Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Kwa nini Iran inaficha hata sauti ya kiongozi wake mpya?

Gazeti hilo linaeleza kuwa mwangwi unaopatikana kwenye rekodi za sauti unaweza kutoa taarifa kuhusu eneo au chumba ambako sauti hiyo ilirekodiwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Habari za hivi punde, Helikopta mbili zagongana wakati wa operesheni ya kuzima moto Ugiriki

    Mamlaka nchini Ugiriki zinaendelea na operesheni ya utafutaji na uokoaji baada ya helikopta mbili zilizokuwa zikishiriki shughuli za kuzima moto kugongana angani.

    Tunachojua kufikia sasa

    • Helikopta mbili zilihusika katika ajali, kila moja ikiwa na wahudumu wawili ndani yake, kwa mujibu wa kikosi cha zimamoto.
    • Katika taarifa yake, kikosi hicho kimesema helikopta hizo ni za aina ya Bell na zilikuwa zimekodishwa na idara ya zimamoto.
    • Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Psatha, magharibi mwa mji mkuu wa Athens.
    • Operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea huku mamlaka zikiendelea kufuatilia hali ya wahusika.

    Tusichokijua

    ·Bado haijafahamika ni nini kilisababisha helikopta hizo kugongana.

    ·Hali ya wahudumu waliokuwa ndani ya helikopta hizo bado haijathibitishwa, wala utambulisho wao haujatolewa hadharani.

  2. Ndege iliyokuwa na watalii 13 yaanguka Peru

    Ndege ndogo iliyokuwa imewabeba watalii imeanguka nchini Peru, na kusababisha vifo vya watu wote 13 waliokuwa ndani yake, kwa mujibu wa maafisa wa serikali na vyombo vya habari vya nchini humo.

    Ndege hiyo ya aina ya Cessna Caravan C-208 ilikuwa ikipaa juu ya eneo maarufu la kihistoria la Nazca Lines wakati ilipoanguka siku ya Jumamosi. Ilikuwa imewabeba abiria 11 pamoja na marubani wawili.

    Miongoni mwa waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikuwa watalii wawili kutoka Ujerumani, wawili kutoka Hispania na saba kutoka Italia.

    Mamlaka nchini Peru zimesema chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika, huku uchunguzi ukiendelea.

    Nazca Lines, ni eneo la Urithi wa Dunia wa UNESCO kusini mwa Peru, na huvutia maelfu ya watalii kila mwaka. Eneo hilo linajulikana kwa michoro mikubwa ya kale ya wanyama na maumbo mbalimbali iliyochorwa kwenye mchanga wa jangwani, na watalii wengi hutumia ndege ndogo kutazama michoro hiyo kutokea angani.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Feri yateketea baharini Indonesia, watu wafariki na wengine hawajulikani walipo

    Watu watano wamefariki dunia huku wengine 41 wakiripotiwa kutoweka baada ya feri iliyokuwa imebeba zaidi ya abiria 250 kushika moto ikiwa baharini nchini Indonesia.

    Kwa mujibu wa mamlaka za uokoaji, nahodha wa feri hiyo aliripoti moto huo uliozuka karibu na kisiwa cha Madura, wakati chombo hicho kikisafiri kutoka Surabaya katika jimbo la Java Mashariki kuelekea Makassar huko Sulawesi Kusini.

    Picha zilizoonyeshwa na vyombo vya habari vya Indonesia zimewaonyesha abiria wengi wakiwa wamevaa makoti ya kujiokoa wakisubiri msaada kwenye boti za uokoaji.

    Video nyingine zimeonyesha baadhi ya watu wakishuka kutoka kwenye feri hiyo huku miali mikubwa ya moto na moshi mzito ukionekana ukifuka kutoka sehemu ya juu ya feri.

    Shirika la Kitaifa la Uokoaji la Indonesia (Basarnas) limesema moto huo ulianza kati ya saa 12:00 na 1:00 asubuhi GMT.

    Mamlaka zilisema sehemu kubwa ya feri hiyo ilighubikwa na moto, huku baadhi ya abiria wakisalia katika sehemu ya mbele ya chombo wakisubiri kuokolewa.

    Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, huku operesheni ya kuwatafuta waliopotea ikiendelea.

    Pia unaweza kusoka:

  4. Ardhi yetu haitatumika kuhatarisha majirani, Iraq yaonya

    Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia al-Sudani, amesema serikali yake haitaruhusu ardhi ya nchi hiyo kutumika kushambulia au kutishia mataifa jirani.

