangaza kuwa Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na jeshi la Iran walijibu kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain, Kuwait na Jordan.

    Wakati huo huo, jeshi la Marekani limetangaza kumaliza operesheni zake za kijeshi zilizozinduliwa kufuatia kuangushwa kwa helikopta yake aina ya Apache.

    Unaweza kusoma;

  6. Mwamuzi wa FIFA, Omar Artan apokelewa kwa shangwe baada ya kurejea Somalia

    Mwamuzi wa Somalia, Omar Artan, aliyewasili kutoka Uturuki, amepokelewa kwa shangwe kubwa mjini Mogadishu baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia Marekani kwa ajili ya Kombe la Dunia.

    Omar Abdikadir Artan, aliyeteuliwa kuwa mwamuzi bora wa kiume barani Afrika mwaka 2025, alikuwa miongoni mwa waamuzi waliochaguliwa kuchezesha mechi za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Marekani, Canada na Mexico.

    Hata hivyo, alipowasili katika uwanja wa ndege wa Miami akitokea Istanbul, alifanyiwa ukaguzi wa ziada na maafisa wa uhamiaji wa Marekani kabla ya kunyimwa kibali cha kuingia nchini humo.

    Artan, mwenye umri wa miaka 34, alikuwa akitarajiwa kuwa Msomali wa kwanza kushiriki rasmi uwanjani katika fainali za Kombe la Dunia. Licha ya kuwa na pasipoti ya kidiplomasia na visa halali ya kuingia Marekani mara moja, alizuiwa kuingia na kurejeshwa alikotoka.

    Akizungumza baada ya kuwasili Mogadishu, Omar Abdikadir Artan alisema:

    "Ninawahakikishia kwamba Mungu akipenda nitakwenda wakati mwingine, na watu wa Somalia watafurahia hilo. Sote tunapaswa kulilinda na kuliheshimu jina la Somalia."

    Pia aliwataka vijana kutokata tamaa na nchi yao licha ya changamoto wanazokumbana nazo.

    "Somalia ni yetu, iwe katika nyakati nzuri au ngumu. Nchi hii ni yetu. Pasipoti hiyo ni yetu sote, tunaimiliki kwa pamoja na tunapaswa kuilinda kwa umoja."

    Maafisa wa uhamiaji wa Marekani walieleza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na kile walichokiita "wasiwasi wa kiusalama katika mchakato wa uhakiki."

    Kurejea kwake Mogadishu kumezua hisia kubwa, huku mamia ya wananchi na wapenzi wa soka wakimlaki kwa shangwe na kumuonesha mshikamano kufuatia tukio hilo lililozua mjadala mpana.

  7. Wahanga wa vita vya Sudan wafungua kesi ya kihistoria Kenya dhidi ya RSF

    Wahanga 12 wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan wamewasilisha malalamiko ya kihistoria ya jinai nchini Kenya, wakiwashutumu wanachama wa kundi la RSF kwa kutenda uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

    Inaaminika kuwa hii ndiyo kesi ya kwanza ya aina yake chini ya sheria za Kenya zinazotoa mamlaka ya kushughulikia uhalifu mkubwa wa kimataifa uliofanyika nje ya mipaka yake.

    Malalamiko hayo yaliwasilishwa Juni 9 kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma wa Kenya (DPP) jijini Nairobi na mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Legal Action Worldwide na African Centre for Justice and Peace Studies kwa niaba ya wahanga hao.

    Iwapo yatakubaliwa, kesi hiyo inaweza kufungua njia kwa mamlaka za Kenya kufanya uchunguzi na hata kuwafungulia mashtaka watu wanaotuhumiwa kwa uhalifu mkubwa wa kimataifa uliotendwa nje ya Kenya.

    Wahanga hao wanataka wanachama 10 wa RSF wachunguzwe. Miongoni mwao ni watu wanaodaiwa kuwa na uhusiano na Kenya au wanaoishi na kusafiri nchini humo.

    Malalamiko hayo yanahusu madai ya uhalifu uliotendwa ndani na maeneo yanayozunguka Khartoum kati ya Aprili 2023 na Machi 2025, wakati ambapo vikosi vya RSF vilidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu wa Sudan.

    Madai hayo yanajumuisha mateso, kuwekwa kizuizini katika mazingira yasiyo ya kibinadamu, ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kingono, utumwa wa kingono, kazi za kulazimishwa, kuzuiliwa kinyume cha sheria na mauaji ya kiholela, yakiwemo mauaji ya wanafamilia.

    Walionusurika wanasema walifanyiwa ukatili mkubwa katika vituo vya kizuizini, vikiwemo Gereza la Soba, kituo cha Al Riyadh na maeneo mengine yasiyo rasmi ya kuwazuilia watu.

    Mkurugenzi Mtendaji wa LAW, Antonia Mulvey, alisema kuwa kwa wahanga wa Sudan, kesi hiyo ni fursa adimu lakini muhimu ya kupata haki wakati njia nyingine za kuwawajibisha wahusika zikiwa chache sana.

    “Kenya haipaswi kuwa mahali salama kwa wahalifu wa kivita,” alisema.

    Kesi hiyo pia inaweza kuwa na athari za kisiasa kutokana na madai ya mara kwa mara kwamba serikali ya Nairobi ina uhusiano na RSF.

    Wakili wa Kenya anayewawakilisha walalamikaji hao, Owiso Owiso, alisema kuwasilishwa kwa kesi hiyo ni mtihani wa kujitolea kwa Kenya katika kusimamia haki za kimataifa.

    “Si tu fursa ya kupima dhamira ya Kenya kwa haki za kimataifa, bali pia ni uthibitisho kwamba njia za kuwawajibisha watuhumiwa bado hazijafungwa kabisa,” alisema.

    Walalamikaji wanasema haiwezekani kupata haki kupitia mfumo wa mahakama wa Sudan kutokana na vita vinavyoendelea.

    Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma wa Kenya anatarajiwa kuamua ndani ya siku 30 iwapo uchunguzi rasmi utafunguliwa.

    Malalamiko hayo yanawasilishwa wakati vita vya Sudan, ambavyo sasa vinaingia mwaka wake wa nne, vikiendelea kuchochea kile ambacho mashirika ya misaada yanaeleza kuwa moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani, huku mamilioni ya watu wakikimbia makazi yao na pande zote za mzozo zikikabiliwa na tuhuma za kutenda ukatili mkubwa.

    Soma zaidi:

  8. NASA yatangaza wanaanga wa misheni ya Artemis III

    NASA imetangaza kuwa Randy Bresnik, Luca Parmitano, Frank Rubio na Andre Douglas watakuwa sehemu ya misheni ijayo katika mpango wake wa kuwarejesha binadamu kwenye uso wa Mwezi ifikapo mwaka 2028.

    Tangazo hilo limekuja chini ya wiki mbili tangu roketi ya New Glenn, iliyotengenezwa na kampuni ya anga za juu ya Blue Origininayomilikiwa na Jeff Bezos, ilipolipuka muda mfupi baada ya kurushwa.

    Maafisa wa NASA walisema Jumanne kwamba chombo cha kutua Mwezini cha Blue Origin bado kitashiriki katika misheni ya Artemis III, hatua inayofuata katika mpango wa shirika hilo wa kuwarejesha binadamu kwenye uso wa Mwezi.

    Hata hivyo, NASA haikutoa maelezo mengi kuhusu iwapo bado itaweza kutekeleza uzinduzi wa Artemis III kufikia katikati ya mwaka 2027, lengo ambalo tayari lilikuwa na changamoto na ambalo huenda likakabiliwa na vikwazo zaidi kufuatia mlipuko wa roketi hiyo.

    Wanaanga wote wanne wa Artemis III ni wanaume, jambo ambalo si la kawaida kwa misheni za NASA. Mara ya mwisho hali kama hiyo ilitokea mwaka 2023 katika misheni ya SpaceX Crew 6, iliyowapeleka wanaanga wanne kwenye Kituo cha Kimataifa cha Anga.

