Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

'Kigogo' Marekani ajiuzulu kupinga vita dhidi ya Iran

Katika barua yake ya kujiuzulu kwenda kwa Rais Donald Trump, Joe Kent anasema haungi mkono vita hiyo ambayo Marekani inashirikiana na Israel dhidi ya Iran akisema "Iran haikuwa tishio lolote la karibu letu".

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu & Asha Juma

  1. ‘Siwezi kuunga mkono vita’ - Mkuu wa Kituo cha Kupambana na Ugaidi Marekani ajiuzulu

    Afisa mkuu wa Marekani anayeshughulikia mapambano dhidi ya ugaidi nchini Marekani Joe Kent, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo akisema "Nikiwa na nia njema, siwezi kuunga mkono vita vinavyoendelea nchini Iran".

    Seneti ilimthibitisha Joe Kent kama chaguo la Trump kwa nafasi hiyo Julai iliyopita.

    Katika katika barua yake ya kujiuzulu kwenda kwa Trump, Kent anasema: "Iran haikuwa tishio lolote kwa taifa letu, na ni wazi kwamba tulianzisha vita hivi kutokana na shinikizo kutoka kwa Israeli na ushawishi wake wenye nguvu kwa Marekani."

    "Ninaunga mkono maadili na sera za kigeni ulizofanya kampeni mwaka 2016, 2020, 2024, ambazo ulizitekeleza katika muhula wako wa kwanza."

    "Hadi Juni 2025, mlielewa kwamba vita vya Mashariki ya Kati vilikuwa mtego ulionasa maisha ya thamani ya wazalendo wetu wa Marekani na kupunguza utajiri na ustawi wa taifa letu."

    "Kama mkongwe aliyejitolea kupigana mara 11 na kama mume wa ‘Gold Star’ niliyempoteza mke wangu mpendwa Shannon katika vita vilivyotengenezwa na Israeli, siwezi kuunga mkono kupeleka kizazi kijacho kupigana na kufa katika vita ambavyo haviwanufaishi watu wa Marekani wala havihalalishi gharama ya maisha ya Wamarekani."

  2. Umoja wa Mataifa waiomba Iran ifanye uchunguzi kuhusu shambulizi baya la shule

    Mwanachama wa ujumbe wa kutafuta ukweli wa Umoja wa Mataifa nchini Iran amesema wachunguzi wanatafuta njia ya kufikia eneo kulikofanyika shambulizi baya dhidi ya shule mwanzoni mwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Max du Plessis anasema Umoja wa Mataifa una ripoti za kuaminika kwamba takriban watu 168 waliuawa katika shambulizi hilo, huko Minab kusini mwa Iran, na wengi wao walikuwa wanafunzi wa kike - wengi wakiwa na umri wa miaka saba.

    Du Plessis amesema Umoja wa Mataifa unajaribu kujua ni nani aliyehusika, sababu ya shambulizi hilo ilikuwa nini, na matokeo ya kisheria, "ikiwa yapo", yanaweza kuwa nini.

    "Tuko katika hatua za mwanzo za uchunguzi," amesema.

    Marekani inafanya uchunguzi wake kuhusu shambulizi hilo, na du Plessis anasema ingawa timu hiyo bado haijazungumza na mtu yeyote kutoka Marekani, watakaribisha taarifa yoyote iliyotolewa, ingawa anasisitiza wajibu wa "huru" wa Umoja wa Mataifa wa kubaini ukweli.

    "Tumeomba turuhusiwe kufika Iran na tutaendelea kutafuta ufikiaji huo," alisema.

    Soma zaidi:

  3. Mamlaka Iran imekamata 'mamia ya vifaa vya Starlink'

    Wizara ya Ujasusi ya Iran inasema katika taarifa kwamba imekamata "mamia ya vifaa vya Starlink vilivyotumwa na adui" - ikimaanisha Marekani na Israeli, vyombo vya habari vya Iran vinaripoti.

    Taarifa hiyo inasema kwamba kwa mujibu wa sheria, kupata na kutumia Starlink ni "uhalifu" na wakati wa vita mtu yeyote anayefanya hivyo atachukuliwa hatua "kali zaidi".

    Kutumia Starlink nchini Iran kuna adhabu ya hadi miaka miwili jela.

    Bado ni vigumu sana kuwasiliana na wale walio ndani ya Iran wakati intaneti ambayo imekuwepo tangu kuanza kwa vita imeminywa, lakini wakazi wenye ujuzi wa teknolojia wamekuwa wakitumia vifaa vya SpaceX vya Starlink na kushiriki miunganisho yao na wengine.

    Soma zaidi:

  4. Mara ya mwisho Larijani kuonekana hadharani

    Ali Larijani alipigwa picha ya mwisho hadharani katika maandamano ya Siku ya Quds huko Tehran mnamo tarehe 13 Machi, kulingana na akaunti yake ya X ambayo ilidaiwa kumwonyesha barabarani akipunga mkono na kuzungumza na wafuasi.

    Siku moja kabla, alimdhihaki Rais Trump kwenye mitandao ya kijamii, akichapisha kwenye X kwamba "Trump anasema anatafuta ushindi wa haraka. Ingawa kuanzisha vita ni rahisi, haiwezi kushindwa kwa kutuma ujumbe mfupi wa Twitter."

    "Hatutakubali hadi uombe msamaha kwa kosa hili kubwa."

    Katika chapisho jingine mnamo Machi 10, Larijani alisema Iran haikuwa na hofu na "vitisho" vya Trump, akiongeza kwamba "hata wale wakubwa kuliko wewe hawawezi kuangamiza taifa la Iran".

    "Kuwa mwangalifu, usiangamizwe," aliongeza.

    Soma zaidi:

  5. Habari za hivi punde, Milipuko ya kujitoa muhanga yaikumba Maiduguri Nigeria

    Msururu wa milipuko mibaya ya kujitoa mhanga yaikumba Maiduguri, mji mkuu wa Jimbo la Borno, Jumatatu jioni, na kuua na kujeruhi idadi ya watu ambayo haijathibitishwa na kuzua hofu mpya katika eneo hilo

    Taarifa ya Jeshi la Nigeria ilisema kuwa milipuko hiyo ilitokea mwendo wa saa 7:05 mchana, katika kipindi cha shughuli nyingi za Iftar, wakati Waislamu walipokuwa wakifungua mfungo wao.

    Ilieleza zaidi kwamba mashambulizi hayo yalitekelezwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Boko Haram wa kujitoa mhanga, ambao walilipua vifaa vyao katika maeneo matatu tofauti - eneo la Posta, mhimili wa Soko la Jumatatu na lango la Hospitali ya Kufundishia la Chuo Kikuu cha Maiduguri (UMTH).

    Jeshi lilielezea tukio hilo kama "jaribio la woga la kusababisha vifo vya watu wengi" katika maeneo ya umma yenye watu wengi. "

    Wanajeshi wa Operesheni Hadin Kai, wakiungwa mkono na timu ya Polisi ya Nigeria ya Kutegua mabomu na mashirika mengine ya usalama, waliingia haraka ili kuzingira maeneo yaliyoathiriwa.

    Wahudumu wa dharura, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Dharura (NEMA), waliwakimbiza waathiriwa katika Hospitali Kuu, kwa matibabu ya haraka," taarifa hiyo ilisema zaidi.

    Ripoti zinaonyesha kuwa washambuliaji wengi wa kujitoa mhanga walisambazwa katika jiji lote, ikionyesha mpango ulioratibiwa kulenga vituo vya shughuli nyingi zaidi vya Maiduguri.

    Mamlaka imewataka wakazi kuwa watulivu lakini wawe waangalifu na kuripoti watu wanaotiliwa shaka au vitu vilivyoachwa kwa vyombo vya usalama.

    Vikosi vya usalama pia vimeimarisha doria, ufuatiliaji na operesheni za kukabiliana na IED ili kuzuia mashambulizi zaidi.

  6. Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad umelengwa

    Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ulilengwa na ndege zisizo na rubani na roketi usiku kucha, huku vyanzo vya usalama vya Iraq vikiambia shirika la habari la AFP kwamba ilikuwa "shambulizi kali zaidi tangu mashambulizi yaanze".

    Tukufahamishe kile ambacho kimekuwa kikiendelea:

    • Moto umetokea katika hoteli ya kifahari huko Baghdad ukitokana na ndege isiyo na rubani katika eneo la Green Zone lenye ngome kubwa jijini humo, ambapo pia majengo ya ubalozi wa Marekani na serikali yapo.
    • Raia wa Pakistani ameuawa na vifusi vya makombora huko Abu Dhabi, kulingana na maafisa wa serikali.
    • Huku Israel ikiendelea na mashambulizi dhidi ya Lebanon - Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uingereza zinazihimiza nchi zote mbili kuanza mazungumzo kufuatia kile wanachosema ni hali ya kibinadamu "inayotisha sana" nchini humo.
    • Akizungumza na BBC Newsnight siku ya Jumatatu, Rais wa Finland Alexander Stubb alimtetea Keir Starmer kufuatia ukosoaji wa Rais Trump dhidi ya Uingereza kuhusu mzozo huo - mwandishi wetu wa Marekani Kaskazini anasema Trump ameonekana kuchanganyikiwa zaidi na washirika wa Ulaya

    Soma zaidi:

  7. Trump: Hakuna kilichosalia kwenye makombora na drone za Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump amedai kuwa Iran sasa ina takriban 8% tu ya makombora yake na idadi ndogo ya ndege zisizo na rubani.

    Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval ya White House Jumatatu jioni, na huku Makamu wa Rais J.D. Vance akiwa amesimama karibu naye, alisema, "Ndio, bila shaka."

    Lakini alipoulizwa ikiwa kweli vita vitaisha wiki hii, aliongeza, "Sidhani hivyo, lakini vitaisha hivi karibuni. Haitachukua muda mrefu."