    Akiongoza kikao cha dharura kilichojadili hali ya usalama katika eneo hilo, Sudani aliamuru kuundwa kwa kamati ya pamoja ya usalama pamoja na kuandaliwa kwa hatua za kuzuia vitendo kama hivyo kutokea tena.

    Pia aliagiza vyombo vya usalama kuhakikisha sheria zinafuatwa kuimarisha amani na usalama, pamoja na kulinda mamlaka ya Iraq na uhusiano wake mzuri na nchi jirani.

    Taarifa iliyotolewa baada ya kikao hicho ilisema vikosi vya usalama vya Iraq vimewekwa katika hali ya tahadhari ili kuzuia jaribio lolote la kutumia ardhi ya nchi hiyo kuhatarisha usalama wa mataifa ambayo Baghdad imeyataja kuwa "marafiki na ndugu zake."

    Pia unaweza kusoma:

  5. Rubio: Mabadiliko ya utawala wa Iran hayamaanishi kuipindua serikali

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa mazungumzo kuhusu "mabadiliko ya utawala" nchini Iran hayamaanishi lazima kuiondoa serikali iliyopo madarakani, bali yanahusu kubadili tabia na mwelekeo wa uongozi wake.

    Akizungumza na Fox News, Rubio alisema huenda kusiwe na mabadiliko ya utawala kwa maana ya kupindua serikali, lakini akaongeza kuwa sera na mwenendo wa utawala wa Iran vinapaswa kubadilika.

    Rubio alidai kuwa kwa miaka mingi Iran imekuwa ikifuata sera za kupanua ushawishi wake nje ya mipaka yake, akisema lengo lake si kuitawala Iran pekee bali pia kuwa na nguvu kubwa katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

    Alisisitiza kuwa hali hiyo inapaswa kubadilika, na kwamba njia pekee ya kuilazimisha Iran kubadili mwelekeo wake ni kuiwekea gharama ambazo haiwezi kuendelea kuzibeba.

    Kwa mujibu wa Rubio, kubadili jinsi serikali ya Iran inavyojiendesha ni jambo tofauti na kuangusha utawala wake, kwani mabadiliko ya tabia na sera ni mchakato unaoweza kuchukua muda mrefu

    Rubio alisema makubaliano ya nyuklia yanaweza kufikiwa na kufuatiliwa kwa urahisi, lakini kuifanya Iran iachane na sera zake za ushawishi katika Mashariki ya Kati ni kazi ya muda mrefu, jambo linalomaanisha kuwa shinikizo dhidi ya Tehran linaweza kuendelea kwa kipindi kisichojulikana

    Soma Zaidi:

  6. Kwa nini Iran inaficha hata sauti ya kiongozi wake mpya?

    Gazeti la Hamshahri, linalomilikiwa na Manispaa ya Tehran, limesema sababu ya kutotolewa kwa sauti ya Mojtaba Khamenei, kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni hofu ya uwezekano wa kufuatiliwa na huduma za kijasusi kupitia teknolojia za kisasa.

    Gazeti hilo linaeleza kuwa mwangwi unaopatikana kwenye rekodi za sauti unaweza kutoa taarifa kuhusu eneo au chumba ambako sauti hiyo ilirekodiwa.

    Gazeti la Hamshahri pia limedai kuwa mashirika ya kijasusi yanaweza kutumia mabadiliko madogo ya mfumo wa umeme uliopo kwenye rekodi za sauti kubaini nchi, tarehe, muda na hata eneo husika lilipofanyika rekodi hiyo.

    Mbali na hilo, aina ya kifaa kilichotumika kurekodi sauti nayo inaweza kutoa taarifa muhimu. Kila simu au kifaa cha kurekodi kina sifa zake za kipekee ambazo zinaweza kutumika katika utambuzi kama alama ya vidole.

    Gazeti hilo limeongeza kuwa sauti za mazingira kama upepo, ndege, wadudu au mifumo ya uingizaji hewa zinaweza kusaidia kubaini eneo la kijiografia la aliyerekodiwa.

    Tangu Mojtaba Khamenei ateuliwe kuwa kiongozi wa tatu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hajaonekana hadharani, hakuna picha mpya wala sauti yake iliyotolewa, huku vyombo vya habari vya Iran vikichapisha tu ujumbe wa maandishi unaodaiwa kutoka kwake.

    Soma Zaidi:

  7. Bin Salman aisihi Marekani kuyapa kipaumbele mazungumzo badala ya vita

    Shirika rasmi la habari la Saudi Arabia, Axios, limethibitisha kuwa Mwanamfalme Mrithi Mohammed bin Salman amefanya mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump, ambapo viongozi hao walijadili hali ya usalama na maendeleo ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bin Salman alisisitiza umuhimu wa kuipa kipaumbele njia ya mazungumzo na diplomasia ili kupunguza mvutano unaoendelea kuongezeka katika ukanda huo.

    Mwanamfalme huyo pia alitoa wito wa kufanyika kwa juhudi zote zinazowezekana ili kurejesha utulivu, akisema hali hiyo inaweza kufungua njia ya suluhisho za kidiplomasia huku ikilinda usalama na uthabiti wa eneo hilo.

    Aidha, alionya kuhusu hatari ya kuenea kwa vita ambayo inaweza kuathiri si tu Mashariki ya Kati bali pia usalama na uthabiti wa kimataifa.

    Rais Trump alikuwa amesema mwishoni mwa Jumamosi kuwa shambulizi kubwa la kijeshi dhidi ya Iran lilikuwa limepangwa, lakini baadaye akatangaza kwamba Marekani na Israel zitasitisha kwa sasa hatua hiyo baada ya ombi kutoka Iran na baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati ili kutoa nafasi kwa mazungumzo.

  8. Mashambulizi ya Israel gaza yaua wapalestina wanane usiku mmoja

    Wapalestina takriban wanane waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel yaliyolenga majengo ya makazi katika Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia Jumapili, na kufanya idadi ya waliouawa katika kipindi cha siku mbili za mashambulizi kufikia 16, kwa mujibu wa vyanzo vya ulinzi wa kiraia na afya vya Gaza.

    Msemaji wa ulinzi wa kiraia, Mahmoud Bassal, alisema mwanaume mmoja na mke wake waliuawa huku watu wengine wanne wakijeruhiwa baada ya helikopta ya jeshi la Israel kushambulia nyumba kusini mwa Deir al-Balah katikati mwa Ukanda wa Gaza.

    Aliongeza kuwa mzee mmoja na mtoto mmoja waliuawa katika shambulio jingine lililolenga jengo la makazi magharibi mwa Mji wa Gaza.

    Katika tukio tofauti, watu watatu, akiwemo mtoto mmoja, waliuawa baada ya jengo la makazi kushambuliwa kaskazini-magharibi mwa Khan Younis, kusini mwa Gaza.

    Vituo vya afya na ulinzi wa kiraia pia viliripoti kuwa Wapalestina wengine wanane waliuawa katika mashambulizi mengine ya Israel yaliyofanyika siku ya Jumamosi.

    Miongoni mwa maeneo yaliyolengwa ni ghala la kuhifadhi dawa na vifaa tiba la Hospitali ya Al-Aqsa Martyrs mjini Deir al-Balah, ambapo Wizara ya Afya ya Gaza ilisema shambulio hilo lilisababisha uharibifu mkubwa.

  9. Awali, Wamarekani walitahadharishwa kujiandaa kuondoka mashariki ya kati

    Serikali ya Marekani ilichukua hatua na kuwatahadharisha raia wake walioko Mashariki ya Kati kuwa waangalifu na kuwa tayari kuondoka endapo hali ya usalama katika eneo hilo itazidi kuwa mbaya.

    Tahadhari hiyo imetolewa wakati kulipokuwa na ripoti kwamba Rais Donald Trump huenda akapanga mashambulizi mapya makali dhidi ya Iran mwishoni mwa wiki.

    Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kuwa vituo vya kidiplomasia vya Marekani, ikiwemo vile vilivyo nje ya Mashariki ya Kati, vimewahi kulengwa hapo awali.

    Pia ilionya kuwa Iran na makundi yanayoiunga mkono yanaweza kulenga maslahi ya Marekani au maeneo yanayohusishwa na raia wa Marekani duniani kote.

    Awali, Iran iliishutumu Marekani kwa kuongeza mvutano katika eneo hilo, ikionya kuwa nchi yoyote itakayoshirikiana na Washington anaweza "kumezwa na vita" hivyo.

    Hata hivyo, baadaye, Trump alisitisha mpango wa kufanya mashambulizi dhidi ya Iran kwa sharti kwamba makubaliano yafikiwe "haraka" kati ya pande hizo mbili.

    Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema aliamua "kufuta shambulio hilo, mradi tu iwezekane kufikiwa kwa MAKUBALIANO kwa haraka", ambayo yatajumuisha kufunguliwa mara moja kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz na kumalizika kwa kile alichokiita "tishio la nyuklia la Iran."

    Soma Zaidi:

  10. Licha ya vikwazo, meli ya Urusi yatua Mali na magari ya kijeshi

    Vikosi vya Urusi na Mali vinavyopambana na waasi kaskazini mwa Mali vimepokea msafara mkubwa wa magari ya kijeshi, ambayo yanaonekana kusafirishwa na meli ya mizigo ya Urusi iliyowekewa vikwazo, uchunguzi wa BBC Verify umebaini.

    Msafara mkubwa wa magari ya kivita ulionekana ukiwasili jijini Bamako katika video zilizothibitishwa na kuonyeshwa na televisheni ya taifa ya Mali tarehe 25 Julai. Waandishi wa habari waliripoti kuwa msafara huo ulisafiri kutoka bandari ya Lomé nchini Togo.

    Kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji wa meli zilizochambuliwa na BBC Verify, meli ya mizigo ya Urusi Mikhail Britnev, ambayo imewekewa vikwazo, ilitia nanga katika bandari ya Lomé tarehe 9 Julai. Picha za satelaiti zinaonyesha kuwa meli hiyo huenda ilikuwa imebeba malori ya kijeshi, magari ya kubeba wanajeshi yenye silaha pamoja na magari mepesi ya kivita yanayofanana na yale yaliyoonekana jijini Bamako.

    Taarifa za ufuatiliaji wa meli zinaonyesha kuwa meli Mikhail Britnev iliondoka katika bandari ya Baltiysk nchini Urusi tarehe 18 Juni, ikapitia Bahari ya Kaskazini kabla ya kuingia katika Mfereji wa Uingereza."

    BBC Verify imeelezwa kuwa meli hiyo ilisindikizwa kupitia mfereji wa Uingereza na manowari ya kivita ya Urusi ya daraja la Ropucha. Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imekataa kutoa maoni kuhusu taarifa hizo.

    Wachambuzi wanasema usafirishaji huo unaonyesha kuwa Urusi inaongeza msaada wake kwa utawala wa kijeshi wa Mali, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi makubwa kutoka kwa waasi wanaoongozwa na kundi la jihadi la Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM) pamoja na waasi wa Kitouareg. Mashambulizi hayo yamewezesha waasi hao kuteka maeneo makubwa kaskazini mwa nchi.

    Urusi imekuwa ikiisaidia serikali ya kijeshi ya Mali tangu kuondoka kwa vikosi vya Ufaransa mwaka 2022, ikipokea malipo ya fedha pamoja na upendeleo wa kufikia migodi na machimbo ya dhahabu nchini humo.

    Awali, kundi la mamluki la Wagner lilikuwa likifanya operesheni zake Mali, lakini shughuli hizo baadaye zilichukuliwa na Africa Corps, kikosi kinachosimamiwa na Wizara ya Ulinzi ya Urusi.

    Serikali ya kijeshi ya Mali imepata pigo mara kadhaa katika uwanja wa mapambano katika wiki za hivi karibuni.

    Siku ya Jumatano, shirika la Amnesty International liliitaka kufanyika uchunguzi wa uhalifu wa kivita kufuatia madai ya kuuawa kwa takriban wanajeshi 19 wa Mali baada ya kuvamiwa mapema mwezi huu.

    Soma Zaidi:

  11. Uganda yafanikiwa kudhibiti Ebola huku DRC ikiendelea kupambana na mlipuko huo hatari

    Uganda imefanikiwa kudhibiti Ebola na kwa sasa haina maambukizi ya ugonjwa huo, huku hali ikiwa tofauti nchini DRC ambako mlipuko unaendelea kuenea na idadi ya vifo vilivyothibitishwa ikizidi 1,500.

    Maafisa wa afya nchini Uganda wanasema mafanikio hayo yametokana na utambuzi wa haraka wa wagonjwa, ufuatiliaji wa waliokutana na maambukizi, pamoja na kuweka wagonjwa kwenye vituo maalum vya matibabu kabla ya ugonjwa kusambaa kwenye jamii.

    Kati ya wagonjwa 20 waliothibitishwa kuwa na Ebola nchini Uganda tangu mwezi Mei, wengi walikuwa wametokea DRC. Hata hivyo, mamlaka zinasema hatua za haraka zilisaidia kuzuia maambukizi makubwa ndani ya nchi.

    Wakati huo huo, DRC inaendelea kukabiliana na changamoto za usalama, uhamaji wa watu na ugumu wa kufuatilia mawasiliano ya wagonjwa, hali ambayo imechangia kuenea kwa virusi hivyo katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika.

    Licha ya kutangaza kutokuwa na wagonjwa wa Ebola kwa sasa, Uganda imeendelea kuimarisha uchunguzi mpakani na imetuma wahudumu wa afya nchini DRC kusaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko huo, huku ikisisitiza kuwa tishio la ugonjwa huo bado halijaisha.

    Soma Zaidi:

  12. Mwanamke alipua bomu mgahawani Urusi, watatu wafariki

    Watu watatu wamefariki dunia na wengine 21 kujeruhiwa baada ya bomu lililotengenezwa kienyeji kulipuka katika mgahawa wa Kiitaliano jijini Moscow, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vilivyonukuu maafisa wa usalama.

    Mlipuko huo ulitokea majira ya saa nane usiku kwa saa za Moscow katika eneo la Kudrinskaya, karibu na katikati ya jiji.

    Kamati ya Kitaifa ya Kupambana na Ugaidi ya Urusi (NAK) imesema mwanamke aliyekuwa amebeba vilipuzi alijaribu kuingia ndani ya mgahawa huo lakini akazuiwa na mlinzi wa usalama. Kifaa hicho kililipuka na kusababisha vifo vya mwanamke huyo, mlinzi pamoja na mteja mmoja wa mgahawa huo.

    Mgahawa huo, uliopo ndani ya moja ya majengo maarufu ya enzi ya Stalin jijini Moscow, ulikuwa ukiandaa hafla binafsi wakati wa tukio hilo.

    Mamlaka hazijatoa taarifa kuhusu orodha ya wageni waliohudhuria hafla hiyo wala kueleza ni nani aliyelengwa na shambulio hilo.

    Mashahidi wamesema waliona watu wakitolewa eneo la tukio wakiwa wamejaa damu kufuatia mlipuko huo.

    Ripoti za awali zilidai mlipuko ulitokea jikoni, lakini baadaye uongozi wa mgahawa ulisema kuwa "tatizo lilitokea nje ya jengo."

    Video iliyochapishwa na shirika la habari la RIA ilionyesha maafisa wa usalama wenye silaha nzito wakiwa eneo la tukio, ambalo lilikuwa limezingirwa na kuzuiwa kwa umma.

    Katika miaka ya hivi karibuni, maafisa kadhaa waandamizi wa jeshi la Urusi wameuawa ndani na maeneo ya karibu na Moscow, huku serikali ya Urusi ikiilaumu Ukraine kwa mashambulizi hayo.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Mashambulizi yasitishwa: Trump aitaka Iran kufanya makubaliano haraka

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema amesitisha mpango wa kufanya mashambulizi dhidi ya Iran kwa sharti kwamba makubaliano yafikiwe "haraka" kati ya pande hizo mbili.

    Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema aliamua "kufuta shambulio hilo, mradi tu iwezekane kufikiwa kwa MAKUBALIANO kwa haraka", ambayo yatajumuisha kufunguliwa mara moja kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz na kumalizika kwa kile alichokiita "tishio la nyuklia la Iran."

    Trump alisema uamuzi huo ulifikiwa kwa ushirikiano na Israel. Kauli hiyo imekuja wakati vyombo vya habari vya Marekani vikiripoti kuwa Marekani ilikuwa ikifikiria kufanya mashambulizi mapya na makali dhidi ya Iran mwishoni mwa wiki.

    Awali, Iran iliishutumu Marekani kwa kuongeza mvutano katika eneo hilo, ikionya kwamba taifa lolote la kikanda litakaloshirikiana na Marekani "litamezwa na vita" hivyo.

    Katika ujumbe wake, Trump alisema Marekani iko "tayari kabisa kwa hatua za kijeshi" dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akidai kuwa nguvu, uwezo wa kijeshi na vitisho vya Marekani vinafikia kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia.

    Hata hivyo, alisema aliamua kusitisha mashambulizi hayo baada ya kuombwa na Iran pamoja na baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati kusubiri ili kutoa nafasi kwa mazungumzo ya kufikia makubaliano.

    Trump pia alidokeza kuwa hatua imepigwa katika mazungumzo hayo, akisema kuwa "misingi ya makubaliano tayari umefikiwa."

    "Hatua hii itajumuisha kufunguliwa mara moja, kikamilifu na bila masharti kwa Mlango wa Hormuz, pamoja na kumaliza tishio la nyuklia la Iran," Trump aliandika.

    Soma Zaidi:

  14. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu ya mubashara ya tarehe 2/08/2026. Mimi ni Asha Juma.