Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Tehran yalenga kambi za Marekani katika nchi za Ghuba baada ya majeshi ya Marekani kuanzisha mashambulizi mapya

Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni, Marekani ilifanya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya maeneo kadhaa nchini Iran, ikisema kuwa yalikuwa jibu kwa kile ilichokiita "uchokozi unaoendelea" wa Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Siku ya Bajeti Afrika Mashariki: Bajeti ‘kubwa zaidi’ Kenya na Rwanda

    Kwa upande wake, Kenya inapanga kusoma bajeti ya $37.2 bilioni (Kes 4.84 trilioni) ambayo ni kubwa zaidi kuwahi kuwasilishwa nchini humo. Katika mwaka wa kifedha uliopita, bajeti ya taifa hilo ilikuwa ya dola $33 bilioni.

    Sekta ambazo zinaratajiwa kunufaika na ongezeko katika bajeti hii ni huduma za usalama wa ndani na ulinzi wa taifa, idara ya ujasusi, pamoja na sekta za nishati, elimu, afya na maji.

    Hata hivyo katika vikao vya umma na pia mitandaoni, kumekuwa na maswali kuhusu iwapo taifa hilo kweli linahitaji bajeti kubwa kiasi hicho.

    Rwanda nayo inatarajiwa kutangaza bajeti ya $5.4 bilioni (Rwf 7.8 bilioni), ambayo ni ongezeko la asilimia 12% kutoka kwa bajeti ya mwaka uliopita ya $4.8 bilioni.

    Bajeti hiyo inatarajiwa kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Rwanda, na asilimia 68% inatarajiwa kufadhiliwa na mapato ya ndani.

    Gharama ya maisha

    Bajeti hizi zinawasilishwa wakati wananchi wakiendelea kukabiliwa na changamoto za kupanda kwa gharama za maisha, hususan bei ya mafuta kutokana na mzozo wa Mashariki ya Kati, pamoja na uhaba wa ajira.

    Hizi ni baadhi ya kauli za wananchi tuliozungumza nao jijini Dodoma:

    "Suala la mafuta ndio linalotuumiza sana. Serikali inatupa ahadi ya kila siku kuwa bei itapunguzwa, lakini hakuna mabadiliko," anasema mkazi mmoja.

    Mwingine alisema: "Bajeti inasomwa lakini matumizi sio mazuri. Hii inapunguza mzunguko wa fedha mtaani."

    Ongezeko la bei ya mafuta limeshuhudiwa katika mataifa yote ya Afrika Mashariki, hali ambayo imesababisha kupanda kwa nauli, chakula na gharama za kufanya biashara kwa jumla.

    Kodi mpya

    Wananchi watakuwa makini kuona ni mapendekezo gani ya kikodi ambayo yatatolewa na serikali za kila nchi ili kufadhili bajeti hizo, na yatakuwa na athari gani kwao.

    Tanzania na Rwanda tayari zimesema zitalenga mapato ya ndani zaidi kufadhili bajeti zao – na wengi wanasubiri kuona ni maeneo gani ambayo yataguswa zaidi.

    Nchini Kenya, bajeti huambatana na mswada wa fedha unaoelezea jinsi bajeti hiyo itakavyofadhiliwa kupitia kodi, mikopo na njia nyinginezo. Wananchi wamekuwa wakitoa maoni kuhusu mapendekezo ya mwaka huu, ambapo baadhi yamezua mjadala kama vile ushuru wa simu za mkononi, miamala ya fedha na mamlaka ya shirika la ukusanyaji ushuru KRA.

  2. Polisi wa China wamkamata mtu mmoja baada ya video za mateso kwa mbwa kuzua hasira mtandaoni

    Mamlaka nchini China zimemkamata mwanaume aliyesababisha hasira kubwa miongoni mwa umma kwa madai ya kuwatesa mbwa na kurekodi ukatili huo ili kuuza video hizo mtandaoni.

    Mwanaume huyo anadaiwa kujifanya kuwa mtu mwenye shauku ya kuasili wanyama, lakini baadaye aliwafanyia ukatili paka na mbwa kadhaa aliowachukua.

    Vitendo vyake vilifichuliwa baada ya rafiki wa mwanamke aliyekuwa ameweka watoto wa mbwa kwa ajili ya kuasili kusimulia matendo hayo mtandaoni.

