Utafiti: Nyani wakubwa hubusiana na kukumbatiana ili kudumisha amani

Chanzo cha picha, Jake Brooker / Chimfunshi Wildlife Orphanage Trust
Wanasayansi wamegundua kuwa kugusana, kukumbatiana na hata kubusiana kabla ya matukio yenye msongo wa mawazo huenda ni tabia ya kale inayosaidia kujenga uaminifu, kulingana na utafiti wa nyani wakubwa walio karibu zaidi na binadamu.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Durham walichunguza tabia za sokwe na bonobo, na kubaini kuwa hutumia mgusano wa mwili kutulizana na kupeana uhakikisho kabla ya migogoro, hasa inayohusiana na chakula.
Moja ya matokeo yaliyowashangaza watafiti ni kwamba sokwe, licha ya kujulikana kwa tabia yao ya ukali, walionekana wakifanya mawasiliano ya karibu, ikiwemo kuweka vidole vyao midomoni mwa wenzao.
"Kabla ya matukio yenye msongo, hukusanyika pamoja, hutulizana, hugusana na kukumbatiana," alisema Profesa Zanna Clay
Profesa Zanna Clay alielezea tabia hiyo kuwa ni "wito wa kuunganisha nguvu" kabla ya tukio lenye msongo wa mawazo, akilinganisha na jinsi wachezaji wa mpira wa miguu hukusanyika pamoja na kutiana moyo kabla ya mechi muhimu.
"Ni zaidi ya 'sisi' kuliko 'mimi'," alisema.
Wataalamu hao walifanya utafiti huo kwa sokwe na nyani aina ya bonobo waliokuwa wakiishi katika vituo viwili vya kuhifadhi nyani wakubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.
Nyani hao walifuatiliwa katika dakika tano kabla ya karanga kuletwa, wakati walipokuwa wakijua kuwa chakula kilikuwa kinakaribia kutolewa.
Watafiti walirekodi matukio mbalimbali ya mgusano wa kuwafariji, yakiwemo kugusana, kukumbatiana na kubusiana.
Timu ya watafiti ilibaini kuwa nyani waliokuwa wakigusana na kukumbatiana walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kupata chakula na kukila kwa amani pamoja na wenzao.
Aidha, makundi yaliyokuwa na uvumilivu mkubwa yalionesha kiwango cha juu zaidi cha mgusano wa kupeana utulivu. Watafiti walielezea hali hiyo kama " kufarijiana", ambapo nyani kadhaa walikuwa wakikumbatiana mmoja baada ya mwingine kabla ya tukio lenye kuwasababishia hali ya msongo.




