Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Ulaya yataka kushiriki mazungumzo ya amani Ukraine, Putin aweka masharti

Ulaya yasema iko tayari kufanya mazungumzo na Urusi kumaliza Vita vya Ukraine

Muhtasari

Ulaya yataka kushiriki mazungumzo ya amani Ukraine, Putin aweka masharti

Moja kwa moja

Na Faidha Ngaga

  1. Mchungaji amekutwa na hatia ya kuhusika na mauaji ya Rais wa Haiti

    Mchungaji mmoja kutoka jimbo la Florida nchini Marekani amepatikana na hatia ya makosa kadhaa yanayohusiana na mauaji ya aliyekuwa Rais wa Haiti, Jovenel Moïse.

    Christian Emmanuel Sanon, raia mwenye uraia wa Marekani na Haiti, amepatikana na hatia ya mashtaka yote manane yaliyokuwa yakimkabili, yakiwemo ya kula njama ya kumuua au kumteka nyara mtu. Anakabiliwa na uwezekano wa kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.

    Sanon, mwenye umri wa miaka 67, alishtakiwa kwa kuhusika katika mpango wa kumuondoa madarakani Moïse na kujichukua nafasi ya urais wa Haiti mwaka 2021. Inadaiwa kuwa alikusudia kufanya hivyo ili baada ya kushika madaraka, aweze kutoa mikataba yenye thamani kubwa kwa kampuni ya ulinzi yenye makao yake Florida.

    Mauaji ya Moïse yameiacha Haiti bila kiongozi kwa kipindi cha miaka mitano. Pengo hilo la uongozi limechangia kuongezeka kwa machafuko yanayosababishwa na magenge ya uhalifu katika taifa hilo maskini la eneo la Caribbean.

    Uchaguzi wa rais umepangwa kufanyika mwaka ujao, huku mke wa Moïse, Martine, ambaye alijeruhiwa katika shambulio lililomuua mumewe, akitangaza wiki hii kuwa anakusudia kugombea urais.

    Kwa mujibu wa CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani, Sanon alipatikana na hatia siku ya Jumatano baada ya kesi iliyodumu kwa wiki nane katika mahakama ya shirikisho mjini Miami.

    Wakili wake amesema Sanon bado anasisitiza kuwa hana hatia na anakusudia kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

    Waendesha mashtaka wamesema Sanon alikuwa na "matamanio ya kisiasa" nchini Haiti na kwamba mwezi Aprili 2021 alikutana na washirika wengine wa njama hiyo kupanga mpango wa kumuondoa Moïse madarakani kupitia shambulio la kutumia silaha katika kasri la rais mjini Port-au-Prince, mji mkuu wa nchi hiyo.

    Miongoni mwa washirika hao walikuwa wakuu wa kampuni za Counter Terrorist Unit Federal Academy na Counter Terrorist Unit Security, ambazo kwa pamoja zilijulikana kama CTU.

    Kampuni hizo zilitarajiwa kufadhili mapinduzi hayo kwa kubadilishana na kupata mikataba ya serikali ya kutekeleza miradi ya miundombinu, pamoja na kutoa vikosi vya ulinzi na vifaa vya usalama.

  2. Mwanamke aliyedungwa dawa na kubakwa na mumewe pamoja na wanaume wengine azungumza.

    Mwanamke aliyedungwa dawa, kubakwa na kutangazwa mtandaoni kwa ajili ya ngono na mumewe amesema "hatawahi kujisikia salama kabisa" baada ya wanaume wanne kupatikana na hatia ya kumfanyia unyanyasaji wa kingono, katika kesi ya kwanza ya aina hiyo nchini England.

    Joanne Young, ambaye ameamua kuondoa haki yake ya kutotajwa jina, amesema: "Mtu niliyemwamini zaidi duniani alinigeuka na kunisaliti kwa njia ya kutisha zaidi."