    Bw Trump pia alisema alihisi "analazimika" kuchukua hatua ya kijeshi, akiongeza kuwa "tutakuwa na ulimwengu salama" baada ya vita kumalizika.

    Amekuwa akidai mara kwa mara kwamba mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel yameharibu sehemu kubwa ya uwezo wa kijeshi wa Iran na kwamba vita hivyo vitamalizika "hivi karibuni sana," ingawa hakuna muda maalum uliotangazwa bado wa kumalizika kwa operesheni hiyo.

    Aidha amesema baadhi ya nchi zimekatisha tamaa kwa kutoiunga mkono Marekani katika vita na Iran.

    Bw Trump alitaja haswa mataifa wanachama wa NATO na kurejelea mazungumzo yake na Keir Starmer, ambaye alisema awali alikuwa akisita kuomba msaada lakini baadaye akatoa usaidizi fulani.

    Bw. Trump aliongeza: "Kwa kuwa sasa tumeshinda tena, hatuhitaji tena meli zako za kubeba ndege."

  8. Trump: 'Hakuna njia nyengine isipokuwa kuahirisha mkutano wangu na China

    Rais Trump alisema Jumatatu kwamba anapanga kuchelewesha ziara ya China baadaye Machi kwa takriban mwezi mmoja kwa sababu ya vita vya Iran.

    "Ni rahisi sana. Tuna vita vinavyoendelea. Nadhani ni muhimu kuwa hapa," alisema, akisisitiza "hakuna hila" na alikuwa akitarajia kumuona Rais Xi Jinping.

    Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Trump kuliambia gazeti la Uingereza la Financial Times kwamba anaweza kuahirisha mkutano huo ikiwa China haitasaidia kufungua mlango wa bahari wa Hormuz - njia muhimu ya maji kwa usafirishaji wa mafuta .

    Matamshi hayo ya Trump yanakuja huku msuguano kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa zaidi duniani ukizidi kuchochewa na vita vya Iran.

    Beijing ni mnunuzi mkuu wa mafuta ya Iran na imekosoa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya nchi hiyo.

    Washington pia ilitangaza kuwa itachunguza mazoea ya biashara kati ya orodha ya nchi, pamoja na Uchina, baada ya sera ya ushuru ya Trump kutupiliwa mbali na Mahakama ya Juu mnamo Februari.

    Wawakilishi kutoka Marekani na China wamekutana mjini Paris katika siku za hivi karibuni kwa mazungumzo kuhusu uwekezaji, ushuru na vikwazo vya kiuchumi.

  9. Kwa nini meli ya mafuta ya Pakistani ilichukua njia ndefu kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz?

    Tumekuwa tukifuatilia meli kadhaa ambazo zinaonekana kupita kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz leo.

    Mojawapo ni Karachi yenye bendera ya Pakistan ambayo imebeba shehena ya mafuta yasiyosafishwa na inamilikiwa na shirika la serikali la Pakistan National Shipping Corporation.

    Tukiangalia data ya ufuatiliaji wa Trafiki ya Baharini tunaweza kuiona iliingia katika eneo la Kiuchumi Pekee la Iran (EEZ), ikisafiri kati ya visiwa vya Qeshm na Larak, na karibu na pwani ya Irani ilipoelekea kusini.

    Tulimuuliza nahodha wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Marekani Bradley Martin kwa nini huenda meli hiyo imechukua njia ndefu na isiyo ya kawaida katika eneo hilo.

    Bradley, ambaye sasa ni mtafiti mkuu katika taasisi ya ulinzi ya Marekani ya Rand Corporation, anasema inaweza kuashiria kuwa meli hiyo "ilikuwa ikijibu baadhi ya maagizo kutoka Iran kuhusu kupita".

    Anaongeza kuwa njia yake inaweza kuashiria uwepo wa mambomu yaliotegwa, au ilichaguliwa na Iran ili iweze kutambuliwa kwa urahisi kati ya meli nyingine katika eneo hilo.

    Jonathan Schroden, mwanasayansi wa utafiti wa kanuni katika Kituo chenye makao yake nchini Marekani cha Uchambuzi wa Wanamaji, anakubali njia ya meli inaweza kuonyesha kuwa kuna ambamu yaliotegwa katika eneo hilo - au kwamba Iran iliichagua kuchukua hatua hiyo kwa sababu inataka kuonyesha kwmba kuna mabomu yaliotegwa katika njia hiyo

  10. Habari za hivi punde, Israel inasema Iran imerusha wimbi jipya la makombora

    Jeshi la Israel linasema makombora yaliyorushwa kutoka Iran yanaelekea nchini humo na limewataka watu kuelekea kwenye makazi yao ili kujilinda.

    "Mifumo ya ulinzi inafanya kazi kuzuia tishio," tahadhari ya dharura iliyotumwa kwenye mtandao wa Telegram imesema.

  11. Natumai hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja