Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Makumi ya watu wauawa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon

Israel inasema imeshambulia maeneo 100 ya miundombinu ya Hezbollah na wapiganaji wake nchini Lebanon, baada ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuapa "kuiangamiza" Hezbollah.

Moja kwa moja

  1. Nasa yazindua hatua zinazofuata za kujenga kituo cha kudumu mwezini

    Nasa imetoa maelezo ya vifaa inayopania kupeleka anga za juu ikiwa ni pamoja na roboti, ndege zisizo na rubani na magari ambayo kama sehemu ya mipango ya Marekani ya kujenga kituo cha anga mwezini.

    Kampuni ya anga ya juu ya mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos ya Blue Origin ni mojawapo ya makampuni kadhaa yaliyochaguliwa kujenga mashine hizo.

    Marekani inataka kuwarejesha Wamarekani kwenye Mwezi kabla ya Rais Donald Trump kuondoka madarakani mwaka 2029.

    Lakini Nasa inashindana na China kurudisha wanadamu mwezini, kumaanisha shirika hilo la anga liko chini ya shinikizo la kushinda mbio mpya za anga.

    China inaendelea mbele na mipango yake ya kuwapeleka wanadamu Mwezini ifikapo 2030.

    Siku ya Jumatatu ilizindua chombo chake cha anga za juu cha Shenzhou-23, na kutuma wafanyakazi wa wanaanga kwenye kituo cha anga za juu cha Tiangong nchini humo.

    Mnamo Machi, Nasa ilitangaza mpango wa dola bilioni 20 wa kujenga kituo cha kudumu itakayoendeshwa na nguvu ya nyuklia na nishati ya jua kwenye ncha ya kusini ya Mwezi ifikapo 2032.

    Msimamizi wa Nasa Jared Isaacman alisema Jumanne kwamba matangazo hayo yanamaanisha Marekani "haitaachana tena na harakati zake mwezini".

    Soma zaidi:

  2. Makumi ya watu wauawa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon

    Makumi ya watu wameuawa katika wimbi kubwa la mashambulizi ya Israel kusini na mashariki mwa Lebanon, baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuapa kuongeza hatua za kijeshi dhidi ya Hezbollah.

    Takriban watu 31 wameuawa katika wimbi la hivi punde la mashambulizi, wakiwemo watoto kadhaa, wizara ya afya ya Lebanon ilisema.

    Jeshi la Israel limesema lilipiga zaidi ya maeneo 100 ya miundombinu ya Hezbollah na wapiganaji wake katika siku ambayo ilikuwa ni moja ya usiku mzito zaidi wa mashambulizi ya mabomu tangu usitishaji vita uliosimamiwa na Marekani uanze kutekelezwa katikati ya mwezi Aprili.

    Haya yanajiri baada ya Netanyahu kusema Jumatatu kwamba ametoa maagizo ya "kushinikiza juhudi zaidi" katika kulenga Hezbollah.

    Akizungumza katika kikao cha baraza la mawaziri la usalama siku ya Jumanne, alisema Israel "inazidisha operesheni nchini Lebanon".

    "IDF [Vikosi vya Ulinzi vya Israel] vinashirikiana na vikosi vikubwa ardhini na kuchukua eneo kubwa," alisema, akiongeza kuwa "wanaimarisha eneo la usalama" kulinda jamii za kaskazini mwa Israel kutokana na mashambulizi ya Hezbollah.

    Usitishaji wa mapigano umekuwa ukikiukwa mara kwa mara na pande zote mbili, na hatua hiyo inatishia kusambaratisha mazungumzo tata yanayoendelea ili kumaliza vita kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Mashambulio ya anga ya Israel yameendelea kila siku, hasa kusini mwa Lebanon, wakati Hezbollah imekuwa ikirusha maroketi na ndege zisizo na rubani kulenga jamii za kaskazini mwa Israel na wanajeshi wa Israel wanaokalia maeneo ya kusini mwa Lebanon.

    Soma pia:

  3. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.