    Zaidi ya watu 100 walikusanyika nje ya nyumba ya mwanaume huyo mapema wiki hii katika mji wa Chongqing kusini-magharibi mwa China wakipinga matendo yake.

    Polisi hawajafichua ni kosa gani hasa mwanaume huyo anachunguzwa nalo. Ukatili dhidi ya wanyama kwa sasa si kosa linaloadhibiwa kisheria nchini China. Hata hivyo, uelewa kuhusu ustawi na haki za wanyama umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni.

    Mwanaume huyo, anayejulikana kwa jina la ukoo la Li, aliweka tangazo kwenye Douyin mapema mwezi huu akisema kuwa anataka kuasili mbwa bila malipo.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo, alidai kwamba watoto wake wawili "waliwapenda sana watoto wa mbwa."

    Siku ya Jumapili, wanaharakati wa kundi la kutetea haki za wanyama waligundua mmoja wa watoto wa mbwa waliokuwa wameasiliwa akiwa ametupwa kwenye ngazi za jengo analoishi Li. Mbwa huyo alikuwa na mguu uliovunjika, mkia uliokatwa na kichwa kilichovimba.

    Video zilizosambazwa mtandaoni zinaonesha zaidi ya watu 100 wakikusanyika nje ya nyumba yake, huku baadhi yao wakibeba mabango ya kupinga vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya wanyama.

  3. Trump asema atasitisha mashambulizi baada ya ombi la Iran

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa mashambulizi dhidi ya Iran "yataisha hivi karibuni" baada ya ombi kutoka Iran.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na Fox News Trump alisema katika mahojiano kwamba aliamuru kusitishwa kwa mashambulizi mapya dhidi ya Iran baada ya kupokea "simu ya moja kwa moja kutoka Iran" na ombi kutoka kwa afisa mwandamizi wa Iran.

    Hata hivyo, vyombo vya habari rasmi vinavyohusishwa kwa karibu na jeshi la mapinduzi ya Iran vimekanusha madai hayo hadharani, vikisema kuwa ni "uongo" kwamba Iran iliomba mashambulizi hayo yasitishwe.

    Mwandishi wa Fox News pia alisema kuwa Trump alieleza katika mahojiano hayo kwamba mashambulizi yaliyofanyika ndani ya Iran yalihusisha makombora ya aina ya Tomahawk, yaliyolenga rada za ulinzi, vituo vya ulinzi na mifumo ya kuongozea ndege zisizo na rubani za Iran.

    Mashambulizi hayo yanaripotiwa kufanyika ndani ya Iran, kilomita chache kutoka mji mkuu, Tehran.

    Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Iran kukataa makubaliano yaliyopendekezwa na Marekani, Trump alijibu:

    "Iwapo watafanya hivyo, watashambuliwa tena kwa mabomu."

    Kauli hizi zinaonesha kuendelea kwa mvutano mkubwa kati ya Marekani na Iran, huku pande zote zikitoa taarifa zinazokinzana kuhusu mawasiliano na juhudi za kusitisha mashambulizi.

    Unaweza kusoma;

  4. Siku ya Bajeti Afrika Mashariki: Bajeti ‘ya kipekee’ Tanzania

    Mawaziri wa fedha kutoka nchi za Afrika Mashariki wanatarajiwa kuwasilisha makadirio ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2026/2027 leo Alhamisi (Juni 11), wakiangazia mipango ya matumizi na mapato ya nchi zao, pamoja na vipaumbele vya kila taifa katika juhudi za kukuza uchumi na kuimarisha maisha ya wananchi.Wananchi watarajie nini? Haya ni mambo matano yanayojitokeza kufikia sasa.

    Tanzania imeahidi kuwa hii itakuwa bajeti ya ‘kipekee’, ikiwa ya kwanza katika awamu ya pili ya rais Samia Suluhu Hassan madarakani kufuatia uchaguzi wa mwaka uliopita.Waziri wa fedha Khamis Mussa Omar amesema kuwa bajeti ya $23.8 bilioni (Tsh 62.3 trilioni) itakayosomwa bungeni Dodoma itafadhiliwa zaidi na mapato ya ndani zaidi, huku serikali ikipunguza utegemezi wa misaada ya nje."

    Kwa bajeti ya mwaka unaofuata, sehemu ya matumizi ambayo itagharamiwa na mapato ya ndani itakuwa ni asilimia 70% ambayo ni kiwango cha juu zaidi ya kiwango cha mwaka wa sasa wa kifedha unaomalizika.

