Moja kwa moja, Mashambulizi kati ya Marekani na Iran yashika kasi baada ya helikopta ya doria ya Marekani kudunguliwa
Marekani na Iran zimeshambuliana baada ya Marekani kutishia kulipiza kisasi kufuatia kudunguliwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani juu ya Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu.
Vyombo vya habari vya Marekani: Trump hakutaka kuishambulia tena Iran
Chanzo cha picha, Getty Images
Alex Ward, ripota wa jarida la Wall Street Journal, anasema kuwa maafisa wa Marekani walisema kuwa Donald Trump hakushawishika na haja ya hatua za kulipiza kisasi dhidi ya Iran hadi mapema Jumanne.
Bw. Trump aliambia jarida la Wall Street Journal Jumanne asubuhi kwamba kuiangusha helikopta ya kijeshi ya Apache "si jambo kubwa" kwa sababu marubani walikuwa salama.
Hata hivyo, rais wa Marekani alibadili uamuzi wake baada ya Waziri wa Vita wa Marekani Pete Hegsett na Dan Kaine, Mwenyekiti wa Wakuu wa Pamoja wa Majeshi wa Marekani, kupendekeza hatua za kijeshi wakati wa mkutano katika Ikulu ya White House, kulingana na maafisa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais wa Marekani hatimaye aliidhinisha mashambulizi dhidi ya shabaha nchini Iran, ambayo maafisa wa Marekani wanasema yalifanywa kujibu kuangushwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani aina ya Apache.
Mashambulizi hayo yalijibiwa kwa wimbi la mashambulizi ya Walinzi wa Mapinduzi na jeshi la Iran kwenye kambi za Marekani Mashariki ya kati
Droni ya majini yaokoa wafanyakazi wa helikopta ya Jeshi la Marekani karibu na Mlango bahari wa Hormuz
Chanzo cha picha, Getty Images
Wafanyakazi wawili wa helikopta ya Jeshi la Marekani iliyodondoka karibu na Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu waliokolewa na droni ya majini ya Marekani, maafisa wa Marekani wamethibitisha.
Hii ni mara ya kwanza jeshi la Marekani kuthibitisha hadharani kuwa aina hiyo ya chombo imetumika katika operesheni ya uokoaji.
Jeshi limesema wanajeshi hao wawili “waliokolewa salama ndani ya takribani saa mbili na wako katika hali nzuri” baada ya helikopta yao ya AH-64 Apache kuanguka “karibu na pwani ya Oman wakati ikifanya doria katika maji ya kikanda.”
Rais wa Marekani Donald Trump alishutumu Iran kwa kuidungua helkopta hiyo wakati ilikuwa ikifanya doria katika Mlango bahari wa Hormuz, na kwa kujibu akaamuru mashambulizi ya kulipiza kisasi nchini humo.
Uingereza na washirika waweka vikwazo dhidi ya “mitandao” inayosaidia vurugu za walowezi Ukingo wa Magharibi
Chanzo cha picha, Reuters
Uingereza, Australia, Canada, Ufaransa na Norway zimeweka vikwazo dhidi ya kile wanachokiita “mitandao” inayohusika na kufadhili na kuwezesha mashambulizi dhidi ya raia wa Palestina na walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel.
Hatua hiyo inalenga “kuwawajibisha walowezi wenye misimamo mikali kwa viwango vya kutisha vya vurugu za walowezi,” nchi hizo tano zimesema.
Ufaransa pia imepiga marufuku kuingia nchini humo kwa Waziri wa Fedha wa Israel mwenye misimamo mikali, Bezalel Smotrich, ambaye ana mamlaka makubwa kuhusu sera za serikali za makazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, ambayo ni haramu chini ya sheria ya kimataifa.
Israel imesema inakataa “hatua hizo za aibu,” zikiziita kuwa ni za kisiasa.
Israel imejenga takribani makazi 160 yanayowahifadhi Wayahudi wapatao 700,000 tangu ilipouteka Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ardhi inayotakiwa na Wapalestina kwa ajili ya taifa lao la baadaye pamoja na Gaza, wakati wa vita vya Mashariki ya Kati mwaka 1967. Inakadiriwa Wapalestina milioni 3.3 wanaishi pamoja nao.
Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya walowezi dhidi ya Wapalestina na mali zao katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Gaza, vilivyochochewa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.
UN imeandika mashambulizi 1,835 ya walowezi dhidi ya Wapalestina mwaka 2025 yaliyosababisha majeruhi au uharibifu wa mali katika takribani jamii 280 za Ukingo wa Magharibi.
Takribani Wapalestina saba waliuawa na 832 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, idadi zote mbili zikiongezeka kwa asilimia 130 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Rubani wa Air Canada aripotiwa kurusha ndege kwa miaka 17 bila kuwa na leseni halali ya urubani
Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka za Canada zimesema rubani wa zamani wa shirika la ndege la Air Canada anatuhumiwa kusafirisha maelfu ya abiria kwa miaka 17 bila leseni halali ya urubani.
Polisi walisema ilibainika kuwa Jeffrey Wall, mwenye umri wa miaka 59 kutoka Ontario, alikuwa akirusha ndege kwa kutumia vyeti bandia tangu alipopandishwa cheo kuwa rubani mwaka 2009, na sasa anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya ulaghai.
Air Canada ilisema rubani huyo alifukuzwa kazi mara moja baada ya kugundulika kwa udanganyifu huo mwaka jana, na ikaongeza kuwa iliripoti tukio hilo kwa hiari kwa mamlaka ya usafiri wa Canada.
Shirika hilo la ndege lilisisitiza kuwa usalama wa abiria haukuwahi kuathiriwa na kwamba marubani wote hupitia mafunzo na mazoezi ya mara kwa mara kila baada ya miezi sita.
Naibu mkuu wa polisi wa eneo la Peel kusini mwa Ontario, Nick Milinovich, alisema Bw. Wall alikuwa akifanya kazi na Air Canada kwa miaka 27, kuanzia mwaka 1998.
Polisi wanasema rubani huyo alikuwa akitoa nyaraka za uongo tangu mwaka 2009, alipopandishwa cheo kuwa kapteni
Kwa kazi hii, marubani wanatakiwa kuwa na Leseni ya Usafiri wa Anga (Air Transport Pilot License - ATPL), ambayo kwa kawaida hupatikana baada ya kufaulu mitihani kadhaa ya maandishi.
Polisi walisema: “Ni kama mtu aliye na leseni ya udaktari wa kawaida lakini anafanya upasuaji wa ubongo kwenye kliniki yake mwenyewe.”
Tetesi za soka Ulaya: Real Madrid wanamsaka Calafiori , Man United wamfukuzia Lewis Hall wa Newcastle
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Ricardo Calafiori
Real Madrid wanavutiwa na mlinzi wa Arsenal na Italia Riccardo Calafiori, 24, ambaye awali alicheza chini ya Jose Mourinho huko Roma. (Sky Sports),
Tottenham wanafikiria kumnunua mlinzi wa Juventus na Brazil Gleison Bremer, 29, kuchukua nafasi ya mchezaji wa kimataifa wa Argentina mwenye umri wa miaka 28 Cristian Romero katika safu ya ulinzi ya kati. (Tuttosport – In Itali),
Manchester United hawana nia ya kumsajili Romero kutoka Tottenham lakini wanavutiwa na mlinzi wa Newcastle mwenye umri wa miaka 21 Lewis Hall. (TeamTalk),
Mmiliki mwenza wa Man United Sir Jim Ratcliffe yuko tayari kukidhi matakwa ya mshahara ya kiungo wa Nottingham Forest Elliot Anderson, 23, ili kumleta Manchester United. {Mirror)
Manchester City wanasalia kuwa mstari wa mbele kumsajili Anderson licha ya juhudi za United kuwapiku wapinzani wao. (Star – Subscription Required)
Mkufunzi anayekuja Real Madrid Jose Mourinho anamtaka kiungo wa kati wa West Ham na Ureno Mateus Fernandes ambaye pia anavutiwa na Chelsea. (AS – In Spanish)
Manchester United pia wanatafuta dili la kumnunua Fernandes huku West Ham wakimthamini mchezaji huyo kwa takriban £80m, lakini klabu hiyo ya London haina haraka ya kumuuza. (Sky Sports)
Manchester United wanafikiria kumnunua mlinda lango wa Uingereza, 35, Karl Darlow, ambaye mkataba wake unamalizika Leeds msimu huu wa joto, huku mlinda lango wa Uturuki Altay Bayindir, 28, akitarajiwa kuondoka Old Trafford. (Sports Talks)
Fulham wana nia ya kumsajili kiungo wa kati wa Nigeria Samuel Chukwueze kutoka AC Milan kufuatia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kuhudumu kwa mkopo wa msimu mzima katika Craven Cottage, lakini wanajaribu kujadili ada ndogo. (Gazzetta dello Sport – In Itali)
Atletico Madrid wana matumaini ya kumshawishi kiungo wa kati wa zamani wa Manchester City Bernando Silva ajiunge nao badala ya Barcelona au Real Madrid kwa sababu wanaweza kumpa Mreno huyo mwenye umri wa miaka 31 muda zaidi wa kucheza. (Marca – In Spanish)
Fulham wanafikiria iwapo wataanzisha kipengele cha kuachiliwa kwa pauni milioni 8 kwa kocha mkuu wa Ipswich, Kieran McKenna, ambaye anaongoza orodha yao ya wagombea kuchukua nafasi ya Marco Silva. (Sports Talk)
Leicester wako kwenye mazungumzo na kocha mkuu wa zamani wa Southampton na Rangers, Russell Martin kuhusu kuchukua mikoba ya klabu hiyo kufuatia kushuka daraja hadi Ligi ya Kwanza. (Leicester Mercury,)
Mashambulizi kati ya Marekani na Iran yashika kasi baada ya helikopta ya doria ya Marekani kudunguliwa kwenye Mlango bahari wa Hormuz
Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani na Iran zimeshambuliana baada ya Marekani kutishia kulipiza kisasi kufuatia kudunguliwa kwa helikopta ya kijeshi ya Marekani juu ya Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu.
Jeshi la Marekani lilisema Jumanne kuwa limekamilisha mashambulizi ya anga yaliyoanza saa 17:00 kwa saa za Marekani Mashariki.
Kwa upande wake, Jeshi la Mapinduzi la Iran (IRGC) lilisema lilifanya shambulio la ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi ya Marekani nchini Bahrain na shambulio la makombora dhidi ya kambi ya Marekani nchini Jordan, huku jeshi la Kuwait likiripoti kuwa lilikuwa likizuia mashambulizi.
Marekani imesema mashambulizi yake ni “jibu” kwa kudunguliwa kwa helikopta hiyo, tukio ambalo Rais Donald Trump alilitaja kuwa lilifanywa na Iran, wakati IRGC likiyaita mashambulizi ya Marekani kuwa “ya kikatili”.
Tukio hilo lilitokea baada ya wafanyakazi wawili wa helikopta ya Marekani ya Apache kuokolewa na droni ya majini ya Marekani siku ya Jumatatu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa jeshi la Marekani kutumia aina hiyo ya chombo katika operesheni ya uokoaji.
Maafisa wa Marekani walisema Iran ilitumia droni kushambulia helikopta hiyo, lakini bado haijathibitishwa kama shambulio hilo lilikuwa la makusudi. Shirika la habari la Mehr liliripoti kuwa Iran haijakiri kuhusika.
Centcom ilisema ndege za kivita za Marekani zilishambulia mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran, vituo vya udhibiti wa ardhini, na rada karibu na Mlango wa Hormuz.
Kwa upande mwingine, IRGC ilisema mashambulizi ya Marekani yameharibu mnara wa mawasiliano na matenki mawili ya maji.