    Philip Young, mwenye umri wa miaka 50, tayari alikuwa amekiri makosa mbalimbali ya kumdunga dawa na kumbaka mkewe kwa kipindi cha miaka 13 katika nyumba yao mjini Swindon, Wiltshire. Aliwaalika wanaume kupitia tovuti na programu kama Craigslist, Grindr na Fab Swingers kwenda nyumbani kwao bila mkewe kujua.

    Siku ya Alhamisi, Norman Macksoni, 48, Richard Wilkins, 62, Connor Sanderson-Doyle, 32, na Mohammed Hassan, 38, walipatikana na hatia ya makosa mbalimbali ya kingono na jopo la majaji katika Mahakama ya Winchester Crown. Wilkins na Macksoni kila mmoja alipatikana na hatia ya kosa moja la ubakaji.

    Joanne Young, ambaye alitalikiana na Philip Young mwaka jana, amesema unyanyasaji huo "umeninyang'anya maisha yangu kama nilivyokuwa nikiyafahamu".

    Akizungumza nje ya mahakama, alisema: "Kilichonitokea hakikuwa kitendo cha mtu mmoja pekee, wengine walialikwa kushiriki na wao wakachagua kufanya hivyo."

    Joanne Young amesema uhalifu uliofanywa dhidi yake umekuwa na "athari kubwa na ya kutisha kwa maisha yangu na ya watoto wangu".

    Alisema: "Ninaishi na maumivu ambayo ni vigumu kuyaelezea kwa maneno, na jambo hili litaathiri maisha yetu milele. Inatisha kufikiria kuwa jambo hili linaweza kumtokea mtu yeyote."

    Unaweza pia kusoma:

  3. Ulaya yataka kushiriki mazungumzo ya amani Ukraine, Putin aweka masharti

    Viongozi wa Ulaya wamesema wako tayari kufanya mazungumzo na Russia kuhusu kumaliza vita vya Ukraine, katika ishara kubwa ya kuunga mkono Kyiv.

    "Ulaya ina msimamo wa wazi, thabiti na wa pamoja katika mazungumzo," amesema Waziri Mkuu wa Uingereza, Andy Burnham, huku Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, akisisitiza kuwa "madai ya Moscow ya kutaka mambo mengi kupita kiasi si ya kweli".

    Viongozi hao walikuwa wakizungumza katika mkutano wa Berlin wa washirika wa Ukraine, unaojulikana kama Coalition of the Willing.

    Jared Kushner, mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye ni mmoja wa wajumbe wawili wa Marekani waliokuwa Berlin, amesema rais huyo anataka kufikia makubaliano na Moscow "akiwa na Ulaya upande wake". Hata hivyo, Rais wa Russia Vladimir Putin amekuwa akikataa hadi sasa Ulaya kushiriki katika mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani.

    Trump awali alifanya mazungumzo ya kihistoria ya pande tatu mjini Shenzhen, kusini-mashariki mwa China, na Putin pamoja na Rais wa China Xi Jinping, na baadaye alishiriki kwa njia ya simu katika mkutano wa Berlin akiwa ndani ya ndege ya Air Force One.

    Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofuata mazungumzo hayo na Trump pamoja na Xi, Putin alizungumzia suala la mazungumzo ya amani yanayohusisha mataifa mbalimbali, akisema Marekani imekuwa ikiitaka Russia "kwa msisitizo" kuruhusu mataifa ya Ulaya kushiriki.

    Putin alidai Russia haipingi wazo hilo, lakini alisema Moscow inataka kufahamu "Ulaya italeta nini katika mazungumzo hayo".

    "Ndiyo maana, kupitia njia za kidiplomasia, tumewaalika Wazungu kuja Moscow ili kubainisha misimamo yao. Baada ya hapo, tutaamua ni kwa mfumo gani tutaendeleza mazungumzo na Ukraine," alisema.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 20/11/2026.