Rais wa Mali Goïta ajiteua kuwa Waziri wa Ulinzi
Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Meja Jenerali Assimi Goïta, amejiteua kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi, akiongeza wadhifa huo kwenye nafasi yake ya sasa ya Rais wa mpito.
Hatua hiyo inafuatia kuuawa kwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Sadio Camara, katika mashambulizi yaliyoratibiwa na wapiganaji wa JNIM pamoja na waasi wa Tuareg FLA. Camara alikuwa na mchanfgo mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na Urusi, hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa jeshi la Mali.
Kama Waziri wa Ulinzi, Goïta ambaye alitwaa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi, sasa ataongoza moja kwa moja vyombo vya usalama akisaidiwa na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo, Jenerali Oumar Diarra, aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi.
Mali kwa sasa inakabiliwa na ongezeko kubwa la mashambulizi na kupoteza maeneo kadhaa kwa makundi ya wapiganaji.
Goïta aliingia madarakani mwaka 2020 akiwa na cheo cha kanali, kabla ya kupanda hadi kuwa Jenerali ndani ya miaka minne.
Wachambuzi wanamkosoa wakisema hajafanikiwa kutimiza ahadi yake ya kurejesha usalama licha ya msaada wa kijeshi kutoka Moscow.