Kutoka Nyoka hadi Buibui: Wanyama hawa ni Hatari kweli au Hisia zetu tu?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Unahisi vipi wakati buibui anapokimbia ghafla sebuleni?

Buibui wengi wana sumu, lakini ni idadi ndogo tu kati yao inayoweza kuhatarisha maisha ya binadamu. Kulingana na Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Mazingira, inakadiriwa kuwa watu wachache kuliko 10 duniani kote hufariki kila mwaka kutokana na kuumwa na buibui, ingawa ni vigumu kupata takwimu sahihi.

Licha ya hayo, watu wengi hukiri kuwa na hofu kubwa isiyo ya kawaida dhidi ya buibui.

Hofu za aina hii mara nyingi humaanisha uwepo wa hofu kali dhidi ya kitu ambacho, kwa asili yake, hakileti tishio kubwa.

Basi, kwa nini hofu hizi ni za kawaida sana, na chanzo chake ni nini?

Kutoka hofu hadi fobia

Kulingana na Vanessa LoBue, profesa wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Rutgers nchini Marekani, hofu ina nafasi muhimu ya kutoa kinga.

"Hofu ni muhimu kwa sababu hutulinda dhidi ya mambo yanayoweza kuwa hatari," anasema.

Hata hivyo, ikiwa hofu hiyo itakuwa kali na kumsababisha mtu kushindwa kabisa kutenda lolote, inaweza kuchukuliwa kuwa fobia, anasema András Zsidó, mkurugenzi wa Maabara ya Utambuzi wa Kuona na Hisia katika Chuo Kikuu cha Pécs nchini Hungaria.

"Unaweza kuliona hili kama mwendelezo. Huanza na hofu ya kawaida kabisa, kwa sababu kila mtu huogopa kitu fulani," anaeleza. "Lakini hofu hiyo inapoanza kuathiri shughuli za kila siku, tunaweza kusema ni fobia."

LoBue pia anasisitiza kuwa hofu ya kawaida huwa kubwa kupita kiasi ikilinganishwa na tishio halisi.

Katika baadhi ya maeneo duniani, kama vile Uingereza, aina nyingi za nyoka hazileti tishio kwa binadamu. Hivyo, kuwa na hofu kubwa dhidi yao kunaweza kuchukuliwa kuwa fobia.

Hata hivyo, katika maeneo ambayo tishio linalotokana na nyoka ni kubwa zaidi, hofu ya namna hiyo inaweza kuwa na uhalali zaidi.

Je, hofu ni ya kuzaliwa nayo?

Ingawa aina fulani za hofu kali ni za kawaida sana, wataalamu wengi wanaamini kwamba hatuzaliwi nazo. LoBue anaamini kuwa hofu ni hisia ambayo watoto wadogo bado hawana uwezo wa kuipata.

"Hofu huja baadaye kwa sababu inahitaji mtu kutambua kuwa kitu fulani ni tishio. Ili kutathmini hilo, unahitaji kuwa na maarifa fulani kuhusu ulimwengu," anasema.

Basi, ikiwa hatuzaliwi na hofu ya buibui au nyoka, kwa nini viumbe hawa mara nyingi huwa chanzo cha hofu hizo kali?

LoBue anaamini kuwa tunajifunza kuwaogopa buibui na nyoka kwa urahisi zaidi kuliko wanyama wengine kwa sababu wanaonekana "wa ajabu" kwetu.

"Fikiria nyoka. Hakuna kiumbe kingine duniani kinachofanana nao kwa muonekano au namna wanavyosonga," anasema.

"Watoto wadogo wanapojifunza kuhusu wanyama, kwa kawaida huwaona wakitembea kwa miguu. Nyoka hawasongi hivyo. Buibui nao husonga kwa njia zisizo za kawaida. Hali hiyo inaweza kutufanya tuhisi wasiwasi."

Wataalamu wengine wanaamini kuwa tabia ya kuogopa vitu fulani inaweza kuwa matokeo ya historia ya mageuzi ya binadamu.

"Mazingira ambayo binadamu wa kale waliishi yalikuwa na hali isiyotabirika kabisa," anasema Zsidó.

"Hofu na woga uliopitiliza hapo awali vilikuwa na msingi wa mantiki katika muktadha wa maendeleo ya binadamu. Hata hivyo, kadiri muda ulivyopita, vilipoteza baadhi ya manufaa na uhalali wake katika maisha ya kila siku."

Hata hivyo, mwelekeo wa kibaolojia wa hofu, unaojulikana kama nadharia ya utayari, hauwezi pekee yake kueleza kwa nini baadhi ya watu hupata hofu kali dhidi ya vitu fulani.

Kulingana na LoBue, njia ya haraka zaidi ya kujenga hofu ni kupitia tukio hasi la moja kwa moja linalohusisha mnyama au kitu fulani, hasa ikiwa mtu tayari alikuwa na mwelekeo wa kuathiriwa na aina hiyo ya hofu.

Hata hivyo, tunaweza pia kujifunza kuogopa kitu fulani kwa kuangalia jinsi watu wengine wanavyokikabili au wanavyokihofia.

"Kuna mwitikio wa kimwili, kwa mfano tunapong'atwa au kuogopeshwa," anasema LoBue.

"Kisha kuna mwitikio wa mzazi, kwa mfano mama anaposema, 'Ndiyo, hiki ni kitu hatari kweli.' Hali hiyo huongeza uwezekano wa mtu kujifunza kukiogopa kitu hicho."

LoBue pia anaamini kuwa kuenea kwa hofu kali dhidi ya buibui na nyoka kunachangiwa kwa kiasi fulani na utamaduni maarufu, ambao huathiri namna hofu zetu zinavyojengeka.

"Tazama filamu au vitabu vyetu," anasema. "Ni mara ngapi umewaona nyoka au buibui wakionyeshwa kama waokoaji? Karibu kamwe."

Kutokuwa na hofu

Wataalamu wengi wanakubali kuwa hofu kali zinaweza kushindwa, na kwamba njia bora zaidi ya kufanya hivyo ni kukabiliana hatua kwa hatua na chanzo cha hofu hiyo.

LoBue anashauri kuanza na hatua ndogo. Kwa mfano, mtu anaweza kuanza kwa kutazama picha za kitu anachokiogopa na kujifunza ukweli kukihusu, kisha kuongeza hatua kwa hatua ukaribu na kitu hicho kinachosababisha hofu.

Hata hivyo, ikiwa hofu hiyo ni kali sana na inaathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya kila siku, ni vyema kutafuta msaada kutoka kwa mtaalamu.

Utafiti wa Zsidó pia unaunga mkono nadharia kwamba kukabiliana na chanzo cha hofu hakuondoi tu hofu iliyopo, bali pia kunaweza kusaidia kuzuia hofu hiyo isitokee baadaye.

"Uzoefu wa kibinafsi ndiyo sababu muhimu zaidi katika kuibuka kwa hali ya wasiwasi," anasema. "Ikiwa uzoefu huo ni mzuri, kwa mfano wakati wa utoto au shuleni, unaweza kuwa na athari ya kinga na kupunguza hatari ya kupata tatizo la wasiwasi."

LoBue anasisitiza kuwa hofu ni muhimu kwa kujilinda na si jambo baya, na kwamba hofu kali inaweza kushindwa.

"Hatuzaliwi tukiwa na hofu ya vitu maalum," anasema. "Ikiwa unaogopa kitu fulani na unataka kuondoa hofu hiyo, kuna njia za kukusaidia kufanya hivyo."