Ufaransa inatafuta uhusiano zaidi ya wa kikoloni na viongozi wa Afrika

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ikishutumiwa kwa ukoloni mamboleo kuingilia kati katika nchi nyingi za Afrika ambapo kwa kawaida imekuwa na uhusiano wa karibu, Ufaransa inapanua wigo wake kwa kuandaa mkutano wa viongozi wa Afrika nchini Kenya inayozungumza Kiingereza kwa mara ya kwanza.
Akizungumza katika Mkutano wa Afrika ulioandaliwa katika mji mkuu wa Nairobi siku ya Jumanne, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alizungumzia mara kwa mara kuhusu "uwekezaji wa pamoja" na "ushirikiano sawa" alipoelezea changamoto zinazowakabili, ikiwa ni pamoja na usalama, utegemezi wa kiuchumi na ushindani wa kijiografia.
Rais wa Kenya William Ruto, ambaye ni mwenyeji mwenza wa mkutano huo wa siku mbili, alishirikisha hisia zake, akiongeza kuwa Afrika lazima isaidie kuunda utaratibu unaoibuka wa kimataifa badala ya kubaki pembezoni mwake.
Macron ametangaza uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni 27 (pauni bilioni 20) barani Afrika katika maeneo kama vile mpito wa nishati, kidijitali na akili mnemba, uchumi wa baharini na kilimo.
"Afrika inafanikiwa. Ni bara changa zaidi duniani ... na inahitaji uwekezaji ili kujitegemea zaidi," alisema Jumatatu, akiongeza kuwa hii itaunda ajira zipatazo 250,000 barani Afrika, na nchini Ufaransa.
"Hatuko hapa tu kuja kuwekeza katika bara la Afrika pamoja nanyi - tunahitaji viongozi wakubwa wa biashara wa Kiafrika kuja kuwekeza nchini Ufaransa," aliwaambia wasikilizaji katika kituo cha mikutano cha Nairobi, shirika la habari la AFP linaripoti.
Mkutano huo unalenga kupanua ushirikiano wa Paris na kufanya mikataba ya uwekezaji barani humo dhidi ya kuongezeka kwa hisia za chuki dhidi ya Ufaransa na kupungua kwa mamlaka katika makoloni yake ya zamani, hasa Afrika Magharibi. Hii inaonyesha mabadiliko ya hatua kwa hatua katika jinsi Paris inavyofikiria uhusiano wake na Afrika.











