Vikosi vya usalama Uganda vyashuhumiwa kuwaua raia wasio na silaha - ripoti

Chanzo cha picha, EPA
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limevishutumu vikosi vya usalama vya Uganda kwa kuwaua raia, kuwakamata kiholela na kuwatesa wafuasi wa upinzani katika kipindi cha kuelekea na baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 15 Januari nchini humo.
Katika taarifa iliyotolewa leo, shirika hilo limesema takriban watu 16 huenda waliuawa kati ya Januari 15 na Januari 18 na wanajeshi na polisi kwa kutumia nguvu zisizo halali.
Inasemekana kuwa waathiriwa hawakuwa na silaha na hawakuwa na tishio lolote.
BBC imewasiliana na mamlaka ya Uganda kupata maoni.
Dhuluma hizo zinazodaiwa kuwalenga wafuasi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), kinachoongozwa na Bw. Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu Bobi Wine ambaye sasa amejihami nchini Marekani.
Amnesty inasema ilinakili matukio 10 ya matumizi ya nguvu kukabili upinzani katika wilaya kadhaa, ikiwa ni pamoja na Butambala, Bulenga na Luwero katikati mwa Uganda.
Katika kisa kimoja, wanajeshi waliripotiwa kuvamia nyumba ya mwanasiasa wa upinzani usiku wa uchaguzi na kuwapiga risasi watu saba waliokusanyika hapo.
Mashahidi waliiambia shirika hilo kwamba hakuna hata mmoja wa wahasiriwa aliyekuwa na silaha.
Ripoti za ukaguzi wa maiti zilizokaguliwa na Amnesty zilithibitisha kwamba watu kadhaa walifariki dunia kutokana na majeraha ya risasi.










