Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Wakaguzi wa nyuklia kutembelea Iran

"Ukaguzi utafanyika," mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi, aliwaambia waandishi wa habari nchini Japani.

Muhtasari

Moja kwa moja

Ambia Hirsi, Rashid Abdallah & Asha Juma

  1. Tunakamilisha matangazo yetu mubashara kwa sasa. Kwaheri.

  2. Ufaransa yaendelea kukubwa na joto

    Maelfu ya watu hawana huduma ya umeme kaskazini mwa Ufaransa huku wimbi la joto kali likiendelea kufukuta katika mataifa mengi ya magharibi mwa Ulaya.

    Joto limekuwa kali mno hapo jana huku Ufaransa ikishuhudia viwango vya joto vikivunja rekodi na hali ya tahadhari ikitangazwa na serikali.

    Italia, Hispania na Uingereza pia zimetahadharisha watu kuwa waangalifu wakati huu wa joto kali ambalo limetatiza shughuli za kawaida.

    Halijoto hii inatarajiwa kuenea Ulaya Mashariki katika siku chache zijazo, huku tahadhari ya joto hili ikitolewa kwa nchi kama vile Poland, Croatia na Hungary.

    Zaidi ya shule 500 nchini Wales zimefungwa kabisa na nyingine kwa muda kutokana na viwango vya juu vya joto.

  3. Mahakama yakataa kumuachia kwa dhamana wakili wa upinzani Uganda

    Mahakama nchini Uganda imekataa kumuachia kwa dhamana wakili wa upinzani anayekabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na vitendo vya uhaini.

    Hayo yanajiri baada ya Mkuu wa Majeshi Uganda ambaye pia ni mwana wa Rais Yower Museveni kujigamba kuwa alimteka.

    Erias Lukwago mwanasiasa na mwanasheria alifikishwa mahakamani wiki iliyopita akishitakiwa kwa kufeli kuripoti njama inayohusishwa na uhaini, waendesha mashitaka wakidai ilipangwa katika taifa jirani la Kenya kati ya 2021-2024, upande wa mashtaka ulisema.

    Eric Lukwago ambaye ni wakili na mwanasiasa mashuhuri nchini Uganda, anakabiliwa na hukumu ya kifungo cha maisha gerezani ikiwa atapatikana na hatia.

    Lukwago ni wakili wa mmoja wa wapinzani wakuu wa rais Yoweri Museveni. Kizza Besigye, ambaye yuko gerezani kutokana na mashtaka ya uhaini, tangu alipokamatwa nchini Kenya na kusafirishwa nyumbani mwaka wa 2024.

    Mwendesha mashtaka mkuu nchini Uganda amesema kuwa kesi ya Lukwago imejumuishwa na ile ya mteja wake na kiongozi wa upinzani Kizza Besigye.

    Lukawago amekanusha mashtaka dhidi yake na kuambia mahakama kuwa tangu kesi hiyo kuanza amekuwa wakili wa mshukiwa na kuhoji ni vipi wakili anaweza kuwa mshukiwa wa kesi ambayo anahusika nayo mahakamani.

    Mawakili wa Lukwago wameiomba mahakama kumuachilia kwa dhamani, kwa misingi ya afya yake lakini jaji anayesikiliza kesi hiyo alikataa ombi hilo.

    Jaji huyo aliagiza Lukwago kupelekewa hospitalini chini ya masaa 24 kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

    Familia ya wakili huyo imesema kuwa Lukwago alikamtwa wiki iliyopita na maafisa wa ulinzi ambao hawakujitambulisha.

    Soma Zaidi:

  4. Kenya haiwezi kuwa na uchaguzi huru katika mazingira ya vitisho – Tume Huru ya Uchaguzi Kenya

    Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imezindua mpango wa kina wa uchaguzi mkuu wa 2027, ukiweka wazi makataa muhimu ambayo vyama vya kisiasa, maafisa wa umma na wagombea wanaotarajiwa wanapaswa kuyazingatia kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 10 Agosti 2027.

    Muda huo umeainishwa katika Mpango wa Uendeshaji wa Uchaguzi (EOP) 2025–2027, mfumo unaotegemea Mpango Mkakati wa IEBC 2024–2029 na ulioundwa kuongoza upangaji, uratibu, utekelezaji na ufuatiliaji wa shughuli zote zinazoelekea katika uchaguzi huo.