    Tangu misheni ya Crew 1 mwaka 2020, karibu misheni zote za NASA kwa ushirikiano na SpaceX kuelekea kituoni hapo zilijumuisha angalau mwanamke mmoja katika timu ya wanaanga.

    Soma Zaidi:

  9. Jaji mkuu wa zamani wa Kenya akosoa uamuzi wa mahakama wa kuhalalisha kuondolewa kwa Gachagua madarakani

    Aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, amesema uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, una dosari na unaweza kufungua mlango wa ukiukaji wa mara kwa mara wa sheria katika kesi za kuondolewa madarakani kwa viongozi wa umma.

    Kwa mujibu wa Maraga, hukumu hiyo ilikuwa na mkanganyiko baada ya mahakama kubaini kuwa haki ya Gachagua ya kusikilizwa kwa haki ilikiukwa, lakini badala ya kubatilisha mchakato wa kutimuliwa kwake uliopitishwa na Seneti mnamo Oktoba 2024, ilimpa fidia ya shilingi milioni 50 za Kenya.

    “Kwa mtazamo wangu, baada ya mahakama kufikia hitimisho hilo, hatua isiyoepukika ilikuwa kubatilisha kutimuliwa kwake,” alisema katika mahojiano na kituo cha radio cha Kenya Spice FM Jumatano.

    “Kwa kuwa haki ya kusikilizwa ni lazima na haiwezi kuondolewa, tafsiri sahihi kwa maoni yangu ilikuwa kubatilisha kile ambacho Seneti ilikuwa imefanya.”

    Maraga alieleza kuwa kifungu cha 25(c) cha Katiba kinatambua haki ya kusikilizwa kwa haki kama haki ya msingi isiyoweza kupunguzwa au kuondolewa katika mazingira yoyote.

    Aliyekuwa Jaji Mkuu huyo alisema kuwa uamuzi uliotolewa na Majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Freda Mugambi unaweza kwenda kinyume na matakwa ya Katiba na kuwafanya wabunge na maseneta kuwa na tahadhari ndogo katika kufuata sheria wakati wa kushughulikia hoja za kuondoa viongozi madarakani siku zijazo.

    “Maafisa wa serikali wataendelea kukiuka Katiba wakijua kwamba hawatawajibishwa binafsi. Hivyo tutakuwa tunaimarisha utamaduni wa kutoadhibiwa ndani ya mifumo yetu,” alisema.

    Maraga, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2027, anaamini kuwa vitendo vya kinyume cha sheria vinapaswa kuambatana na adhabu kali ili kulinda heshima na uadilifu wa sheria.

    “Iwapo hatutachukua hatua thabiti katika baadhi ya matukio, Katiba itageuka kuwa pendekezo tu badala ya amri ya lazima. Hapo ndipo taifa huanza kudhoofika taratibu na kuelekea kuwa dola iliyoshindwa,” aliongeza.

    Soma zaidi:

  10. Watu 12 wameuawa katika shambulio la risasi jijini Johannesburg, polisi wamesema

    Polisi nchini Afrika Kusini wamesema watu wasiopungua 12 wameuawa katika shambulio la risasi lililotokea katika eneo la makazi yasiyo rasmi la Cleveland, karibu na Johannesburg.

    Watu wengine tisa walijeruhiwa katika shambulio hilo lililotokea usiku wa Jumanne, huku polisi wakianzisha msako mkali wa kuwatafuta washukiwa.

    Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, zaidi ya washukiwa 10 walishushwa kutoka kwenye gari jeupe aina ya Toyota Quantum karibu na kituo cha mafuta katika eneo la Cleveland.

    Washukiwa hao walidaiwa kuingia katika makazi hayo kupitia njia mbili tofauti na kuanza kufyatua risasi kwa wakazi na wanajamii katika maeneo mbalimbali kabla ya kutoroka kwa kutumia gari hilo hilo.

    Afrika Kusini ina moja ya viwango vya juu zaidi vya mauaji duniani, ambapo wastani wa watu takribani 60 huuawa kila siku.

    Mashambulizi ya risasi katika makazi yasiyo rasmi ni jambo la kawaida nchini humo na mara nyingi huhusishwa na vurugu za magenge au migogoro binafsi.

    Polisi wa eneo hilo walisema walipokea taarifa ya “shambulio la risasi linaloendelea” majira ya saa 11:10 jioni kwa saa za huko, na huduma za dharura za matibabu zilitumwa kuwahudumia majeruhi.

  11. Vyombo vya habari vya Marekani: Trump hakutaka kuishambulia tena Iran

    Alex Ward, ripota wa jarida la Wall Street Journal, anasema kuwa maafisa wa Marekani walisema kuwa Donald Trump hakushawishika na haja ya hatua za kulipiza kisasi dhidi ya Iran hadi mapema Jumanne.

    Bw. Trump aliambia jarida la Wall Street Journal Jumanne asubuhi kwamba kuiangusha helikopta ya kijeshi ya Apache "si jambo kubwa" kwa sababu marubani walikuwa salama.

    Hata hivyo, rais wa Marekani alibadili uamuzi wake baada ya Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegsett na Dan Kaine, Mwenyekiti wa Wakuu wa Pamoja wa Majeshi wa Marekani, kupendekeza hatua za kijeshi wakati wa mkutano katika Ikulu ya White House, kulingana na maafisa.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais wa Marekani hatimaye aliidhinisha mashambulizi dhidi ya shabaha nchini Iran, ambayo maafisa wa Marekani wanasema yalifanywa kujibu kuangushwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani aina ya Apache.

    Mashambulizi hayo yalijibiwa kwa wimbi la mashambulizi ya Walinzi wa Mapinduzi na jeshi la Iran kwenye kambi za Marekani Mashariki ya kati

  12. Droni ya majini yaokoa wanajeshi wa helikopta ya Jeshi la Marekani karibu na Mlango bahari wa Hormuz

    Wanajeshi wawili wa helikopta ya Jeshi la Marekani iliyodondoka karibu na Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu waliokolewa na droni ya majini ya Marekani, maafisa wa Marekani wamethibitisha.

    Hii ni mara ya kwanza jeshi la Marekani kuthibitisha hadharani kuwa aina hiyo ya chombo imetumika katika operesheni ya uokoaji.

    Jeshi limesema wanajeshi hao wawili “waliokolewa salama ndani ya takribani saa mbili na wako katika hali nzuri” baada ya helikopta yao ya AH-64 Apache kuanguka “karibu na pwani ya Oman wakati ikifanya doria katika maji ya kikanda.”

    Rais wa Marekani Donald Trump alishutumu Iran kwa kuidungua helkopta hiyo wakati ilikuwa ikifanya doria katika Mlango bahari wa Hormuz, na kwa kujibu akaamuru mashambulizi ya kulipiza kisasi nchini humo.

    Unaweza kusoma;

  13. Uingereza na washirika waweka vikwazo dhidi ya “mitandao” inayosaidia vurugu za walowezi Ukingo wa Magharibi

    Uingereza, Australia, Canada, Ufaransa na Norway zimeweka vikwazo dhidi ya kile wanachokiita “mitandao” inayohusika na kufadhili na kuwezesha mashambulizi dhidi ya raia wa Palestina na walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel.

    Hatua hiyo inalenga “kuwawajibisha walowezi wenye misimamo mikali kwa viwango vya kutisha vya vurugu za walowezi,” nchi hizo tano zimesema.

    Ufaransa pia imepiga marufuku kuingia nchini humo kwa Waziri wa Fedha wa Israel mwenye misimamo mikali, Bezalel Smotrich, ambaye ana mamlaka makubwa kuhusu sera za serikali za makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, ambayo ni haramu chini ya sheria ya kimataifa.

    Israel imesema inakataa “hatua hizo za aibu,” zikiziita kuwa ni za kisiasa.

    Israel imejenga takribani makazi 160 yanayowahifadhi Wayahudi wapatao 700,000 tangu ilipouteka Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ardhi inayotakiwa na Wapalestina kwa ajili ya taifa lao la baadaye pamoja na Gaza, wakati wa vita vya Mashariki ya Kati mwaka 1967. Inakadiriwa Wapalestina milioni 3.3 wanaishi pamoja nao.

    Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya walowezi dhidi ya Wapalestina na mali zao katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Gaza, vilivyochochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.

    UN imeandika mashambulizi 1,835 ya walowezi dhidi ya Wapalestina mwaka 2025 yaliyosababisha majeruhi au uharibifu wa mali katika takribani jamii 280 za Ukingo wa Magharibi.

    Takribani Wapalestina saba waliuawa na 832 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, idadi zote mbili zikiongezeka kwa asilimia 130 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

    Unaweza kusoma;

  14. Rubani wa Air Canada aripotiwa kurusha ndege kwa miaka 17 bila kuwa na leseni halali ya urubani

    Mamlaka za Canada zimesema rubani wa zamani wa shirika la ndege la Air Canada anatuhumiwa kusafirisha maelfu ya abiria kwa miaka 17 bila leseni halali ya urubani.

    Polisi walisema ilibainika kuwa Jeffrey Wall, mwenye umri wa miaka 59 kutoka Ontario, alikuwa akirusha ndege kwa kutumia vyeti bandia tangu alipopandishwa cheo kuwa rubani mwaka 2009, na sasa anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya ulaghai.

    Air Canada ilisema rubani huyo alifukuzwa kazi mara moja baada ya kugundulika kwa udanganyifu huo mwaka jana, na ikaongeza kuwa iliripoti tukio hilo kwa hiari kwa mamlaka ya usafiri wa Canada.

    Shirika hilo la ndege lilisisitiza kuwa usalama wa abiria haukuwahi kuathiriwa na kwamba marubani wote hupitia mafunzo na mazoezi ya mara kwa mara kila baada ya miezi sita.

    Naibu mkuu wa polisi wa eneo la Peel kusini mwa Ontario, Nick Milinovich, alisema Bw. Wall alikuwa akifanya kazi na Air Canada kwa miaka 27, kuanzia mwaka 1998.

    Polisi wanasema rubani huyo alikuwa akitoa nyaraka za uongo tangu mwaka 2009, alipopandishwa cheo kuwa kapteni

    Kwa kazi hii, marubani wanatakiwa kuwa na Leseni ya Usafiri wa Anga (Air Transport Pilot License - ATPL), ambayo kwa kawaida hupatikana baada ya kufaulu mitihani kadhaa ya maandishi.

    Polisi walisema: “Ni kama mtu aliye na leseni ya udaktari wa kawaida lakini anafanya upasuaji wa ubongo kwenye kliniki yake mwenyewe.”

  15. Tetesi za soka Ulaya: Real Madrid wanamsaka Calafiori , Man United wamfukuzia Lewis Hall wa Newcastle

    Real Madrid wanavutiwa na mlinzi wa Arsenal na Italia Riccardo Calafiori, 24, ambaye awali alicheza chini ya Jose Mourinho huko Roma. (Sky Sports),

    Tottenham wanafikiria kumnunua mlinzi wa Juventus na Brazil Gleison Bremer, 29, kuchukua nafasi ya mchezaji wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 28 Cristian Romero katika safu ya ulinzi ya kati. (Tuttosport – In Itali),

    Manchester United hawana nia ya kumsajili Romero kutoka Tottenham lakini wanavutiwa na mlinzi wa Newcastle mwenye umri wa miaka 21 Lewis Hall. (TeamTalk),

    Mmiliki mwenza wa Man United Sir Jim Ratcliffe yuko tayari kukidhi matakwa ya mshahara ya kiungo wa Nottingham Forest Elliot Anderson, 23, ili kumleta Manchester United. {Mirror)

    Manchester City wanasalia kuwa mstari wa mbele kumsajili Anderson licha ya juhudi za United kuwapiku wapinzani wao. (Star – Subscription Required)

    Mkufunzi anayekuja Real Madrid Jose Mourinho anamtaka kiungo wa kati wa West Ham na Ureno Mateus Fernandes ambaye pia anavutiwa na Chelsea. (AS – In Spanish)

    Manchester United pia wanatafuta dili la kumnunua Fernandes huku West Ham wakimthamini mchezaji huyo kwa takriban £80m, lakini klabu hiyo ya London haina haraka ya kumuuza. (Sky Sports)

    Manchester United wanafikiria kumnunua mlinda lango wa Uingereza, 35, Karl Darlow, ambaye mkataba wake unamalizika Leeds msimu huu wa joto, huku mlinda lango wa Uturuki Altay Bayindir, 28, akitarajiwa kuondoka Old Trafford. (Sports Talks)

    Fulham wana nia ya kumsajili kiungo wa kati wa Nigeria Samuel Chukwueze kutoka AC Milan kufuatia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kuhudumu kwa mkopo wa msimu mzima katika Craven Cottage, lakini wanajaribu kujadili ada ndogo. (Gazzetta dello Sport – In Itali)

    Atletico Madrid wana matumaini ya kumshawishi kiungo wa kati wa zamani wa Manchester City Bernando Silva ajiunge nao badala ya Barcelona au Real Madrid kwa sababu wanaweza kumpa Mreno huyo mwenye umri wa miaka 31 muda zaidi wa kucheza. (Marca – In Spanish)

    Fulham wanafikiria iwapo wataanzisha kipengele cha kuachiliwa kwa pauni milioni 8 kwa kocha mkuu wa Ipswich, Kieran McKenna, ambaye anaongoza orodha yao ya wagombea kuchukua nafasi ya Marco Silva. (Sports Talk)

    Leicester wako kwenye mazungumzo na kocha mkuu wa zamani wa Southampton na Rangers, Russell Martin kuhusu kuchukua mikoba ya klabu hiyo kufuatia kushuka daraja hadi Ligi ya Kwanza. (Leicester Mercury,)

  16. Mashambulizi kati ya Marekani na Iran yashika kasi baada ya helikopta ya doria ya Marekani kudunguliwa kwenye Mlango bahari wa Hormuz

    Marekani na Iran zimeshambuliana baada ya Marekani kutishia kulipiza kisasi kufuatia kudunguliwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani juu ya Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu.

    Jeshi la Marekani lilisema Jumanne kuwa limekamilisha mashambulizi ya anga yaliyoanza saa 17:00 kwa saa za Marekani Mashariki.

    Kwa upande wake, Jeshi la Mapinduzi la Iran (IRGC) lilisema lilifanya shambulio la ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi ya Marekani nchini Bahrain na shambulio la makombora dhidi ya kambi ya Marekani nchini Jordan, huku jeshi la Kuwait likiripoti kuwa lilikuwa likizuia mashambulizi.

    Marekani imesema mashambulizi yake ni “jibu” kwa kudunguliwa kwa helikopta hiyo, tukio ambalo Rais Donald Trump alilitaja kuwa lilifanywa na Iran, wakati IRGC likiyaita mashambulizi ya Marekani kuwa “ya kikatili”.

    Tukio hilo lilitokea baada ya wafanyakazi wawili wa helikopta ya Marekani ya Apache kuokolewa na droni ya majini ya Marekani siku ya Jumatatu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa jeshi la Marekani kutumia aina hiyo ya chombo katika operesheni ya uokoaji.

    Maafisa wa Marekani walisema Iran ilitumia droni kushambulia helikopta hiyo, lakini bado haijathibitishwa kama shambulio hilo lilikuwa la makusudi. Shirika la habari la Mehr liliripoti kuwa Iran haijakiri kuhusika.

    Centcom ilisema ndege za kivita za Marekani zilishambulia mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran, vituo vya udhibiti wa ardhini, na rada karibu na Mlango wa Hormuz.

    Kwa upande mwingine, IRGC ilisema mashambulizi ya Marekani yameharibu mnara wa mawasiliano na matenki mawili ya maji.

    Unaweza kusoma;

  17. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo