Baada ya zaidi ya
saa 18 za mazungumzo, wadau katika sekta ya usafiri wa anga nchini Kenya
wamekubaliana kusitisha mgomo uliodumu kwa siku mbili.
Katika taarifa
iliyochapishwa mapema Jumanne, Waziri wa Uchukuzi wa Umma nchini Kenya, Davis
Chirchir, amesema: "Kufuatia makubaliano yaliyofikiwa, KAWU inatangaza
kusitisha mgomo huo mara moja na kuwaelekeza wafanyakazi walioathirika kurejea
katika majukumu yao ya kawaida."
Kwa sasa, pande zote zimeahidi kujitolea kurejesha haraka
shughuli za kawaida za usafiri wa anga, kudumisha amani ya viwanda na kutatua
malalamiko yoyote yaliyosalia au yatakayojitokeza baadaye kupitia mazungumzo,
upatanishi na mifumo iliyoanzishwa kisheria.
Hata hivyo, baadhi ya watu tuliozungumza nao wameeleza hofu
ya kukumbwa na ucheleweshaji wa safari kutokana na safari nyingi kuahirishwa
awali. Wengi wana hofu kuwa itachukua muda kabla ya hali ya kawaida kurejea.
Taarifa hii imekuja kama afueni kwa maelfu ya wasafiri
waliokwama katika viwanja vya ndege si tu nchini Kenya bali pia katika maeneo
mengine duniani. Maelfu ya wasafiri walikwama katika miji kama Doha, London na
Johannesburg wakisubiri safari ambazo zilitarajiwa kutua Nairobi au
kuunganishwa kupitia Nairobi, baada ya kuahirishwa kwa zaidi ya saa sita.
Kwa mujibu wa Chama cha Wahudumu wa Usafiri wa Anga nchini
Kenya (KAAO), Shirika la Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) na Shirikisho la
Utalii nchini Kenya (KTF), hasara iliyopatikana katika siku mbili za mgomo
huenda ikafikia dola bilioni moja za Marekani, sawa na ilivyoshuhudiwa mwezi
Februari mwaka huu wakati Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege nchini
Kenya (KAWU) kilipoitisha mgomo mwingine.
Kulingana na mwandishi huru na mtaalamu wa masuala ya
uchumi, Julian Amboko, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) una
umuhimu mkubwa kwa wasafiri wengi, hasa kutoka Afrika Magharibi ambao hutegemea
Kenya Airways kwa usafiri wao. Kwa sababu hiyo, safari nyingi kutoka eneo hilo
hupitia Nairobi, huku wengi wakitumia uwanja huo kuunganisha safari kuelekea
Ulaya, Mashariki ya Kati, Asia na mataifa ya Kusini mwa Afrika.
Wengi wameulizia iwapo viwanja vingine vya ndege katika
ukanda wa Afrika Mashariki vinaweza kuziba pengo linaloachwa wazi wakati wa
matatizo kama yale yaliyoshuhudiwa nchini Kenya katika siku mbili zilizopita.
Kulingana na Amboko, ikiwa Kenya haitafanya juhudi za
kupanua JKIA au kujenga uwanja mpya wa ndege, upanuzi wa viwanja vya ndege na
ujenzi wa viwanja vipya katika mataifa jirani unaweza kuiondoa JKIA katika
nafasi yake ya sasa kama kitovu kikuu cha usafiri wa anga katika ukanda huo kwa
kuzingatia idadi ya wasafiri wanaopita katika uwanja huo kila siku.
Baada ya mazungumzo ya siku nzima, Waziri wa Uchukuzi wa
Umma nchini Kenya, Davis Chirchir, alitangaza kwamba pande hizo zilikubaliana
kuwa ada za wakala zinazoshikiliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Kenya (KAA)
zitarejeshwa kwa KAWU mara moja.
Kuhusu masuala ya Mkataba wa Majadiliano ya Pamoja (CBA) wa
KCAA, Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) imejitolea kuwashirikisha wahusika
ndani ya mfumo husika wa kisheria na kiudhibiti, kwa kuzingatia uwezo wa
mashirika ya serikali yanayohusika kulipa.
Suala la mkataba wa utambuzi kati ya KAWU na Jambojet
linasubiri maelekezo ya mahakama. Pande hizo zimesema zinaheshimu mchakato
unaoendelea wa kimahakama na zitaendelea kuongozwa na matakwa yote ya kisheria
na kiutaratibu yanayohusiana na suala hilo.
Huku mgomo ukisitishwa kwa sasa, pande husika zinatarajiwa
kuendelea kufanya vikao vya kutatua malalamiko yaliyosalia ya wafanyakazi hao
katika wiki chache zijazo.
Kwa sasa, kampuni kama Kenya Airways na Jambojet zimetangaza
kurejelewa kwa safari za ndege, huku wasafiri wengi wakielekea viwanjani
kuthibitisha iwapo wataweza kusafiri kwa muda uliopangwa.