    Akiongea wakati wa uzindizu wa mipangilio ya uchaguzi mkuu ujao, mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi nchini Kenya Erastus Ethelon, amesema kuwa uchaguzi mkuu nchini utafanyika tarehe kumi Agosti mwaka ujao.

    Aidha Ethelon amesema kuwa watumishi wote wa umma ambao wanapania kuwania viti vya kisiasa, wakati wa uchaguzi huo wanapaswa kujiuzulu ifikipo Februari mwaka ujao.

    Mwenyekiti huyo ameelezea wasi wasi wa tume hiyo kuhusiana na kuongezeka kwa ghasia za uchaguzi na wanasiasa kutumia fedha kuwashawishi wapiga kura wakati wa uchaguzi.

    Ameonya kuwa Kenya haiwezi kuwa na uchaguzi huru na wakuaminika katika mazingira ambayo imeghubikwa na vitisho, uvunjaji wa sheria na ukosefu wa usalama.

    Ethelon amesema kuwa kutokana na uchaguzi mdogo uliokamilika hivi karibu, tume hiyo ina wasi wasi kuwa visa vilivyoshuhudiwa vinaweza kutishia uhalali wa mchakato wa uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

    Amesema kuwa tume hiyo imeshuhudia visa ambavyo wanasiasa wanakusanya makundi ya vijana yaliyojihami na silaha butu wakati wa uchaguzi kwa madai ya kulinda kura.

    Ameongeza kuwa uhusiano wa siasa nchini Kenya na ghasia na Pesa inafanya majukumu ya tume hiyo kuwa magumu zaidi.

    Amesema vifo na majeruhi vimeripotiwa kutokana na ghasia kati ya makundi hasimu ya kisiasa, hali ambayo inatishia mchakato wa uchaguzi.

    Tume hiyo imesema kuwa tayari imechukua hatua dhidi ya makosa ya uchaguzi na itaendelea kufanya kazi na washikadau ili kuzuia ghasia na kulinda uadilifu wa chaguzi zijazo.

  5. Wanafunzi walioshtakiwa kwa mkasa wa moto shuleni Kenya kusalia rumande

    Wanafunzi walioshtakiwa kwa kuwasha moto shule ya Utumishi Academy watabaki rumande kusubiri kusomewa shtaka la mauaji.

    Mahakama Kuu ya Naivasha imekubali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuwashikilia washukiwa wanane wanaohusishwa na kisa cha moto katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Utumishi kwa siku mbili zaidi.

    Amri hiyo ilitolewa leo na Hakimu Mkuu Abdulqadir Ramadhan Lorot wakati shauri hilo lilipokuja kutajwa ili kuthibitisha hali ya uchunguzi na kutoa maelekezo zaidi.

    Hata hivyo, mahakama iliamuru kuachiliwa kwa mmoja wa washukiwa na kuelekeza akabidhiwe kwa wazazi wake baada ya uchunguzi kubaini kuwa hakuwa na hatia katika kutekeleza kosa hilo.

    Washukiwa wanane waliobaki wataendelea kushikiliwa kisheria na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani tarehe 26 Juni 2026

    Wakisubiri kufikishwa mahakamani, mahakama imeelekeza kuwa washukiwa hao wazuiliwe katika Kituo cha Kulelea Watoto cha Nakuru au Kituo cha Kulelea Watoto cha Nairobi.

    Soma Zaidi:

  6. Wakaguzi wa nyuklia kutembelea Iran

    Mkuu wa shirika la kimataifa la ulinzi wa nyuklia amesema timu ya shirika hilo itafanya ukaguzi nchini Iran chini ya makubaliano ya awali ya amani kati ya nchi hiyo na Marekani.

    "Ukaguzi utafanyika," mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, Rafael Grossi, aliwaambia waandishi wa habari nchini Japani. "Tutaeleza kuhusu tarehe, taratibu, maeneo - hivi karibuni."

    Mkataba uliosainiwa wiki iliyopita ulisema "wazi" uyeyushaji wa urani iliyorutubishwa utafanywa chini ya usimamizi wa IAEA, aliongeza.

    Hata hivyo, naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran alisema ufikiaji wa vituo vyake vya nyuklia vilivyoharibika na nyenzo za nyuklia utaelezwa ndani ya makubaliano ya mwisho na Marekani.

    Maoni ya Grossi yanakuja huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio akizuru mataifa ya Ghuba kujadili makubaliano ya Marekani na Iran. Siku ya Jumatano alikutana na Rais wa UAE Mohamed bin Zayed Al Nahyan na anatarajiwa kusafiri hadi Kuwait na Bahrain.

    Makubaliano ya awali kati ya Marekani na Iran pia yalisema Iran itaruhusu meli kupita katika Mlango-Bahari wa Hormuz huku Marekani ikiondoa kizuizi cha majini kwenye bandari za Iran.

    Siku ya Jumatano bei ya mafuta ghafi ilishuka kwa mara ya kwanza tangu vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vianze.

    Wakati huo huo Umoja wa Mataifa ulisema baadhi ya meli tayari zimepita chini ya mpango wa kuwahamisha maelfu ya mabaharia ambao wamekwama kwenye meli kutokana na vita.

    Grossi alisema ukaguzi huo utafanyika kwa ushirikiano na serikali ya Iran. "Iwe hili litatokea kesho, au ndani ya wiki moja, au ndani ya siku 10, ni muhimu."

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi, alionekana kupinga maoni hayo.

    Chini ya makubaliano ya vipengele 14, Marekani na Iran zimeahidi kujadili makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60.

    Kabla ya kuanza kwa vita kati ya Marekani na Israeli na Iran tarehe 28 Februari, IAEA iliripoti kwamba Iran ilikuwa na kilo 440 (pauni 970) za urani ambazo zilirutubishwa hadi 60%, ambayo ni karibu na kiwango cha silaha. Kiwango hicho kingetosha, ikiwa kingerutubishwa hadi 90%, kwa mabomu 10.

    Iran inasisitiza shughuli zake za nyuklia ni za amani na haitajaribu kamwe kutengeneza au kupata silaha za nyuklia.

    Chini ya makubaliano ya mwaka 2015 na Marekani na mataifa mengine matano yenye nguvu duniani, Iran ilikubali kupunguza shughuli zake za nyuklia na kuruhusu ufuatiliaji.

    Hata hivyo, Trump aliachana na makubaliano hayo wakati wa muhula wake wa kwanza mwaka 2018, na akarejesha vikwazo vya Marekani.

    Iran ililipiza kisasi kwa kukiuka zaidi makubaliano hayo, hasa vile vinavyohusiana na urutubishaji wa urani.

    Soma Zaidi:

  7. Mwanamke aliyeshambuliwa na papa azinduka baada ya wiki moja

    Mwanamke aliyeumwa na papa zaidi ya wiki moja iliyopita alipokuwa akiogelea katika ufuo maarufu wa Sydney, Australia amezinduka kutoka kwenye hali ya kukosa fahamu, familia yake imesema.

    Leah Stewart alishambuliwa na papa Jumamosi tarehe 13 Juni katika Ufuo wa Coogee, na kutafunwa mara kadhaa mikononi na miguuni na kupoteza damu nyingi.

    Mama huyo mwenye umri wa miaka 34 alipelekwa hospitalini akiwa katika hali mbaya na kufanyiwa upasuaji kadhaa ikiwemo kukatwa mkono wake.

    Siku ya Jumanne, kaka yake alisema bado yuko katika chumba cha wagonjwa mahututi na alifanyiwa upasuaji kwa siku tano katika wiki iliyopita, huku upasuaji mingine itafanyika katika wiki zijazo.

    Stewart, mwalimu, alikwenda Coogee Beach Jumamosi asubuhi kuogelea na alikuwa ndani ya maji karibu na ufuo wakati shambulio hilo lilipotokea.

    Kumekuwa na mfululizo wa mashambulizi ya papa nchini Australia mwaka huu, huku mashambulizi manne katika kipindi cha siku mbili mwezi Januari yakihusisha mvulana mdogo aliyeng'atwa kwenye ufuo wa Sydney na baadaye akafa kutokana na majeraha yake hospitalini.

    Mwezi uliopita, kulikuwa na mashambulizi mawili mabaya ya papa ambapo mtu mmoja aliuawa na papa huko Queensland alipokuwa akivua samaki kwa mkuki na huko Australia Magharibi, baba wa watoto wawili Steven Mattaboni, mwenye umri wa miaka 38, alifariki baada ya kuumwa na papa mwenye urefu wa mita 4 (futi 13).

    Pia unaweza kusoma:

  8. Zaidi ya shule 1,000 zimefungwa huku joto kali likiongezeka Uingereza

    Zaidi ya shule 1,000 nchini Uingereza na Wales zimefungwa mapema huku halijoto ikipanda kote Uingereza.

    Kusini mwa Uingereza kunatabiriwa viwango vya juu vya joto vya takriban 37C leo na watabiri wa hali ya hewa wanaeleza halijoto "inaonekana" inaweza kuwa kubwa zaidi.

    Ni kiwango kikubwa zaidi kwa mujibu wa Ofisi ya Met na inamaanisha kunaweza kuwa na hatari kwa maisha pamoja na kutatiza usafiri.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Ufaransa yathibitisha kisa cha kwanza cha Ebola

    Ufaransa imethibitisha kisa cha kwanza cha Ebola, kutoka kwa daktari ambaye amerejea kutoka misheni ya kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Daktari huyo "alilazwa mara moja katika kituo maalum" na yuko katika hali nzuri, wizara ya afya ya Ufaransa imesema Jumatano.

    DR Congo ilitangaza mlipuko wa Ebola mwezi uliopita, lakini wataalamu wanaamini virusi hivyo vilianza kusambaa kwa wiki kadhaa kabla.

    Zaidi ya watu 260 wamethibitishwa kufariki kutokana na virusi hivyo katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati, huku watu 1,000 wakiambukizwa.

    Katika taarifa yake siku ya Jumatano, wizara ya afya ya Ufaransa ilisisitiza kwamba hatari kwa watu iko "chini sana".

    Iliongeza kuwa mamlaka inafanya kazi kuwatafuta watu ambao huenda wamekutana na daktari huyo.

    Wafanyakazi wa afya wako katika hatari kubwa ya kupata Ebola, ambayo husambazwa kupitia majimaji ya mwili.

    Mlipuko wa sasa wa Ebola unasababishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo, ambavyo kwa sasa hakuna chanjo yake.

    Wizara ya afya ilisema Ufaransa imeanzisha "mfumo maalum wa ufuatiliaji" kwa wafanyakazi wa misaada wanaorejea kutoka DR Congo.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Mwanamke anayesema alishikiliwa mateka na mumewe kwa miaka 12 ameokolewa Pakistan

    Polisi nchini Pakistani wamemkamata mwanaume mmoja ambaye inadaiwa alimshikilia mke wake na watoto wake mateka nyumbani na kuwatendea vibaya kwa zaidi ya muongo mmoja.

    Mkewe, raia wa Ufaransa anayeitwa Sylvie Yasmina, anadai mwanaume huyo alishambulia familia yake kimwili na kiakili "kila siku" na kumtaja kama "mkali sana", polisi wa eneo hilo waliambia BBC Urdu.

    Mmoja wa wana wao alifanikiwa kutoka kisiri ili kutoa ripoti polisi, jambo lililosababisha uvamizi wa nyumba yao huko Bara, mji wa mbali katika jimbo la milimani la Khyber Pakhtunkhwa.

    Polisi waliwapata Yasmina na watoto wake watano katika chumba chenye msongamano na "chakavu sana", wakiwa na michubuko miilini mwao.

    Yasmina na watoto wake wamepelekwa kwenye makazi ya wanawake huko Peshawar. Polisi wanasema wanapanga kurejea Ufaransa.

    Kulingana na Yasmina, mwenye umri wa miaka 54, mumewe "alikuwa amewafunga gerezani" familia hiyo tangu walipohamia Pakistan kutoka Australia mwaka 2014.

    "Kulingana na mwanamke huyo... Hakuruhusiwa kukutana na mtu yeyote, watoto wao wawili wakubwa hawakusomeshwa shuleni, huku watoto watatu wadogo wakizaliwa Pakistani na hawakuwahi kujiandikisha shuleni," afisa mkuu wa polisi aliambia BBC Urdu.

    Mamlaka hazijataja jina la mume wa Yasmina, raia wa Pakistani ambaye wanasema alikuwa "akiishi kinyume cha sheria" nchini Australia wakati wanandoa hao walipokutana.

    Walioana mwaka 2003 na kuishi Australia hadi mwaka wa 2014, walipohamia Pakistani na watoto wao wawili wakubwa. Yasmina anadai kuwa hajawasiliana na ulimwengu wa nje tangu wakati huo.

    "Tulinyimwa uhuru [wetu], mume wangu hakututunza jinsi anavyopaswa kama mume na baba wa watoto wangu. Anatupiga na kuweka shinikizo katika maisha yetu kila siku," Yasmina aliandika katika taarifa yake kwa polisi, ambayo sehemu zake zimechapishwa na vyombo vya habari vya ndani.

    "Nilihisi mustakabali wangu tayari umeharibika, mustakabali wa watoto pia ungeharibika."

    Pia unaweza kujibu:

  11. Kenya kuwashtaki wanafunzi kwa mauaji kufuatia moto uliosababisha vifo shuleni

    Waendesha mashtaka wa Kenya wanasema wanajiandaa kuwashtaki wanafunzi kadhaa kwa mauaji ya wanafunzi wenzao kufuatia shambulio la kuchoma moto shule mwezi uliopita.

    Wanafunzi kumi na sita, wenye umri wa kati ya miaka 15 na 18, walifariki na wengine kadhaa walijeruhiwa wakati moto ulipozuka katika bweni la Shule ya Wasichana ya Utumishi huko Gilgil, yapata kilomita 120 (maili 77) kaskazini-magharibi mwa mji mkuu, Nairobi.

    Wanafunzi wanane walikamatwa baada ya polisi kusema huenda walihusika katika kuchoma moto kwa kuwasha magodoro karibu na njia ya kutokea.

    "Baada ya kutathmini kwa makini ushahidi, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameidhinisha mashtaka dhidi ya wanafunzi wanaotuhumiwa," ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali ilisema katika taarifa.

    Moto wa Mei 28 uliharibu ghorofa ya juu ya bweni lenye vitanda 135 vya kulala na malazi ya wanafunzi 202, na kuwalazimisha kukimbia kupitia mlango mmoja baada ya njia ya dharura kushindwa kufunguliwa.

    Baada ya mahojiano na wanafunzi na wafanyakazi na uchunguzi wa picha za CCTV, wanafunzi wanane shuleni walishikiliwa kuhusiana na mipango na utekelezaji" wa moto huo," polisi walisema.

    Washukiwa hao, ambao wanazuiliwa, wanatarajiwa kushtakiwa rasmi mahakamani, kufuatia mapitio ya ushahidi uliokusanywa na wachunguzi.

    "Washukiwa watakabiliwa na mashtaka kumi na sita (16) ya mauaji yanayotokana na tukio hilo," ilisema Ofisi ya DPP.

    Waendesha mashtaka hawakusema ni washukiwa wangapi watakaoshtakiwa au ni lini mashtaka hayo yatafikishwa mahakamani. Wanafunzi hao wanatarajiwa kufika mahakamani mjini Naivasha siku ya Jumatano.

    Kenya ina historia ndefu ya moto shuleni - miaka miwili tu iliyopita watu 21 walikufa katika moto wa bweni katikati mwa Kenya.

    Msongamano mkubwa katika mabweni na kushindwa kufuata miongozo ya usalama, kama vile kuweka njia za kutokea wazi na madirisha yakiwa wazi, mara nyingi husababisha idadi kubwa ya majeruhi.

  12. Marekani inachunguza madai ya makampuni ya mafuta 'kuwapunja' wateja - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza makampuni makubwa ya nishati kuchunguzwa baada ya madai kuibuja kwamba ''wanawapunja'' wateja kwa kutopunguza bei ya petroli licha ya gharama ya mafuta ghafi kushuka katika masoko ya kimataifa.

    Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii kwamba ameamuru Idara ya Haki (DOJ) "kuanza mara moja kuchunguza hili", akiongeza kuwa anatarajia kuona bei ya petroli ikishuka "haraka zaidi kuliko ninavyoona."

    Hakutaja kampuni zozote za mafuta kwenye chapisho hilo.

    Matamshi yake yanakuja baada ya bei ya mafuta kushuka baada ya kupanda zaidi wakati wa wa vita vya Iran lakini badobei ya bidhaa hiyo iko juu kuliko kabla ya mzozo kuanza.

    BBC imewasiliana na DOJ na Ikulu ya White House kupata ufafanuzi zaidi.

    Marekani na Israel ziliposhambulia Iran tarehe 28 Februari. Tehran ilijibu mashambulizi ya Marekani na Israel kwa kufunga Mlango wa Bahari wa Hormuz Strait hatua ambayo ilivuruga sana usafirishaji wa mafuta na gesi na kusababisha bei ya nishati duniani kupanda.

    Soma zaidi:

  13. Marekani na Israel zina 'mpango wa kukabidhi' jeshi la Lebanon eneo la kusini mwa nchi hiyo

    Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa Israel na Lebanon zinafanya mradi wa majaribio unaoungwa mkono na Marekani ambapo majeshi ya Israel yatakabidhi udhibiti wa sehemu za kusini mwa Lebanon kwa jeshi la nchi hiyo.

    Shirika la habari la Reuters, limewanukuu maafisa watatu waandamizi wa Israel, na kuripoti kwamba vikosi vya Lebanon vilivyohusika katika mpango huo vitapitia mafunzo ya Marekani na ukaguzi wa usalama ili kuhakikisha kuwa havina uhusiano na Hezbollah.

    Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Israel itasalia katika eneo hilo hadi usalama wa maeneo ya kusini mwa Lebanon utakapokabidhiwa kwa wanajeshi wa Lebanon.

    Marekani na Israel bado hazijathibitisha rasmi taarifa hiyo.

    Mazungumzo kati ya Israel na Lebanon yanaendelea leo mjini Washington.

    Suala la kujiondoa majeshi na kusitisha vita kwa pande zote, ikiwemo Lebanon, ni kipengee cha kwanza cha mkataba wa maelewano kati ya Marekani na Iran.

    Unaweza kusoma:

  14. Trump alisuta bunge la Marekani kwa kusitisha hatua za kijeshi dhidi ya Iran: Hii ni kumsaidia adui

    Rasi wa Marekani Donald Trump amekosoa vikali kura ya Seneti ya Marekani kuhusu azimio la kutaka kusitishwa kwa hatua za kijeshi dhidi ya Iran.

    Trump aliandika kwamba maseneta hao walituma ujumbe kwa Iran kwamba "hawajafurahishwa na hatua zangu dhidi yao na ni lazima nisitishe mapigano. Wamemsaidia adui."

    Aliendelea kusema: ''Nilikuwa nimeiweka Iran chini ya shinikizo kali, walikuwa tayari kurudi nyuma, na walikuwa karibu kutupatia chochote. Kwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa, Iran iliiheshimu sana Marekani na rais wake, (mimi). Lakini Bunge la Seneti la Marekani liliamua wakati mbaya zaidi, kupiga kura isiyo na maana ya Sheria ya Nguvu za Kivita,

    Anasema Warepublican wanne walipiga kura na Democrats, na sasa Iran inawauliza wawakilishi wangu, 'Kura hii inamaanisha nini?'.

    ''Maseneta hawa wamefanya kazi yangu kuwa ngumu zaidi, lakini sitarudi nyuma, hata iweje, kwa sababu hivyo ndivyo ninavyofanya kazi kila wakati!".

    Soma Zaidi:

  15. Oman yatangaza kuunda njia ya muda ya baharini kuwezesha meli kupita Hormuz

    Oman imetangaza kuanzisha njia ya muda ya baharini kwa ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) ili kurahisisha usafiri wa meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Shirika la habari la serikali ya Oman liliripoti kwamba meli zinazonuia kuvuka Mlango-Bahari wa Hormuz lazima zifanye mipango inayohitajika na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini na mamlaka ya Oman.

    Taarifa hizi zinakuja saa chache baada ya Mohammad Baqer Qalibaf, mkuu wa ujumbe wa wanadiplomasia wa Iran, kuzuru nchi hiyo.

    Ilikuja baada ya Iran na Oman kutangaza katika taarifa ya pamoja siku ya Jumanne kwamba zimejitolea kudumisha Mlango-Bahari wa Hormuz kama njia ya maji salama na iliyo wazi kwa meli za kimataifa, wakati huo huo zikitilia mkazo uhuru wao na haki zao za kujitawala juu ya eneo la bahari la Hormuz.

    Pia wametangaza kwamba watachunguza usimamizi wa siku zijazo wa Mlango-Bahari wa Hormuz na gharama ya huduma zinazotolewa katika njia hii ya maji kwa kuunda kamati ya pamoja.

    Kauli hiyo imetolewa baada ya mkutano kati ya maafisa wakuu kutoka nchi hizo mbili mjini Muscat.

    Baada ya kuondoka Uswizi, Mohammad Baqer Qalibaf, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Iran na Abbas Araqchi,

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran walikwenda Oman na kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Badr Busaidi na Sultan Haitham bin Tariq, Mfalme wa Oman.

    Siku ya Jumanne, Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini, ambalo ni mshirika wa Umoja wa Mataifa,

    lilitangaza kuanza kwa mchakato wa kuwarejesha nyumbani wanamaji zaidi ya 11,000 waliokuwa wamenasa kwenye Mlango Bahari wa Hormuz; mabaharia ambao wamekwama katika eneo hilo tangu vita vya Marekani na Israel na Iran na kuzuiliwa kwa trafiki katika Mlango wa bahari wa Hormuz.

    Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini limesema kuwa operesheni ya kuwahamisha mabaharia hao itafanywa kwa ushirikiano wa karibu na nchi zote za eneo hilo na Marekani.

    Maelezo zaidi:

  16. Kombe la Dunia 2026: DRC yalazwa na Colombia

    Katika mechi ya mwisho siku ya Jumanne, timu ya soka ya Colombia ilifanikiwa kuishinda DRC Congo kwa bao moja na kujihakikishia kusonga mbele kwa pointi 6.

    Colombia walianza mchezo kwa kasi kuanzia dakika za kwanza kabisa, na mshambuliaji wa timu hiyo Luis Diaz, alifunga dakika ya 10, lakini mwamuzi akatangaza kuwa ameotea.

    Diaz pia alifunga bao zuri mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kuwapiga chenga walinzi kadhaa wa Congo, lakini mwamuzi akakataa tena kuwa ameotea mara tu alipopata pasi.

    Mchezaji wa Colombia Mones, hatahivyo aliifungia Colombia bao la pekee katika dakika ya 76.

    Hivyo, Colombia, ambayo ilikuwa imeishinda Uzbekistan katika mechi ya kwanza, ilipata pointi 6 kupitia ushindi huo na kuwaweka kileleni mwa jedwali juu ya Ureno na kusonga mbele.

    Soma:

  17. 'Nimerudi' - Ronaldo awajibu wakosoaji baada ya kuvunja rekodi

    "Nimerudi! Nimerudi!" alisema Baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 5-0 wa timu yake dhidi ya Uzbekistan, Cristiano Ronaldo alikodolea macho kamera ya televisheni na kuwakejeli kwa wale waliodai kuwa yeye ndiye tatizo la Ureno kwenye Kombe la Dunia la 2026.

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41 hakuweza kuficha hisia zake, wala kuzuia furaha yake alipokuwa akisherehekea mafanikio ya kihistoria ya kuwa mchezaji wa kwanza kuzifumania nyavu katika matoleo sita ya michuano hiyo mikubwa zaidi ya kandanda. Ilikuwa pia jibu kamili kwa wakosoaji ambao walikuwa wamempuuza.

    Ronaldo alikosolewa vikali baada ya Ureno kutoka sare ya 1-1 na DR Congo katika mechi yao ya kwanza ya Kundi K, huku nyota wengine wa kimataifa wakiwemo Lionel Messi wa Argentina, mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe, Erling Haaland, wa Norway, Vinicius Jr wa Brazil na nahodha wa Uingereza Harry Kane wote wakionyesha umahiri wao katika wiki mbili za kwanza za michuano ya Kombe la Dunia 2026.

    Ronaldo alihitaji dakika sita pekee kufunga bao lake la kuvunja rekodi, akitumia vyema krosi ya Joao Cancelo, na kisha akafunga bao lengine kabla ya kipindi cha mapumziko kwa ushirikiano na Bruno Fernandes.

    Licha ya juhudi za wachezaji wenzake kipindi cha pili, nahodha huyo wa timuya taifa ya Ureno hakufanikiwa kupata hat-trick aliyotamani.

    Maelezo zaidi:

  18. Umoja wa Mataifa kuwahamisha mabaharia waliokwama katika Mlango-Bahari wa Hormuz

    Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya baharini (IMO) linajianda kuwahamisha zaidi ya mabahari 11,000 ambao wamekwama katika eneo la Ghuba kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Katibu mkuu wa IMO Arsenio Dominguez amesema "operesheni hiyo kubwa" itafanywa kwa ushirikiano na Iran, Oman, Marekani, mataifa mengine ya pwani katika eneo hilo.

    "Tumehakikishiwa usalama wetu na tumethibitisha kwa kina masharti ya urambazaji salama ili kusaidia shughuli hizi," aliongeza.

    Makubaliano ya muda yalitiwa saini wiki iliyopita ili kumaliza mzozo huo, lakini Marekani na Iran zinaendelea kuzozana kuhusu maelezo ya Mkataba wa Maelewano (MoU).

    Marekani imesema Makubaliano hayo yanajumuisha hakikisho la mpango wa silaha za nyuklia wa Iran kufanyiwa ukaguzi na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).

    Rais wa Marekani Donald Trump alichapisha ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii Jumanne kusema kuwa: "Iran imekubali kufanywa jwa ukaguzi wa Nyuklia wa kiwango cha juu zaidi hadi siku zijazo (usio na kikomo!!!). Hii itahakikisha 'Usalama wa Nyuklia.'

    Muda mfupi kabla ya ujumbe huo wa Trump, Iran ilisema shirika hilo la Umoja wa Mataifa halitaweza kukagua maeneo ya nyuklia yaliyolipuliwa na Marekani na Israel mwaka jana.

    Soma zaidi:

  19. Bunge la Marekani laidhinisha mpango wa kusitisha vita na Iran

    Bunge la Seneti la Marekani linalodhibitiwa na chama cha Republican limeidhinisha mswada ambao utamlazimu Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha vita na Iran au kutafuta kibali cha bunge kabla ya kuendelea na hatua za kijeshi.

    Katika kura iliyopigwa Jumanne jioni, maseneta kadhaa wa chama cha Republican walijiunga na wenzao wa Democratic kupitisha mswada huo kwa kura 50 dhidi ya 48, hatua inayoonyesha upinzani wa pande mbili dhidi ya kuendeleza vita.

    Mswada huo pia ulipitishwa katika Bunge la Wawakilishi la Marekani mwezi Juni, ambapo wabunge wanne wa Republican walipiga kura ya ndio pamoja na wabunge wate wa Dempcratic wote, na matokeo yakiwa 215 kwa 208.

    Hii ni mara ya kwanza tangu kupitishwa kwa Sheria ya Nguvu za Kivita mwaka 1973 ambapo mabunge yote mawili ya Marekani yamepitisha azimio la pamoja la kusitisha hatua ya kijeshi ya rais.

    Hata hivyo, azimio hilo kwa kiasi kikubwa ni la kiishara, kwani licha ya kuidhinishwa na mabunge yote mawili, halitatumwa kwa rais kutiwa saini na halilazimishi kisheria.

    Umuhimu wa kura hii ni kwamba inaongeza shinikizo kwa Ikulu ya White House kumaliza vita na Iran, haswa wakati huu ambapo bei ya mafuta imepanda na upinzani wa umma dhidi ya vita hivyo umeongezeka.

    Hata hivyo, afisa wa Ikulu ya White House aliambia BBC kwamba tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalikubaliwa Aprili 7, kwa sasa hakuna mzozo wowote ambao utahitaji kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani.

    Soma Zaidi:

  20. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.