    Nayo misaada kutoka nje haitafika hata Tsh trilioni moja kwenye bajeti hiyo ya Tsh 62.3 trilioni," alisema Waziri Khamis Mussa katika kikao na waandishi wa habari jijini Dodoma, siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa makadirio ya bajeti bungeni.

    Maeneo makuu ya kipaumbele mwaka huu nchini humo yatakuwa miradi ya maendeleo ya kimkakati kama kuendeleza mradi wa reli ya kisasa (SGR), barabara, uwekezaji katika sekta za nishati na sekta nyinginezo ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

  5. Bill Gates ajutia kukutana kwake na Jeffrey Epstein

    Mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates, amesema kuwa Jeffrey Epstein alitaka kuwa na uhusiano wa karibu wa binafsi naye.

    Gates alisisitiza kwamba hakuwahi kumdhuru au kumtumia vibaya mtu yeyote, huku akikabiliwa na maswali kutoka kwa kamati ya Bunge la Marekani inayochunguza uhusiano kati ya Epstein, aliyetuhumiwa kwa makosa ya kingono na watu matajiri na wenye ushawishi, akiwemo yeye mwenyewe.

    Katika taarifa iliyoandaliwa mapema na kuchapishwa kwenye tovuti yake binafsi, Gates alisema hajawahi kutembelea kisiwa cha Epstein, mashamba yake, wala nyumba yake iliyoko Florida.

    Aliongeza kuwa hakuwahi kuona dalili zozote kwamba Epstein alikuwa akijihusisha na shughuli za uhalifu.

    Bilionea huyo ameeleza tena majuto yake kuhusu mikutano aliyokuwa nayo na Epstein, akiitaja kuwa "kosa kubwa la maamuzi". Alisisitiza kuwa mikutano yao ilihusu tu majadiliano kuhusu misaada na ufadhili wa shughuli za hisani kupitia taasisi yake ya kutoa misaada.

    Unaweza kusoma;

  6. Trump asema ‘anapenda mfumuko wa bei’ wakati bei nchini Marekani zikiongezeka kwa kasi kubwa

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa "anapenda mfumuko wa bei" baada ya bei nchini Marekani kupanda mwezi uliopita kwa kasi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitatu.

    Takwimu za Bureau of Labor (BLS) zilionesha kuwa bei ziliongezeka kwa asilimia 4.2 mwezi Mei ikilinganishwa na mwaka uliopita.

    Hili ni ongezeko kutoka asilimia 3.8 mwezi Aprili. Kuongezeka huko kulichangiwa na kupanda kwa gharama za nishati kufuatia vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    "Ninapenda. Takwimu zilikuwa nzuri. Mnajua ninachopenda zaidi? Ninapenda mfumuko wa bei," Trump alisema akiwa Ikulu ya Marekani.

    Hata hivyo, aliahidi kuwa bei hizo zinazopanda "zitashuka kwa kasi kubwa" mara tu vita na Iran vitakapomalizika. Baadaye siku hiyo, jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi ya anga dhidi ya Iran.

    Akizungumzia takwimu za mfumuko wa bei siku ya Jumatano, rais huyo alisema vikosi vya Marekani vilifanya operesheni za usiku na kuchukua "mamilioni ya mapipa" ya mafuta kutoka Iran, jambo ambalo alisema limechangia kushuka kidogo kwa bei za mafuta.

    "Mgogoro huu ukimalizika... mtashuhudia bei ya mafuta ikishuka na kurudi katika kiwango ilichokuwa kabla ya vita," aliwaambia waandishi wa habari katika Ikulu ya Marekani.

    Trump pia alirejelea safari yake katika jimbo la Iowa mapema mwaka 2026, akisema aliona petroli ikiuzwa kwa dola 1.85 kwa galoni moja, na kuongeza kuwa "tutarudi kwenye viwango hivyo hivi karibuni."

    Hata hivyo, bei ya mafuta ghafi ya aina ya Brent crude bado inaendelea kuuzwa kwa kiwango cha juu zaidi ikilinganishwa na bei zilizokuwepo kabla ya vita kuanza.

    Unaweza kusoma;

  7. Tetesi za soka Alhamisi:Arsenal yamuwinda Williams

    Arsenal bado inaendelea kuweka juhudi katika mbio za kumsajili Nico Williams, winga wa Athletic Club na timu ya taifa ya Hispania mwenye umri wa miaka 23.

    Liverpool, Manchester City na Manchester United pia zinaonyesha nia ya kumsajili.

    Juventus ipo kwenye mazungumzo na Aston Villa kwa ajili ya kumsajili mlinda lango wa Argentina Emiliano Martinez (33), ambaye anaripotiwa tayari amekubaliana masharti binafsi.

    Paris Saint-Germain inatarajia kujaribu kumsajili mshambuliaji wa Ufaransa Michael Olise (24) kutoka Bayern Munich msimu huu wa kiangazi.

    Manchester United inamfuatilia mshambuliaji wa Senegal Iliman Ndiaye (26) wa Everton huku ikitafuta kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya kurejea kwenye UEFA Champions League msimu ujao.

    Liverpool iko tayari kumuuza mshambuliaji wa Italia Federico Chiesa (28) kwa takribani pauni milioni 17, huku mchezaji huyo akipendelea kurejea katika ligi ya Italia, Serie A.

    Barcelona inafahamu kuwa Chelsea na Arsenal zinamuwania winga wa Hispania Dani Olmo (28), lakini haitamruhusu kuondoka isipokuwa thamani yake ya pauni milioni 60 ilipwe.

    Mshambuliaji wa Ufaransa Mathys Tel (21) anaweza kufanya uhamisho wa kushangaza kutoka Tottenham Hotspur kwenda AFC Bournemouth msimu huu wa kiangazi.

    Barcelona inapanga kumuuza kiungo wa Hispania Marc Casado (22) ili kupata fedha za kufanya usajili mwingine. Bayer Leverkusen pamoja na vilabu vya Ligi Kuu ya England vinamfuatilia.

    Leeds United inataka kuvunja rekodi yake ya usajili kwa kumsajili mlinzi wa Ivory Coast Ousmane Diomande kutoka Sporting CP kwa dau linaloweza kufikia pauni milioni 35 pamoja na nyongeza ya pauni milioni 8.

    Crystal Palace inajiandaa kushindana na Everton katika mbio za kumsajili kiungo wa England Hayden Hackney (23) kutoka Middlesbrough kwa ofa ya pauni milioni 20.

    Unaweza kusoma;

  8. Tehran yalenga kambi za Marekani katika nchi za Ghuba baada ya majeshi ya Marekani kuanzisha mashambulizi mapya

    Iran imeshambulia kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Ghuba kulipiza kisasi duru ya hivi karibuni ya mashambulizi ya Marekani, yaliyokuja baada ya Donald Trump kusema kwamba ataishambulia Iran “kwa nguvu kubwa”.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema imekamilisha siku ya pili mfululizo ya mashambulizi ya “kujilinda”, yaliyofanyika usiku mmoja baada ya Trump kusema kwamba Tehran ilikuwa imechukua “muda mrefu sana kufikia makubaliano” ya kumaliza vita.

    Kwa kujibu, Iran ilisema imeshambulia vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Kuwait, ambayo ni malengo yale yale yaliyolengwa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Iran siku iliyotangulia.

    Kuongezeka huku kwa mashambulizi ya kulipizana kisasi katika siku za hivi karibuni kumefanya juhudi za makubaliano ya usitishaji kuwa dhaifu kati ya nchi hizo mbili.

    Baada ya shambulio la hivi karibuni la Marekani, milipuko ilisikika katika miji ya kusini mwa Iran karibu na Mlango bahari wa Hormuz, ambapo vikosi vya Marekani pia vilishambulia mifumo ya ulinzi wa anga, rada na maeneo mengine katika duru ya awali ya mashambulizi.

    Katika ongezeko hili jipya la mzozo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) pia lilisema limepiga meli mbili za kubeba mafuta zilizokuwa zikivuka Mlango wa Hormuz, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, ingawa hakukuwa na uthibitisho wa haraka kutoka vyanzo huru.

    Hii ilikuja baada ya vyombo vya habari vya serikali ya Iran kuripoti kwamba Mlango bahari wa Hormuz ulikuwa “umefungwa kabisa kwa aina zote za meli”. Hata hivyo, CENTCOM ilisema kwamba “meli za kibiashara zinaendelea kupita kuingia na kutoka katika Mlango wa Hormuz”.

    Bei za mafuta zilipanda muda mfupi baada ya kutangazwa kufungwa kwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa baharini na baada ya taarifa za shambulio dhidi ya meli hizo kutolewa.

    Unaweza kusoma;

  9. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo