Ni nini kilisababisha kuporomoka kwa barafu na kusababisha mafuriko na maafa Nepal?

Chanzo cha picha, Reuters
Mafuriko makubwa yaliyoikumba Nepal na Tibet, na kusababisha mamia ya watu kufariki na wengine kupotea inasemekana kutokana na kuporomoka kwa barafu, kulingana na wanasayansi.
Picha zilizopigwa wakati wa maafa hayo zinaonyesha watu wakikimbia sekunde chache kabla ya maporomoko makubwa ya matope kupita katika maeneo ya makazi na kuharibu madaraja, majengo na miundombinu mingine.
Mwanzoni, wanasayansi waliamini kuwa chanzo cha maafa hayo ni tetemeko la ardhi. Hata hivyo, baadaye waligundua kuwa mitikisiko iliyorekodiwa ilisababishwa na kuporomoka kwa barafu kutoka kwa milima.
Basanta Raj Adhikari, mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Maafa katika Chuo Kikuu cha Tribhuvan nchini Nepal, aliiambia BBC kuwa kuna hatari ya kutokea "wimbi la pili na la tatu" la mafuriko.
Kwa mujibu wa Adhikari, hakuna mvua kubwa inayotarajiwa, lakini maporomoko mapya ya ardhi yanaweza kutokea.
"Tuko katika hali ya tahadhari. Hatungeweza kujua kwamba jambo hili lingetokea," alisema.
Adhikari pia amesema watafiti wamekuwa wakifuatilia hatari zinazohusishwa na milima ya Himalaya, akisema hali hiyo ni ishara kwamba "mabadiliko ya tabianchi yanatokea kweli."
Kuporomoka kwa barafu ya mlima ndicho chanzo kinachoangaziwa kuchochea mafutiko hayo makubwa.
Kuporomoka kwa barafu ya mlima ndicho chanzo kinachoangaziwa kuchochea mafuriko hayo makubwa.

Chanzo cha picha, Reuters
Msemaji wa serikali ya Nepal na taasisi za kijiolojia awali walisema mafuriko hayo yalisababishwa na tetemeko la ardhi.
Shirika la Utafiti wa Jiolojia la Marekani (USGS) ilirekodi mtikisiko mkubwa muda mfupi kabla ya mafuriko kutokea.
Hata hivyo, saa chache baadaye, taasisi hiyo ya Marekani ilirekebisha taarifa yake, ikisema mtikisiko huo haukusababisha mafuriko, bali ulitokana na maporomoko makubwa ya barafu.
Kwa maneno mengine, sehemu kubwa ya barafu ya mlima ilikatika kutoka milimani na kushuka kwa kasi.
Nadharia hii pia inaungwa mkono na uchunguzi uliofanywa kupitia picha za satelaiti.

Chanzo cha picha, Reuters
Simon Cook, profesa wa Nishati, Mazingira na Usalama katika Chuo Kikuu cha Dundee nchini Scotland, na mtaalamu wa masuala ya barafu milimani, aliiambia BBC kuwa mmoja wa wenzake katika timu yake aligundua kwamba sehemu ya chini ya barafu ya mlima karibu na eneo lililoathiriwa ilikuwa imetoweka.
Kwa mujibu wa Cook, picha hiyo ilionyesha kuwa kulikuwa na "aina fulani ya maporomoko ya barafu au kuporomoka kwa barafu ya mlima."
Mkusanyiko huo wa barafu, mawe na vifusi ulifika katika mto Lhende Khola na huenda ukazuia kwa muda mtiririko wa maji.
Kizuizi hicho kilipovunjika, wimbi kubwa la maji, barafu, mawe na matope yalisonga kwa nguvu kuelekea maeneo ya chini ya mto.
Wataalamu waliozungumza na Idhaa ya BBC Nepal wanasema jiografia ya eneo hilo, yenye mabonde membamba na maeneo yenye miteremko yalichangia mawimbi hayo ya maji na vifusi kusambaa kwa kasi.
Hata hivyo, wanasayansi bado wanahitaji kuthibitisha kwa undani matukio hayo.

Chanzo cha picha, Reuters
Athari ya mabadiliko ya tabianchi
Bado ni mapema mno kubaini ni kwa kiwango gani mabadiliko ya tabianchi yalichangia maafa hayo.
Cook anasema timu yake "ilishtushwa na ukubwa wa janga hilo", na anakumbuka kuwa matukio kadhaa yanayofanana yameripotiwa katika miaka ya hivi karibuni katika maeneo kama Himalaya, Uswisi na Dolomites nchini Italia.
Kwa mujibu wa Cook, ongezeko la joto duniani huenda linasababisha permafrost . Permafrost husaidia kushikilia pamoja baadhi ya miteremko ya milima. Inapopoteza uimara, mazingira ya milima mirefu yanaweza kuwa katika hatari zaidi ya kuyumba.
Hali hiyo inaweza kusababisha kuongezeka kwa maporomoko ya ardhi, kuyeyuka kwa barafu, kupasuka kwa maziwa ya barafu na kuporomoka kwa barafu ya milimani.
Hata hivyo, bado haiwezekani kubaini kwa usahihi ni kwa kiwango gani mabadiliko ya tabianchi yalichangia maafa haya.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Nepal tayari imepoteza karibu theluthi moja ya barafu yake katika miongo mitatu iliyopita, huku barafu zake zikiyeyuka kwa kasi kati ya mwaka 2011 na 2020.

Chanzo cha picha, Reuters
Kwa nini eneo hili liko katika hatari kubwa?
Wataalamu wanasema eneo la mpakani kati ya Nepal na Tibet, eneo linalodhibitiwa na China, liko katika hatari kubwa ya kukumbwa na majanga ya asili kutokana na jiografia yake.
Eneo hilo lina baadhi ya milima mirefu zaidi duniani, barafu kubwa, maeneo yaliyofunikwa na theluji, pamoja na miteremko mikali isiyo imara.
Mito inayotiririka kutoka Nyanda za Juu za Tibet hushuka kwa kasi kupitia mabonde yenye kina kirefu kabla ya kufika katika maeneo yenye watu wengi nchini Nepal.
Wanasayansi wanaeleza kuwa hali hii huunda mazingira yanayoweza kusababisha mfululizo wa majanga kutokea.
Hatari ya mafuriko zaidi

Chanzo cha picha, Reuters
Mawimbi makubwa ya maji, matope na vifusi yalisonga kwa kasi ya kutisha katika maeneo ya kaskazini mwa Nepal, likiwemo eneo linalotembelewa na mahujaji na watalii wengi.
Picha za maafa hayo zinaonyesha ukuta mkubwa wa matope ukisomba majengo, madaraja na magari huku watu wakijaribu kutoroka.
Wimbi hilo la maji na vifusi lilifika kwanza katika mto Lhende Khola na baadaye kusonga kupitia mito mingine iliyounganishwa nao, ikiwemo Bhote Koshi, Trishuli na Narayani.
Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo Jumuishi ya Milima (ICIMOD) kilionya katika ripoti yake kwamba mafuriko zaidi yanaweza kutokea katika siku zijazo.
Timu za uokoaji pia zinaendelea kuwatafuta watu waliopotea na kuwahudumia waliojeruhiwa, katika operesheni inayokabiliwa na changamoto kutokana na hali ya kijiografia na tabianchi ya eneo hilo.
Je, aina hii ya janga inaweza kuzuiwa?

Chanzo cha picha, Reuters
Matukio kama maporomoko ya ardhi, maporomoko ya theluji na kuporomoka kwa barafu ya milimani hayawezi kuzuiwa kabisa, lakini wataalamu wanasema madhara yake yanaweza kupunguzwa.
Mifumo ya tahadhari ya mapema inazidi kuwekwa katika mabonde yaliyo katika hatari na maeneo yanayozunguka maziwa ya barafu.
Mifumo hiyo inaweza kufuatilia mabadiliko yanayotokea na tahadhari ya watu kuhama maeneo hatari inaweza kutolewa haraka.
Watafiti pia wanasema ushirikiano bora zaidi kati ya nchi ni muhimu, kwa kuwa matukio mengi ya aina hii huanzia katika maeneo ya mbali ya Tibet kabla ya kuathiri Nepal.
"Kama lingetokea Nepal, tungeweza kuliona kutoka hapa. Lakini katika matukio kama haya, ni muhimu kuimarisha mfumo wa kubadilishana taarifa kati ya nchi," alisema Basanta Raj Adhikari, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Majanga katika Chuo Kikuu cha Tribhuvan nchini Nepal.
Wataalam pia wanasema kupunguza idadi ya watu na shughuli zilizo katika maeneo hatarishi kunaweza kuwa njia bora zaidi ya kujikinga na majanga haya.











