Vikosi vya
Urusi na Mali vinavyopambana na waasi kaskazini mwa Mali vimepokea msafara
mkubwa wa magari ya kijeshi, ambayo yanaonekana kusafirishwa na meli ya mizigo
ya Urusi iliyowekewa vikwazo, uchunguzi wa BBC Verify umebaini.
Msafara
mkubwa wa magari ya kivita ulionekana ukiwasili jijini Bamako katika video
zilizothibitishwa na kuonyeshwa na televisheni ya taifa ya Mali tarehe 25
Julai. Waandishi wa habari waliripoti kuwa msafara huo ulisafiri kutoka bandari
ya Lomé nchini Togo.
Kwa mujibu
wa taarifa za ufuatiliaji wa meli zilizochambuliwa na BBC Verify, meli ya
mizigo ya Urusi Mikhail Britnev, ambayo imewekewa vikwazo, ilitia nanga katika
bandari ya Lomé tarehe 9 Julai. Picha za satelaiti zinaonyesha kuwa meli hiyo
huenda ilikuwa imebeba malori ya kijeshi, magari ya kubeba wanajeshi yenye
silaha pamoja na magari mepesi ya kivita yanayofanana na yale yaliyoonekana
jijini Bamako.
Taarifa za
ufuatiliaji wa meli zinaonyesha kuwa meli Mikhail Britnev iliondoka katika
bandari ya Baltiysk nchini Urusi tarehe 18 Juni, ikapitia Bahari ya Kaskazini
kabla ya kuingia katika Mfereji wa Uingereza."
BBC Verify
imeelezwa kuwa meli hiyo ilisindikizwa kupitia mfereji wa Uingereza na manowari
ya kivita ya Urusi ya daraja la Ropucha. Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imekataa
kutoa maoni kuhusu taarifa hizo.
Wachambuzi
wanasema usafirishaji huo unaonyesha kuwa Urusi inaongeza msaada wake kwa utawala
wa kijeshi wa Mali, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi makubwa kutoka
kwa waasi wanaoongozwa na kundi la jihadi la Jama'at Nusrat al-Islam
wal-Muslimin (JNIM) pamoja na waasi wa Kitouareg. Mashambulizi hayo yamewezesha
waasi hao kuteka maeneo makubwa kaskazini mwa nchi.
Urusi
imekuwa ikiisaidia serikali ya kijeshi ya Mali tangu kuondoka kwa vikosi vya
Ufaransa mwaka 2022, ikipokea malipo ya fedha pamoja na upendeleo wa kufikia
migodi na machimbo ya dhahabu nchini humo.
Awali, kundi
la mamluki la Wagner lilikuwa likifanya operesheni zake Mali, lakini shughuli
hizo baadaye zilichukuliwa na Africa Corps, kikosi kinachosimamiwa na Wizara ya
Ulinzi ya Urusi.
Serikali ya
kijeshi ya Mali imepata pigo mara kadhaa katika uwanja wa mapambano katika wiki
za hivi karibuni.
Siku ya
Jumatano, shirika la Amnesty International liliitaka kufanyika uchunguzi wa
uhalifu wa kivita kufuatia madai ya kuuawa kwa takriban wanajeshi 19 wa Mali
baada ya kuvamiwa mapema mwezi huu.